Kutub al-Ar’baa (Vitabu Vinne)

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Kutubu al-ar'baa)

Kutub al-Ar’baa (Vitabu Vinne) au Usul al-Ar’baa (Kiarabu: الكتب الأربعة) ni Vitabu Vinne vya hadithi vya Waislamu wa Madhehebu ya Kishia. Mashia wanavitambua vitabu hivyo kuwa ndio vitabu vyao muhimu na vyanzo vyenye itibari katika hadithi. Vitabu hivyo ni: al-Kafi, Man Laa Yahdhurun al-Faqih, Tahdhib al-Ahkam na al-Istibsar. Kitabu al-Kafi kimeandikwa na Sheikh Kulayni huku kitabu cha Man Laa Yahdhurun al-Faqih mwandishi wake akiwa ni Sheikh Swaduq. Ama vitabu viwili vilivyobakia vinavyokamilisha orodha ya Kutub al-Ar’baa ambavyo ni Tahdhib al-Ahkam na al-Istibsar vimeanmdikwa na Sheikh Tusi.

Shahidi Thani ndiye kwa mara ya kwanxza alitumia istilahi ya Kutub al-Ar’baa akiashiria vitabu hivi tulivyotaja wakati alipopata idhini ya kunukuu hadithi. Baada ya hapo, istilahi hii ikawa inatumika katika maandiko ya Fiqihi na hatua kwa hatua ikaenea. Baadhi ya Maulamaa wa Kishia wanaamini kwamba, hadithi zote zilizoko katika vitabu hivi vine (Kutub al-Ar’baa) zina itibari; hata hivyo akthari ya wanazuoni wa Kishia wanazikubali lile kundi la hadithi ambazo ni mutawatir (mapokezi yake yamekuwa mengi) au zenye sanadi na mapokezi yenye itibari (ya kuaminika).

Nafasi

Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanaamini kuwa, vitabu vine vya al-Kafi, Man Laa Yahdhurun al-Faqih, Tahdhib al-Ahkam na al-Istibsar ndio vitabu vyao muhimu na vyanzo vyao vyenye itibari (kuaminika) katika hadithi na wanaviita kwa jina la Kutub al-Ar’baa ambavyo kiisitilahi vinajulikana kama Vitabu Vinne vya Hadithi. Akthari ya wanazuoni na Maulamaa wa Kishia hawaoni kama ni wajibu kuzifanyia kazi hadithi zote zilizokuja katika vitabu hivyo bali ili kuzifanyia kazi hadithi hizo kuna haja ya kuzifanyia uchunguzi kuhusu sanadi na mapokezi yake.

Chimbuko la Istilahi ya Kutub al-Ar’baa

Shahidi Thani ndiye alimu na msomi wa kwanza ambaye aliitumia istilahi ya Kutub al Hadith al-Ar’baa. Ilikuwa mwaka 950 Hijria wakati alipopata ijaza (idhini) ya kunukuu hadithi. Kisha baadaye katika ijada kadhaa nyingine za kunukuu aliitumia ibara hii na ibara ya al-Kutub al-Ar’baa. Baada ya takriban miongo mitatu kuanzia wakati huo, Muhaqqiq Ardebili akaitumia istilahi hii katika kitabu chake cha fiqih cha Maj’amau al-Faidah Wal-Burhan ambacho alianza kukiandika mwaka 977 Hijria na kukikamilisha mwaka 985 Hijria. Na kwa muktadha huo, istilahi hii ikawa imetoka katika anga ya hadithi na kuingia katika vitabu vya Fiqih. Baada ya hapo ikatumika katika vitabu vya Zubdatul Bayan (kilichoandika mwaka 989 Hijria na Muntaqaa al-Juman (kilichoandikwa mwaka 1006 Hijria) na Al-Wafiyah (kilichoandikwa mwaka 1059 Hijria) kwa utaratibu.

Itibari ya Kutub al-Ar’baa

Mafakihi (wanazuoni wa elimu ya fikihi) wa Kishia wamekubali itibari jumla ya vitabu hivi vine vya hadithi. Sheikh Ansari hakuna kama ni jambo lililo mbali kwamba, kuamini itibari vitabu mashuhuri vikiwemo vitabu hivi vine vya hadithi ni katika dharura za madhehebu. Pamnoja na hayo, miongoni mwa wasomi na wanazuoni wa Kishia wametofautiana kuhusiana na kauli moja au kutokuweko na kauli moja na kasha baada ya hapo wametofautiana kuhusiana na itibari na usahihi wa hadithi zote zilizopo ndani ya vitabu hivi. Kuhusiana na hili, tunaweza kuashiria mitazamo mitatu:

  • Kusema kwa uhakika (bila shaka) na itibari ya hadithi zote: Akhbariyuun wanaamini kwamba, hadithi zote zilizoko katika vitabu vya Kutub al-Ar’baa zina itibari na ni za kuaminika na wanaamini kwamba, ni jambo lisilo na shaka kuzinasibisha hadithi hizi na Maasumina. Mtazamo wa Sayyid Murtadha unakaribiana na wa Akhbariyuun. Yeye anaamini kwamba, akthari ya hadithi za vitabu hivi ni mutawatir au za kutolea kauli moja na ya uhakika (bila shaka).
  • Usahihi wa Hadithi Zote na kutotolea kauli moja na ya uhakika (bila shaka): Baadhi ya wanazuoni wa Fiqih kama Fadhil Toni , Mullah Ahmad Naraqi na Mirza Muhammad Hussein Naini hawajakubaliana na kutolea kauli moja na ya uhakika (bila shaka) juu ya hadithi zote zilizoko katika vitabu hivi vinne ingawa wameafiki itibari ya hadithi zake.
  • Akhtari ya hadithi hizo ni dhana na hoja kwa zile hadithi zenye sanadi: Mtazamo ulioenea baina ya mafaqihi Usuliyuun wa Kishia ni kwamba, ukiondoa hadithi chache ambazo ni mutawatir, hadithi nyingine katika kitabu cha al-Kafi ni dhana na hoja ni kwa zile hadithi ambazo kwa upande wa sanadi na mapokezi zimetimiza masharti. Licha ya kuwa, kuna hitilafu kuhusiana na masharti ya itibari ya hadithi.

Kitabu cha al-Kafi

Kitabu hiki kimeandika katika zama za Ghaibat Sughra (Ghaiba Ndogo ya Imam Mahdi). Mwandishi wake ni Sheikh Abu Ja’afar Kulayni (aliyeaga dunia 329 Hijria). Kitabu hiki kina takribani hadithi 16,000 na kina sehemu tatu: Usul, Furuu na Rawdhah . Usul Kafi inahusiana na hadithi za kiitikadi, Furuu Kafi inahusiana na hadithi za Fiqih na Rawdhat al-Kafi sehemu hii inajumuisha majimui ya hadithi mbalimbali.

Kitabu cha Man Laa Yahdhur al-Faqif

Kitabu hiki kimendikwa na Sheikh Swaduq (aliyeaga dunia 381 Hijria). Kinajumuisha takribani hadithi 6,000 ambapo maudhui zake ni Fiqihi na hukumu za kivitendo. Katika kitabu hiki Sheikh Swaduq amekusanya hadithi ambazo anaamini kuwa ni sahihi na yeye mwenyewe alikuwa akitoa fatuwa kwa mujibu wa hadithi hizo.

Kitabu cha Tahdhib al-Ahkam

Mwandishi wa kitabu hiki ni Sheikh Tusi (aliyeaga dunia 460 Hijria). Kitabu hiki kina sehemu 393 na hadhithi 13,590 na maudhui yake ni Fiqih. Sheikh Tusi aliandika kitabu hiki kwa agizo la Sheikh Mufid kwa ajili ya kutoa maelezo na ufafanuzi wa kitabu cha al-Muq'niah

Kitabu cha al-Istibsar Fi Ma Ikhtalafa Minal Akhbar

Sheikh Tusi aliakiandika kitabu hiki baada ya kitabu cha Tahdhib al-Ahkam akijibu ombi la baadhi ya wanafunzi wake waliomtaka afanye hivyo. Katika kitabu Sheikh Tusi alikusanya hadithi ambazo zinakinzana katika masuala mbalimbali ya Kifiqih. Kwa msingi huo, kitabu hiki hakijumuishi masuala yote ya Kifiqih.

Rejea

Vyanzo

  • Asterabadi, Muhammad Amin bin Muhammad Sharif, al-Fawaid al-Madinah, Tabriz, Bina, 1321 Hijria.
  • Amini, Abdul-Hussein, al-Ghadir Fil Kitab Wassunnah wal-Adab, Qum, Kituuo cha al-Ghadir Lidirasat al-Islamiyah, 1416 Hijria/1995 Miladia.
  • Ansari, Murtadha, Fawaid al-Usul, Qum, Maj'maa al-Fikr al-Islami, 1428 Hijria.
  • Baqiri, Hamid, Chohar Kitab Hadithi Emamiyah va ravaj Istilah "al-Kutub al-Ar'baa", Kukosioa mtazamo wa Andrew Newton, Mtandao wa Tomar Andishe.
  • Kkhui, Sayyid Abul-Qassim, Muujam Rijal al-Hadith watafsil Tabaqat al-Ruwat, Qum, Markaz Nash al-Thaqafah al-Islamiyayh Fil Alam, 1372 Hijria Shamsia.
  • Fadhil Toni, Abdallah bin Muhammad al-Wafiyah Fi Usul al-Fiqih, Mhakiki Radhawi Kishmiri, Qum, Maj'maa al-Fikr al-Islami, 1415 Hijria.
  • Karaki, Hussein bin Shahab al-Din, Hidayat al-Abrar Ilaa Tariq al-Aimat al-At'har, Mhakikki: Rauf Jamalul al-Din, Najaf, Ihyaa al-Ahyaa, 1396 Hijria.
  • Mudir Shanechi, Kadhim, Tarikh Hadith, Tehran, Intisharat Samt, 1377 Hijria Shamsia.
  • Mudir Shanechi, Kadhim, Ilm al-Hadith, Intisharat Eslami, Chapa ya 16, 1381 Hijria Shamsia.