Adhabu ya Milele

Kutoka wikishia

Adhabu ya Milele au Kubakia Milele Motoni (Kiarabu: الخلود في النَّار أو العذاب الأبدي) ni moja ya mafundisho ya Uislamu na dini nyingi za Mwenyezi Mungu. Aya mbalimbali za Qur’ani zinataja adhabu ya milele kwa ibara ya «خَالِدِينَ فِيهَا» (watadumu humo milele) na mfano wa hayo zikiashiria adhabu ya milele; kama ambavyo hadithi nyingi zilizopokewa na Waislamu wa madhehebu ya Shia zinasisitiza juu ya kubakia milele katika moto wa jahanamu.

Miongoni mwa wanafikra, kuna mitazamo tofauti kuhusu kubakia milele motoni: Watu kama vile Muhyiddin Arabi, Mulla Sadra (hata hivyo ni katika baadhi ya kazi zake) na Imam Khomeini ni miongoni mwa wale ambao hawakubali mtazamo wa kubakia milele motoni na wanaamini kwamba hatimaye adhabu ya motoni itaisha. Wanachukulia kubakia na kudumu milele motoni kuwa ni kinyume na uadilifu, hekima na huruma ya Mungu, na wanasema kwamba wakazi wote wa motoni wataondoka humo, au kama watabakia basi hawatateseka tena. Kutoisha na kutomalizika kwa asili ya Kimungu ya mwanadamu pia ni moja ya sababu nyingine zinazotolewa kundi hili la kutokuwepo kwa adhabu ya milele.

Kwa upande mwingine, waungaji mkono wa mtazamo wa adhabu ya milele motoni wanaona kuwa ni ya pekee kwa makafiri wenye uadui ambao wametimiziwa na kufikiwa na hoja. Wanaamini kwamba wenye dhambi na watu waliokandamizwa na kudhoofishwa kifikra hawatabakia motoni milele. Wanachuoni wa Kishia wanaamini kwamba adhabu ya milele inaweza kuelezwa kwa nadharia ya mfanano wa matendo na udhihirisho wa ukweli wa matendo katika Siku ya Kiyama. Aidha, imeelezwa katika Qur'ani ya kwamba, baadhi ya watu hawatatoka motoni. Makhawariji pia wanaamini kwamba, mbali na makafiri, watenda madhambi makubwa waliokufa bila kutubia watapata adhabu ya milele.

Nafasi

Kudumu na kubakia milele roho ya mwanadamu baada ya kifo ni miongoni mwa mafundisho ya dini ya Uislamu na dini nyingine nyingi ukiwemo Uyahudi na Ukristo.[1] Kwa ujumla, watu au makundi haya yameahidiwa katika Qur'ani kubakia milele motoni: Makafiri[2], washirikina[3] na wanafiki.[4]

Tofauti za kimitazamo katika suala la adhabu ya milele ni kubwa kiasi kwamba baadhi ya watu wanaona kuwa ni maafikiano (ijmaa) na ni dharura ya kidini, na wengine wanaona kuwa ni mbali na akili kwamba haiwezi kuhusishwa na dini.[5] Wanaoafiki mtazamo wa adhabu ya milele wameegemea zaidi juu ya maandiko ya kidini kama hoja.[6] Inaelezwa kuwa Aya 85 za Qur'an zimezungumzia suala la kubakia milele, na aya 34 zinahusiana na kudumu milele motoni.[7] Aya ya 169 ya Surat al-Nisaa, Aya ya 65 ya Surat al-Ahzab na Aya ya 23 ya Surat al-Jinn zinazungumzia kuhusu makafiri, madhalimu na waliomuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kisha baada ya ibara ya “Khalidin fiha” (kudumu milele)” limekuja neno Abadaa yaani milele.[8]

Kuna hadithi nyingi zilizokuja kuzungumzia suala la kubakia motoni milele. Kwa mujibu wa Muhammad Hussein Tabatabai, hadithi zilizopokewa kutoka kwa Ahlul Bayt zinazozungumzia asili ya adhabu ya milele zimekuja na kufikia kiwango cha Istifadha (hadithi ambayo idadi ya wapokezi wake ni zaidi ya mtu mmoja lakini haijafikia kiwango cha mutawatir.[9] Katika baadhi ya hadithi, suala la kudumu milele katika moto wa jahanamu na adhabu ya milele, limetambuliwa kuwa ni mahususi kwa makafiri wakanaji na washirikina.[10]

Mitazamo Mitatu Kuhusu Adhabu ya Milele

Adhabu ya Milele Kwa Ajili ya Makafiri na Watenda Madhambi Makubwa

Wanateolojia walio wengi wa Kiislamu kutoka katika madhehebu mbalimbali wanaamini juu ya kubakia milele makafiri katika moto wa jahanamu.[11] Lakini kuhusiana na kubakia milele katika moto wa jahanamu mtu ambaye ni fasiki au kwa maneno mengine, muumini ambaye ametenda dhambi kubwa na kuaga dunia bila ya kutubia, kuna hitilafu kubwa.[12]

Makhawariji walikuwa wakiamini kwamba, anayetenda dhambi kubwa anakuwa kafiri na atabakia milele katika moto wa jahanamu.[13] Mkabala na wao kuna Mu’tazila ambao walikuwa wakiamini kwamba, Mwislamu wa namna hiyo sio fasiki wala muumini, bali nafasi yake ni sehemu baina ya sehemu mbili; pamoja na kuwa akthari yao kama walivyokuwa Makahariji walikuwa wakiamini kwamba, mtu wa aina hiyo atabakia milele katika moto wa jahanamu.[14]

Adhabu ya Milele; Maalumu Kwa Makafiri

Jahidh (aliaga dunia 255 H) na Abdallah bin Hassan Anbari (aliishi katika karne ya 2 Hijria (walikuwa wakiamini kwamba, adhabu ya milele ni mahususi kwa makafiri wenye uadui; lakini kama mtu atajitahidi na kisha hoja za haki zisimdhihirikie na hivyo kutosilimu atahesabiwa kuwa mwenye udhuru na adhabu yake katika jahanamu itasitishwa (sio ya milele).[15]

Upinzani Dhidi ya Adhabu ya Milele

Kuna upinzani baina ya Maulamaa wa madhehebu tofauti kuhusiana na adhabu ya milele, lakini upinzani huo una mtazamo mmoja. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa, inawezekana kuwagawa wapinzani wa adhabu ya milele katika makundi sita:[16]

  1. Kutolewa watu wa motoni na kuingizwa peponi.[17]
  2. Kuteketea jahanamu waliomo ndani yake.[18]
  3. Kupewa watu wa jahanamu nguvu ya subira na kusahau adhabu.[19]
  4. Adhabu iliyochanganyika na neema.[20]
  5. Kubadilika adhabu na kuwa ladha.[21]
  6. Kubakia milele kwa aina fulani.[22]

Imeelezwa kuwa, ukimtoa Jahm bin Safwan na baadhi ya wafuasi wake ambao wana imani juu ya kuteketea na kumalizika jahanamu na pepo na kwa hivyo hawakuwa na imani juu ya kubakia motoni milele,[23] Muhyiddin bin Arabi ndiye mpinzani mkuu wa nadharia ya kubakia milele watu wa motoni[24] na ameandika kwamba, watu wa motoni baada ya kuwa wameonja adhabu ya moto kwa kiwango cha amali na matendo yao, wakiwa humo humo peponi watajumuishwa katika fadhila na rehma za Mwenyezi Mungu na hivyo hawatahisi tena adhabu ya moto.[25] Mulla Sadra Shirazi katika baadhi ya vitabu na athari zake, ana imani kama ya Ibn Arabi kwamba, hatimaye adhabu ya motoni itamalizika na watu wa jahanamu hawatahisi tena uchungu wa adhabu.[26]

Imamu Ruhullah Khomeini pia amewekwa katika orodha ya Maulamaa hawa ambaye anaamini juu ya kuokoka na adhabu ya moto kupitia shifaa[27) na anasema kuwa, ili kuthibitisha madai haya ameshikamana na rehma jumla za Mwenyezi Mungu na kutoisha na kutomalizika kwa asili ya Kimungu ya mwanadamu.[28]

Imani ya Maulamaa wa Kishia

Kwa mujibu wa maudhui na mjadala uliotajwa na Sheikh Qardab Qaramalaki ambaye ameboibea katika elimu ya teolojia ni kuwa, kwa hakika asili ya kubakia milele katika moto wa jahanamu kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni na Maulamaa wa Kishia iko wazi na imekubaliwa kwa pamoja[29] na kwa mujibu itikadi ya wanateolojia wa Kishia kwa hakika kubakia milele motoni ni mahususi kwa makafiri.[30]

Adhabu ya Milele; Mahususi Kwa Makafiri Wenye Uadui

Kwa mujibu wa Sheikh Mufid ni kuwa, Shia wanaamini kwamba, adhabu ya milele ni maalumu kwa makafiri na watenda madhambi hata kama wataingia katika moto wa jahanamu, lakini hawatabakia humo milele.[31] Mulla Sadra sambamba na kuunga mkono kwamba, chimbuko la kubakia milele katika moto wa jahanamu ni kukufuru tu anasema kuwa, kubakia milele kwa makafiri katika moto wa jahanamu ni kwa sababu ya ufisadi wa itikadi yao; kinyume na ufisadi katika amali na matendo kuna uwezekano wa kuondoka hilo.[32]

Allama Tabatabai anasema kuwa, Qur'ani Tukufu imebainisha wazi kuhusiana na kubakia milele na adhabu ya milelele kama ambavyo Aya ya 167 ya Surat al-Baqarah imebainisha wazi kwamba, hawatakuwa wenye kutoka motoni. Hadithi mbalimbali pia zilizonukuliwa kutoka kwa Ahlu-Bayt (as) ziko wazi kuhusiana na maudhui hii; kwa msingi huo, hadithi zilizopokewa na wasiokuwa Mashia ambazo zinaonyesha juu ya kusimamishwa na kusitishwa adhabu ya motoni, zinapingana na Qur'ani na hivyo inapaswa kuziweka kando na kutozifanyia kazi.[33]

Hoja za Wanateolojia wa Kishia

Wanachuoni wa kidini wa Shia wametaja Aya za Qur'ani na hadithi na vilevile dalili zenye mantiki kutoa hoja kwamba adhabu ya milele si ya ulimwengu wote na inajumuisha makafiri wenye chuki na uadui tu; miongoni mwa yaliyosemwa kuhusiana na hilo na kutolewa hoja ni ibara ya «إِلَّا مَا شَاءَ اللَّهُ» "ila apendavyo Mwenyezi Mungu" katika Aya ya 128 ya Surat al-An'am ambapo kuna watu ambao wametolewa katika hukumu ya adhabu ya milele na kwa kuzingatia kauli moja na maafikiano yaliyopo ya kwamba, kafiri hatatoka motoni, hivyo makusudio ya Aya ni kumuondoa fasiki aliyefanya dhambi kubwa ambaye adhabu yake itasimamishwa na kusitishwa kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu.[34] Muhammad Baqir Majlisi amefikia natija hii kuhusiana na majimui ya hadithi zilizoptajwa kuhusiana na kubakia milele motoni kwamba: Watu ambao kuna mapungufu katika akili yao au hoja haikuwafikia, hawatakumbwa na hatima ya kubakia milele motoni.[35]

Kwa mujibu wa wanateolojia wa Kishia, muumini aliyefanya dhambi kubwa anastahili malipo ya kudumu kutokana na imani yake. Kwa sababu katika Aya ya 7 ya Surat Zilzal, hata tendo jema dogo hulipwa, na imani ni tendo jema kubwa zaidi, na kwa kuwa malipo ya imani ni malipo ya milele, basi mtu kama huyo lazima kwanza aadhibiwe na kisha apate malipo ya milele peponi. [36]

Adhabu ya Milele na Rehema ya Mwenyezi Mungu

Kundi la wanazuoni wa Kiislamu ambao wana utendaji wa kifalsafa na kiirfani zaidi na wanapinga adhabu ya milele na kudumu ndani ya moto wa jahanamu, [37] wanaona kuwa, adhabu ya milele haiafikiani na rehema ya Mwenyezi Mungu.[38]

Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa Allama Tabatabai, mfasiri na mwanafalsafa wa Kishia, rehema ya Mungu haimaanishi huruma ya moyo, hisia za huruma na kuguswa na jambo; kwa sababu hali hizi ni sifa za wanadamu wa kimaada; badala yake, rehema humaanisha kutoa kitu kinacholingana na kipaji cha mtu.[39]

Kwa mujibu wa Ibn Arabi, maumbile ya baadhi ya watu yameumbwa kwa rehema na huruma, na lau Mwenyezi Mungu angewaruhusu kusimamia na kutawala mambo ya waja wake, wangeondoa mateso na adhabu duniani. Sasa, Mungu ambaye amewapa baadhi ya watumishi wake ukamilifu huo, bila shaka Yeye anastahili zaidi na anaweza kuondoa kabisa adhabu hiyo. Mwenyezi Mungu amejitaja kwa sifa ya kuwa ni Mwingi wa rehema kwa waja wake.[40]

Adhabu ya Milele na Uadilifu na Hekima ya Mwenyezi Mungu

Baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu wanaona adhabu ya milele inapingana na uadilifu wa Mwenyezi Mungu na wamezusha swali hili kwamba, kwa nini mtu ambaye amefanya dhambi kwa muda mfupi katika ulimwengu huu aungue milele motoni?[41]

Wanafikra wengine pia wamezungumza kuhusu kupingana kwa adhabu ya milele na hekima ya Mwenyezi Mungu[42] na wamedai kwamba, kumuumba kiumbe ambacho kitakuja kukaa katika adhabu ya milele si jambo la hekima.[43]

Kubainisha Adhabu ya Milele na Mfanisho wa Matendo

Baadhi ya wanazuoni wa kidini wanaamini kwamba utangamano wa adhabu ya milele na uadilifu wa Mwenyezi Mungu unawezekana tu kupitia nadharia ya mfananisho wa matendo.[44] Kwa mujibu wao, kutooana kwa adhabu na uadilifu chimbuko lake ni imani ya adhabu ya kimkataba na ya kiitibari; kwa sababu kuzijua adhabu za akhera kama ni za kimkataba huandaa uwanja wa maswali juu ya uwezekano wa adhabu ya milele, na haiwezekani kuuchukulia kuwa ni msukumo wa kiakili kwa ajili ya adhabu ya milele.[45] Ni kwa sababu hii, ndio maana kundi miongoni mwao limeshikamana na nadharia ya ufananisho wa matendo. [46] Katika upande mwingine, wametilia ishkali kwamba, nadharia ya mfananisho wa matendo inaweza kwa kiwango cha juu zaidi kuthibitisha uwezekano wa kubakia milele katika moto wa jahanamu na sio kuwa na uhakika wa mia kwa mia kuhusiana na hilo.[47]

Kuhusiana na hili, Allamah Tabatabai anaeleza kuwa, adhabu ya milele imetokana na msingi wa falsafa ya Hikmat Mutaaaliyah. Yeye anaamini kwamba ikiwa nyuso mbaya hazitaunganishwa na nafsi ya mwanadamu, nafsi itaachiliwa baada ya muda wa mateso yenye mipaka; lakini ikiwa dhambi zimekuwa sehemu ya nafsi yake, na nafsi ikajiingiza katika dhambi bila shinikizo lolote na kuridhika na dhambi, atabakia katika adhabu ya milele.[48]

Rejea

Vyanzo