Suratu al-Nasr
Surat al-Nasr (Kiarabu: سورة النصر) ni sura ya 110 katika mpangilio wa msahafu. Sura hii ni katika sura zilizoshuka Madina (Madani) na ipo katika Juzuu ya 30 ya Qur’an Tukufu. Jina la sura hii limechukuliwa katika Aya yake ya kwanza yaani al-Nasr yenye maana ya ushindi. Majina mengine ya sura hii ni Idha Ja’a. Katika sura hii kuna mambo matatu yamatabiriwa na na habari muhimu ya ghaibu:
- Fat’h Makka ,(ushindi na kukombolewa Makka) ushindi mkubwa na pigo la mwisho la Uislamu.
- Kuamini Uislamu watu wa Makka na viunga vyake na kuingia katika dini hii tukufu na kumpa baia na kiapo cha utii Mtume (s.a.w.w).
- Kuaga dunia Bwana Mtume (s.a.w.w)
Inaelezwa kuwa, miongoni mwa sifa maalumu za kusoma sura hii ni kujibiwa dua na kupata ushindi mbele ya maadui.
Utambulisho
- Kupewa jina
Jina mashuhuri la sura hii ni al-Nasr. Sababu ya kuitwa kwa jina hili ni kwamba, neno al-Nasr limekuja na kutumika katika Aya ya kwanza na kumezungumziwa ushindi wa Mwenyezi Mungu. Jina jingine la sura hii ni: Idha Ja’a kwa sababu imeanza kwa neno hili. Jina la tatu la suta hii ni al-Tawdi’i. Sura hii ilishuka mwishoni mwa umri mtukufu wa Bwana Mtume (s.a.w.w) na kuagwa Mtume na Mwenyezi Mungu na Jibril inaelezwa kuwa sababu ya sura hii kuitwa pia kwa jina hilo. [1]
- Mpangilio na mahali iliposhuka
Surat al-Nasr ni miongoni mwa sura zilizoshuka Madina ambazo zinajulikana kwa jina la Madani na katika mpangilio wa kushuka kwake inahesabiwa kuwa sura ya 102 iliyoshushwa kwa Bwana Mtume (s.a.w.w). Katika mpangilio wa sasa wa msahafu, sura hii ni ya 110. [2] Baadhi ya wafasiri wameitambua sura hii kuwa ni ya 110 [3] au 111 au 112 kushushwa kwa Mtume. Surat al-Nasr ni moja kati ya sura 14 mpaka 16 ambazo Aya zake zote zimeshuka katika sehemu moja.[4] Imenukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Mussa al-Ridha naye amenukuu kutoka kwa baba yake ambapo naye amenukuu kutoka kwa Imam Sadiq (a.s) ya kwamba amesema”: Sura ya kwanza kushuka ni Iqraa Bismilla Rabbika na sura ya mwisho kushushiwa Mtume ni Idha Ja’a. Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai mwandishi wa Tafsiri ya Qur’ani ya al-Mizan amejaalia kwamba, huenda makusudio ya sura ya mwisho ni kwamba, Aya zake zote zilishuka sehemu moja na kwa ukamilifu kwa Mtume. [5]
- Idadi ya Aya na maneno yake
Surat al-Nasr ina Aya 3, ina maneno 19 na herufi 80 na ni miongoni mwa sura zenye Aya fupi ambazo zinatambulika kwa jina la Sura za Mufassalat.[6]
Maudhui
Katika Surat al-Nasr, Mwenyezi Mungu anamuahidi ushindi na msaada Mtume wake na anatangaza kuwa, muda si mrefu watu wataingia katika Uislamu makundi kwa makundi. Hivyo anampa amri Mtume ya kumsabihi, kumdhukuru na kumtakasa Mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa ushindi huu, amhimidi na kuomba msamaha pia. Kwa mujibu wa rai ya baadhi ya wafasiri wa Qur’an kama Allama Tabatabai ni kwamba, sura hii imeshuka Madina baada ya sulhu ya Hudaybiyah na kabla ya Fat’h Makka; hivyo makusudio ya Fat’h na ushindi ambao Mwenyezi Mungu anauahidi katika sura hii ni ushindi wa kukombolewa Makka (Fat’h Makka). [7]
Maudhui ya Surat al-Nasr
Usimsahau Mwenyezi Mungu unapopata mafanikio makubwa
Nukta ya kwanza: Aya ya 1-2; bishara ya ushindi mkubwa kwa Waislamu
Ushindi wa kwanza: Aya ya 1; kukombolewa Makka na Waislamu kwa msaada wa Mwenyezi Mungu
Ushindi wa pili: Aya ya 2; Kuingia katika Uislamu idadi kubwa ya watu baada ya Fat’h Makka.
Nukta ya pili: Aya ya 3; jukumu la Mtume na Waislamu baada ya kupata ushindi
Jukumu la kwanza: Aya ya 3; kumsabihi Mwenyezi Mungu na kukumbuka neema na ukamilifu Wake.
Jukumu la pili: Aya ya 3; kufuata amri za Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha wa dhambi.
Zama za kushuka kwake na utabiri wake
Kuna mitazamo tofauti kuhusiana na zama za kushuka Surat al-Nasr kwa maana kwamba, ilishuka lini; kwa mfano Ali bin Ibrahim Qomi anasema, sura hii ilishuka Mina katika Hijjatul-Wida [9] au Vahidi Neyshabouri anasema: Sura hii ilishuka wakati Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akirejea kutoka katika Vita vya Hunayn na Mtume hakuishi kwa zaidi ya miaka miwili baada ya hapo; [10] hata hivyo baadhi ya wafasiri wa Qur’ani kama Sheikh Tabarsi na Allama Tabatabai wanaamini kwamba, sura hii ilishuka baada ya Sulh ya Hudaybiyah na baada ya Fat’h Makka; [11] kwa muktadha huo makusudio ya Fat’h (ukombozi), ushindi na kuijiunga watu wengi na Uislamu kulikobainishwa na Mwenyezi Mungu katika Aya za 1 na 2 za Surat al-Nasr ni Fat’h Makka (kukombolewa Makka na kuangukia mikononi mwa Waislamu); kwa sababu ni baada ya ushindi huu ambapo watu waliingia katika Uislamu makundi kwa makundi. [12]
Sura hii, ina utabiri wa mambo matatu na kutangazwa habari ya ghaibu:
- Fat’h Makka iliambatana na ushindi mkubwa na pigo la mwisho la Uislamu;
- Kuamini watu wa Makka na viunga vyake na kuingia katika Uislamu na kumpa baia na kiapo cha utii Mtume (s.a.w.w);
- Kuaga dunia Bwana (s.a.w.w) [13] Katika kitabu cha Tafsri ya Majma’ al-Bayan inaelezwa kuwa, wakati sura hii iliposhuka, Mtume (s.a.w.w) aliwasomea masahaba zake. Masahaba wote walifurahi na wakawa wakibashiriana. Lakini Abbas aliposikia sura hii alilia, Mtume akauliza: Kwa nini unalia ami? Abbas akasema: Ewe Mtume wa Allah, mimi ninadhani kwamba, sura hii inatoa habari ya kifo chako. Mtume akasema: Ndio, sura hii inasema kile kile ambacho wewe umekifahamu. Baada ya kushuka sura hii, Mtume hakuishia zaidi ya miaka miwili, kwani aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake. Baada ya kushuka sura hiyo hakuna mtu aliyemuona akicheka na akiwa na furaha. Madhumuni na maana hii imekuja katika hadithi kwa ibara tofauti. [14]
Nafasi ya tasbihi na istighfari katika Surat al-Nasr
Kwa kuzingatia kwamba, tukio la Fat’h Makka lilikuwa ni kudhalilishwa shirki na ukafiri, na kupatikana utukufu na heshima kwa tawhidi, kuangamizwa batili na kuibuka mamlaka na utawala wa haki, hivyo kutokana na kuangamizwa batili, Mtume alitakiwa kumtakasa Mwenyezi Mungu na kumsabihi, na kutokana na haki kutawala ambayo ni neema ya Mwenyezi Mungu, alitakiwa amhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kumhimidi na kumsabihi Mwenyezi Mungu kuna nafasi na daraja kubwa mno katika Uislamu na hili linadhihirika wazi hasa kupitia hadithi mbalimbali zilizonukuliwa zinazobainisha suala hili. Ummu Salamah mke wa Mtume amenukuu ya kwamba: Mwishoni mwa umri wake, Mtume hakuwa akisimama, kukaa, kwenda na kurejea isipokuwa alikuwa akisema: (سبحان الله و بحمده و استغفر الله و اتوب الیه), Tukamuuliza sababu ya hilo. Mtume akasema: Mimi nimeamrishwa kufanya hili, na kisha alikuwa akisoma Surat al-Nasr. Hata hivyo, kuhusiana na maudhui hii hii Bibi Aisha mke mwingine wa Mtume amenukuu kutoka kwa Mtume dhikri hii: (سبحانك اللهم و بحمدك أستغفرك و أتوب إليك)
Fadhila na sifa maalumu
- Makala asili: Fadhila za sura
Kwa mujibu wa hadithi inayonasibishwa na Bwana Mtume (s.a.w.w) ni kwamba, mwenye kusoma sura hii atapata thawabu za mtu ambaye alipigana vita pamoja na Mtume katika Fat’h Makka na akauawa shahidi. [16] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi nyingine: Kila ambaye ataswali rakaa nne katika usiku wa tarehe 9 Shaaban na katika kila rakaa baada ya al-Hamdu akasoma Surat al-Nasr mara 10, Mwenyezi Mungu atauharamisha mwili wake na moto wa jahanamu (kwa maana kwamba, hatoadhibiwa katika moto wa jahanamu), na kwa kila Aya anayoisoma anapatiwa thawabu za mashahidi 10 wa vita vya Badr na thawabu za Maulamaa wa kidini. [17] Surat al-Nasr inasomwa pia katika rakaa ya tatu ya Sala ya Ja’far al-Tayyar. [18] Kadhalika kuna sifa maalumu zimenukuliwa kuhusiana na sura hii kama vile, kujibiwa dua na kupata ushindi mkabala na maadui. [19]
Surat al-Nasr na tarjuma yake
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ وَالْفَتْحُ «۱» وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ أَفْوَاجًا «۲» فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُ ۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا «۳»
Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu, Itakapo kuja nusura ya Mwenyezi Mungu na ushindi, na ukaona watu wanaingia katika dini ya Mwenyezi Mungu kwa makundi, zitakase sifa za Mola wako Mlezi, na umwombe msamaha; hakika Yeye ndiye anayepokea toba.
(Quran: 110)
Vyanzo
- Baḥrānī, Sayyid Hāshim b. Sulaymān. Al-Burhān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Bunyād-i Biʿthat, 1416 AH.
- Ibn Ṭāwūs, ʿAlī b. Mūsā. Iqbāl al-aʿmāl. Edited by Jawād Qayyūmī. Qom: Markaz al-Nashr al-Tābiʿ li-Maktab al-Aʿlām al-Islāmī, 1416 AH.
- Khurramshāhī, Bahāʾ al-Dīn. Dānishnāma-yi Qurʾān wa Qurʾān pazhūhī. Tehran: Dūstān-Nāhīd, 1377 Sh.
- Maʿrifat, Muḥammad Hādī. Āmūzish-i ʿulūm-i Qurʾān. [n.p]: Markaz Chāp wa Nashr-i Sāzmān-i Tablīghāt, 1371 Sh.
- Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Qom: Dār al-Kitāb, 1367 Sh.
- Suyūṭī, ʿAbd al-Raḥmān b. Abī Bakr al-. Al-Itqān fī ʿulūm al-Qurʾān. Edited by Fawāz Aḥmad Zamarlī. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, [n.d].
- Ṭabāṭabāyī, Mūhammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1374 Sh.
- Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Edited by Hāshim Rasūlī & Yazdī Ṭabāṭabāyī. Third edition. Tehran: Intishārāt-i Nāṣir Khusru, 1372 Sh.
- Wāḥidī Niyshābūrī, ʿAlī b. Aḥmad al-. Asbāb al-nuzūl. Translated to Farsi by ʿAlī Riḍā Dhikāwatī. Tehran: Nashr-i Niy, 1383 Sh.