Kuonekana Mwenyezi Mungu

Kutoka wikishia
Kitabu «Kuonekana Kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu» kilicho andikwa na Dar-Qutni.

Kuonekana Mwenyezi Mungu (Kiarabu:رؤية الله) ni maudhui ya kiteolojia (kiitikadi) nayo ni kuhusiana na uwezekano wa kumuona Mwenyezi Mungu kwa macho. Wasomi wa elimu ya teolojia wa madhehebu ya Shia Imamiyyah na wale wa kundi la Mu’tazila wanaamini kwamba, Mwenyezi haonekani kwa macho hapa duniani wala kesho akhera. Mtazamo wao ni kwamba; kumuona Mwenyezi Mungu kwa macho kunalazimu Muumba huyo awe na mwili na umbo, na chenye mwili kina sehemu maalumu. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu Mwenyezi Mungu hana mwili wala sehemu. Hata hivyo mkabala na wao, madhehebu mengi ya kitheolojia ya Ahlu-Sunna kama Ash’ari, Ahlul-Hadithi, al-Mujassamiya, al-Karamiyyah na Salafiyah yenyewe yanaamini kwamba, kuna uwezekano wa kumuona Mwenyezi Mungu.

Historia ya kadhia hii ya kumuona Mwenyezi Mungu katika Uislamu inarejea nyuma katika karne ya pili Hijiria. Kwa mtazamo wa baadhi ni kwamba, suala hili liliingizwa katika maudhui na mijadala ya Kiislamu na Mayahudi na Wakristo waliokuwa wakijidhihirisha kwamba ni Waislamu. Maudhui ya kumuona Mwenyezi Mungu mbali na kujadiliwa katika elimu ya theolojia, imezungumziwa pia katika Qur’an, hadithi na elimu ya irfan na kumeandikwa vitabu mbalimbali kuhusiana na kadhia hii miongoni mwavyo ni: “Ru’yatullah fi dhaui al-kitab wasunnah wal-aql al-sarih”, kilichoandikwa na Ja’afar Subhani.

Maana na Nafasi

Kumuona Mwenyezi Mungu ni maudhui ya kiteolojia (kiitikadi) nayo ni kuhusiana na je, inawezekana kumuona Mwenyezi Mungu kwa macho au la.[1] Katika baadhi ya Aya kumezungumziwa suala la kumuona Mwenyezi Mungu; kama vile Aya za 22 na 23 za Surat al-Qiyamah, Aya ya 15 ya Surat al-Mutaffifin, Aya ya 16 ya Surat Yunus na Aya za 11-13 za Surat Najm. Katika baadhi ya Aya pia suala la kumuona Mwenyezi Mungu limeelezwa kuwa halipo. Mfano wa Aya hizo ni: Aya ya 103 ya Surat al-An’am, Aya ya 143 ya Surat al-A’raf, Aya ya 55 ya Surat al-Baqarah, Aya ya 153 ya Surat al-Nisaa na Aya ya 21 ya Surat al-Furqan.[2] Katika vyanzo vya hadithi vya Kishia na Kisuni kuna hadithi zingine zilizonukuliwa ambazo zinazungumzia uwezekano wa kumuona au kutomuona Mwenyezi Mungu.[3]

Wafasiri wa Qur’an wanaopinga na wale wanaoafiki suala la kumuona Mwenyezi Mungu, wametoa maelezo chini ya Aya hizi na kujadili kadhia ya kuonekana Mwenyezi Mungu.[4]

Historia Yake

Katika Uislamu, mjadala wa kitheolojia kuhusiana na kuonekana Mwenyezi Mungu unarejea nyuma katika karne ya Pili Hijiria[5] katika karne hiyo makundi mawili ya kiitikadi ya Jahmiyyah na Mu’tazila yalikana suala la kuonekana Mwenyezi Mungu kwa jicho. Mwanzoni mwa karne ya tatu Hijiria, suala la uwezekano wa kumuona Mwenyezi Mungu likawa katika itikadi kuu za Ahmad ibn Hanbal mmoja wa Maimamu wanne wa madhehebu ya Ahlu-Sunna na wafuasi wake. Makundi mengine ya kitheolojia kama Matrudiyyah, Ashairah, Mujassimah, Mushabbah, Karamiyyah na Salafiyah[6] walikubaliana na suala la uwezekano wa kuonekana Mwenyezi Mungu kwa macho.[7]

Baadhi ya wanatheolojia akiwemo Sheikh Ja’afar Subhani, mwanatheolojia wa Kishia anaamini kwamba, fikra ya kuonekana Mwenyezi Mungu iliingizwa katika hadithi, maudhui na mijadala ya Kiislamu na baadhi ya Mayahudi na Wakristo waliokuwa wakijidhirisha kuwa ni Waislamu kama Ka’ab al-Ahbar.[8] Kwa mtazamo wa Ja’afar Sobhani ni kwamba, hadithi zote zinazohusiana na kuonekana Mwenyezi Mungu kwa macho ziliingizwa katika vyanzo na vitabu vya hadithi vya Waislamu na Mayahudi na Wakristo waliokuwa wakijifanya kuwa ni Waislamu.[9]

Kuonekana Mwenyezi Mungu Katika Dini Nyingine

Kabla ya Uislamu, suala la kuonekana Mwenyezi Mungu lilikuweko na lilizungumziwa katika Injili na Torati.[10] katika Torati, kitabu kitakatifu cha Mayahudi, Mwenyezi Mungu anamhutubu Nabii Mussa (a.s) akisema: “Huwezi kuniona; kwani mtu ambaye ataaniona mimi hawezi kubakia hai.”[11] Imekuja katika Injili ya kwamba, wenye nyoyo safi watamuona Mwenyezi Mungu;[12] lakini katika Aya nyingine inaelezwa kuwa, katu hakuna mtu ambaye amemuona Mwenyezi Mungu.[13]

Mtazamo wa Madhehebu za Kiislamu Kuhusu Kuonekana Mungu

Kuna mitazamo mitatu mikuu kuhusiana na suala la kuonekana Mwenyezi Mungu: Mujassimah na Karramiyah miongoni mwa makundi ya kitheolojia ya Ahlu-Sunna yanaamini kuwa, inawezekana kumuona kwa macho Mwenyezi Mungu hapa duniani na kesho akhera; kwao wao wanamueleza Mwenyezi Mungu kwamba, ana mwili na ana sehemu.[14]

Makundi mengine ya kitheolojia ya Ahlu-Sunna kama Asha'irah,[15] na Ahlul-Hadith[16] wanasema, Mwenyezi Mungu ataonekana kwa macho akhera tu; licha ya kuwa wao hawaamini kwamba, Mwenyezi Mungu ana umbo na mwili.[17]

Makundi mengine ya Kiislamu kama Imamiya[18], Zaydiyah[19] na Mu’tazilah.[20] yanaamini kwamba, ni muhali na jambo lisilowezekana kumuona kwa macho Mwenyezi Mungu hapa duniani na hata huko akhera na wana mtazamo mmoja katika hili.[21]

Hoja za Uwezekano wa Kuonekana Mwenyezi Mungu Akhera

Wanaoafiki uwezekana wa kuonekana Mwenyezi Mungu wakiwa na lengo la kuthibitisha kwa hoja mtazamo wao huu, wametumia hoja za kiakili na kinakili [22] na baadhi yazo ni:

Hoja za Kiakili

Baadhi ya hoja za kiakili za wanaoafiki kuonekana Mwenyezi Mungu ni :

  • Kwa mtu ambaye yeye mwenyewe anaona na kushuhudia vitu, kuna uwezekano wa watu wengine nao wakamuona. Kwa kuzingatia kwamba, Mwenyezi Mungu anaviona Yeye mwenyewe vitu vingine, basi kuna uwezekana akatupatia uwezo wa kumuona Yeye.[23]
  • Vitu vingi vilivyopo (vyenye uwepo) vina uwezekano wa kuonekana na uwezekano wa kuonekana kwao kunahusiana na dhati ya uwepo wao. Katika hali hii Mwenyezi Mungu naye ana uwepo (yupo) hivyo lazima iwezekane kuonekana kwake.[24]

Hoja za Kinakili

Hoja za kinakili za Aya za Qur’an na hadithi zinajumuisha:

Miongoni mwa Aya hizo ni Aya ya 143 ya Surat al-A’raf ambayo inasema:

“Na alipokuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi akamsemeza, alisema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi Mungu akasema: Hutoniona. Lakini utazame huo mlima. Ukibaki pahala pake basi utaniona. Basi alipojionyesha Mola Mlezi wake kwa mlima, aliufanya uvurugike, na Musa akaanguka chini amezimia. Alipozindukana alisema: Subhanaka, Umetakasika! Natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini.”

Wanatoa hoja wakisema kwamba, kama kumuona Mwenyezi Mungu lingekuwa jambo muhali na lisilowezekana katu, basi Nabii Mussa (a.s) asingetoa ombi kama hilo kwa Mwenyezi Mungu.[25]

Wenye kuamini kuonekana Mwenyezi Mungu wakiwa na lengo la kuhalalisha mtazamo wao na kuujengea hoja wanatumia pia Aya zingine za Qur’an kama ya 55 ya Surat al-Ah’zab, Aya za 22 na 23 za Surat al-Qiyamah, Aya ya 15 ya Surat al-Mutaffifin,[26] na Aya ya 1-3 ya Surat al-An’am.[27]

Ili kutubitisha kumuona Mwenyezi Mungu huko akhera, wahusika wametumia hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w);[28] kama hadithi hii ya Mtume:[29]"Utamuona Mola wako kama unavyouona na kushuhudia mwezi wa usiku wa 14".[30]

Hoja za Kutoonekana Mwenyezi Mungu

Wapinzani wa uwezekano wa kuonekana Mwenyezi Mungu nao wametumia hoja za kiakili na kinakili kuthibitisha msimamo wao:

Hoja za Kiakili

Ja’far Subhani anasema, kwa mujibu wa hoja za kiakili ni kwamba, kumuona Mwenyezi Mungu kulazimu awe na mwili au sifa za kuwa na umbo na mwili Mwenyezi Mungu.[31] Baadhi ya hoja za kiakili ni:

  1. Kuona kwa macho kunalazimu Mwenyezi Mungu awe na masafa, sehemu na zama; katika hali ambayo, Mwenyezi Mungu ametakasika na sifa hizo.[32]
  2. Mwenyezi Mungu ima aonekana kwa dhati yake yote au sehemu ya dhati yake. Mtazamo wa kwanza uunaishi katika hatua ya kwamba, Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye mipaka na anayepatikana sehemuu fulani, na mtazamo wa pili inalazimu awe na vitu kama umbo na sehemu na sura zote mbili ni muhali na ni batili. Kwa muktadha huo, haiwezekani kumuona Mwenyezi Mungu.[33]

Hoja za Kinakili

Kitabu «Kuonekana kwa Mwenyezi Mungu» kilicho andikwa na Ayatollah Subhani.

Hoja za kinakili za wanaopinga kuonekana Mwenyezi Mungu, mojawapo ni Aya ya 143 ya Surat al-A’raf ambayo imetumiwa pia kama hoja na wanaoafiki suala la Mungu kuonekana ambapo ndani ya Aya hii Mwenyezi Mungu anamwambia Nabii Mussa: “Hutoniona” ambapo hapa limetumina neno Lan Tarani. Kuutuumika Lan maana yake ni kwamba, hutoniona milele. Hivyo basi Aya hii inakana kuonekana Mwenyezi Mungu milele.[34]. Aya nyingine ni ile isemayo:

لَا تُدْرِ‌کهُ الْأَبْصَارُ‌ وَهُوَ یُدْرِ‌ک الْأَبْصَارَ‌
Macho hayamfikilii bali Yeye anayafikilia macho.[35]

Kwa mujibu wa mtazamo wa wanatheolojia wa Shia Imamiyyah na Mu’tazila ni kwamba, Aya hii inathibitisha na kutoa hoja kwamba, haiwezekani kumuona Mwenyezi Mungu kwa macho ya dhahiri.[36]

Hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Maimamu wa Kishia (a.s) nazo zinaonyesha kwamba, haiwezekani kumuona Mwenyezi Mungu kwa macho haya ya dhahiri.[37] Katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) ni kwamba, Bwana mmoja alimuuliza Imam Ali, hivi umewahi kumuona Mwenyezi Mungu? Imam akamjibu kwa kumwambia, siwezi kumuabudu Mungu ambaye simuoni; lakini inawezekana kumuona Mwenyezi Mungu kwa hakika ya imani na sio kwa macho.[38]

Kwa mujibu wapinzani wa uwezekano wa kuonekana Mwenyezi Mungu ni kwamba, hadithi za Mtume zinazotumiwa na wanaoafiki uwezekano wa kuonekana Mwenyezi Mungu, kama tutajaalia kwamba, hadithi hizo ni sahihi, zinaashiria kuwa na elimu na maarifa juu ya Mwenyezi Mungu, na sio kuona kwa macho ya dhahiri; kwani kama makusuio ya kuona ni kuona kwa macho ya dhahiri, basi hadithi italazimu Mwenyezi Mungu awepo katika sehemu, jambo ambalo ni muhali.[39]

Monografia

Kumeandikwa vitabu mbalimbali katika elimu ya teolojia, tafsiri na baadhi ya vitabu vya kiirfani na vya hadithi vyenye maudhui ya kuonekana Mwenyezi Mungu. Juu ya hayo, kumeandikwa vitabu vinavyojitegemea vyenye maudhui ya kuonekana Mwenyezi Mungu. Baadhi ya vitabu hivyo ni:

  • Kalimat Hawla Ru’yat: Kitabu hiki kimeandikwa na Abdul-Hussein Sharafuddin Amili. Kitabu hiki kina mtazamo wa Kishia na kinathibitisha kuwa muhali suala la kuonekana Mwenyezi Mungu.[40]
  • Ru’yatullah fi Dhaw al-kitab wasunnat wal-aq al-Sarih: Mwandishi, Ja’afar Subhani. Katika kitabu hiki, Ayatullah Ja’far Subhani anaeleza kwamba, suala la kuonekana Mwenyezi Mungu ni nadharia ya iliyoingizwa katika uislamu na mayahudi na hivyo anatoa hoja za kuibatilisha na wakati huo huo kutetea mtazamo wa Shia akitumia hoja za kiakili, Qur’an na hadithi.
  • Ru’yatullah Jalla Waala, kimeandikwa na Ali bin Omar Darul-Qutni. Darul Qutni ni katika wanazuoni na wapokezi wa hadithi mashuhuri wa Kisuni katika karne ya 4 Hijiria. Katika kitabu hiki, amekusanya Aya na hadithi za kuthibitisha kuonekana Mwenyezi Mungu. [39]
  • Kitabu kingine ni Ru’yatullah baina al-Tanzih wal Tashbih, kimeandikwa na Abdul-Karim Bahbahani.

Rejea

  1. Subhani, Ruu'yatu Allāh fī Dhau' al-Kitāb wa as-Sunnah wa al-'Aql Aswarih, uk. 26 & 27; Subhani, al-Iāhiyyāt, juz. 2, uk. 127; Bahbahani, Ruu'yatu Allāh Bain at-Tanzīh wa at-Tashbīh, uk. 16.
  2. Dhakiry wa digaran ((Ruu'yat)), uk. 799-802
  3. Tazama riwaya za Shia: Kulaini, al-Kāfī, babu: Ibthāl ar-Ruu'yat, juk. 1, uk. 95-110; Sheikh Saduq, at-Tauhīd, babu: Mā Jā'a fī ar-Ruu'yat, uk. 107-122; Nahj al-Balāghah, Tas-hih Subhi Saleh, Khutbe 91, uk. 124, Khutbe 185, hlm. 269, Khutbe 186, uk. 273; Sharafuddin, Ruu'yatu Allāh wa Falsafah al-Mīthāq wa al-Wilāyah, uk. 53-81; Tazama riwaya za Ahlu-Sunnah: Bukhari, Sahīh Bukhārī, juz. 1, uk. 115, juz. 6, uk. 139, juz. 9, uk. 127-129; Dar Qatni, Ruu'yatu Allāh Jallā wa 'Alā, uk. 7-94
  4. Tazama mifano ya tafsiri za wenye kupinga kuonekana kwa Mwenyezi Mungu katika kitabu cha: Tusi, at-Tibyān, juz. 1, uk. 249-253, juz. 10, uk. 197-199; Tabataba'i, al-Mīzān, juz. 8, uk. 237-243; Zamakhshari, al-Kashāf, juz. 1, uk. 141; juz. 2, uk. 151-157; Pia tazama mifano ya tafsiri za wenye kukubaliana na kuonekana kwa Mwenyezi Mungu: Fakhrurrazi, Tafsīr Kabīr, juz. 3, uk. 519-520, juz. 14, uk. 354-358, juz. 30, uk. 730-733.
  5. Subhani, Ruu'yatu Allāh fī Dhau' al-Kitāb wa as-Sunnah wa al-'Aql Aswarīh, uk. 24-25; Dhakiry wa digaran «Ruu'yat», uk. 802.
  6. Ibn Taimiyah, Minhāj as-Sunnah an-Nabawiyyah, juz. 2, uk. 316, 329-349, juz. 3, uk. 341, 344 & 347.
  7. Tazama: Dhakiry wa digaran «Ruu'yat», uk. 810
  8. Tazama, Subhani, al-Iāhiyyāt, juz. 2, uk. 138 & 139; Subhani, Ruu'yatu Allāh fī Dhau' al-Kitāb wa as-Sunnah wa al-'Aql Aswarīh, uk. 24-25; Bahbahani, Ruu'yatu Allāh Baina at-Tanzīh wa at-Tashbīh, uk. 99 & 100.
  9. Tazama: Subhani, Ruu'yatu Allāh fī Dhau' al-Kitāb wa as-Sunnah wa al-'Aql Aswarih, uk. 16
  10. Dhakiry wa digaran «Ruu'yat», uk. 802
  11. Biblia, Kutoka, sura ya 33, mstari wa 20.
  12. Biblia, Kutoka, sura ya 33, mstari wa 23.
  13. Biblia Takatifu, Injili ya Yohana, mstari wa 1, Aya ya 18.
  14. Biblia Takatifu, Injili ya Mathayo, sura ya 5, mstari wa 8.
  15. Biblia Takatifu, Injili ya Yohana, sura ya 1, mstari wa 18.
  16. Subhani, al-Iāhiyyāt, juz. 2, uk. 125; Fakhrurazi, al-Arba'īn fī Usūl ad-Dīn, juz. 1, uk. 266 & 267; Bahbahani, Ruu'yatu Allāh Baina at-Tanzīh wa at-Tashbīh, uk. 15.
  17. 'Ash'ari, al-Ibānah 'an Usūl ad-Diyānah, uk. 25 & 51; Amady, Ghāyatu al-Marām, uk. 142.
  18. Allamah Hilli, Kashf al-Murād, uk. 46; Subhani, Ruu'yatu Allāh fī Dhau' al-Kitāb wa as-Sunnah wa al-'Aql aswarīh, uk. 27; Jawadi Amuli, Tauhid Dar Quran, uk. 256 & 257.
  19. Subhani, Ru'yah Allāh fī Dhau' al-Kitāb wa as-Sunnah wa al-'Aql aswarīh, uk. 27; Ash'ari, Maqālāt al-Islāmiyyīn, juz. 1, uk. 172.
  20. Qadhi Abdul-Jabbar, al-Mukhtashar fī Usūl ad-Dīn, uk. 190; Shahrestani, al-Milal wa an-Nihal, juz. 1, uk. 57 & 114.
  21. Ash'ari, Maqālāt al-Islāmiyyīn, juz. 1, uk. 131 & 172; Amady, Ghāyah al-Marām, uk. 142; Shahrestani, al-Milal wa an-Nihal, juz. 1, uk. 5; Subhani, al-Ilāhiyyāt, juz. 2, uk. 125.
  22. Tazama: 'Ash'ari, al-Ibānah 'an Usūl ad-Diyānah, uk. 35-55.
  23. Tazama: 'Ash'ari, al-Ibānah 'an Usūl ad-Diyānah, uk. 35-55.
  24. Amady, Ghāyah al-Marām, uk. 142; Shahrestani, al-Milal wa an-Nihal, juz. 1, uk. 113.
  25. 'Ash'ari, al-Ibānah 'an Usūl ad-Diyānah, uk. 41; Fakhrurazi, al-Arba'īn fī Usūl ad-Dīn, juz. 1, uk. 278.
  26. Tazama: 'Ash'ari, al-Ibānah 'an Usūl ad-Diyānah, uk. 53.
  27. Fakhrurazi, Tafsīr Kabīr, juz. 13, uk. 97.
  28. Tazama: Dar-Qatni, Ruu'yatu Allāh Jallā wa 'Alā, uk. 7-94.
  29. Bukhari, Sahīh Bukhārī, juz. 1, uk. 139, juz. 9, uk. 127-129.
  30. 'Ash'ari, al-Ibānah 'an Usūl ad-Diyānah, uk. 49; Ibn Taimiyah, Minhāj as-Sunnah an-Nabawiyyah, juz. 2, uk. 332, juz. 3, uk. 341.
  31. Subhani, al-Ilāhiyyāt, juz. 2, uk. 128.
  32. Allamah Hilli, Kashf al-Murād, uk. 46 & 47.
  33. Subhani, al-Ilāhiyyāt, juz. 2, uk. 128.
  34. Subhani, Ruu'yatu Allāh fī Dhau' al-Kitāb wa as-Sunnah wa al-'Aql aswarīh, uk. 64-66.
  35. Surat al-An-am; 103
  36. Jawadi Amuli, Tauhid Dar Quran, uk. 258; Subhani, Ruu'yatu Allāh fī Dhau' al-Kitāb wa as-Sunnah wa al-'Aql aswarīh, uk. 55; Qadhi Abdul-Jabbar, Sharh Usūl al-Khamsah, uk. 156.
  37. Tazama: Kulaini, al-Kāfī, babu: Ibthāl ar-Ruu'yat, juz. 1, uk. 95-110; Sheikh Saduq, at-Tauhīd, babu: Mā Jā'a fī ar-Ruu'yat, uk. 107-122.
  38. Nahj al-Balāghah, juz. 1, uk. 258, Khutba no. 179.
  39. Qadhi Abdul-Jabbar, al-Mukhtasar fī Usūl ad-Dīn, uk. 191 & 192.
  40. Amini Pur, Nim Negahi be Unwanha-e Mausū'ah al-Imām as-Sayyid Abd al-Husein Sharaf ad-Dīn, Majalah Ketabha-e Eslami, juz: 22 & 23, uk. 25 & 26.

Vyanzo

  • Biblia Takatifu, Toleo jipya.
  • Āmadī, Sayf al-Dīn. Ghāyat al-marām fī ʿilm al-kalam. Chapa ya kwanza. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1413 AH.
  • Amīnīpūr, ʿAbd Allāh. "Nīm nigāhī bi ʿunwān-hāyi Mawsūʿat al-imām al-sayyid ʿAbd al-Husayn Sharaf al-Dīn." Kitāb-hāyi Islāmī 22 and 23. (1384 Sh)
  • Ashʿarī, Abu l-Ḥassan ʿAlī al-. Al-Ibāna ʿan uṣūl al-diyāna. Chapa ya kwanza. Cairo: Dār al-Anṣār, 1397 AH.
  • Ashʿarī, Abu l-Ḥassan. Māqalāt al-islāmīyyīn wa ikhtilāf al-muṣalīn. Chapa ya kwanza. [n.p]: Maktabat al-ʿAṣrīyya, 1426 AH.
  • Bihbahānī, ʿAbd al-Karīm. Fī riḥāb Ahl al-Bayt. Chapa ya pili. Qom: al-Majmaʿ al-ʿĀlamī li Ahl al-Bayt, 1426 AH.
  • Bukhārī, Muḥammad bin Ismāʿīl al-. Ṣaḥīḥ al-Bukhārī. First edition. Mhariri: Muḥammad Zuhayr b. Nāṣir al-Nāṣir. [n.p]. Dār Ṭawq al-Najāt, 1422 AH.
  • Dārquṭnī, ʿAlī bin ʿUmar. Ruʾyat Allāh jall wa-ʿalā. Mhariri: Aḥmad Farīd Mazīdī. Chapa ya kwanza. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1426 AH.
  • Dhākirī, Muṣṭafā. "Ruʾya". In Dānishnāmah-yi Jahān Islām, juz. 20. Tehran: Bunyād Dāʾirat al-Maʿārif al-Islāmī, 1394 Sh.
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad bin al-ʿUmar al-. Al-Arbaʿīn fī uṣūl al-din. Chapa ya kwanza. Cairo: Maktabat al-Kullīyyāt al-azharīyya, 1986.
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad bin al-ʿUmar al-. Tafsīr al-kabīr. Chapa ya tatu. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
  • Ḥillī, al-Ḥasan bin Yūsuf al-. Kashf al-murād fī sharḥ tajrīd al-iʿtiqād. Chapa ya tatu. Mhariri: Jaʿfar Subḥānī . Qom: Muʾassisat Imām al-Ṣādiq, 1382 Sh.
  • Ibn Taymīyya, Aḥmad b. ʿAbd al-Ḥalīm. Minhāj al-sunna al-nabawīyya fī naqd kalām al-shīʿa al-qadarīyya. Mhariri: Muḥammad Rashād Sālim. Riyadh: Jāmiʿat al-Imām Muḥammad bin Saʿūd al-Islāmīyya, 1406 AH/1986.
  • Jawādī Āmulī, ʿAbd Allāh. Tawhīd dar Qurʾān. Qom: Markaz-i Nashr-i Asrāʾ, 1395 Sh.
  • Kulaynī, Muḥammad bin Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Mhariri: ʿAlī Akbar Ghaffārī & Muḥammad Ākhūndī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Muḥammadī, ʿAlī. Sharḥ Kashf al-murād. Chapa ya nne. Qom: Dār al-Fikr, 1378 Sh.
  • Muʿtazilī, Qāḍī ʿAbd al-Jabbār. Al-mukhtaṣar fī uṣūl al-din. Mahariri: Muḥammad ʿAmāra. Beirut: Dār al-Hilāl, 1971.
  • Muʿtazilī, Qāḍī ʿAbd al-Jabbār. Sharḥ uṣūl al-khamsa. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1422 AH.
  • Nafīsī, Shādī. "Dārquṭnī, Abū l-Ḥasan ʿAlī b. ʿUmar.". In Dānishnāmah-yi Jahān Islām, juz. 16. Tehran: Bunyād Dāʾirat al-Maʿārif al-Islāmī, 1393 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad bin ʿAlī al-. Al-Tawḥīd. Chapa ya kwanza. Qom: Jāmiʿa Mudarrisīn, 1398 AH.
  • Sayyid Raḍī, Muḥammad Ḥussein. Nahj al-balāgha. Mhariri: Ṣubḥī Ṣaliḥ. Qom: Hijrat, 1414 AH.
  • Shahristānī, Muḥammad bin ʿAbd al-Karīm. Al-Milal wa al-niḥal. Chapa ya tatu. Mhariri: Muḥammad Badrān. Qom: al-Sharīf al-Raḍī, 1364 Sh.
  • Sharaf al-Dīn, ʿAbd al-Ḥussein. Ru'yat Allah wa-falsafat al-mithaq wa-l-wilaya. Mhariri: Mahdī Anṣārī Qummī. Qom: Lawḥ-i maḥfūẓ, 1423 AH.
  • Subḥānī, Jaʿfar. Al-Ilāhīyāt ʿalā hudā al-kitāb wa al-sunnat wa al-ʿaql. Chapa ya tatu. Qom: Markaz al-Alāmī li-Dirāsāt al-Islāmiyya, 1412 AH.
  • Subḥānī, Jaʿfar. Ruʾyat Allāh fī ḍawʾ al-kitab wa-l-sunna wa-l-ʿaql al-sarih. [n.p], [n.d].
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥussein al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Chapa ya pili. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī li-l-Maṭbūʿāt, 1390 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad bin al-Ḥassan al-. Al-Tibyān fī tafsīr al-Qurʾān. Mhariri: Aḥmad Qaṣīr al-ʿĀmilī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d].
  • Zamakhsharī, Maḥmūd bin ʿUmar al-. Al-Kashshāf ʿan ḥaqāʾiq ghawāmiḍ al-tanzīl wa ʿuyūn al-aqāwīl fī wujūh al-tʾawīl. Chapa ya tatu. Beirut: Dār al-Kitāb al-ʿArabī, 1407 AH.