Kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s)

Kutoka wikishia

Makala hii inahusiana na kuwapenda Ahlul-Beiti (a.s). Kama unataka kufahamu kuhusiana na Aya yenye maudhui hii basi angalia Aya ya Mawaddah.


Mawaddah kwa Ahlul-Beiti a.s (Kiarabu: مودة أهل البيت (ع)) maana yake ni kuwapenda watu wa kizazi cha Bwana Mtume (s.a.w.w) ambao kwa mujibu wa Aya ya 23 ya Surat al-Shuura, kufanya hivyo kunatajwa kuwa ujira wa risala ya Bwana Mtume (s.a.w.w). Kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa na Waislamu wa Kishia na Kisuni kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w), kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume ni msingi wa Uislamu. Sayyied Muhammad Tijani anasema: Waislamu wamekubaliana kwa kauli moja kuhusiana na kuwa wajibu suala la kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume (Ahlul-Beiti); na ni kwa muktadha huo ndio maana wakalitambulisha hilo kama sababu mwafaka ya umoja wa Waislamu. Baadhi ya wahakiki wanaamini kwamba, falsafa ya kuwa wajibu mapenzi kwa Ahlul-Beiti (kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume) ni kuwatii.

Kumetajwa athari tofauti za kidunia na Akhera kuhusiana na suala la kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume. Kupata shafaa ya Ahlul-Beiti, kutakabaliwa amali na kuwa thabiti na kutotetereka katika sirati ni baadhi ya athari za Akhera na kwamba, kufanya toba kabla ya kuaga dunia, kutokuwa na tamaa na mali za watu na kuzungumza kwa hekima ni miongoni mwa mambo yaliyotambuliwa kuwa ni athari za kidunia za kuwapenda watu wa nyumba ya Bwana Mtume (s.a.w.w). Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, kuwapenda Ahlul-Beiti ni ishara ya kuwa mtoto wa halali na kufanya urafiki na maadui zao kumetajwa kuwa ishara ya kutokuwa na mapenzi ya kweli kwa Ahlul-Beiti (a.s).

Muhammad Muhammadi Reyshahri amelitambua suala la kufanya maombolezo kwa ajili ya Ahlul-Beiti kwamba, ni moja ya njia za kuonyesha mapenzi kwao; kama ambavyo imeelezwa kuwa, kuzuru makaburi ya Maimamu (a.s), kuwa na furaha katika hafla zao za furaha, kuwapa watoto majina ya Ahlul-Beiti (a.s) ni njia nyingine za kuonyesha mapenzi kwa watu hao wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w). Baadhi ya wahakiki wametaja mbinu na mikakati ya kuandaa mazingira ya kuwapenda Ahlul-Beiti (a.s) ambapo kutaja fadhila na utamaduni wao na kuandaa kamati za kidini (kwa ajili ya kuandaa hafla za kutaja wasifu wao) ni miongoni mwa mikakati hiyo.

Baadhi ya watu wakitumia hadithi za kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume wamesema, kuwa kufanya hivyo ni jambo linalotosha kwa ajili ya kufikia saada na ufanisi huko Akhera. Wanaamini kwamba, kuwa na mapenzi ya namna hii, hata kama watafanya dhambi hilo haliwezi kuwadhuru huko Akhera. Hata hivyo Maulamaa wa Kishia wamekosoa upuuzaji huu wa dhambi na kubainisha maana nyingine ya hadithi hizi; kwa mfano wamesema, hadithi hizi zinahusiana na dhambi ambazo zimefanywa katika hali ya kughafilika na hazina uhusiano kabisa na dhambi zilizofanywa kwa makusudi.

Kuhusiana na maudhui ya kuwapenda Ahlul-Beiti, kumeandikwa vitabu mbalimbali ambapo baadhi ya vitabu hivyo ambavyo tunaweza kuviashria ni: Hubbu Ahlul-Beit Fil Kitab Wassunnah", kilichoandikwa na Muhammad Taqi Sayyied Yusuf al-Hakim. Kitabu kingine ni Qur'an va Mahabbat Ahl Beit (a.s), kilichoandikwa na Alireza Azimifar.


Umuhimu na nafasi ya kuwapenda Ahlul-Beiti

Mawaddah kwa Ahlul-Beit ni istilahi iliyochukuliwa kutoka katika Aya ya 23 ya Surat al-Shuura ambayo ina maana ya kuwapenda watu wa nyumba ya Bwana Mtume (s.a.w.w) ambapo kwa mujibu wa Aya hii, kuwapenda watu wake kumetajwa na kutambulishwa kuwa ndio ujira wa risala ya Mtume (s.a.w.w). [1] Mawaddah yametambuliwa kuwa ni mahaba (mapenzi) [2] na kupenda (sambamba na kutawalisha (tawalli) na kuwakubali Ahlul-Beit kwamba ni viongozi) [3] au ni daraja iliyo juu zaidi ya mahaba na tawi la huba na mapenzi kwa Mwenyezi Mungu. Katika ziyara ya Jamiat al-Kabira kunaelezwa kuwa, kuwapenda Ahlul-Beit (a.s) ni kumpenda Mwenyezi Mungu [6] na zimenukuliwa hadithi na Waislamu wa madhehebu ya Shia na Suni kutoka kwa Bwana Mtume ya kwamba, kuwapenda Ahlul-Beit ni msingi wa Uislamu. [7] Kuna hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir (a.s) ambayo imetambua kuwa, kuwapenda Ahlul-Beiti ndio ile imani na kuwafanyia uadui ni ukafiri. [8]

Muhammad Taqi Misbah Yazdi mmoja wa Maulamaa wa karne ya 14 Hijria anasema: Kuwapenda Ahlul-Beit (a.s) hakujafanywa kuwa jambo la lazima kutokana na nasaba yao kwa Mtume, bali hilo limekuwa jambo la lazima kutokana na waja hao kufikia kilele cha uja na uchaji Mungu. [9]


Kutukuza nembo

Muhammad Muhammadi Reyshahri mtafiti wa hadithi wa Kishia amelitambua suala la kufanya maombolezo kwa ajili ya Ahlul-Beiti kwamba, ni moja ya njia za kuonyesha huba na mapenzi kkwao na kwamba, ni kielelezo na mfano muhimu kabisa wa kutukuza nembo (taadhim Shaair). [10] Vilevile inaelezwa kuwa,, kuzuru makaburi ya Maimamu (a.s), [11] kuwa na furaha katika hafla zao za furaha, [12], kutaja fadhila za Ahlul-Beit [13] na kuwapa watoto majina ya Ahlul-Beit (a.s) ni njia nyingine za kuonyesha mapenzi kwa watu hao wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w). [14]

Wajibu wa kuwapenda Ahlul-Beiti

Baadhi ya wahakiki wamesema kuwa, kuwapenda Ahlul-Beiti ni katika haki za watu hao wa nyumba ya Mtume ambayo wanapaswa kutendewa na Waislamu. Yaani ni haki ambayo iko katika mabega ya Waislamu [15], ni katika itikadi za pamoja (wanazoshirikiana) Waislamu [16] na wenzo mwafaka kwa ajili ya umoja wa Waislamu. [17]. Sayyied Muhammad Tijani mtafiti wa masuala ya Kiislamu na Mtunisia aliyekuwa Msuni kisha akaingia katika Ushia anaamini kuwa, Waislamu wameafikiana kuhusiana na kuwa wajibu suala la kuwapenda Ahlul-Beiti (a.s). [18] Shamsuddin al-Dhahabi, mmoja wa Maulamaa wa Kisuni naye pia anapinga shaka ya aina yoyote kuhusiana na kwamba, ni wajibu kuwapenda Ahlul-Beit (a.s). [19] Fakhrurazi mmoja wa wafasiri wa Qur’an wa Kisuni anasema kuwa, kuwapenda Ahlul-Beiti (a.s) ni wajibu akitumia hoja kwamba, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akiwapenda Ali, Fatma, Hassan na Hussein, hivyo kwa kumfuata Bwana Mtume ni wajibu kwa umma wote wa Kiislamu kuwapenda Ahlul-Beiti wake. [20] Allama Hilli, fakihi na mwanatheolojia wa Kishia wa karne ya 8 Hijiria akitumia hoja kwamba, kupingana na Imam Ali (a.s) kunakinzana na kuwa na mapenzi juu yake katika hali ambayo kumpenda Imam Ali ni wajibu na kuwapenda makhalifa wengine sio jambo la wajibu” analitumia hilo kama hoja ya Uimamu wa Imam Ali (a.s) na kwamba, Ushia ni madhehebu ya haki. [21]


Falsafa ya kuwa wajibu

Allama Sayyied Muhammad Hussein Tabatabai, mfasiri wa tafsiri ya Qur’an ya al-Mizan anaamini kuwa, hekima na falsafa ya kuwa wajibu kuwapenda Ahlul-Beiti (a.s) ni kuwa kwao marejeo ya kielimu ili kupitia kuwapenda kwao, Waislamu waweze kuwarejea katika masuala ya elimu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana analitambulisha suala la “kuwapenda Ahlul-Beiti (a.s) kwamba, ni dhamana ya kubakia kwa dini”. [22]

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu ya Iran ameyatambua mapenzi kwa Ahlul-Beiti kuwa ngome kwa ajili ya kuwatii Ahlul-Beit. Anaamini kuwa, kwa kuonyesha huba na mapenzi, itikadi za watu kwa Wilaya (uongozi wa Ahlul-Beiti) huhifadhiwa na kubakia. [23] Kadhalika Ali Rabbani Golpaygani, mmoja wa walimu wa elimu ya theolojia katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Qom anaamini kwamba, falsafa ya kuwa wajibu haya mapenzi, ni katika kuwatii Ahlul-Beit (a.s) na mapenzi na huba ya kweli hupatikana kwa kuwafuata tu. [24] Jawad Mohaddesi, mmoja wa waandishi wa Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Qom anasema: Kadiri huba na mapenzi yanavyokuwa kwa kiwango kikubwa, basi vivyo hivyo, kuwafuata wao kutakuwa kwa kiwango kikubwa zaidi. [25]

Athari za kuwapenda Ahlul-Beiti

Wahakiki wanaamini kuwa, kuwapenda Ahlul-Beiti (a.s) ni wenzo wa kumfanya mtu apige hatua kuelekea ukamilifu mutlaki, [26] ni wenzo wa kuweko mafungano ya kinyoyo baina ya wapenzi na maashiki wa Ahlul-Beiti [27] na ni chimbuko la nidhamu na umoja na mshikamano wa kidini. [28] Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ali (a.s) na kunukuliwa na Abu Naim Isfahani na Abdallah Haskani (miongoni mwa wanazuoni wa Kisuni katika karne ya 5 Hijria) inaeleza kuwa, Waumini tu ndio wanaochunga na kuzingatia suala la kuwapenda Ahlul-Beiti (a.s). [29]


Athari za kiakhera

Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ni kuwa, matunda ya kumpenda yeye na watu wake wa nyumbani (Ahlul-Beiti) yanadhihirika katika maeneo saba:

  1. Wakati wa Kifo.
  2. Kaburini.
  3. Siku ya Kiyama.
  4. Wakati wa kupokea kitabu cha amali.
  5. Wakati wa kuhesabiwa amali.
  6. Kando ya Mizani.
  7. Wakati wa Kupita katika sirati (ambayo ni njia nyembamba sana). [30]

Kwa mujibu wa hadithi nyingine iliyonukuliwa na Waislamu wa Kisuni ni kuwa: Mtu ambaye ataaga dunia hali ya kuwa alikuwa ni mwenye kuwapenda Ahlul-Beiti ni mithili ya shahidi aliyesamehewa dhambi zake, anakufa akiwa na imani kamili, na wakati wa kufa, anapewa bishara ya pepo, katika kaburi lake hufunguka milango miwili kuelekea peponi na Mwenyezi Mungu anaainisha malaika kuwa wenye kulizuru kaburi lake. [31] Athari nyingine zinazopatikana kwa wanaowapenda Ahlul-Beiti (a.s) ambazo zimetajwa ni:

  • Kupata shufaa; imekuja katika hadithi za Bwana Mtume ya kwamba: Kila ambaye atakuwa na mapenzi na Ahlul-Beiti ataingia peponi kwa shafaa (uombezi) yao. [32]
  • Kufufuliwa pamoja na Ahlul-Beiti (a.s); kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), vipenzi vya Ahlul-Beiti watafufuliwa pamoja nao Siku ya Kiyama. [33]
  • Kutakabailiwa amali; katika hadithi iliyonukuliwa na Abu Hamza Thumali kutoka kwa Imam Ali (a.s) inaelezwa kuwa, Siku ya Kiyama watu kwa kuwa na mapenzi na Ahlul-Beit amali zao nyingine pia hutakabaliwa, lakini kama mtu hakuwa akiwapenda Ahlul-Beiti amali zake nyingine hazitakubaliwa. [34].
  • Kuwa Thabiti na imara (kutotetereka) katika sirati; kwa mujibu wa hadithi iliyoko katika kitabu cha Ja’fariyat ni kuwa, kila mtu ambaye atakuwa na mahaba na mapenzi zaidi na Ahlul-Beiti (a.s) atakuwa imara na asiyeteteka wakati wa kupita katika sirati. [36]
  • Kusamehewa dhambi; hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) inaonyesha kuwa, kuwapenda Ahllul-Beiti kunapelekea mtu kusamehewa dhambi zake. [37] Ibn Hajar Haytami mmoja wa Maulamaa wa Ahlu Sunna katika karne ya 10 Hijiria sambamba na kunukuu hadithi ya mlango wa Hittah anaamini kwamba, kama ambavyo Mwenyezi Mungu alilifanya suala la Bani Israel kuingia kupitia mlango wa Hittah kuwa sababu ya kusamehewa dhambi zao, katika umma wa Kiislamu pia amelifanya suala la kuwapenda Ahlul-Beiti kuwa sababu ya kusamehewa dhambi zao. [38]

Athari za kidunia

Kuna hadithi zilizopokewa kutoka kwa mbora wa viumbe Bwana Mtume (s.a.w.w) ambazo zinaonyesha matokeo mazuri na athari chanya za kuwapenda watu wa nyumba ya Bwana Mtume (Ahlul-Beiti): Miongoni mwa athari hizo ni zuhdi (kuipa mgongo dunia), kuwa na shauku na hamu ya kufanya kazi, kuwa na uchaji Mungu katika dini, kuwa na hamu na shauku ya kufanya ibada, kufanya toba kabla ya kuaga dunia, nishati ya kukesha (kwa ajili ya kufanya ibada na kuomba dua), kutokuwa na tamaa na mali za watu, ukaribu, kuchunga maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu na kutoipenda dunia. [39] Imam Muhammad Baqir (a.s) amenukuliwa akisema kwamba, Mwenyezi Mungu hutakasa mioyo ya watu wanaowapenda Ahlul-Beiti. [40] Kwa upande wake Imam Ja’afar Swadiq (a.s) amenukuliwa akisema: Mtu ambaye atalifanya suala la kuwapenda Ahlul-Beiti kuwa thabiti na la kudumu katika moyo wake, basi hutiririka hekima kutoka katika kinywa chake (huwa ni mwenye kuzungumza kwa hekima na busara). [41]

Alama

Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir (a.s) ni kuwa, kuwapenda Ahlul-Beiti na wakati huo huo kuwapenda maadui zao ni mambo mawili ambayo hayakusanyiki mahali pamoja; na kama itatokea mtu akampenda adui wa Ahlul-Beiti basi hiyo ni ishara na alama ya kutokuwa na mapenzi ya kweli kwa Ahlul-Beiti. [42] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi kutoka kwa Imam Ali (a.s) ni kwamba: Mtu ambaye hawapendi watu wanaowapenda Ahlul-Beiti si katika wapenzi wakweli wa Ahlul-Beiti. [43] Kwa mujibu wa hadithi nyingine wanaume wasio na ghera (wivu), watoto wa zina, watu wanaojifafanisha na wanawake na watu ambao mama zao walipata ujauzito wakiwa katika hali ya hedhi hawawapendi Ahlul-Beiti (a.s). Vilevile imekuja katika hadithi ya kwamba, kuwapenda Ahlul-Beiti ni ishara na alama ya kuwa mtoto wa halali. [45] Kuwatii kivitendo Ahlul-Beiti kumetajwa kuwa moja ya mfano muhimu na ishara na alama ya ukweli ya mtu anayesema na kuonyesha kwamba, anawapenda watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w). [46]

Kupuuza dhambi kwa kutegemea kuwapenda Ahlul-Beiti (a.s)

Kuna kundi la miongoni mwa watu wa dini ambalo linaamini kwamba, kila dhambi aifanyayo mtu inaondolewa kwa sababu ya kuwa na mapenzi na Ahlul-Beiti, na kufanya dhambi watu wanaowapenda watu wa nyumba ya Mtume ni jambo ambalo halina madhara yoyote kwa saada yao huko Akhera. [47] Ali Nasiri, mmoja wa wahakiki wa Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) anasema: Akthari ya wapuuzaji wa dhambi hawana mashiko imara ya kielimu bali wanajengea hoja madai yao kwa kutumia hadithi kama: Mapenzi kwa Ali ni jema ambalo halidhuriwi na dhambi yoyote ile, na chuki dhidi ya Ali, ni dhambi ambayo kwa kuweko kwake hakuna jema lolote lenye faida na manufaa [48]. Hiyo ndio hoja yao. [49] Mhakiki Bahrani (1121-1075 H) ameitaimbua hadithi hiyo kuwa ni mustafidh, [50]. Hata hivyo baadhi ya Maulamaa wa Kishia wametaja maana nyingine ya hadithi hii ambayo haioani na fikra ya upuuzaji dhambi; [51] kwa mfano Sheikh Mufid mmoja wa wanatheolojia wa Kishia anasema kuwa, kuna uwezekano huu kwamba, watenda dhambi ambao wana maarifa na Ahlul-Beiti wataadhibiwa tu katika ulimwengu wa barzakhi ili Siku ya Kiyama watakaswe kunako madhambi yao na hivyo kuokolewa na moto wa jahanamu. [52]

Baadhi ya wahakiki pia wanaamini kwamba, dhambi ambazo zimefanywa katika hali ya kughafilika tu ndizo ambazo zitasamehewa kutokana na wahusika kuwa na mapenzi na Ahlul-Beiti, na sio dhambi ambazo zimefanywa kwa makusudi. [53]

Ali Nasiri anasema, fikra kama hii ilikuweko huko nyuma katika dini nyingine na katika dini ya Uislamu na baadhi ya makundi kama Murji’ah na Karramiyah kutoka katika madhehebu ya Kisuni na Maghulati kutoka katika madhehebu ya Kishia wana itikadi zinazofanana. [54] Yeye anaamini kuwa, itikadi ya kuupuza dhambi imeibuka baina ya watu kutokana na kutozingatia kwao mitazamo na fat'wa na Maulamaa wa dini. [55]Jawad Mohaddesi, mmoja wa waandishi wa Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Qom anasema: Kudai kuwa na mapenzi na Ahlul-Beiti na wakati huo huo kufanya matendo ya dhambi ni aina fulani ya ukinzani (mgongano). Anaamini kwamba, mapenzi ya kweli ni yale ambayo yanaambatana na kuwafuata na kuwatii. [56] Katika fikihi ya al-Ridha (a.s) (kitabu kinachonasibishwa na Imam Ridha(a.s)) mahusiano ya amali njema na mapenzi kwa Ahlul-Beiti limetambuliwa kuwa, jambo la pande mbili. Kwa maana kwamba, moja kati ya hayo halibakubaliwi pasi ya jingine. (yote yanapaswa kuwa pamoja). [57] Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir (a.s) inasema: Kila ambaye atamtii Mwenyezi Mungu ana mapenzi kwa Ahlul-Beiti (a.s) na kila ambaye atakengeuka na kuasi amri za Mwenyezi Mungu, ni adui wa Ahlul-Beiti (a.s). [58]

Monografia

Kitabu "Mawadat Ahlul-Bayt na fadhila zao katika Kitabu na Sunnah" kilichoandikwa na Muhammad Taqi Al-Sayyied Yusuf Al-Hakim juu ya mada ya mapenzi ya Ahlul-Bayt (a.s)

Baadhi ya vitabu ambavyo vimeandikwa kuhusiana na maudhui ya kuwapenda Ahlul-Beiti ni:

  • “Hubbu Ahllul-Beit Fil Kitab wal-Sunnah”, mwandishi Muhammad Taqi Sayyied Yusuf al-Hakim; kitabu hiki kimegawanywa katika faslu tano kuu na kina kurasa 278. Kitabu hiki kimechapishwa kwa jitihada za Taasisi ya al-Fikr al-Islami 1424 Hijria. [59]
  • “Qur’ani va Mahabbat Ahle Beit (a.s)”, mwandishi Alireza Azimifar; katika kitabu hiki, mwandishi huyu amefanya uchunguzi na tathmini ya “mapenzi kwa Ahlul-Beiti katika Qur’ani” na katika sehemu ya mwisho ya kitabu hiki ametoa majibu ya shubha na utata unaoonyeshwa na Ahlu Sunna kuhusiana na Aya ya Mawaddah. [60]. Kitabu hiki kimesambazwa na Chuo cha Usul Ddin 1394 Hijria Shamsia kikiwa na kurasa 360 [61].
  • “Mabani Nazari va amali Hub Ahl Beyt (a.s)”, kilichoandikwa na Asghar Taherzadeh. Kitabu hiki kwa hakika asili yake ni hotuba za mwandishi ambazo baadaye zilikuja kuandikwa na kufanywa kitabu. Kilichapishwa na kusambazwa na Lubb al-Mizan 1388 Hijria Shamsia kikiwa na kurasa 333. [62]
  • “Mahabbat Nejat Bakhsh”, mwandishi: Alireza Jamali, kitabu kitabu hiki mwandishi amejadili na kuchunguza athari za kuwapenda Ahlul-Beiti dunia, katika ulimwengu wa barzakhi na Siku ya Kiyama. [63] Kitabu hiki kilichapishwa 1393 Hijria Shamsia kwa hima ya Taasisi ya Uchaopishaji ya Zamzam Hedayat. [64]

Rejea

Vyanzo