Nenda kwa yaliyomo

Kuuawa Malik ibn Nuwayrah

Kutoka wikishia
Makala inahusiana na kuuawa Malik bin Nuwayrah. Ili kujua kuhusu mtu mwenye jina hili soma makala ya Malik bin Nuwayrah.

Kuuawa kwa Malik bin Nuwayrah (Kiarabu: قَتل مَالك بن نُويرة) ni moja ya matukio yalitokea katika zama za ukhalifa wa Abu Bakr, ambapo Malik bin Nuwayrah, mmoja wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w), aliuawa na Khalid bin Walid, na ikawa moja ya changamoto za kiteolojia baina ya Mashia na Masunni. Shia kwa kuamini upotovu wa kimaadili wa Khalid na kufanya mauaji haya, wameikosoa nadharia ya uadilifu ya Masahaba. Kwa mujibu wa watafiti wa Kishia, Malik alikataa kutoa Zaka kwa serikali kutokana na kutotambua uhalali wa ukhalifa wa Abu Bakr, na hii ndiyo iliyokuwa sababu ya kuuawa kwake.

Baadhi ya waandishi wa Kisunni wamemchukulia Malik kama murtadi ili kuhalalisha kitendo chaa Khalid bin Walid. Lakini Mashia na baadhi ya Masunni wamekanusha kuritadi kwake wakitumia ushahidi wa masahaba kadhaa kuhusu Uislamu wake na kutolewa dia ya Malik na Abu Bakr. Kama ambavyo Omar bin Khattab alimchukulia Khalid bin Walid kuwa anastahili kutekelezwa adhabu ya kisasi kwa kosa la kumuua Malik, na kustahili kupigwa mawe kwa kosa la kulala na mkewe. Kwa upande mwingine, Abu Bakr alimchukulia Khalid kuwa alikuwa na udhuru katika ijtihadi yake.

Malik bin Nuwayrah alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa katika zama za ujahilia na Uislamu, ambaye alisilimu wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w.w). Baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w), Malik alimpinga Abu Bakr kwamba, kwa nini hakumuachia ukhalifa Imam Ali (a.s) kwa mujibu wa kauli ya Mtume (s.a.w.w). Sheikh Abbas Qomi anaamini kwamba Malik aliuawa kwa sababu ya mapenzi yake kwa Ahlul-Bayt (a.s).

Vitabu kadhaa vimeandikwa kuhusu kuuawa kwa Malik bin Nuwayrah. Miongoni mwavyo ni «Majaraye-Qatl Malik bin Nuwayrah» (Tukio la Kuuawa Malik bin Nuwayrah) kilichoandikwa na Ali Labbaf.

Umuhimu wa Tukio Hili katika Mijadala ya Kiteolojia

Tukio la mauaji ya Malik bin Nuwayrah ni moja ya masuala yenye changamoto za kiteolojia (kiitikadi) miongoni mwa Fariqain (Masuni na Mashia). [1] Kuuawa kwa Malik na Khalid bin Walid na ndoa yake na mke wa Malik kunachukuliwa kuwa ni moja ya matukio yenye utata zaidi kuhusiana na Vita vya Riddah. [2] Wahakiki wa Kishia wakitegemea tukio hili la kihistoria, wameikosoa nadharia ya Waislamu wa Kisuni kwamba, masahaba wote ni waadilifu na wanaamini kwamba nadharia hii ililetwa ili kuhalalisha baadhi ya tabia na vitendo visivyofaa vya Maswahaba vilivyofanywa katika Vita vya Riddah. [3] Kwa mujibu wa Maqdisi, mwandishi wa historia wa karne ya nne Hijria ni kwamba, baada ya suala la Uimamu, hitilafu za Waislamu zilidhihirika katika Vita vya Riddah, ingawa Abu Bakr aliamini kwamba alipaswa kupigana vita na Ahl Riddah (watu walioritadi) lakini Waislamu walikuwa walipingana naye. [4]

Shia na baadhi ya Sunni wanaona kuwa, madai ya kuritadi Malik bin Nuwayrah hayana ukweli na wanamtambua kuwa ni Mwislamu. [5] Ushahidi wa masahaba kadhaa kuhusu Uislamu wake, hatua ya Abu Bakr ya kulipa dia ya Malik, na amri yake kutenganishwa Khalid na mke wa Malik ni miongoni mwa hoja zao. [6] Hata hivyo, Masunni hawana maoni sawa juu ya kuwa kwake Mwislamu, na wengine wamemchukulia kama murtadi (aliyetoka katika Uislamu). [7] Muhammad Hussein Heikal, akiwa na lengo la kuhalalisha kitendo cha Khalid, anaamini kwamba, kuuawa kwa Malik na kufanya kwake mapenzi na mke wa Malik ni suala dogo ikilinganishwa na huduma zake nyingi alizotoa kwa serikali ya wakati huo. [8]

Malik bin Nuwayrah

Makala kuu: Malik bin Nuwayrah

Malik bin Nuwayra bin Jamrah Tamimi alikuwa mmoja wa maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na mmoja wa shakhsia wakubwa katika zama za ujahilia na Uislamu. [9] Malik alikuwa mshairi na alikuwa na diwani ya mashairi. Alikwenda kwa Mtume (s.a.w.w) na kusilimu. [11] Mtume akamfanya mwakilishi wake katika kabila lake ili kukusanya Zaka kutoka kwao. [12]

Kwa mujibu wa Sheikh Abbas Qomi, mmoja wa wanachuoni wa hadithi wa Kishia, katika karne ya 14 Hijria ni kwamba, Malik bin Nuwayrah aliuawa kwa sababu ya mapenzi yake kwa Ahlul-Bayt (a.s). [13] Kwa mujibu wa nukuu ya Fadhl bin Shadhan ni kuwa, baada ya kuaga dunia Bwana Mtume (s.a.w.w), Malik alikwenda Madina na alipotambua kwamba, Abu Bakr ndiye Khalifa alimpinga na kuhoji kwa nini hakuacha ukhalifa kwa Imam Ali (a.s) kwa mujibu wa maagizo ya Mtume (s.a.w.w). [14]

Kuuawa Malik bin Nuwayrah katika Vita vya Riddah

Allamah Amini [15] na Rasul Jafarian, [16] miongoni mwa wanahistoria wa Kishia wanasema kuwa, hapana shaka yoyote kwamba, Malik bin Nuwayrah aliuawa kutokana na upotovu wa kimaadili wa Khalid bin Walid. Malik alikataa kutoa Zaka kwa serikali ya Abu Bakr na badala yake akaigawanya miongoni mwa watu wake. [17] Kwa mujibu wa Sayyid Abdul-Hussein Sharafuddin, mwandishi wa kitabu cha Al-Nas Wal-Ijtihad ni kwamba, Malik alikataa kutoa Zaka kutokana na kutilia kwake shaka uhalali wa ukhalifa wa Abu Bakr na usahihi wa kumpa Zaka. [18]

Khalid bin Walid alikwenda kukabiliana na kuritadi kwa Malik na kabila lake katika eneo la Butah kwa amri ya Abu Bakr. [19] Abu Bakr alikuwa ametoa amri ya kufanyiwa tathmini na uchunguzi wa watu hao juu ya kufungamana kwao na Sala kabla ya kuanza vita ili upatikane ukweli kuhusiana na kuritadi kwao. [20] Malik, ambaye alikuwa na habari ya ujio wa Khalid, akiwa na lengo la kuonyesha nia yake njema na kuzuia udanganyifu kwamba wameandaa jeshi, alitawanya mkusanyiko wa watu wa kabila lake, ili wasidhaniwe kuwa wako vitani. [21] Baadhi ya Maansari ambao waliona kufungamana Malik na kabila lake na suala la Sala, walimpinga Khalid bin Walid, lakini Khalid hakuwajali. [22]

Ili kuthibitisha kwamba hawakuritadi, Malik alikuja kwa Khalid pamoja na mkewe, Ummu Tamim, lakini Khalid alipomuona mkewe, ambaye alikuwa mwanamke mrembo, akamuua Malik, na usiku uleule akalala na mke wa Malik, ambaye alikuwa katika eda ya kifo cha mumewe. [23] Kulingana na ripoti ya Ya’qubi mwanahistoria wa karne ya tatu, Khalid alipomuona Ummu Tamim alisema, "Naapa kwa Mungu, sitapata ulicho nacho isipokuwa kwa kukuua tu. Hivyo akamuua Malik. [24] Kwa mujibu wa ripoti ya Waqidi, mwanahistoria wa karne ya Pili Hijria, muda mrefu kabla Khalid alikuwa akimtamani Ummu Tamim. Malik naye kabla ya kuuawa, alisema na kueleza sababu ya Khalid kumuua ni kuwa ni uzuri wa mke wake. [25] Kifo chake kimetajwa katika matukio ya mwaka 11 Hijria. [26]

Masahaba Walalamikia Kuuawa Malik

Vitendo vya Khalid dhidi ya sheria viliibua malalamiko ya baadhi ya masahaba, kama vile Abu Qatadah Ansari na Abdullah bin Omar. [27] Baada ya taarifa ya jeshi la Khalid kufika Madina, Omar Ibn Khattab alijadiliana Abu Bakr kuhusu vitendo vya Khalid dhidi ya sheria na akamtaka amuuluzu kutoka katika cheo cha kamanda wa jeshi. [28] Omar bin Khattab alimchukulia Khalid bin Walid kuwa anastahili kutekelezwa adhabu ya kisasi kwa kosa la kumuua Malik na kustahili kupigwa mawe kwa kosa la kulala na mkewe. [29] Lakini Abu Bakr alikataa ombi la Omar na alimchukulia Khalid kuwa alikuwa na udhuru katika ijtihadi yake. [30] Alimtambua Khalid kama mmoja wa panga za Mwenyezi Mungu zilizotolewa dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu. [31]

Baada ya Mutammim bin Nuwayrah kaka yake Malik, kwenda kwa Abu Bakr kuomba kisasi cha damu ya kaka yake, Abu Bakr aliamuru dia ya Malik ilipwe kutoka kwa Beit al-Mal (Hazina ya Dola). [32] Pia alimuamuru Khalid kumpa talaka mke wa Malik, lakini Khalid kamwe hakutii amri hiyo ya Abu Bakr. [33] Kwa mujibu wa Muhammad Hussein Heikal, mwanahistoria wa Misri, kwa vile Abu Bakr alimhitaji Khalid katika serikali yake, aliendelea kumwajiri. [34] Lakini Omar hakusahau kosa lake na ndio maana baada ya kifo cha Abu Bakr na yeye kuwa Khalifa alimuondoa Khalid katika wadhifa wa kamanda wa jeshi. [35]

Monografia

Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa kuhusiana na kuuawa Malik bin Nuwayrah ni:

  • «Majaraye Qatl Malik bin Nuwayrah», (Tukio la Kuuawa Malik bin Nuwayrah) kilichoandikwa na Ali Labbaf. Maudhui ya kitabu hiki yamechukuliwa kutoka katika athari za Sayyid Murtadha Askari na kusambazwa na Taasisi ya Uchapishaji ya Munir Tehran mwaka 2013. [36]
  • «Pezhuheshi Dar Hayat Siyasi Va Mobarezati Malik bin Nuwayrah», mwandishi Hassan Ali Purvahid. Kitabu hiki kilichapishwa na Taasisi ya Uchapishaji ya Kiislamu mwaka 2017 kikiwa na kurasa 685. [37]
  • «Malik bin Nuwayrah», ni athari nyingine ya Hassan Ali Purvahid. Katika kitabu hiki mwandishi anafanya uchunguzi wa tukio linalohusiana na Malik kwa njia ya tathmini. [38] Kitabu hiki kimesambazwa na Taasisi ya Uchapishaji ya Dalil Ma mwaka 2023 kikiwa na kurasa 616. [39]

Rejea

Vyanzo