Nenda kwa yaliyomo

Tukio la Ifk

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na tukio la Ifk (uzushi na tuhuma). Ili kujua kuhusiana na tukio la Ifk katika Qur'ani angalia Aya za Ifk.

Tukio la Ifk (Kiarabu: حادثة الإفك) ni mkasa wa tuhuma za mambo machafu na maovu zilizotolewa na kundi fulani la watu dhidi ya mmoja wa wake za Mtume (s.a.w.w) mwanzoni mwa Uislamu. Wahakiki wamelitambulisha tukio hili kuwa njama ya kimsingi zaidi ndani ya wanafiki dhidi ya utawala wa Mtume (s.a.w.w); kwani wahusika walitaka kupitia kitendo chao hiki watie dosari na kubomoa shakhsia ya Mtume na hivyo kutilia shaka ustahiki wa kuwa kwake kiongozi; hata hivyo Mwenyezi Mungu kwa kushusha Aya za Ifk (tuhuma) akasambaratisha njama hii ya maadui.

Katika vyanzo kuna ripoti mbili kuu kuhusiana na mtu aliyetuhumiwa: Kwa mujibu wa vyanzo vya Waislamu wa Ahlu-Sunna na vilevile baadhi ya vyanzo vya Waislamu wa madhehebu ya Shia ni kuwa, Aya za Ifk zilishuka baada ya wanafiki kumtuhumu Bibi Aisha, mke wa Mtume (s.a.w.w). Kwa mujibu wa ripoti hii, Bibi Aisha alikuwa pamoja na Mtume (s.a.w.w) katika vita vya Bani Mustaliq na akawa ameachwa na jeshi la Waislamu na kwa kusaidiwa na Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Safwan bin Muattal akawa amefanikiwa kuungana na jeshi. Wanafiki kama Abdullah ibn Ubayy na Hassan bin Thabit walimtuhumu Aisha na Safwan kwamba, wana mahusiano haramu. Baada ya muda zikashuka Aya za Ifk na kuwalaumu vikali Waislamu kutokana na kueneza uzushi.

Ripoti ya kutuhumiwa Aisha mbali na kuwa jambo lisilo na shaka kwa Waislamu wa madhehebu ya Sunni, ni mashuhuri pia kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na baadhi ya Mashia kama Sheikh Mufid na Sheikh Tusi wamekikubali kisa hicho kwamba, ndio sababu ya kushushwa Aya; hata hivyo kundi la wahakiki wa Kishia linaamini kwamba, ripoti hii ina walakini mwingi kwa upande wa Sanadi, matini na mapokezi; kama vile kukinzana kwake dhana mbaya ya Mtume kwa Aisha na suala Isma (Umaasumu) ya Mtume, kuomba ushauri Mtume kutoka kwa mtoto katika jambo muhimu na kutochukuliwa wake za Mtume katika vita vingine. Kwa msingi huo haiwezekani kutegemewa na kufanywa hoja.

Ripoti ya pili imenukuliwa katika moja ya vyanzo vya Mashia yaani Tafsiri Qummi na ndani yake kumeelezwa kuwa, tuhuma ya Aisha kwa Maria al-Qibtiyya imetambulishwa kuwa sababu ya kushuka Aya. Kwa mujibu wa ripoti ya Ali ibn Ibrahim Qummi, wakati Ibrahim mtoto wa Mtume (s.a.w.w) alipoaga dunia, Aisha alimtuhumu Mariya na kusema kuwa, Ibrahim sio mtoto wa Mtume bali ni mtoto wa Bwana mmoja anayejulikana kwa jina la Jurayh. Kutokana na maneno hayo ya Aisha, Mtume (s.a.w.w) alimpa jukumu Imamu Ali (a.s) la kumu Jurayh. Wakati Imamu Ali alipokutana ana kwa ana na Jurayh akafahamu juu ya kuwa uwongo tetesi hiyo na wakati huo Mwenyezi Mungu akashusha Aya za Ifk (tuhuma) kwa Mtume (s.a.w.w). Ripoti hhii pia imekabiliwa na walakini; kama vile kutoafikiana na Aya za Qur'an agizo la Mtyume kwa Aali la kuuawa mtuhumiwa bila ya uchunguzi na kutotekelezwa adhabu ya tuhuma ya zinaa au liwati (had Qadhf) kwa waliotoa tuhuma.

Baadhi ya wanazuoni wa Kishia, kama vile Muhammad Hussein Tabatabai, Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah, Makarem Shirazi na Jafar Sobhani, hawajakubali mojawapo ya ripoti ripoti yoyote kati ya ripoti hizo mbili kutokana na walakaini na matatizo yaliyoko ndani ya ripoti hizo. Tabatabai ameunga mkono tu kwamba, kwa mujibu wa Aya za Ifk, mtu aliyesingiziwa alikuwa maarufu na mtu wa familia ya Mtume (s.a.w.w).

Kuna ripoti nyingine tofauti tofauti, katika vyanzo vya Shia na Sunni, ambazo zinaunga mkono tuhuma ya Aisha kwa Maria al-Qibtiyya; lakini hakuna hata ripoti moja kati ya hizo inayotaja kuteremshwa kwa Aya za Ifk. Miongoni mwa wanazuoni wa Kishia, ni wanachuoni wa zama za hivi karibuni tu, kama vile Sayyid Abul-Qassim Khui na Sayyid Murtadha Askary, ambao wameitambua Aya ya Ifk kuwa inahusiana na tukio na mkasa wa kutuhumiwa Maria al-Qibtiyya.

Imesemekana kuwa, utafiti wa Tukio la Ifk ni moja ya mada ngumu sana katika historia ya Uislamu, ambayo ina mfungamano na mada za kitafsiri, kiteolojia, kifiqhi na kiutambuzi wa wapokezi wa hadithi, na mielekeo ya kisiasa na kimadhhebu imeifanya mada hii kuwa ngumu na tata zaidi. Kuhusiana na tukio la Ifk, kumeandikwa vitabu kama vile Hadith al-Ifk kilichoandikwa na Sayyid Jafar Murtadha al-Amili na Hadith al-Ifk Man al-Mandhur al-I'lami, kilichoandikwa na na Ali Mahmoud Rashwan.

Umuhimu wa tukio la Ifk katika historia ya Uislamu

Ifk (kwa maana ya uwongo [1] na tuhuma [2] inaashiria tukio lililotokea katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) ambapo mmoja wa wake za Mtume (s.a.w.w) alituhumiwa kwa jambo chafu na kufuatia hilo Mwenyezi Mungu akashusha Aya za Ifk (Aya ya 11-16 za Surat al-Nur). [3] Inaelezwa kuwa, watoa tuhuma walikusudia kupitia kitendo chao hiki watie dosari na kuchafua haiba na shakhsia ya Bwana Mtume (s.a.w.w); hata hivyo, Mwenyezi Mungu kwa kushusha Aya na kuwalaumu waeneza uzusha akawa ameweka wazi ukweli na uhakika na hivyo kusambaratisha njama hiyo ya maadui. [4]. Baadhi ya wahakiki wamelitambulisha tukio hili kuwa njama ya kimsingi zaidi ya ndani ya wanafiki dhidi ya utawala wa Mtume (s.a.w.w); [5] kwani wahusika walitaka kupitia kitendo chao hiki watie dosari na kubomoa shakhsia ya Mtume na hivyo kutilia shaka ustahiki wa kuwa kiongozi; [6] na hivyo kumfanya Mtume atengwe. [7] Baadhi wanasema kuwa, kufanyia utafiti Tukio la Ifk ni moja ya mada ngumu sana katika historia ya Uislamu, ambayo ina mfungaano na mada za kitafsiri, kiteolojia, kifiqhi na kiutambuzi wa wapokezi wa hadithi, na mielekeo ya kisiasa na kimadhhebu imeifanya mada hii kuwa ngumu na tata zaidi. [8]

Aya za Ifk

Makala asili: Aya za Ifk

Katika Aya za 11 hadi 16 za Surat al-Nur, kumebainishwa tuhuma ya uchafu ya mmoja wa Waislamu na Mwenyezi Mungu anawalaumu watoa tuhuma kutokana na tuhuma hii. [9] Kwa mujibu wa Muhammad Hussein Tabatabai, mwandishi wa tafsiri ya al-Mizan ni kuwa, kupitia Aya za Qur'an inaeleweka kwamba, mtu aliyetuhumiwa ni mashuhuri na alikuwa ni katika familia ya Bwana Mtume (s.a.w.w) na watoa tuhuma lilikuwa kundi la watu. [10] Katika Aya hizi, Mwenyezi Mungu anawatishia kwa adhabu kubwa wato tuhuma na anawalaumu waumini kwa kuwaambia kwamba, kwa nini walikubalia uzushi huo bila ya hoja na bila ya kufanyia uchunguzi. [11]

Katika Aya hizi, Mwenyezi Mungu anawakemea vikali watu na kuwakataza wasiwatuhumu wanawake wanaojiheshimu na kuwa na wanawake wasafi na watakasifu amewatambua kuwa wako mbali na tuhyuma hizo. [12]

Ripoti tofauti kuhusu tukio la Ifk

Kuna tofauti za kimitazamo kuhusiana na mtu aliyetuhumiwa katika tukio la Ifk. [13] Katika baadhi ya ripoti za Shia, Maria al-Qibtiyya ametambulishwa kama mtuhumiwa; lakini katika hadithi za Sunni na vile vile katika ripoti nyingine za Shia, Aisha ametambulishwa kuwa ndiye mtutumiwa. [14] Kupitia maneno ya Ali ibn Ibrahim Qummi, mwandishi wa kitabu cha Tafsir al-Qummi [15] inafahamika kuwa, Mashia hawana tofauti za kimitazamo kuhusiana na kushuka Aya za Ifk kumhusu Maria al-Qibtiyya au kwa uchache kwa mtazamo wa Waislamu wa Kishia, kushuka Aya za Ifk (tuhuma na uzushi) kuhusiana na Maria al-Qibtiyya ni jambo mashuhuri zaidi; [16] lakini kwa mujibu wa baadhi ya wahakiki, kwa mtazamo wa Waislamu wa Kishia ni kuwa, kushuka Aya za Ifk kumhusu Maria al-Qibtiyya sio tu kwamba, hilo sio mashuhuri, bali kwa Maulamaa wa mwanzo kushuka Aya hizo kumhusu Aisha ndilo lililokuwa mashuhuri zaidi; [17] kama ambavyo Allama Hilli, mtaalamu wa sheria za Kiislamu na mwanateolojia wa Kishia wa karne ya 8 Hijria anasema kuwa, Aya za Ifk zilishuka kuhusiana na kutuhumiwa Bibi Aisha na akaonyesha kutokuwa na taarifa kuhusiana na kuweko tukio jingine kinyume na hilo. [18]


Ripoti ya Kwanza: Tuhuma dhidi ya Aisha

Kwa mujibu wa Mohammad Javad Mughniyeh, mmoja wa wafasiri wa Kishia katika karne ya 14 Hijria ni kuwa, wengi wa wafasiri na wanahistoria wanaamini kwamba, Aya za Ifk zinahusiana na tukio lililotokea wakati wa kurejea kwa Mtume (s.a.w.w) kutoka katika vita vya Bani Mustaliq (mwaka wa 5 [19] au wa 6 Hijiria [20]) [21] Kwa mujibu wa riwaya ya Aisha, Mtume, ambaye siku zote alifuatana na mmoja wa wake zake katika vita, alimchukua Aisha pamoja naye katika Vita vya Bani Mustaliq. [22] Njiani wakati wa kurudi kutoka katika vita hivi, wakati misafara iliposimama kupumzika, Aisha aliondoka kambini ili kukidhi haja, na kwa kuwa alipoteza mkufu wake, alitumia muda kuutafuta. [23] Askari, ambao hawakujua kuhusu kutokuwepo kwa Aisha, wakaondoka na kupeleka kiti cha mwavuli kilichofungwa katika mgongo wa ngamia au farasa wakidhani kwamba Aisha yupo humo. [24] Baada ya Aisha kurejea kambini, alikuta patupu na akakaa sehemu ile ile mpaka alipomfikia mtu aliyeitwa Safwan bin Mu’attal na kumchukua. Bwana yule alimpatia Aisha ngamia wake na kwenda naye mpaka walipolifikia jeshi na kuungana nalo. [25] Aisha, ambaye alikuwa mgonjwa baada ya kurejea kutoka safari hii, aliona mabadiliko ya tabia ya Mtume (s.a.w.w) na pia uvumi kuhusu uhusiano wake na Safwan. [26] Baada ya muda fulani, Aya za Qur'ani ziliteremshwa zikiwawakemea watoa tuhuma. [27]

Miongoni mwa wanachuoni wa Kishia waliolichukulia tukio la Ifk kuwa linahusiana na tuhuma dhidi ya Aisha, wapo watu hawa: Nasr bin Mozahim katika kitabu Waqa'ah Siffin, [28] Nu'mani katika tafsiri inayonasibishwa kwake, [29] Sheikh Mufid katika Al-Jamal, [30] Sheikh Tusi katika Al-Tibyan, [31] Tabarsi katika Ilam al-Wara, [32] Qutb al-Din Rawandi katika Fiqh al-Qur'an [33] na Muqaddas Ardabili katika Zubda al-Bayan.[34]


Watoa tuhuma walikuwa akina nani?

Katika Aya za Ifk, watoa tuhuma kimetajwa kuwa ni kikundi cha watu na hakujaashiriwa majina yao. [35] Hata hivyo, baadhi ya vyanzo vimetaja majina ya wanafiki kama vile Abdullah ibn Ubayy, Hassan ibn Thabit, na Mistah ibn Uthatha kama viongozi wa tukio la Ifk [36]


Kumuandalia fadhila Aisha

Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanalihesabu suala la kushuka Aya za Ifk kumhusu Aisha kuwa ni fadhila kubwa. [37] Ingawa riwaya hii imetajwa katika riwaya mbalimbali za Kisunni, kwa mujibu wa Sayyid Jafar Murtadha Amili, mwanahistoria wa Kishia, karibu riwaya hizi zote zilisimuliwa na kubainisha na Aisha mwenyewe. [38] Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba, Aisha aliibua baadhi ya mambo na hivyo akalishusha jambo hili na kulifanya kuwa la kibinafsi [39] na alijizingatia kuliko kawaida na akajiandalia na kujitengenezea fadhila. [40] Hili limewafanya Mashia kuwa na shaka juu ya usahihi wa kisa hiki. [41] Kwa kuzingatia hili, wamesema kwamba, hata kama Aya za Ifk ziliteremshwa kuhusu Aisha, hii inaashiria tu utakaso wake na haithibitishi uadilifu mwingine wowote kwake. [42]


Ripoti ya Pili: Tuhuma dhidi ya Maria al-Qibtiyya

Kulihusisha tukio la Maria al-Qibtiyya na kuteremshwa kwa Aya za Ifk kwa mara ya kwanza lilizungumziwa katika kitabu cha Tafsir Ali Ibn Ibrahim Qommi. [43] Kwa mujibu wa riwaya ambayo Ali Ibn Ibrahim Qommi aliipokea kutoka kwa Imam Baqir (a.s), Aisha alimtuhumu Maria al-Qibtiyya kwamba alikuwa na uhusiano haramu wa kimapenzi na Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Jurayh Qibti. [44] Kwa mujibu wa riwaya hii, wakati Mtume (s.a.w.w) alipokuwa na huzuni kutokana na kifo cha mwanawe Ibrahim, alikumbana na maneno haya ya Aisha kwamba: "Usihuzunike kuhusu kifo cha Ibrahim; kwa sababu alikuwa mtoto wa Jurayh". [45] Kwa hiyo, Mtume (s.a.w.w) alimtaka Imam Ali (a.s) akamuuwe Jurayh. [46] Jurayh, ambaye alifahamu nia ya Imam Ali, alikimbilia juu ya mti. [47] Na katika hali hiyo nguo zake zilipepeperuka na kumua uchi na Ali (a.s) akatambua kwamba hakuwa na uume. [48] Kwa njia hii, tuhuma dhidi ya Maria al-Qibtiya ya kuwa na mahusiano haramu na Bwana huyo ikaondolewa na Aya za Ifk zikateremka. [49]

Inaelezwa kwamba miongoni mwa wanazuoni wa Kishia, ni wanachuoni wa zama za hivi karibuni tu walioichukulia Aya ya Ifk kuwa inahusiana na kisa cha Maria. [50] Miongoni mwa wanavyuoni hao, tunaweza kumtaja Sayyid Abul Qasim Khui, [51] Sayyid Jafar Murtaza Amili [52] na Sayyid Murtaza Askary [53]. Sheikh Mufid ambaye ameandika risala inayojitegemea juu ya tukio la Maria al-Qibtiyya, iitwayo Risalah Hawla Khabar-e Mariah, anaichukulia kadhia na tukio hili kwamba, halina shaka na anaamini kwamba wanavyuoni wote wanaichukulia riwaya hii kuwa ya kuaminika; [54] lakini katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwake, hakujaashiriwa juu ya kuteremshwa Aya za Ifk; [55] kama ambavyo katika vyanzo mbalimbali, tukio la kutuhumiwa Maria limeripotiwa bila ya kuashiriwa kushuka Aya za Ifk; miongoni mwa vyanzo hivyo ni kitabu cha Amali cha Sayyid Murtadha, [56] Al-Hidayah Al-Kubra, [57] Dalail al-Imamah [58] na Al-Manaqib [59]. Wanachuoni wa Kisunni wamenukuu hadithi zinazohusiana na kisa cha tuhuma za wanafiki dhidi ya Aisha chini ya Aya za Ifk; lakini pamoja na hayo, tuhuma dhidi ya Maria pia imetajwa katika vyanzo vya Kisunni, baadhi yao ni: Sahih Muslim, [60] al-Tabaqat al-Kubra, [61] Ansab al-Ashraf, [62] Al-Mustadrak Ala al-Sahihain [63] na Safwat al-Safawa [64].

Uchunguzi wa mapungufu ya ripoti hizi mbili

Baadhi ya matatizo na mapungufu yametajwa kwa kila moja ya ripoti hizi mbili, na baadhi ya wafasiri kama vile Muhammad Hussein Tabatabai, [65] Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah, [66] Makarem Shirazi [67] na Jafar Sobhani kwa kuzingatia nakisi na mapungufu haya wamezikataa ripoti zote mbili. [68] Kwa kuzingatia kutokuwa sahihi ripoti zote mbili, imeelezwa kuwa, kuna uwezekano kwamba aya hiyo iliteremshwa kuhusu mtu wa tatu. [69] Kwa upande mwingine, baadhi ya watafiti wanaamini kwamba, kuna uwezekano kwamba matukio yote mawili ni sahihi; kwa maelezo kwamba Aya za Ifk ziliteremshwa kwa ajili ya tukio la Aisha, lakini hakuna Aya iliyoteremshwa kwa ajili ya tukio la Maria. [70]

Monografia

Waislamu wa Kisunni na Kishia wameandika vitabu mbalimbali kuhusiana na tukio la Ifk. Miongoni mwavyo ni:

  • Hadith al-Ifk, mwandishi wa kitabu hiki ni Sayyid Ja’far Murtadha al-Amili. Katika kitabu hiki mwandishi anachambua matukio mawili yanayohusishwa na tuhuma dhidi ya Bibi Aisha na Maria al-Qibtiyya. [89] Mwandishi ameandika katika kitabu hiki kwamba, tukio la tuhuma dhidi ya Aisha siyo sahihi na kwamba, hadithi zinazohusiana na tukio la tuhuma dhidi ya Maria ndio sahihi. [90]
  • Hadith al-Ifk Man al-Mandhur al-I'lami, kilichoandikwa na na Ali Mahmoud Rashwan: Mwandishi wa kitabu hiki ni Msuni. Yeye amekubaliana na tukio la tuhuma dhidi ya Aisha na hakuashiria tukio la tuhuma dhidi ya Maria al-Qibtiyya. [93].

Vyanzo

  • Qurʾān, 24:20-26.
  • ʿĀmilī, Jaʿfar Murtaḍā al-. Al-Ṣaḥīḥ min sīrat al-Nabīyy al-aʿẓam. Qom: Dār al-Ḥadīth, 1426 AH.
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. ʿUmar. Mafātīḥ al-ghayb (al-Tafsīr al-kabīr). Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, n.d.
  • Ḥusaynīyān Muqaddam, Ḥusayn. 1384 Sh. "Barrasī-yi tārīkhī tafsīrī-yi ḥāditha-yi Ifk". Tārīkh-i Islām Dar Āyina-yi Pazhūhish 7: (159-190).
  • Ibn Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Muḥammad. Usd al-ghāba fī maʿrifat al-Ṣaḥāba. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, n.d.
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik. Sīrat al-nabawīyya. Edited by Muṣṭafā al-Saqā & Ibrāhīm al-Abyārī & ʿAbd al-Ḥafīẓ Shalabī. Beirut: Dār al-Maʿrifa, n.d.
  • Makārim Shīrāzī, Nāsir. Al-Amthāl fī tafsīr-i kitāb Allāh al-munzal. Qom: Madrisat Imām ʿAlī b. Ibī Ṭālib, 1421 AH.
  • Qummi, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Qom: Dār al-Kitāb, 1367 Sh.
  • Qurashī Banāyī, ʿAlī Akbar. Qāmūs al-Qurʾān. Fourteenth edition. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1384 Sh.
  • Subḥānī, Jaʿfar. Furūgh-i abadīyyat. Qom: Būstān-i Kitāb, 1384 Sh.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad Abu l-Faḍl Ibrāhīm. Second edition. Beirut: Dār al-Turāth, 1387 AH.
  • Ṭabāṭabāyī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʿān. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī-yi Jamiʿa-yi Mudarrisīn, 1417 AH.
  • Wāqidī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Al-Maghāzī. Edited by Marsden Jones. Qom: Markaz Nashr Maktab al-Aʿlām al-Islāmī, 1414 AH.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Beirut: Dār al-Ṣādir, n.d.
  • Yūsufī Gharawī, Muḥammad Ḥadī. Mawsūʿat al-tārīkh al-Islāmī. Qom: Majmaʿ al-Fikr al-Islāmī, 1423 AH.