Maisha ya amani ya pamoja
Maisha ya amani ya pamoja: ni dhana inayobeba umuhimu wa kuishi kwa maelewano na mshikamano miongoni mwa watu wa imani, itikadi, na tamaduni tofauti. Dhana hii katika Uislamu, inahisabiwa kuwa ni moja ya msingi bora ya jamii na ndio lengo la juu kabisa la maisha ya kijamii. Dini ya Kiislamu inahimiza kuheshimu haki za walio wachache kidini, pia inawataka Waislamu kushirikiana nao kwa misingi ya heshima na uadilifu. Mafundisho ya Kiislamu yanasisitiza umuhimu wa kujenga maelewano baina ya watu, kuondoa mifarakano, na kudumisha mshikamano wa kibinadamu kwa ajili ya amani na ustawi wa kijamii.
Sheria kuhusianana na Ahlu al-dhimma (wasio Waislamu waishiwo ndani ya nchi za Kiislamu kulingana na kanuni za Kiislamu) katika fiqhi ya Kiislamu, zinachukuliwa kuwa ni msingi muhimu wa kuimarisha mazingira ya kuishi pamoja kwa amani kati ya makundi ya kidini madogo na Waislamu. Mikataba ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na makabila mbalimbali, pamoja na utekelezaji wa ahadi za mikataba hiyo, ni mfano wa wazi wa mwenendo wa bwana Mtume (s.a.w.w) katika kukuza amani na mshikamano wa kijamii.
Kuna mifano mingi katika maisha (sira) nyenendo za Ahlul-Bait (a.s), zinazoonesha umuhimu wa kuishi kwa amani na watu wenye imani tofauti. Mifano hii ni pamoja na kuheshimu mambo yanayohisabiwa kuwa matakatifu na watu wa dini nyingine, kuvumilia mitazamo ya watu wengine, kutowatusi wafuasi wa dini na madhehebu mengine, na kushirikiana na wasio Mashia katika mambo mbali mbali ya kijamii. Mambo haya yote yanaonesha jitihada za Ahlul-Bait (a.s) katika kukuza utangamano na mshikamano ndani ya jamii. Hata hivyo, imeelezwa kuwa; Kwa mtazamo wa Ahlul-Bait (a.s), kuishi pamoja kwa amani na wumini wa imani mbali mbali, kunahitaji kutekelezwa kulingana na misingi ya kidini.
Maana na Hadhi ya Kuishi Pamoja kwa Amani
Kuishi pamoja kwa amani kumetafsiriwa kwa maana ya kule watu wa watu wa jamii moja, licha ya tofauti za imani na dini zao, ila bado kuendelea kuishi kwa utulivu na kushirikiana kwa upendo, huku wakitatua tofauti zao kwa njia za amani na maelewano. [1] Aina hii ya maisha ya pamoja kati ya wanadamu ni njia inayozingatia umuhimu wa mshikamano wa kijamii bila kujali ukweli au usahihi wa madhehebu na mitazamo yao. Lengo kuu ni kufanikisha maisha ya kijamii yaliyojaa amani na kutambua haki za kijamii za kila mmoja kati yao. [2]
Kwa mujibu wa maelezo ya Ja'far Subhani, ni kwamba; Kuishi pamoja kwa amani ni mojawapo ya sababu zilizosababisha kujadiliwa kwa wazo la wingi wa dini (pluralism), au uwepo wa haki zaidi ya moja, ambalo liliibuka baada ya vita vikali vya kimadhehebu na kidini. [3]
Aidha, baadhi ya wanazuoni wanahusisha suala hili na dhana ya mwanadamu kuwa na maisha kijamii, wakisema kuwa msingi wa kuishi kijamii umesimama juu ya kuishi pamoja kwa amani, na kwa kushirikiana bila ya ubaguzi wa dini au madhehebu. [4]
Kuishi Pamoja kwa Amani katika Jamii kwa Mtazamo wa Uislamu
Amani na kuishi kwa maelewano kati ya watu wa imani na dini mbalimbali, ni moja kati ya rasilimali yenye thamani muhimu na ni miongoni mwa malengo makuu ya Uislamu.[5] Katika mafundisho ya Kiislamu, kundi pekee lililowekwa nje ya kanuni za kuishi kwa pamoja kwa amani, ni kundi la wale wanaoshiriki katika uadui na uvamizi dhidi ya haki za wanadamu. Kundi amabo kiuhalisia linatakiwa kupigwa viti, hii ni kwakuwa wao ndio kikwazo cha kupatikana amani katika jamii. [6] Zaidi ya hayo, maisha ya kuvumiliana katika muktadha wa Kiislamu yametajwa kama ndio msingi muhimu wa kuishi pamoja kwa amani. [7]
Kulingana na watafiti mbalimbali, miongoni mwa nyenzo zinazopelekea kuishi pamoja kwa amani katika Uislamu ni pamoja na:
1. Usawa wa Wanadamu - Uislamu unasisitiza kwamba wanadamu wote ni sawa, bila kujali rangi, jinsia, au hali ya kijamii.[8]
2. Kuwatambua au kwakubali Mitume - Uislamu unatambua mitume waliotumwa kwa mataifa mbalimbali na umuhimu wa mafundisho yao kwa jamii zote.
3. Kupambana na Udanganyifu wa Ukuu wa Kidini - Uislamu unakataa dhana ya ubaguzi wa kidini na kuhimiza usawa wa kibinadamu. [9]
4. Kufanya Mazungumzo na Wapinzani - Uislamu unahimiza mazungumzo yenye maelewano na wale wenye mitazamo tofauti ili kuimarisha maelewano ya kijamii.
5. Wito wa Kushirikia Katika Yahusishayo Itikadi za Pamoja- Uislamu unahimiza ushirikiano kwenye masuala yenye uwiano wa kiitikadi baina ya Waislamu na wasio Waislamu.
6. Uhuru wa Dini na Imani – Uislamu unachunga na kusisitiza haki ya mtu kuchagua na kufuata dini au madhehebu fulani bila kulazimishwa.
7. Heshima ya Asili ya Binadamu - Uislamu unasimamia heshima ya binadamu kama kiumbe aliyeheshimiwa na mwenye haki za kimsingi.
Pia, Usilamu unazhimiza amani, haki, na hisani kwa wapinzani. [10]
Zaidi ya hayo, kukubali haki za dini ndogo ndogo [11] na kuamiliana kwa heshima na wasio Waislamu [12] ni miongoni mwa kanuni za msingi za kuishi pamoja kwa amani katika Uislamu. [13]
Katika fiq’hi ya Kiislamu, mijadala inayohusiana na dini ndogo ndogo hufanyika chini ya dhana ya hukumu za Ahl al-Dhimma [14] Dhana hii inarejelea haki na sharia zinazohusiana na wale wanaoishi chini ya utawala wa Kiislamu lakini wao wenyewe si wafuasi wa dini ya Kiislamu. Imeelezwa kwamba; falsafa ya sheria hizi ni kuhakikisha kuwepo kwa mazingira ya kuishi pamoja kwa amani kati ya dini ndogo ndogo na Waislamu. [15]
Zaidi ya hayo, kanuni ya wajibu wa kuheshimu mikataba na ahadi katika sheria za Kiislamu imetajwa kama ni moja ya nyaraka muhimu zinazoimarisha kuishi pamoja kwa amani kati ya dini tofauti. [16]
Maisha ya Maasumina Katika Kuamiliana na Wasiokuwa Waislamu
Amani na kuishi kwa utulivu kati ya wanadamu ni miongoni mwa malengo makuu ya Mitume ya Mwenye Ezi Mungu, hususan Mtume Muhammad (s.a.w.w). [18]
Katika Sira (nyenendo) za Mtume Muhammad (s.a.w.e), kuna mifano mbalimbali yenye kuthibitisha kuishi pamoja kwa amani. Mifano hii inajumuisha:
1. Uvumilivu na tabia ya amani dhidi ya wapinzani: Bwaba Mtume (s.a.w.w) aliamiliana na wale waliopingana naye kwa njia ya mamani na uvumilivu, akionyesha tabia bora ya Kiislamu katika maingiliano yake na watu wa imani tofauti au wapinzani wa ujumbe wake. [19]
2. Mwaliko na wito kwa wafuasi wa dini za tauhidi kwa ajili ya umoja: Kama ilivyoainishwa katika Qur'ani Tukufu, bwana Mtume (s.a.w.w) aliwalingania Mayahudi, Wakristo, na wafuasi wa dini nyengine za tauhidi kushikamana na msingi ya kumuabudu Mwenye Ezi Mungu mmoja bila ushirikina. [20]
3. Mikataba ya amani na makabila mengine pamoja na uaminifu kwa makubaliano hayo: Mtume (s.a.w.) alianzisha mikataba ya amani na makabila tofauti, [21] akisisitiza kuheshimu makubaliano hayo kwa manufaa ya pande zote. [22] [23]
Sunna ya Mtume (s.a.w.w) Katika Kuamiliana na Watu wa Kitabu (Ahlulkitab)
Miongoni mwa Sunna za Mtume Muhammad (s.a.w.w), katika kuamiliana na Watu wa Kitabu (yaani, Mayahudi na Wakristo) ilikuwa ni kuamiliana nao kwa njia ya amani na haki. Mtume (s.a.w.w) alionyesha mfano wa maadili ya juu katika kuamiliana na Watu wa Kitabu, kwa kutekeleza mambo yafuatayo:
· Kuwalinda Watu wa Kitabu dhidi ya uvamizi wa nje na dhuluma za ndani: Mtume alihakikisha usalama wa Watu wa Kitabu waliokuwa chini ya himaya ya serikali ya Kiislamu dhidi ya mashambulizi ya nje na ukandamizaji wa ndani.
· Kuruhusu ndoa kati ya mwanaume Mwislamu na wanawake wema kutoka upande wa Watu wa Kitabu: Sheria za Kiislamu, kwa kuongozwa na fafanuzi Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w), zinaruhusu ndoa ya aina hii kama ni ishara ya kutambua heshima yao.
· Haki ya Watu wa Kitabu ya kimakazi na ajira: Mtume (s.a.w.) aliwahakikishia Watu wa Kitabu nafasi za kuishi na kufanya kazi katika ardhi za Kiislamu bila kuwanyimwa haki zao.
· Kupokea ushahidi wao na kuwaamini: Ushahidi wa Watu wa Kitabu ulitambuliwa katika mahakama za Kiislamu pamoja na kukubaliana na ushahidi wao, hii ni kwa ajili ya kuonesha uadilifu katika mfumo wa sheria.
· Heshima kwa Watu wa Kitabu: Mtume (s.a.w.) aliamiliana na Watu wa Kitabu kwa heshima, ikiwa ni pamoja na kuwajulia hali wanapokuwa wagonjwa, kuwa jirani mwema kwao, na kuwapa sadaka.
· Kuhakikisha haki na usawa kwa Ahl al-Dhimma: Mtume alisisitiza umuhimu wa kuwahudumia watu wa dhimmi kwa haki, bila ubaguzi wa kidini au kijamii.
· Uhuru wa kidini kwa Watu wa Kitabu: Mtume (s.a.w.) aliheshimu haki za Watu wa Kitabu kuendelea kufuata dini zao bila kulazimishwa kubadili imani zao. [24]
Sunna (Nyenendo) za Ahlul-Bait (a.s) Kuhusiana na Kuishi pamoja kwa Amani
Katika sira (nyenendo) za Ahlul-Bait (a.s), kuna mafunzo muhimu yanayosisitiza umuhimu wa umoja na kuishi kwa amani kati ya Waislamu na jamii zinazofuata dini mbali mbali. Mambo muhimu yaliyoangaziwa katika maadili yao ni pamoja na:
· Kuheshima Mambo Matakatifu ya Wengine Pamoja na Kuvumilia Mitazamo Tofauti:
Ahlul-Bait (a.s) walihimiza kuheshimu imani na itikadi za wengine, hata zile zinazotofautiana na zile za Uislamu. Kuvumiliana huku kulikuza maelewano kati ya watu wa imani mbalimbali. [25]
· Subira na Wema kwa Watu Wote:
Walionyesha uvumilivu na tabia njema kwa kila mtu, wakisisitiza tabia ya kuepuka matusi au dharau kwa wafuasi wa dini na madhehebu mengine. [26]
· Kushiriki katika Masuala ya Kijamii na Kidini:
Ahlul-Bait (a.s) walishiriki na watu wa kidini tofauti katika shughuli mbali mbali za kijamii, wakionyesha umuhimu wa mshikamano wa kijamii katika kujenga amani.
· Mahusiano Mazuri na Wapinzani:
Ahlul-Bait (a.s) walihimiza urafiki na maelewano hata na wale waliokuwa na mitazamo ya upinzani, tende lenye kuonesha kwamba; maelewano ya kijamii yanaweza kufanikishwa bila chuki.
· Kusamehe Makosa na Kuficha Dosari za Wengine:
Ahlul-Bait (a.s) walifundisha umuhimu wa kuwa na moyo wa kusamehe na kuepuka kuanika mapungufu ya wengine hadharani. [27]
· Kujali masuala ya Waislamu na Kutilia Mkazo Suala la Kujenga Amani:
Ahlul-Bait (a.s) walisisitiza umuhimu wa kujali maslahi ya Waislamu wote kwa jumla na kuwapa ushauri wa kujenga amani.
· Kuwajulia Hali Wagonjwa wa Upande wa Wazinzani na Kuepukana na Ubaguzi wa Kikabila:
Ahlul-Bait (a.s) walihimiza amani na kupinga kwa nguvu zote aina yoyote ya ubaguzi wa kikabila au upendeleo wa kimaumbile. [28]
Imeripotiwa kuwa; mtazamo wa Ahlul-Bait (a.s) kuhusiana na kuishi kwa amani unahusisha uzingatiaji wa misingi ya kidini katika utendaji wa suala hili. Misingi ambayo lengo lake ni kudumisha maelewano huku ikiimarisha imani sahihi ya mtu. Wakati wa kuishi kwa mshikamano na watu wa imani tofauti, Ahlul-Bait walihakikisha kuwa imani msingi za Kiislamu haziathiriwi na mahusiano ya amani ya dini na madhehebu mbali mbali. [29]
Mfano wa Sira (Nyenendo) za Imamu Ja'far al-Sadiq (a.s.):
Moja ya mifano dhahiri ya sira ya Ahlul-Bait (a.s) juu ya kuishi kwa amani, ni jinsi Imamu Ja'far al-Sadiq (a.s) alivyoamiliana na watu wenye mitazamo tofauti, wakiwemo walimu wa fikra za kipagani na washirikina. Tabia yake ilijikita katika:
1. Hekima na Subira:
Katika kukabiliana na wapinzani, Imam alionyesha hekima na subira. Badala ya kuonesha hasira au chuki, alihimiza mazungumzo yenye lengo la kuelewana na kushughulikia changamoto za kiitikadi.
2. Majadiliano ya Kielimu na Kimantiki:
Imam alijishughulisha na mazungumzo ya kina na wapinzani wake, akitumia hoja za kimantiki na kielimu kubainisha ukweli wa imani ya Kiislamu.
3. Kuepuka Ukatili:
Licha ya kukutana na upinzani mkali, Imamu katika majadiliani yake aliendeleza mazungumzo yake kwa heshima huku akiiepuka kabisa kutumia njia za ukatili au matusi. [30]
Maisha ya Amani ya Pamoja Katika Mahusiano ya Kimataifa na Msisitizo wa Uislamu Juu Yake
Abbas Ali Amidi Zanjani, mtaalamu maarufu wa sheria za Kishia, amlihisabu suala la kuishi kwa amani kati ya mataifa kuwa ni miongoni mwa kanuni msingi za Uislamu zinazohusiana na mahusiano ya kimataifa. [31] Yeye amesisitiza kwamba; msingi wa kuishi kwa amani katika siasa za kimataifa ni miongoni mwa mikakati muhimu zaidi ya kisasa iliyo tekelezwa na Uislamu, [32] na ndiyo chanzo msingi cha kinachopelekea upendo na urafiki baina na wenyeji na wageni. [33]
Kwa kuzingatia mwelekeo wa vitendo vya Ma’sumina (a.s), ianabainika kwamba; Kanuni kuu katika siasa za nje za Uislamu ni amani na kuishi kwa kustahamiliana. [34] Imeripotiwa kwamba; Kulingana na mtazamo wa Imamu Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, uhusiano wa amani na ushirikiano kati ya mataifa mbali mbali, ni kanuni muhimu inayopaswa kuzingatiwa katika siasa za kimataifa. [35]
Biliografia
Kuna vitabu kadhaa vilivyoandikwa kuhusiana na mada ya kuishi pamoja kwa amani, miongoni mwavyo ni:
1. Islam wa Hamzisti Musalimat-omiz (Islam na Kuishi Pamoja kwa Amani), kazi ya Abbasali Amidi Zanjani, Chapa ya Tehran, Dar al-Kutub al-Islamiyya, mwaka 1344 Shamsia.
2. Hamzisti Musalimat-omiz dar Islam wa Huquqe Baina Milali (Kuishi Pamoja kwa Amani katika Uislamu na Sheria za Kimataifa), kazi ya Mohammad Mahdi Karimi Nia, Chapa ya Taasisi ya Elimu na Utafiti ya Imamu Khomeini (RA), mwaka 1387 Shamsia.
3. Islam wa Hmzisti Musalimat-omiz (Islam na Kuishi Pamoja kwa Amani), kazi ya Ali Akbar Alikhani, Chapa ya Be-Afarin, mwaka 1392 Shamsia.