Tuhuma

Kutoka wikishia

Tuhuma ni kunasibishwa mambo yasiyofaa kwa mtu au watu wengine kwa kutumia dhana tu. Chimbuko la tuhuma ni kuwa na dhana mbaya kwa vitendo vya watu wengine. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu ni haramu kutoa tuhuma (kutuhumu) na kitendo hicho kinahesabiwa kuwa ni katika madhambi makubwa. Adhabu ya aliyefanya kosa hilo ni taazir (makosa ambayo dini ya Uislamu haijabainisha adhabu yake na mtawala wa Kiislamu ndiye mwenye jukumu la kuainisha adhabu hizo). Katika Qur’ani watoa tuhuma wameahidiwa adhabu. Tofauti ya tuhuma na uwongo na uzushi ni kwamba, mtoa tuhuma hana yakini juu ya kuweko aibu na mapungufu ya anayemtuhumu. Lakini anayezua na kuzusha juu ya mtu fulani ana yakini kabisa juu ya kuwa uwongo yale ayasemayo dhidi ya mtu fulani. Katika hadithi na riwaya mbalimbali katika Uislamu, watu wamekatazwa kuweko katika maeneo ambayo hupelekea kuibuka dhana mbaya dhidi yao na ambayo husababisha watu hao kuwa na uwezekano wa kuwatuhumu watu wengine. Moja ya matokeo ya kutoa tuhuma ni kuondoka imani ya mtu na njia ya kutibu maradhi hayo ni kutochunguza mambo ya watu.

Utambuzi wa maana na nafasi ya tuhuma

Kutoa tuhuma kunahesabiwa kuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa. [1] Katika hadithi, kutoa tuhuma au kuwatuhumu wengine kunatambuliwa kuwa jambo baya kwa namna ambayo hata shetani anachukia kufanya jambo hilo. [2] Katika vyanzo vya hadithi kumetengwa sehemu maalumu ya kubainisha uharamu wa jambo hili. [3] Tuhuma maana yake ni kubainisha dhana mbaya [4] na dhana mbaya ni jambo ambalo lililoingia katika moyo wa mwanadamu kuhusiana na muamala, kitendo na hali ya mtu mwingine. [5] Hata hivyo, madhali ufahamu mbaya na dhana mbaya haijadhihiri bayana, huhesabiwa kuwa ni dhana mbaya tu na sio tuhuma. [6] Tuhuma (hasa katika zama hizi) inajumuisha mambo kama kumtuhumu mtu kwa maandishi, ishara na kwa suhula na vyombo kama simu, kompyuta na mitandao ya kijamii. [7] Katika hadithi kigezo na kielelezo kibaya kabisa cha tuhuma kimetajwa kuwa ni kufanya khiyana katika amana. Kwa maana kwamba, kutoa tuhuma dhidi ya mtu ambaye ni muaminifu katika mambo yake. [8]

Tofauti yake na uwongo na uzushi

Tuhuma, uwongo na uzushi kimaana ni maneno ambayo yanashabihiana na katika ada na mazoea, maneno haya kila moja wakati mwingine hutumika sehemu ya jingine; pamoja na hayo maneno haya yanatofautiana. Tuhuma ni wenzo wa dhana mbaya ambapo chimbuko lake ni dhana mbaya; [9] hata hivyo dhana hii ima haina ukweli na uhalisia au ukweli wake bado haujathibiti. [10] Lakini uwongo ni kunasibisha mambo fulani ya uwongo [11] dhidi ya mtu au watu wengine ambapo anayefanya kitendo hiki mwenyewe ana yakini kabisa juu ya kuwa uwongo na kuitokuwa kweli hayo ayasemayo kuhusu mtu fulani. Kadhalika uongo yamkini ukaambatana na kutoa hoja na dalili kutoka kwa mzushi [12] lakini uzushi ni uwongo wa wazi kabisa [13] ambao hauna hoja wala dalili [14] kama kusema kwamba, Mwenyezi Mungu ana mtoto. [15]

Hukumu za kisheria kuhusu tuhuma

• Kutoa tuhuma na kuzieneza kwa mtazamo wa mafakihi ni haramu [16] na adhabu yake ni taazir (makosa ambayo dini ya Uislamu haijabainisha adhabu yake na mtawala wa Kiislamu ndiye mwenye jukumu la kuainisha adhabu hizo). [17] Lakini kama tuhuma itolewayo itakuwa ni mtu kumtuhumu mwenzake kwa tuhuma ya zinaa au liwati, adhabu yake ni viboko 80. [18]

• Katika suala la kuwa haramu tuhuma au kutoa tuhuma, hakuna tofauti baina ya kutoa tuhuma mbele ya mhusika mwenyewe au kutokuweko kwake. [19]

• Kama tuhuma zitatolewa mbele ya mhusika mwenyewe basi kitendo hicho kitakuwa ni kielelezo na mfano wa kuvunjia heshima na jambo hilo ni haramu. [20]

• Haifai kusikiliza tuhuma dhidi ya watu wengine na kama mtu atasikia basi anapaswa kumtetea mtuhumiwa. [21]

• Mtoa tuhuma anapaswa kutubia dhambi yake na kwa mujibu wa tahadhari ya sunna aombe msamaha kutoka kwa aliyemtuhumu ikiwa kufanya hivyo hakutakuwa na matokeo mabaya.

Athari na matokeo yake

• Adhabu ya Mwenyezi Mungu: Katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Swadiq (as) ni kwamba, Aya ya 23 ya Surat Nur imetambuliwa kuwa hoja ya kwamba, kutoa tuhuma na kumsingizia mtu ni katika madhambi makubwa. [23] Katika Aya hii Mwenyezi Mungu ameambatanisha laana duniani na akhera pamoja na adhabu kubwa hususan wale ambao wanawasingizia wanawake wanaojiheshimu na wakawaharibia heshima zao kwa kuwatuhumu kwamba, wamefanya zinaa. Kadhalika Aya za Ifk (uwongo na uzushi) wanaotoa tuhuma dhidi ya mmoja wa watu wa familia ya Bwana Mtume (s.a.w.w) [24] wametishiwa adhabu kubwa. [25]

• Tuhuma hupelekea kuondoka imani ya muumini. [26]

• Tuhuma huwa sababu ya kuondoka kabisa heshima ya udugu na mahusiano ya kibinadamu baina ya watu katika jamii na kuandaa mazingira kuibuka hali ya kutoaminiana na uoga baina ya wana jamii. [27]

Njia za kuzuia na kutibu

• Kutoingiliana na watu wenye kufanya mambo mabaya. [28]

• Kutohudhuria vikao vya watu wenye matendo mabaya. [29]

• Kutokaa kando ya sehemu ambayo kuna jambo baya linafanyika na vilevile kujiepusha kukaa sehemu na mahali ambapo pananasibishwa na watu wafanyao matendo mabaya.

• Kutofanya ujasusi (kutochunguza chunguza mambo ya watu) katika mambo ya watu na kuyachukulia kwa njia bora kabisa maneno ya pande mbili ambayo yanasemwa (tuhuma zinazotolewa) pamoja na vitendo vya watu vinavyonasibishwa kwao. [31]

Hadith al-Mubahitah

Makala ya asili: Hadith al-Mubahitah

Mubahitah ni istilahi ya kifikihi ambayo imechukuliwa kutoka katika ibara ya ‘Bahituhum’ katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) [32] [33]. Kwa mtazamo wa wa elimu ya fiq’h ni kwamba, baadhi wametambua maana yake kuwa ni kutoa tuhuma na wakitegemea hilo, wametoa hukumu ya kujuzisha na kuidhinisha kuwatuhumu watu wa bidaa; [34] lakini baadhi wameona hilo kama maana yake ni hoja madhubuti na ya kustaajabisha [35] na matokeo yake wanasema kuwa, haijuzu kuwatuhumu watu wa bidaa. (uzushi katika dini). [36]