Tatbir
Tatbir (Kiarabu: التطبير) ni katika ada za maombolezo kwa baadhi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika maombolezo ya Imamu Hussein (a.s) ambapo ndani yake hutumia kujipiga miili yao kwa panga na jambia na kupelekea kuchirizika damu. Kitendo hiki ni ada potofu na ambayo inapelekea kuchafua jina la madhehebu ya Shia. Tatbir (kujipiga na kujikata) wakati wa maombolezo ya Imamu Hussein ilienea takribani katika karne ya 10 Hijria na hii leo ada hii inafanyika katika mataifa mbaliimbalii yakiwemo ya Iraq, Lebanon, India na wakati mwingine Iran. Wanaoafiki ada hii wanasema kuwa, ni katika shaari za Ashura na wanalitambua jambo hili kwamba, linaimariisha madhehebu hii. Mkabala na wao, akthari ya Maulamaa wa Kishia, wanasema kuwa, kujipiga na kujikata na kupelekea damu kuchirizika wakati wa maombolezo ya Imamu Hussein ni kitendo ambacho kinachafua sura ya Ushia na kwa mujibu wa sheria za Kiislamu ni haramu kujidhuru mwili.
Wanazuoni wa Kishia wametoa nadharia kadhaa kuhusiana na kujuzu (kuruhusiwa), kuwa mustahabu au kuharamishwa tatbir (kujikata) kwa mujibu wa mazingira ya zama na kudhuru mwili. Mafakihi kama Muhammad Hussein Naini wanaona kuwa, tatbir inajuzu kwa sharti kwamba, isiwe na madhara kwa mwili na kuchungwe baadhi ya masharti. Mkabala na mtazamo huo kuna Maulamaa wengine kama Sayyid Abul-Hassan Isfahani na Imamu Khomeini wao wameharamisha tatbir. Sayyid Muhsin Amini kwa mara ya kwanza alieneza andiko la kukosoa tatbir na Sayyid Ali Khamenei Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 1373 Hijria Shamsia alitoa hotuba dhidi ya tatbir.
Utambuzi wa Maana
Tatbir ni katika ada za maombolezo kwa baadhi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika maombolezo ya Imamu Hussein (a.s) ambapo ndani yake hutumia kujipiga miili yao kwa panga na jambia na kupelekea kuchirizika damu. [1] Kitendo hiki ni ada potofu na ambayo inapelekea kuchafua jina la madhehebu ya Shia. Wakati wa kufanya maombolezo haya, watu husikika wakitoa sauti kubwa «Haidar Haidar». Aidha wakipiga ngoma na matarumbeta wakiwa pia na bendera za rangi nyekundu. [2]
Wanaoafikiana na ada hii wanasema kuwa, inapasa kufanyika usiku wa siku ya Ashura. [3] Huko nyuma ada hii ilikuwa ikifanyika pia mwezi 21 Ramadhani. [4] Kuvaa nguo nyeupe (kama sanda) na kunyoa nywele ni katika ada na mazoea yaliyoenea wakati wa kufanya tatbir. [5]
Historia Yake
Asili Yake
Maoni mbalimbali yametolewa kuhusu asili ya tatbir (Qama Zani) yaani kujipiga na upanga. Baadhi wamekichukulia kitendo hicho cha kujikata kwa mapanga kuwa ni ishara ya kitendo cha Zainab (a.s) alichokifanya alipokiona kichwa cha Imamu Hussein (a.s) kwenye mkuki alipokuwa njiani kutoka Karbala kuelekea Sham, alipoteza fahamu na kugonga kichwa chake kwenye nguzo na kusababisha damu kutoka. [6] Watafiti wengi wanaona kuwa kisa kilichotajwa hakina itibari. Kwa mujibu wa Sheikh Abbas Qomi kisa hiki hakipo isipokuwa katika vitabu viwili vya Noor Al-Ain na al-Muntakhab Lil-Tarihi, na vyote viwili viko katika kiwango cha chini cha kusadikika, na zaidi ya hayo, simulizi hii haikutajwa katika kitabu chochote miongoni mwa vitabu na vyanzo vya kuaminika. Zaidi ya hayo, kwa mtazamo wa kiakili, hadithi ya kugonga kichwa Bibi Zainab katika nguzo imepotoshwa. [7]
Kwa upande mwingine, kundi jingine linaamini kuwa, tatbir haina asili ya Kiislamu; Ali Shariati anasema kuwa, kujikata na mfano wa hayo ni mambo yaliyochukuliwa kutoka marasimu ya mateso ya Kristo, ambayo Wakristo wa Orthodoksi walifanya katika kumbukizi ya kifo cha Yesu (a.s). [8] Murtaza Mutahari anaamini kwamba «kujikata kwa panga na kupiga ngoma na tarumbeta zilienea hadi Iran kutoka kwa Waothordoksi wa Caucasus, na kwa sababu nafsi na mioyo ya watu ilikuwa tayari kuikubali, ilienda kila mahali kama umeme». [9] Mkabala na msimamo huo, baadhi wanaamini kwamba, ada hii ilikuwa imeenea baina ya Waturuki wa Iraq, kundi la Sufi na Wakurdi wa magharibi mwa Iran na ikaenea na kupenya hadi Iraq kupitia mazuwwari wa Kituruki. [10]
Historia ya Tatbir Nchini Iran
Historia ya Tatbir nchini Iran inarejea katika zama za Safawiyah. [11] Katika baadhi ya maandiko ya kumbukumbu za safari za wazungu katika zama hizo kumeashiriwa kujikatakata kwa upanga na kujichanja kwa wembe; miongoni mwazo ni ripoti ya Adam Olearius katika marasimu ya kujichanja kwa wembe katika siku ya Ashura katika mji wa Erbil katika zama za Shah Safawi. Ada hii ilienea sana katika zama za utawala wa Qajar hususan katika kipindi cha uongozi wa Nassir al-Din Shah Qajar. [12] Abdallah Mustawfi anaamini kwamba, msababishaji wa hilo alikuwa Mulla Agha Darbandi, msomi na mwanazuoni aliyeishi katika zama za Nassir al-Din Shah Qajar.
Katika safari za kitalii za kuzunguka dunia za wageni wengine waliokuja Iran katika kipindi hiki na kushuhudia maombolezo ya Muharram, kuna ripoti za maandishi za watu kama vile Dk. Feuvrie, daktari maalumu wa Nassir al-Din Shah Qajar, Henry Rene D'Allemagne, na Benjamin balozi mkubwa wa Marekani katika zama za Nassir al-Din Shah Qajar.
Wakati wa utawala wa Ridha Shah, kuanzia 1314 Shamsia, tatbir ilipigwa marufuku kama zilivyopigwa marufuku ada zingine za maombolezo. [13] Marufuku hii iliendelea hadi 1320 Hijria Shamsia na hata baada ya kuondolewa madarakani Ridha Shah. Lakini baada ya hapo, marufuku hiyo kama marufuku zingine, nayo ilifutwa na ada hii ikaanza tena kutekelezwa katika baadhi ya maeneo ya Iran. Katika zama za Pahlavi ada hii ya kujikatakata katika mapombeozo ya Muharram ilikuwa na hali ya panda shuka. Katika baadhi ya miaka (kama mwaka 1343 Hijria Shamsia) ilipigwa marufuku kwa amri ya Shaharbani (polisi) na Shirika la Intelijensia na Usalama wa Taifa la utawala wa Shah (SAVAK) na katika baadhi ya miaka hususan katika baadhi ya maeneo ilikuwa ikifanywa kwa uhru kamili. [14]
Utendaji wa Mafakihi
Tatbir ni miongoni mwa mambo ambayo yana hitilafu baina ya mafakihi wa Kishia kuanzia katika zama za utawala wa Qajar hadi sasa. Kwa muktadha huo, inawezekana kuwagawa mafakihi katika makundi mawili ya wanaoafiki na wanaopinga hili. Mafakihi kama Mirza Naini, Muhammad Taqi Bahjat na Mirza Jawad Tabriz wanaona kuwa, hili linajuzu na kuruhusiwa. Mkabala na wao, Mamujitahidi kama Sayyid Abul-Hassan Isfahani, Sayyid Muhsin Amin, Sayyid Ali Khamenei, Hussein-Ali Muntazari na Nassir Makarim Shirazi wametangaza kuwa, tatbir ni kuvunjia heshima madhehebu ya Shia na hivyo ni haramu kuifanya.
Wanaoafiki
Sababu na hoja kuu na muhimu ya wale wanaoafiki na kuunga mkono tatbir mbali na suala la kutukuza shaari na nembo wanasema kuwa, kufanya hivyo ni katika kulinda na kuhifadhi sunna na ada za Kishia, kuonyesha nguvu ya jamii ya Mashia [15] na fat’wa ya Mirza Naini. Miongoni mwa Marajii ambao wameruhusu kujipiga na kujikata na hata wakati mwingine kutoa hukumu ya kuwa mustahabu jambo hilo ni:
- Muhammad Taqi Bahjat [17].
- Mirza Jawad Tabrizi [18].
- Sayyid Muhammad Sadiq Rouhani. [19]
- Sayyid Sadiq Shirazi [20]
Wapinzani
Miongoni mwa fat’wa muhimu na zenye taathira katika kupinga tatbir ni fat’wa ya Sayyid Abul-Hassan Isfahani:
- Utumiaji huu wa mapanga, minyororo, ngoma na matarumbeta kunakofanywa hii leo katika maombolezo ya Ashura ni haramu na kinyume cha sheria. [21]
Imamu Khomeini katika kutoa jibu la swali la fat’wa aliloulizwa anasema: Uharamu au uhalali wa kujikata kunategemea madhara na mazingira ya zama na kutokana na mazingira ya zama aliharamisha hilo. [23] Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema mwaka 1373 Hijria Shamsia kuhusiana na tatbir: Tatbir ni katika mambo yaliyo kinyume, bandia na yasiyo sahihi ambapo inasikitisha kwamba, katika miaka kadhaa ya hivi karibuni baadhi ya watu wamelieneza hili. Kujikata ni jambo ambalo sio maombolezo na bila shaka ni bidaa na hapana shaka kuwa, Mwenyezi Mungu hayuko radhi na hili na binafsi pia siko radhi na watu wanaodhihirisha hili. [24] Baadhi ya Maulamaa wakiunga mkono maneno haya ya Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanasema kuwa, kufanya tatbir ni jambo ambalo si halali na linavunjia heshima madhehebu ya Shia. [25]
Baadhi ya Marajii Taqlidi wengine ambao wamepinga tatbir katika fat’wa zao ni:
- Muhammad Fadhil Lankarani. [26]
- Hussein-Ali Muntazari. [27]
- Nasser Makarem Shirazi. [28]
- Abdallah Jawadi Amuli. [29]
- Sayyid Muhammad Alavi Gorgani. [30]
- Qurban-Ali Muhaqiq Kabuli. [31]
- Hussein Noori Hamedani. [32]
Hoja kuu za kuharamisha tatbir kwa mtazamo wa wapinzani:
- Kukinzana na sheria; miongoni mwa hoja inayotumiwa ni kanuni ya fikihi inayosema: “haramu kudhuru nafsi”. [34]
- Bidaa.
- Kutoingia akilini.
- Linapelekea kukuvunjia heshima dini na madhehebu (kudogosha dini na madhehebu mbele ya watu wa dini na madhehebu zingine). [35] [36]