Nenda kwa yaliyomo

Vita vya Bani Mustaliq

Kutoka wikishia
Vita vya Bani Mustaliq
Makala hii inahusiana na Vita vya Bani Mustaliq. Ili kujua kuhusiana na kabila lenye jina hili, angalia makala ya Kabila la Bani Mustaliq.

Vita vya Bani Mustaliq au Vita vya Muraysi ni miongoni mwa vita ambavyo Bwana Mtume (s.a.w.w) alishiriki kwa ajili ya kukabiliana na kabila la Bani Mustaliq. Vita hivi vilitokea mwaka wa 5 au 6 Hijria. Katika vita hivi Abu Dhar al-Ghiffari alikuwa mrithi wa Mtume mjini Madina baada ya Mtume kwenda vitani na idadi kadhaa ya Munafiqin pia waliandamana na jeshi la Uislamu kwa lengo la kupata ngawira za vita.

Awali Mtume (s.a.w.w) alilingania Uislamu kabila la Bani Mustaliq, lakini baada ya kukataa kuukubali Uislamu na kurusha mishale dhidi ya Waislamu, alitoa amri ya kushambulia.

Kwa mujibu wa vyanzo vya historia, baada ya adui kushindwa, Waislamu walikuwachukua mateka watu 200 na kuchukua ghanima ngamia 2000 na kondoo 5000. Mateka na ghanima ziligawanywa baina ya Waislamu na Mtume aliainisha fidia kama sharti la kuachiwa huru mateka.

Juwairiyah binti wa Harith, kiongozi wa kabila la Bani Mustaliq pia alichukuliwa mateka katika vita hivi ambapo Mtume alitoa fidia na kumuachilia huru. Baada ya kuachiliwa huru Juwairiyah alisilimu na kisha akaolewa na Bwana Mtume (s.a.w.w).

Kwa mujibu wa ripoti za baadhi ya vitabu vya tafsiri, Aya ya 1-8 za Surat Munafiqun zilishuka zikibainisha vitendo na nyendo za Munafiqun hususan Abdallah bin Ubayy wakati wa vita hivi. Kadhalika inaelezwa kwamba, tukio la Ifk (uzushi na uwongo) lilitokea baada ya vita hivi.

Sababu ya Kutokea Vita

Vita vya Bani Mustaliq[1] au Vita vya Muraysi[2] ni miongoni mwa vita ambavyo Mtume (s.a.w.w) alishiriki. Kwa mujibu wa vyanzo vya historia, vita hivi vilitokea mwaka wa 5[3] au wa 6 Hijria[4]. Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti za kihistoria, habari ilimfikia Mtume ya kwamba, Harith bin Abi Dhirar, kiongozi wa kabila la Bani Mustaliq amekusanya kaumu inayonasibishwa na kabila la Khuza'a, kaumu yake na kundi kutoka kaumu za Waarabu na amejiandaa kwa ajili ya kupigana vita na Waislamu.[5] Kabila la Bani Mustaliq lilikuwa na uhusiano wa karibu na Kuraishi na likiwa na nia ya kulinda maslahi yake ya kibiashara, lilikataa kuingia katika Uislamu na Mtume (s.a.w.w) kutokana na sababu mbalimbali aliamua kuamiliana nalo kwa kulifumbia macho.[6]

Ili kupata uhakika kwamba, Bani Mustaliq wameandaa jeshi kwa ajili ya kupigana vita na Waislamu, Mtume (s.a.w.w) alimtuma Buraidah bin Husayb ili kuhakikisha ukweli wa taarifa hiyo. Baada ya kuwa na uhakika juu ya taarifa ya kujiandaa maadui kwa ajili ya kupigana na Waislamu, alitoa amri ya kutumwa jeshi kuelekea eneo la kabila la Bani Mustaliq.[7] Waqidi ameandika, wakati wa kuanza safari ya kwenda vitani, kundi la munafiqun[8] kutokana na kuwa karibu na eneo la vita na likiwa na lengo la kupata ghanima za vita, liliungana na jeshi la Waislamu.[9] Andalusi anasema, wakati Mtume anaondoka kuelekea vitani alimteua Abu Dhar al-Ghiffari na kumfanya kuwa mrithi wake mjini Madina;[10] hata hivyo baadhi ya wanahistoria wametawaja watu kama Namilah bin Abdallah al-Laythi[11] na Zayd bin Haritha kuwa, warithi wa Mtume mjini Madina alipoondoka kwa ajili ya kwenda kupigana vita na Bani Mustaliq.[12]

Hatima ya Vita

Kwa mujibu wa Salehi Dimashqi, mmoja wa wanahistoria wa karne ya 10 Hijria, ni kwamba, wakati Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akielekea kwa Bani Mustaliq, mmoja wa majasusi wa Harith alikamatwa na Waislamu; lakini alikataa kutoa habari kwa Mtume (s.a.w.w). Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w) alimtaka asilimu; lakini pia alikataa kuukubali Uislamu. Kwa sababu hii, aliuawa kwa amri ya Mtume (s.a.w.w).[13] Kuuawa kwa jasusi huyo kulizua hofu kwa Harith na masahaba wake na kutawanyika kwa makabila mengine pamoja na jeshi la Harith. Matokeo yake, hakuna aliyebaki kwenye uwanja wa vita isipokuwa Harith na wasaidizi wake.[14] Kwa mujibu wa vyanzo, Mtume (s.a.w.w) alipofika eneo la Muraysi, aliwapanga masahaba zake. Alimpa Ammar bin Yasir bendera ya Muhajirina na kwa mujibu wa kauli nyingine ni kuwa alimpa bendera hiyo Abu Bakr, na akamkabidhi Saad bin Ubada bendera ya Ansari na akajiandaa kwa vita.[15]

Awali Mtume (s.a.w.w) alilingania Uislamu kabila la Bani Mustaliq, lakini baada ya kukataa kuukubali Uislamu na kurusha mishale dhidi ya Waislamu, alitoa amri ya kushambulia.[16] Waislamu wakipiga nara «Ya Mansur Amit» (Ewe mshindi ua) walishambulia maadui.[17]

Katika vita hivi, masahaba 10 wa Harith waliuawa na waliobakia wakachukuliwa mateka[18] na baadhi walikimbia.[19] Aidha ngawira nyingi ziliangukia mikononi mwa jeshi la Uislamu.[20] Tabari mwanahistoria anaandika, Hashim bin Dhabab wakati anarejea katika jukumu la kufuatilia maadui aliuawa kimakosa na mmoja wa Waislamu[21] ambapo Mtume alitoa amri ya kulipwa dia ya damu yake.[22]

Kugawanya Ngawira

Kwa mujibu wa Waqidi katika kitabu cha Al-Maghazi, baada ya kumalizika kwa vita, Mtume (s.a.w.w) alimpa jukumu Buraidah bin Husayb la kuwalinda mateka na akamuamuru kuwafanyia wema upole mateka hao.[23] Kadhalika ngawira zote kuanzia mali, silaha na wanyama zilikusanywa sehemu moja na kwa amri Mtume, mtumishi wake Shaqran alipewa jukumu la kutunza ngawira hizo.[24] Aidha alichaguliwa Mahmiyyah bin Juz'i kwa ajili ya kufanya kazi ya kuainisha khumsi na hisa za Waislamu.[25]

Kulingana na vyanzo vya kihistoria, mateka 200, ngamia 2000 na kondoo 5000 walichukuliwa kama ngawira katika vita ya Bani Mustaliq.[26] Baadhi ya vitabu vimenukuu kwamba, awali Mtume alitenganisha Khumsi ya ngawira na kisha akagawa mali na mifugo kati ya Waislamu.[27]

Wakati wa kugawanya mali, kila ngamia mmoja alijaaliwa kuwa sawa na kondoo 10, na kila farasi mmoja alijaaliwa hisa mbili, hisa moja kwa ajili ya mwenye farasi na hisa nyingine kwa ajili ya askari watembeao kwa miguu.[28] Vyanzo mbalimbali vimeandika kwamba, Mtume akiwa na lengo la kuwahifadhi mateka, aliwagawanya baina ya Waislamu na akaainisha kiwango na fidia inayopaswa kulipwa kwa ajili ya kukombolewa na kuachiliwa huru mateka hao. Inaelezwa kuwa, fidia ya kila mwanamke na kila mtoto ilikuwa ni kutoa ngamia sita. Watu kutoka Bani Mustaliq walikuwa wakija Madina na kuwakomboa mateka ndugu na jamaa zao kwa kulipa fidia. Kulingana na ripoti, baadhi waliachiliwa huru bila hata kulipa fidia.[29]

Mtume Amuoa Juwairiyah

Wakati wa ugawaji wa mateka, utunzaji wa Juwairiyah, binti ya Harith bin Abi Dhirar (mkuu wa kabila la Khuza'a), ulikabidhiwa kwa Thabit bin Qays.[30] Kwa mujibu wa Tarikh Tabari, Thabit bin Qays alikubaliana na Juwairiya kwamba, endapo atatoa kiwango fulani cha dhahabu basi atamuachilia huru.[31] Kwa ajili ya uhuru wake, Juwayriyah alikwenda kwa Mtume (s.a.w.w) na baada ya kutoa shahada mbili (kusilimu na kuingia katika Uislamu) alimwomba Mtume amlipie fidia ya kuachiliwa kwake huru. Mtume (s.a.w.w) alilipa gharama yake kisha akamuoa.[32] Kuenea kwa habari hii miongoni mwa watu kuliwafanya Waislamu kuwatoa mateka wote kutoka kwa Bani Mustaliq na kuwaachilia huru kwa sababu ya undugu wao sasa na Mtume (s.a.w.w).[33] Katika baadhi ya ripoti pia imesemwa kwamba sharti la ndoa ya Juwayriyah lilikuwa ni kuachiliwa mateka wote au mateka 100 au mateka 40 wa watu wake.[34]

Kushuka Aya za Mwanzoni mwa Surat al-Munafiqun

Ali bin Ibrahim Qumi ameleta katika tafsiri yake kwamba, katika vita hivi, kulitokea ugomvi baina ya masahaba wawili juu ya kuvuta maji kutoka kisimami na kupelekea kujeruhiwa mmoja wa Ansari. Abdallah bin Ubayy, baada ya kusikia habari hii alikasirika sana na kutishia kwamba, atakaporejea Madina atawatimua kutoka katika mji huo «Watu Haqir» (dhalili).[35] Zayd bin Arqam ambaye alishuhudia tukio hili, alikwenda na kumueleza Mtume kuhusiana na maneno na vitisho hivyo vya Abdallah bin Ubayy; hata hivyo Bin Ubayy alikwenda kwa Mtume na kutoa shahada mbili na kukanusha maneno ya Zayd. Baada ya muda, Aya ya 1-8 za Surat al-Munafiqun zikashuka.[36] Allama Tabatabai ameandika katika tafsiri yake ya al-Mizan kwamba, makusudio ya Abdallah bin Ubayy aliposema "Watu Haqir" (dhalili) yalikuwa ni Mtume (s.a.w.w) na kwa maneno yake haya alikusudia kutoa vitisho dhidi ya Mtume.[37]

Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, tukio la Ifk pia lilitokea baada ya kurejea katika safari hii.[38]

Rejea

Vyanzo