Kundi la Othmaniyya

Kutoka wikishia

Kundi la Othmaniyya (Kiarabu: العُثمَانِيَّة) ni kundi linalo tambulikana kwa msimamo wake wa uhasama na upinzani mkali dhidi ya Imam Ali (a.s) na kizazi cha bwana Mtume (s.a.w.w), hususan katika masuala ya kisiasa, kijeshi, na kielimu. Asili ya kundi hili inarejea kwenye matukio muhimu ya kihistoria, ikiwemo tukio la kukataa kutoa kiapo cha utiifu kwa Imam Ali (a.s) baada ya kuuawa kwa Othman, ambapo wafuasi wa Othmaniyya walimpendekeza Muawiyah ibn Abu Sufyan na kumtambua kama ni kiongozi wa kisiasa (khalifa). Inasadikika kwamba neno Othmaniyya lilianzishwa likiwa ni kinyume cha neno Shia katika kipindi cha vita vya Jamal, vilivyohusisha upinzani dhidi ya uongozi wa Imamu Ali (a.s).

Kulingana na utafiti, wafuasi wa kundi la Othmaniyya walimlazimisha Imamu Ali (a.s) na wafuasi wake kuingia vitani katika vita vya Jamal na Siffin, ambavyo vilikuwa ni vipindi viwili muhimu katika mgongano wa kiitikadi kati ya Othmaniyya na Shia (wafwasi wa Ahlul-Bait) (a.s). Katika kipindi hicho, si tu kwamba wafuasi wa Othmaniyya walishiriki katika mapigano ya moja kwa moja, bali pia walihusika katika matendo ya kutumia lugha ya kukashifu, kuwatukana Ahlul-Bait na hata kutumia sera za ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Kishia, ikiwa ni pamoja na kuwaua, kuwatia magerezani na kuwahamisha kutoka katika miji yao.

Kundi la Othmaniyya liliacha athari kubwa kwenye nyanja za elimu mbali mbali kweneye ulimwengu wa Kiislamu; ikiwemo elimu ya hadithi, fiqhi, theolojia, pamoja na historia. Athari za kielimu zilizotika katika kundi hili, ziliibua tafsiri na mtazamo mpya katika kuutambua Uislamu. Kulizaliwa mielekeo mipya ya kisiasa, sambamba na itikadi katika zama za utawala wa makhalifa watatu wa mwanzo pamoja na Muawiyah. Mpini wa elimu katika kipindi hichi, ulikuwa ndani ya mikono mwa kundi la Othmaniyya, kikijumuisha wanazuoni wenye chuki zaidi dhidi ya Imamu Ali na Ahlul-Bait (a.s), hali iliyozidisha mgawanyiko wa kiitikadi ndani ya Uislamu.

Rekodi za mwisho kuhusiana na uwepo wa Othmaniyya zinarejea katika karne ya nne Hijiria, ambapo kundi hili lilianza kupoteza ushawishi wake wa kisiasa ndani ya kijamii mbali mbali.

Othmaniyya, Kundi Lililokabiliana na Imam Ali (a.s)

Kulingana na simulizi za kihistoria zilizotolewa na Tabari, kundi la Othmaniyya liliibuka baada ya kuuawa kwa Khalifa Othman, ambapo baadhi ya watu walikataa kumpa kiapo cha utiifu Imam Ali (a.s) [1] au walivunja kiapo chao [2] na kuachana naye. [3] Katika maandiko yalioko katika kitabu kiitwacho Masail al-Imama, imeelezwa kuwa; wafuasi wa kundi la Othmaniyya waliamua kumuunga mkono Muawiya katika mgogoro wa uongozi uliozuka kati ya Imam Ali (a.s) na Muawiya. [4]

Masahaba kama Talha, Zubair, Aisha, na Muawiya wametajwa na kuainishwa kuwa ni miongoni mwa wafwasi wa kundi hili. [5] Kwa mujibu wa maelezo ya Wilfred Madelung, mtaalamu wa tafiti juu ya Uislamu na mwandishi wa kitabu kiitwacho The Succession to Muhammad: A Study of the Early Caliphate ni kwamba; Sifa muhimu zaidi kuhusiana na utambulisho wa kundi la Othmaniyya, ni msimamo wao wa upinzani dhidi ya Imamu wa kwanza wa Mashia, ambaye ni Imamu Ali (a.s). [6] Kulingana na makala iliyochapishwa katika jarida la Pajuheshnameh Tarikh Tashayyu, ni kwamba; wafuasi wa Othmaniyya walipinga uhalali wa ukhalifa wa Imamu Ali (a.s), wakisisitiza kuwa; Muawiya ndiye khalifa halali anaye stahiki kushika nafasi ya ukhalifa baada ya Othman. [7] Walidai uhalali huu kwa kuzingatia uhusiano wa kifamilia kati ya Muawiya na Othman, pamoja na Muawiya kujitwika jukumu la kulipiza kisasi kwa damu ya Othman. [8]

Inasemekana kuwa Othmaniyya walihusika kwa kiwango kikubwa katika uhasama wa kisiasa, kijeshi, na kielimu dhidi ya Imam Ali (a.s) na familia ya bwana Mtume (Ahlul-Bait) (a.s). [9] Kulingana na Rasul Jafarian, mwanahistoria wa Kishia, wafuasi wa Othmaniyya walimlazimisha Imamu Ali (a.s) na wafuasi wake kutumbukia kwenye vita vya Jamal na Siffin. [10] Licha ya kushindwa katika vita vya Jamal, Othmaniyya waliendelea kuwa na ushawishi kwa kubadili mji wa Basra na kuufanya kuwa ngome ya misimamo yao ya Kiothmaniyya. Baada ya vita vya Siffin, waliimarisha udhibiti wao juu ya ardhi ya Iraq na kuendeleza itikadi zao ndani ya utawala wa Bani Umayyah. [11]

Kulingana na maoni ya Muhammad Muhsin Muruji Tabasi, yaliyo andikwa katika jarida la Farhang Ziarat, ni kwamb; Othmaniyya walipata uthibitisho wa kisiasa wakati wa utawala wa Umawiyya. Katika kipindi hiki, mbali na kupigana na Mashia, pia walijihusisha na vitendo vya kuwalaani na kuwatusi Ahlul-Bait (a.s), pamoja na kuwaua, kuwafunga gerezani, na kuwafukuza Mashia na hata Masunni waliokuwa wakisimulia sifa na nafasi za Ahlul-Bait (a.s). [12]

Kwa mujibu wa Patricia Crone, mtaalamu wa masuala ya Uislamu na mwanahistoria, ni kwamba; taarifa za mwisho zinazohusiana na kundi la Othmaniyya zinapatikana katika vyanzo vya kihistoria, [13] ni ripoti chache kuhusiana na harakati zao katika karne ya nne Hijiria. [14]

Tafiti Juu ya Istilahi ya Othmaniyya

Rasul Jafarian, katika kitabu chake Taarikh Tashayyu’ dar Iran, anaeleza kwamba; istilahi ya Othmaniyya iliibuka ikiwa ni kinyume cha istilahi ya "Shia", na chimbuko lake lilianza mwanzo mwa mwa vita vya Jamal. [15] Katika mashairi yaliyosomwa katika vita vya Jamal, baadhi ya askari wa jeshi la Jamal walionekana kuwaita wafuasi wa Imam Ali (a.s) kwa jina la “Wafwasi wa Dini ya Ali.” [16] Pia kulingana na maelezo ya Jafarian, istilahi ya “Dini ya Othman” iliibuka katika kipindi hicho hicho, ikiwa ni kama njia ya kupingana istilahi ya “Dini ya Ali”. [17]

Katika vita vya Siffin, baadhi ya washairi waliokuwa katika jeshi la Sham waliwatambua watu wa Sham kwa jina la “Wafwasi wa Dini ya Othman". [18] Kwa upande mwingine, Rifa'ah bin Shaddad, mmoja wa wafuasi wa Imam Ali (a.s), alijitambulisha katika mashairi yake kama ni mfwasi wa "Dini ya Ali". [19]

Matumizi ya istilahi ya "Dini ya Othman" pia yameripotiwa katika tukio la Ashura kutoka upande wa jeshi la watu wa mji wa Kufa. [20] Mwelekeo ambao, baadae ulikuja kulijulikana kwa jina la "Othmaniyya". [21] Kwa mujibu wa ushahidi wa kihistoria, jina hili lilianza kutumika kabla ya mwaka 145 Hijiria. [22] Aidha, al-Mas’udi alipokuwa akitoa wasifu wa kundi la Othmaniyya katika kitabu chake Al-Tanbih wal-Ishraf, alilitaja kundi la Othmaniyya kwa jina la Shiat Al- Othmaniyya. [23]

Mtiririko wa Kihistoria

Patricia Crone, katika makala yake yenye jina la Othmaniyya, amegawanya historia ya Othmaniyya katika vipindi vinne:

  1. Kipindi cha Wendelevu wa Uaminifu na Ushikamanifu kwa Othman.
  2. Kipindi cha Nadharia ya Makhalifa Watatu Halali.
  3. Kipindi cha Kukubalika kwa Makhalifa Wanne.
  4. Kipindi cha Uungaji Kuwaunga Mkono Bani Umayyah. [24]

Imani ya Uhalali wa Ukhalifa wa Othman na Uovu wa Kuuawa Kwake

Kipindi cha kwanza cha fikra za Kiothmaniyya kilitawaliwa na imani juu ya uhalali wa ukhalifa wa Othman na kulaani vikali kuuawa kwake. [25] Wafuasi wa Othmaniyya walishikilia itikadi isemayo kuwa; ukhalifa wa Imamu Ali (a.s) haukuwa ni ukhalifa halali, wakimtuhumu Ali (a.s) kushiriki katika mauaji ya Othman [26] kisha kuchukuwa nafasi ya ukhalifa bila kushirikisha umma. [27] [28]

Kwa mujibu wa Patricia Crone, kuna uwezekano mkubwa kwamba wale waliokataa kushiriki katika ghasia dhidi ya Othman waliegemea msimamo wa kuunga mkono fikra na nyenendo za Kiothmaniyya, [29] na kuanzia hapo hadi kufikia mwaka wa 70 Hijria, mtazamo huu ukawa tayari umeshashika mizizi katika ulimwengu wa Kiislamu. [30] Rasul Jafarian anaeleza kuwa; wengi miongoni mwa wa kawaida katika jamii ya Waislamu, waliambukizwa fikra za Kiothmaniyya katika kipindi hiki. [31]

Matukio muhimu kama vile vita vya Jamal na Siffin, [32] kutwaa ukhalifa, kuanzishwa kwa utawala wa Bani Umayyah, [33] laana dhidi ya Imam Ali (a.s), [34] kuuawa kwa Imam Hassan (a.s), [35] tukio la Ashura, [36]  pamoja na mashinikizo dhidi ya Mashia, yote kwa pamoja yamehisabiwa kuwa ni miongoni mwa hatua za kisiasa zilizofanywa na wenye fikra za Kiothmaniyya. [37]

Watu mashuhuri wa kundi la Othmaniyya katika kipindi hichi walijumuisha Talha, Zubair, Muawiya, na Aisha, pamoja na Abdullah bin Salam na Mughira bin Shu'uba, ambao walikataa kumpa Imamu Ali (a.s) kiapo cha utiifu, na badala yake wakaelekea Shamu kumuunga mkono Muawiya. [38] Miongoni mwa Maansari waliokataa kumtii Imamu Ali (a.s) ni Hassan bin Thabit, Ka'b bin Malik, Abu Said Khudri, Muhammad bin Maslamah, Nu’man bin Bashir, na Zaid bin Thabit, ingawa wengi wa Ansar walimuunga mkono. [39]

Imani ya Kukubaliana na Uhalali wa Makhalifa Watatu

Katika kipindi cha pili cha historia ya Othmaniyya, ambacho kilianza wakati wa enzi za Marwaniyya moja ya koo za Amawiyya (64-132 Hijria), Masahaba waliojali zaidi utoaji wa taaluma za Hadithi, walihusisha ukhalifa halali (makhalifa waongofu) kwa makhalifa watatu wa kwanza tu. [40] Kwa mujibu wa maelezo ya Patricia Crone, katika kipindi hichi, wafwasi wa fikra za Kiothmaniyya waliamua kunyamazia kimya na kutozungumzia suala la uhalali wa khalifa aliyefuata baada ya Othman, na waliona kipindi cha ukhalifa wa Imamu Ali (a.s), kama kipindi cha fitna na ghasia. [41] Watu kama Abdullah bin Omar na Sa’d bin Abi Waqqas, ambao walijitenga na ushiriki wa moja kwa moja katika fitna, walionekana kufuata misimamo ya Kiothmaniyya. Kujiweka kwao mbali na mgogoro huo kulitafsiriwa kama kuunga mkono makhalifa watatu wa mwanzo, huku wakipuuza uhalali wa ukhalifa wa Imam Ali (a.s). [42]

Imani ya Kukubaliana na Uhalali wa Makhalifa Makhalifa Wanne Waongofu

Katika kipindi cha tatu cha historia ya Othmaniyya, mtu aliyefuata mwelekeo wa Kiotmaniyya alitambuliwa kuwa ni yule aliyemboresha Othman na kumpa kipau mbele zaidi kuliko Imamu Ali (a.s), huku akimhisabu kila khalifa kuwa ni mtu bora kuliko wengine walioko katika zama zake, huku akiwaona makhalifa wote wanne kuwa ni wenye daraja inayolingana na namba ya ukhalifa wake. Katika kipindi hichi, Othmaniyya walijitofautisha na kujibagua na Mashia wenye mirengo ya kisiasa, [Maelezo 1] au hata Masunni waliokuwa na mwelekeo wa kumuunga mkono Imamu Ali (a.s) na kumuona bora zaidi ya Othman. Makundi mawili haya, yalimwona Imamu Ali (a.s), kuwa ni mwenye hadhi zaidi kuliko Othman. [44] Kwa mujibu wa maelezo ya Crone, nadharia hii ilianza kupata msingi thabiti zaidi katikati ya karne ya tatu Hijria, wakati ambapo nadharia ya kukubaliana na makhalifa wanne waongofu (nadharia ya tarbi'i) ilijengeka na kuimarika rasmi, hasa kupitia misimamo ya wanazuoni kama Ahmad bin Hanbal, ambaye aliunga mkono mtazamo huu kwa nguvu, na hivyo kuimarisha zaidi msimamo wa Othmaniyya. [45]

Kuungwa Mkono kwa Bani Umayya

Kwa mujibu wa makala ya Patricia Crone, mwishoni mwa karne ya tatu Hijria, kufuatia kupotea kwa Masahaba wenye mtazamo wa kushikamana na Hadithi, ambao ni wenye mrengo wa Kiothmaniyya, kulipelekea kuibuka kwa kundi maalum lililojulikana kama ni kundi la Kiothmaniyya, ambao walikubaliana na uhalali wa ukhalifa wa Bani Umayyah, ambao walihimiza na kuendeleza mwelekeo huu katika zama za utawala wa Bani Umayyah huko Andalusia. [46] Katika maandiko ya Abul Faraj Isfahani, imeelezwa kwamba; hadi karne ya nne Hijria, kundi hili la Othmaniyya bado liliendelea kuwepo, huku likiwa na msikiti wao maalum huko Kufa nchini Iraq, ambako Mashia walikwepa kuswali kwa sababu ya tofauti zao za kiitikadi na kundi hili. [47]

Athari za Othmaniyya katika Sayansi za Kiislamu

Imeelezwa ya kwamba; tangu mwanzoni wa kuibuka kwa kundi la Othmaniyya, kundi hili limeonekana kuwa na athari mkubwa katika nyanja za elimu mbalimbali za Kiislamu ikiwemo; Hadithi, fiq’hi, theolojia, na historia. [48] Kwa mujibu wa Rasul Jafarian, mtazamo wa Kiothmaniyya katika nyanja hizi ulikuja kutoa tafsiri mpya za mafundisho ya Kiislamu, ambazo zililenga zaidi misingi ya kisiasa na kifikra za utawala wa makhalifa watatu wa mwanzo pamoja na Muawiya. [49] Wanazuoni wa Hadithi, fiq’hi, na wanatheolojia wenye na misimamo mikali ya kiupinzani dhidi ya Imamu Ali (a.s) na Ahlul-Bait (a.s) waliibuka katika kipindi hichi na kujenga fikra na hoja zinazodhoofisha nafasi ya Imamu Ali (a.s) katika jamii za Kiislamu. [50]

Hadithi na Fiqhi

Kwa mujibu wa maandishi ya Mehdi Farmanian, mtafiti wa historia ya madhehebu, ni kwamba; ripoti za kihistoria zinaonesha kuwa wanazuoni wa Kiothmaniyya walikuwa na mchango mkubwa katika nyanja za Hadithi na fiq’hi ndani ya vituo vikuu vya kielimu vya Uislamu katika karne za mwanzo za Hijria. [51] Miji iliyokuwa muhimu kielimu wakati huo ni pamoja na Madina, Basra, Kufa, Makka, na Sham. [52] Kwa hivyo, masahaba muhimu waliokuwa na misimamo ya kuaminika katika Ahlu-Sunna huko Madina walikuwa ni wenye mwelekeo wa Kiothmaniyya, [53] akiwemo Aisha, [54] Abdullah bin Umar, [55] na Abu Hurayra. [56]

Kwa mujibu wa Farmanian, mtazamo thabiti miongoni mwa wanazuoni wa fiq’hi na Hadithi wa Kiothmaniyya huko Madina ulikuwa ni kusimulia sifa na kutangaza uadilifu wa makhalifa watatu wa mwanzo, huku wakijenga uadui dhidi ya Imamu Ali (a.s). [57] Imeelezwa kwamba; wanazuoni saba maarufu wa fiq’hi wa mjini Madina [58] [Maelezo 2] [59] walikuwa na mwelekeo wa Kiothmaniyya, ila viwango vya itikadi zao juu ya suala hili ilikuwa na viwango tofauti. [60]

  • Mwelekeo wa Kiothmaniyya katika Miji ya Basra, Kufa na Makka

Pia, kulingana na ripoti za Ibn Abd Rabbi katika Al-‘Iqd Al-Farid, ni kwamba; mara nyingi watu wa mji wa Basra walionyesha kuwa na mwelekeo wa Kiothmaniyya. [61] Anas bin Malik [62] na Muhammad bin Sirin (aliyeaga dunia: 110 H) [63] wametajwa na Ibn Abi Al-Hadid pamoja na Ibn Jowzi na kuorodheshwa kama ni wanazuoni muhimu wa Fiq’hi na Hadithi wa Kiothmaniyya huko Basra. [64] Farmanian anabainisha akisema kwamba; mtazamo ulioenea miongoni mwa wanazuoni wa fiq’hi na Hadithi wa Kiothmaniyya wa Basra ulifumbia mdomo na kubaki kimya kuhusiana na ukhalifa wa Imam Ali (a.s), na badala yake walionesha kutokukubaliana na hadhi yake maalumu mbele ya wengine. [65]

Huko mjini Kufa, licha ya kuwepo kwa Mashia na Masunni waliokuwa na mwelekeo wa Kishi'a, ila pia kuna rikodi zinazoeleza kuwepo kwa mafa’qihi wanahadithi wa Kiothmaniyya mjini humo, akiwemo Shaqiq bin Salama (aliyeaga dunia: 82 H). [66] [67] Aidha, kuna baadhi ya wanazuoni kadhaa wa kiq’hi na Hadithi kutoka Makka wenye misimamo ya Kiothamniyya, ambao miongoni mwao ni Maymun bin Mehran (aliyeaga dunia: 116 H). [68] [69] Imesemekana kuwa wanazuoni wengi katika Sham wakati wa utawala wa Bani Umayya walikuwa na mwelekeo wa Kiothmaniyya. Wanzuoni kazi yao ilikuwa ni kueneze Hadithi (bandia) kuhusiana na sifa za Bani Umayyah. [70]

Uwanja wa Historia

Pia katika nyanja ya uandishi wa historia, kumetajwa uwepo wa "Mirengo ya Kiothmaniyya kwenye Uandishi wa Historia ya Kiislamu", [71] ambapo kwa mtazamo huu, kuna wanahistoria wa Kiothmaniyya waliofadhiliwa na Bani Umayyah walijaribu kubadilisha historia ili kuhalalisha utawala wa Bani Umayyah. [72] Vyanzo vya kihistoria vinaonesha kuwa; wanahistoria wa Kiothmaniyya waliweza kushika hatamu na kuwa na ushawishi mkubwa katika nyanja ya historia. [73]

Sifa kuu ya mrengo huu ni kukinzana na Imamu Ali (a.s) kwa kukataa kutaja sifa zake na kuandika Hadithi za kumdharau, huku wakimjengea hadhi Othman na baadhi ya Masahaba wengine, wakijitahidi kukabiliana na Maansari na kuhakikisha kuwa sifa zao hazitajwi kwa njia yoyote ile. [74] Aban bin Usman na Saif bin Omar al-Tamimi wametajwa kama ni baadhi ya wanahistoria wanaohusishwa na mrengo wa Uandishi wa Historia wa Kiothmaniyya. [75] Kulingana na maelezo ya Jafarian ni kwamba; mnamo karne ya tatu, mrengo huu ulianza kukabiliwa na udhaifu ndani yake, hii ni baada ya kuimarika kwa wanahistoria wa kutoka upande wa madhehebu ya Kishi'a. [76]

Nyanja ya Kitheolojia

Moja ya nyanja muhimu yenye changamoto za kiakili kutoka upande wa mrengo wa Kiothmaniyya dhidi ya wapinzani wao, ni kitabu Maqalat al-Othmaniyya, kilichoandikwa na Al-Jahiz (160-255H). [77] Kulingana na Hassan Ansari, mtafiti wa historia ya Uislamu, Al-Jahiz katika kitabu hichi analinganisha fikra za Kiothmaniyya dhidi ya fikra za Kishi'a, huku akisimamisha hoja za kundi hili kwa undani kabisa dhidi ya dalili za kundi la Imamia kuhusiaana na suala la uongozi. Moja ya hoja za kitabu hichi ni madai ya kuto kuwepo kuwa maandiko juu ya ukhalifa na Imamu, wala ubora wa Imamu wa Imamu Ali (a.s) dhidi ya wengine. [88] Pia kitabu hichi kimesimama kupinga madai ya Mashia juu ya Haki ya Imamu Ali (a.s) katika Vita vya Jamal, Siffin, na Nahrawan. [79]

Aidha, Mas'udi anataja kuwepo kwa kitabu chenye kutetea uongozi wa Bani Umayya, kiitwacho Al-Barahin fi al-Imamah al-Umwiyyina kutoka kwenye kundi la Othmaniyya. [80] Kulingana na ripoti ya Al-Mas'udi, katika kitabu hichi, uongozi wa Bani Umayya wa Andalusia unachukuliwa kama ni muendelezo wa uongozi wa Othman na Bani Umayya. [81]

Maelezo

  1. Mashia wenye msimamo wa kisiasa au Mashia wa Kiiraqi, ni kundi la Waislamu wa Kishia waliosihi katika karne mbili za mwanzo za Hijria, ambao waliamini juu ya hadhi na ubora wa kipekee wa Imam Ali (a.s) wenye kumpiku Othman na kumtanguliza Ali (a.s). Ila ubora huu ni kwa upande wa kisiasa tu, na sio kwa upande wa kiitikadi (Jafarian, Taarikh Tashayyu dar Iran, 1388 H. Sh., uk. 22-27).
  2. Hawa ni wanazuoni saba wa fiqhi wa zama moja ambao walikuwa ni wakazi wa mji wa Madina, na miongoni mwa kundi la Taabi'un, nao ni: Abu Bakar bin Abdurrahman Makhzumi (aliyefariki mwaka 94 Hijria), Kharija bin Zaid Ansari (aliyefariki mwaka 99 Hijria), Said bin Musayyib (aliyefariki mwaka 91 Hijria), Sulaiman bin Yasar (aliyefariki mwaka 107 Hijria), Ubaidullah bin Abdullahi Makhzumi (aliyefariki mwaka 98 Hijria), Urwa bin Zubair (aliyefariki mwaka 94 Hijria), na Qasim bin Muhammad bin Abi Bakr (aliyefariki mwaka 108 Hijria).

Rejea

Vyanzo