Nenda kwa yaliyomo

Vitabu vya upotovu

Kutoka wikishia

Vitabu vya upotovu / upotoshaji (کُتُب الضَلال') ni maandiko ambayo yanapelekea wasomaji wake kuingia katika upotofu. Baadhi ya mafakihi wanaamini kuwa, maandiko au vitabu vya upotofu ni vile ambavyo mbali na kuwa vinapotosha tu, bali vimeandikwa pia kwa nia ya kupotosha. Neno vitabu vya upotofu haliishi kwa vitabu tu; bali inajumuisha pia makala, barua, majarida na magazeti yenye upotoshaji. Kadhalika makusudio ya upotofu hayashii katika masuala ya kiitikadi tu; bali yanajumuisha pia hukumu za kisheria.

Suala la vitabu vya upotofu liliiingizwa katika Fiqhi ya Kishia na Sheikh Mufid. Baada ya hapo, jambo hilo likaingia katika vitabu vingine vya mafakihi na kukajadiliwa hukumu zake kwa mujibu wa fiq’h. Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihi wa Kishia ni haramu kuweka vitabu vya upotofu, kununua na kuuza, kukopi, kusambaza, kusoma na kuvifundisha na ni wajibu kuteketeza maandiko hayo isipokuwa kama maandiko hayo yatatumika kwa ajili ya kuthibitisha haki na kupinga batili.

Maana ya kifiq’h

Vitabu vya upotovu (Kutub Dhal au Kutub Dhalal) katika maana yake ya kiada na kimazoea huitwa maandiko ambayo kupitia kwayo msomaji hupotea na kuingia katika upotovu; [1] lakini katika vitabu vya Fiqhi kuna fasili na maana tofauti na hiyo: Baadhi ya mafakihi wamechagua maana hii hii ya kiada na mazoea (iliyozoeleka baina ya watu). [2] Kundi jingine limesema kuwa, vitabu vya upotofu ni vile ambavyo vinaandikwa kwa nia na kusudio la kupotosha na kupoteza watu. [3] Aidha kwa mtazamo wa baadhi ya wengine ni kwamba, ni vitabu ambavyo vimeandikwa kwa nia na kusudio la kupotosha watu na vinapelekea watu kukumbwa na upotofu. [4]

Neno kutub katika ibara ya "Kutub Dhalal" linajumuisha kila andiko; iwe ni kitabu kwa maana hii inayofahamika au iwe ni makala au barua. [5]

Historia fupi na nafasi yake

Kwa mujibu wa baadhi ya wahakiki ibara ya "Kutub Dhalal" kwa mara ya kwanza ilizungumziwa na Sheikh Mufid katika kitabu chake cha al-Muq’nia’h [6] kwa anuani mbili “Kutub Kufr” na “Kutub Dhalal”. [7] Baada yake, mafakihi wengine akiwemo Sheikh Tusi. [8] Ibn Barraj, [9] Ibn Idris, [10] na Allama Hilii, [11] walitumia hizi anuani mbili.

"Kutub Dhalal" na "Kutub Dhal" ni anuani mbili ambazo kutokana na kutumika sana [12] taratibu zikazoeleka katika athari za Kifiq’h hususan athari za kifiq’h za zama hizi. [13]

Katika vitabu vya Fiq’h maudhui ya vitabu vya upotofu pamoja na hukumu zinazohusiana nayo haijazungumziwa kwa sura ya kujitegemea; bali imetajwa ndani ya mijadala na maudhui katika milango ya biashara, wakfu, kukodisha, wasia na kuazima. Katika kitabu chake cha Makasibu Sheikh Ansari chini ya anuani: "Vitu ambavyo kutokana na kuwa kwake haramu ni haramu kuvitumia kwa ajili ya chumo" amezungumzia maudhui yenye anuani "Kuhihadhi (kumiliki) Vitabu vya Upotofu". [14]

Upotoshaji katika nini na kwa ajili ya watu gani?

Kwa mujibu wa fat'wa ya mafakihi, dhalal (upotoshaji) au kupotosha kunarejea katika misingi mitano ya madhehebu; katika hukumu za kisheria yaani kila kitabu ambacho kinapelekea upotofu iwe ni katika misingi ya madhebu au katika hukumu za kisheria kinahesabiwa kuwa ni cha upotofu. [14] Kadhalika Ayatullah Montazeri ameandika, makusudio ya upotofu ni kupotea na kuingia katika upotofu aghalabu ya wasomaji; yaani isiwe kwamba, hata kama atasoma kitabu hicho mtu mmoja na akapotea basi kihesabiwe kuwa ni kitabu cha upotofu; kwani vitabu vyote hata Qur’an na vitabu vya hadithi vinaweza kuwapoteza watu wasio na elimu na wenye ufahamu mdogo au wasio na weledi na ufahamu wa mambo. [16]

Vielelezo vya upotofu

Katika maandiko ya fiq’h kuna mifano na vielelezo vya kutub dhal (vitabu vya upotofu) vilivyotajwa; hata hivyo kuna hitilafu za kimtazamo katika uga huu kuhusiana na hili. Kwa mfano, Allama Hilli (648-726 Hijiria), Muhaqqiq Karaki (aliaga dunia 940 Hijiria), torati na injili vimehesabiwa kuwa ni vitabu vya upotofu; kwa hoja hii kwamba, vitabu hivi vimepotoshwa; [17] lakini kwa mujibu wa Sheikh Ansari, kwa Waislamu ni jambo la wazi kwamba, vitabu hivi vilifutwa. Kwa msingi huo, havipelekei upotofu kwao. [18]

Kadhalika Yusuf Bahrani (1107-1186 Hijiria) mmoja wa Maulamaa wa Akhbariy wa Kishia anasema kuwa, maandiko na vitabu vya Ahlu-Sunna katika Usul al-Fiqh na kadhalika sehemu ya maandiko na vitabu vya Maulamaa wa Kishia katika elimu ya Usul al-Fiqh ambapo waliwafuata Ahlu-Sunna, ni mfano na kielelezo cha Kutub Dhal (vitabu vya upotofu); lakini Sayyid Jawad Amili (1160-1226-, mwandishi wa kitabu cha Mafatih al-Karamah ameyatambua haya maneno ya Bahrani kwamba, ni mfano na kielelezo cha upotofu. [19]

Sheikh Ansari ameandika pia: Hoja za kuharamishwa vitabu vya upotofu vinajumuisha vitabu ambavyo vinapelekea upotofu na kuna vitabu vingi vya wapinzani wa Mashia ambavyo haviko hivi. [20] Na anaona baadhi tu ya vitabu vya Sunni ambavyo vina itikadi kama vile kuthibitisha Jabr na kuonyesha ubora wa makhalifa kuwa ni mifano ya vitabu vya upotofu. [21] Baadhi ya mafakihi wamesema, vitabu vya falsafa na irfan ambavyo vinapelekea upotofu ni mifano na vielelezo vya wazi vya vitabu vya upotofu; hata kama yaliyoandikwa yatakuwa ni ya haki. [22]

Kundi la Marajii Taqldi wa zama hizi, Ayatullah Mkarim Shirazi na Ayatullah Safi Golpeygani, wanaamini kwamba, magazeti na majarida ambayo yana matusi na uchafu na ambayo yanapelekea ufisadi na upotofu katika jamii ni mifano ya wazi ya vitabu vya upotofu. [23]

Hukumu

Kwa mujibu wa mtazamo wa mafakihi, ni wajibu kuteketeza vitabu vya upotofu. [24] Baadhi ya mambo ambayo ni haramu kuhusiana na vitabu vya upotofu:

  • Ni haramu kuhifadhi vitabu vya upotofu na kupata kipato kupiti kwavyo. [25]
  • Kutoa nakala na kusambaza. [26]
  • Kuuza na kununua. [27]
  • Kusoma, kufundisha na kujifunza. [28]
  • Kufanya wakfu mali kwa ajili ya kueneza na kusambaza vitabu vya upotofu. [29]
  • Kuacha wasia kwa ajili ya kutumika mali kwa ajili ya kazi hii. [30]
  • Kuchukua ujira kwa ajili ya kutengeneza jalada na makaratasi ya vitabu hivi. [31]

Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihi, hakuna tatizo kusoma vitabu hivi kwa mtu ambaye ni msomi na mwenye elimu na lengo likiwa ni kwa ajili ya kuthibitisha haki na kupinga na kukosoa batili. [32] Kadhalika kwa mujibu wa fat’wa ya Ayatullah Wahid Khorasani kukunua na kuuza vitabu vya upotofu kutakuwa ni haramu kama kuna uwezekano wa kuleta upotofu. [33]

Fat’wa tofauti

Ayatullah Montazeri anaamini kwamba, leo hii, kutokana na maendeleo ya zana za uchapishaji na usambazajii, kuharibu na kuteketeza kitabu sio tu kwamba hakupelekei kipotee, bali pia kunaongeza shauku na hamu ya watu kuelekea kitabu hicho. Pia, kuhifadhi na kuchapisha vitabu vya upotofu kutokana na ukweli kwamba vina imani potofu na udanganyifu kunabatilisha yaliyomo ndani ya vitabu hivi. Kwa hiyo, si haramu kuvihifadhi (kuvimiliki) na wala si wajibu kuviangamiza. [34]

Hoja za kifiq’h

Mafaqihi wakiwa na nia ya kunyambua na kutoa hukumu zinazohusiana na vitabu vya upotofu wametumia Adilat al-Ar’baa (Hoja nne): Aya za Qur’an ikiwemo Aya ya 6 katika Surat Luqman [35] na Aya ya 30 ya Surat al-Hajj, [36] hadithi kama iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) katika kitabu cha Tuhaf al-Uqul, [37] [38], Ijma'a (makubaliano na maafikiano ya Maulamaa) na Adilat al-Aqli (hoja za kiakili) kama kung’oa mizizi ya ufisadi [40] na kuzuia madhara tarajiwa. [41]

Miongoni mwa mafakihi, Yusuf Bahrani (1107-1186 Hijiria) ametilia shaka hukumu ya kuharamisha kuhifadhi na kuwa na vitabu vya upotofu na wajibu wa kuviangamiza. Yeye anaamini kwamba, hakuna hoja ya kisheria ya jambo hili. [42[

Vitabu vya upotofu katika sheria ya Iran

Katika sheria za Iran ibara ya "Kutub Dhal" (Vitabu vya Upotofu) ilitumika kwa mara ya kwanza mwaka 1285 Hijiria Shamsia na katika kipengele kamilifu cha Katiba ya Mashrooteh. [43] Hili limekuja katika kipengele kikuu cha 20 cha sheria kuhusiana na uhuru wa magazeti na majarida: Magazeti yote isipokuwa vitabu vya upotofu na mada zinazodhuru dini, yako huru na vingine ni marufuku. [44] Aidha imekuja katika kipengele kikuu cha 20 cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila kutaja anuani ya "vitabu vya upotofu" ya kwamba: "Majarida na magazeti yapo huru katika kubainisha na kueleza mambo mbalimbali, isipokuwa kama yatatia dosari misingi ya Uislamu na haki za watu". [45]

Vitabu vya upotofu na uhuru wa kutoa maoni

Baadhi ya hukumu zinazohusiana na vitabu vya upotofu vimetambuliwa kuwa vinakinzana na uhuru wa kusema (kutoa maoni), fikra na uhakiki. [46] Ukosoaji huu umejibiwa namna hii kwamba; dini ya Uislamu, imewashajiisha watu kutafuta elimu na kufanya uhakiki na haijapinga kuwa na fikra huru na uhuru wa kusema na kutoa maoni, lakini imezingatia pia suala la uzima wa kifikra na kiitikadi wa jamii na ukiwa na lengo la kuzuia upotoshaji wa kiitikadi na kimaadili katika jamii, umeainisha mipaka ya uhuru, kujieleza na kutoa maoni. [47]