Tukio la kuuawa kwa Othman

Kutoka wikishia

Tukio la kuuawa kwa Othman (Kiarabu: حادثة مقتل عثمان) ni tukio linaloashiria kuuwawa kwake kupitia uasi wa watu wa mwaka wa 35 Hijiria dhidi ya Khalifa wa tatu Othman bin Affan. Uasi huu ulifanywa na watu wa Misri kama ni radiamali ya kujibu tukio la kuezuliwa kwa Amru bin 'Aas Al-Sahamiy na kuvuliwa cheo cha ugavana wa Misri, na nafasi yake kushikwa na Abdullah bin Abi Sarh. Bila shaka, mfumo na njia ya utawala wa Othman ulikuwa na dosari kadhaa. Miongoni mwa mambo yaliowaudhi baadhi ya Maswahaba wa Mtume (s.a.w.w) katika utawala wake, ni kukabidhi nyadhifa muhimu za serikali kwa Bani Umayyah ambao ni jamaa zake , pamoja na kuwachotea na kuwarithisha wao mali kutoka katika hazina ya Waislamu.

Waandamanaji wa Misri walikwenda Madina kufanya maandamano na hatimae wakarejea Misri kupitia usuluhishi wa Imam Ali (a.s) baaya ya yeye (Othman) kuahidi kurekebisha na kusawazisha matatizo katika uongozi wake hou. Walipokuwa njiani waandamanaji hao wakielekea Misri, walikabiliwa na barua ya Othman aliyomtumia gavana wake wa Misri, akimtaka kuwauwa na kuwatia kizuizini waandamanaji hao. Papo hapo waliamua kurudi Madina na kumtaka Othman ajiuzulu na achane na nafsi ya ukhalifa, ila Othman hakukubaliana na ombi lao. Katika hali hiyo waandamanaji hao aliizingia nyumba ya Othman na baada ya siku arubaini za kuzingiwa kwake, hatimae aliuawa na maiti yake ikakataliwa kuzikwa katika makaburi ya Waislamu.

Haidhuru Imam Ali (a.s) alikuwa akielewa fika matatizo na kasoro alizokuwa nazo Othman katika utawala wake, hata hivyo hakukubaliana na kuuwawa kwake, badala yake akawaamuru baadhi ya watu kama vile, Imamu Hassan (a.s) na Abdullah bin Zubeir kwenda kuilinda nyumba ya Othman kutokana na janga hilo.

Kuuawa kwa Othman kulisababisha kuanza kwa migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa Waislamu. Miongoni mwa migogoro hiyo ni; Mgogoro kati ya Bani Hashim na Bani Umayyah ulipamba moto kwa mara nyengine tena, Aisha, Talha na Zubeir nao wakaanzisha Vita vya Jamal kwa kisingizio cha kutaka kulipa kisasi dhidi tukio la umwagwaji damu ya Othman. Tukio la kuuwawa kwa Othman limezingatiwa kuwa ndiyo chanzo cha fitna katika ulimwengu wa Kiislamu.

Umuhimu na nafasi yake katika historia ya Uislamu

Tukio la kuuliwa kwa Othman linahisabiwa kuwa ni moja ya matukio muhimu zaidi ya zama za baada ya Mtume wa Muhammad (s.a.w.w). Kwa mujibu wa baadhi ya watafiti; Baada ya kuuawa kwake, historia ya Kiislamu iliingia katika awamu mpya kabisa. [1] Pia, mauaji ya Othman yalifuatiwa na matokeo mengine mbalimbali. Tukio hili lilikuwa na ushawishi mkubwa katika kuunda na kuzuka kwa matukio mengine malimbali yaliyofuatia baada yake. Mwanahistoria wa Kisunni Ibn Hajar Asqalani (aliyefariki mwaka wa 852 Hijiria) amelihisabu tukio la kuuawa kwa Othman kama chanzo cha fitna katika ulimwengu wa Kiislamu. [2]

Ufafanuzi juu ya tukio

Kwa mujibu maelezo ya vyanzo mbali mbali ni kwamba; Baada ya kuuzuliwa kwa Amru bin 'Aas na kuteguliwa katika nafasi ya ugavana wa serikali ya Misri, na badala yake nafasi yake kushikwa na Abdullah bin Abi Al-Sarh, Wamisri wapatao mia sita walifanya maandamano wakielekea mjia wa Madina, na hayo yakawa ndiyo maandamano ya mwanzo kabisa dhidi ya Othman. [3] Pia Baadhi ya wengine wamesema ya kwamba; Sababu hasa ya maandamano hayo, ni kule Othman kuwachotea jamaa zake ruzuku ya mali kutoka katika hazina ya Waislamu. [4] Baada ya waandamanaji kuondoka na kuelekea Madina, waliandika barua na kuwaita wengine waende katika mji wa Madina.

Kuwasili kwa aandamanaji Madina na toba ya Othman

Wapinzani walipofika karibu na mji wa Madina, Othman alimtaka Imam Ali (a.s) aingilie kati ili awarudishe waandamanaji hao nchini kwao Misri. [6] Kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuu ripoti hii; Othman alitoa ahadi kwa waandamanaji hao ya kwamba, watu waliohamishwa kutoka katika miji au vitongoji vyao watarudishwa katika makazi yao, haki itazingatiwa katika mgawanyo wa mali katika jamii na watu waaminifu na imara watawekwa katika kushugulikia mambo hayo. [7] Othman katika kuhakikisha watu wameamini hadi zake, alipanda mimbari na akahutubia watu na kuomba toba kwa matendo yake. Othman aliwataka watu kuwa mashahidi juu ya aliyoyasema na ahadi alizozitoa. [8] Baada ya hapo, waandamanaji wakaridhika na wakaamua kurudi katika miji yao. [9]

Waandamanaji kurudi Madina

Wakati waandamanaji waliporudi kutoka Madina, walimkuta mtumwa wa Khalifa akiwa ameficha barua fulani. [10] Barua hiyo ilikuwa na muhuri wa Khalifa ikiamuru kuuawa na kufungwa kwa waasi hao. Baada ya waasi hao kuikamata barua hiyo na kujuwa dhamira ya Othman, waliamua kurudi tena Madina. [11] Baada ya watu wa mji wa Kufa kupata habari za tukio hilo, nao pia walirudi Madina . [12] Waasi hao moja kwa moja walikwenda kwa Imam Ali (a.s) na wakaenda naye kwa Othman. Katika hali hiyo Othman akala kiapo ya kwamba yeye hakuandika aina yoyote ile ya barua, na wala hana habari yoyote ile kuhusian na suala hilo. [13] Waasi hao kamwe hawakusadiki maneno yake, na badala yake wakamtaka Othman ajiuzulu kutoka katika nafasi ya ukhalifa. [14] Katu Othman hakukubali na mawazo yao, na badala yake akaahidi kutubia. Waasi hao wakirejelea toba yake ya awali ambayo Othman aliivunja bila ya kujali, wao waliendelea kushikilia msimamo wao wa kumtaka Othman kujiuzulu na kuachana na nafasi ya, wao walisisitiza kushikamana na msimamo wao huo hadi moja kati ya mawili yapatikane, nayo ni wao wauwawe au Othman ajiuzulu. [15]

Kuzingirwa kwa nyumba ya Othman

Waandamanaji waliizingia nyumba ya Othman na kuzuia maji na chakula kuingia ndani ya nyumba hiyo. [16] Wazingiaji wa nyumba hiyo, walikuwa ni watu kutoka Misri, Basra, Kufa na baadhi ya watu wa Madina. [17] Kuzingiwa kwa nyumba ya Othman kuliendelea kwa muda wa siku arubaini. [18] Katika kipindi hichi, Othman alimtumia barua Muawiyah na Ibn 'Aamir na kuwaomba msaada. [19] Kupitia amri ya Imam Ali (a.s), nyumba ya Othmani ilipata himaya ya ulinzi kupitia Imam Hassan (a.s) pamoja na watu wengine kama vile, Abdullah bin Zubeir na Marwan bin Hakam. [20]

Othman alimwomba Imam Ali (a.s), Talha, Zubeir na wakeze Mtume wamletee maji. [21] Imam Ali (a.s) na Ummu Habiba mke wa Mtume (s.a.w.w), walikuwa ndio watu wa mwanzo waliojaribu kumletea maji Othman, ila jaribio hilo lilifeli, kutokana na waasi hao kuzuia zoezi hilo. [22] Baada ya waasi hao kuzuia kuingia kwa maji na chakula, Imam Ali (a.s) alilani tendo lao na akwambia kuwa, kufanya kwao hivyo, hakufanani kabisa na matendo ya waumini au hata makafiri. Imamu Ali (a.s) aliwauliza; Ni kisingizio gani ni mashiko gani walioshikamana nayo katika kujuzisha matendo yao na kuhalalisha mauwaji yake. [23] Bila shaka, kulikuwa na baadhi ya makundi yaliyoweza kumfikishia maji khalifa kwa nji ya siri. [24]

Kuuawa na kuzikwa kwa Othman

Kuna ripoti tofauit kuhusiana na mauaji ya Othman. [25] Kulingana na baadhi ya nukuu juu ya tukio hili ni kwamba; Kuna kikundi cha watu fulani ambacho kilishambulia nyumba hiyo na watu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo wakawafukuza watu wa kikundi hicho na kuwatoa nje. Watu hao walishambulia tena kwa mara ya pili, shambulio hili la pili ndilo ndilo lililofanikisha kumuuwa Othman. [26] na mkewe naye ambaye alijulikana kwa jina la Naela, aliambulia kukatwa vidole . [27]

Mauaji ya Othman yameripotiwa kutokea mnamo tarehe 18 Dhul-Hijjah, mwaka wa 35 Hijiria. [28] Tukio la kuuliwa kwa Othman katika historia, linajulikana kwa jina la «واقعة یوم الدار» "Tukio la Yaum al-Daar" [29] Kwa mujibu wa ripoti iliyosimuliwa na Tabari; Mwili wa Othman uliachwa bila ya kuzikwa kwa muda wa siku tatu. Baada ya hapo, baadhi ya watu wakachukuwa mwili wake na kuupelekwa Baqi'i, lakini kundi la baadhi ya watu likazuia maziko hayo katika eneo hilo. Mwishowe maiti ya Othman ikazikwa katika mava ya "Hushu-Kaukab" (katika makaburi ya Kiyahudi), ambapo baadaye Muawiya aliitanua mava hiyo na kuiunganisha na mava ya Baqi'i. [30]

Sababu zilizopelekea kutoridhika na kusababisha Uasi

Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba; Kutoridhika kwa wanajamii na hatimae kupelekea uasi dhidi ya Othman, halikuwa ni tukio lililozuka ghafla bila ya kuwa na sababu za mwanzo zililizopelekea kupatikana kwa hali hiyo, bali kulikuwa na sababu mbalimbali zilisababisha kuundwa kwa upinzani na kuzuka kwa uasi huo. [31] Kuna mambo haya yalihusiana na kuzuka kwa hali hiyo, sababu muhimu zaidi, ni hali nzima inayohusiana na utendaji wa Khalifa huyo. [32] Miongoni mwao:

Kuhawilisha kwa majukumu ya uongozi kwa Bani Umayyah

Kwa mujibu wa maelezo ya mtafiti wa historia, bwana Rasul Jafarian (aliyezaliwa mwaka 1343 Shamsia); Othman alizihawilisha nyadhifa muhimu za serikali kwa Bani Umayya, jambo ambalo lilipelekea mamlaka yote ya serikali yakaangukia mikononi mwao. [34] Emeelezwa ya kwamba; Othman alihawilisha vyeo vya kiserikali kwa Bani Umayyah, ikasi ya kwamba iliweza kusadikika kuwa yeye alikuwa na nia ya kuigeuza serikali na kuipa umba la serikali ya Kibani Umayyah. [35] Vyanzo vya kihistoria vikielezea baadhi ya nyadhifa za jamaa zake Othman na majukumu yao katika serikali, vimeelezea na kuorodheshwa kama ifuatavyo:

Jina Nasabu na Ujamaa Wake na Othman Wadhifa
Walid bin Uqbah Kaka yake kwa upande wa mama Kiongozi wa Kufa
'Abdullah bin 'Amin Mtoto wa Mjomba Kiongozi wa Basra
Abdullah bin Abi Sarh Ndugu wa kunyonya pamoja Kiongozi wa Misri
Muawiah bin Abi Sufian Bani Umayyah Kiongozi wa Sham
Marwan bin Al-Hakam Mtoto wa ami na shemegi yake Mwandishi
Said bin 'Aas Bani Umayyah Kiongozi wa Kufa


Kuteuliwa kwa jamaa za Othman nakupewa nyadhifa muhimu za kiserikali na pia namna wanavyotawala, kulisababisha Waislamu wengi kulalama. [42] Malalamiko ya Waislamu juu ya utezi huo hayakuwa ni malalamiko ya ovyo, kwa mfano; Abdullah bin Amer alikuwa na historia ya kuritadi [43] Walid bin Uqbah abaye Qur'an imemhutubu kwa jina la fasiki (mwovu), Marwan bin Hakam pamoja na baba yake naye alifukuzwa na Mtume (s.a.w.w) na akatolewa katika mji wa Madina, lakini Othman akaamua kumrudisha tena Madina. [45]

Kuchota katika hazina ya Waislamu

Baaada ya Othman kushika wadhifa wa ukhalifa, aligeuka kuwa ni miongoni mwa watu tajiri mno. [46] Moja ya matatizo nyeti yaliyotambuliwa kuhusiana na Othman, ni kuchota mali kutoka katika hazina ya Waislamu (Baitul-Mali). [47] Yeye alichota kiwango kikubwa cha mali na kuwagawia Banu Umayyah. 49] Katika nyakati fulani, alimpa kiwango kikubwa cha mali Abdullah bin Abi Sarh. [50] Pia Othman alimimina mali nyingi kwa Harith bin Hakam, [51] Hakam bin Abi Al-'Aas, [52] Abdullah bin Khalid bin Usaid n.k. Kufanya hivyo kulikuwa ni kinyume na utendaji wa makhalifa waliopita kabla ya Othman. [54] Kwa kweli jambo hilo lilileta athari mbaya mno kwwnye jamii na kusababisha kutoaminika kwa viongozi wa viongozi wa Kiislamu. [55]

Abdullah Bin Saba

Baadhi ya wanahistoria wa Kisunni wanaamini ya kwamba; Abdullah bin Saba alihusika katika kueneza na kuunda uasi na maandamano dhidi ya Othman. [56] Kwa upande mwingine, kundi kubwa la watafiti wa Kishia [57] na Kisunni [58] wametilia shaka uwepo wa mtu aitwaye Abdullah bin Saba. Pia, kwa mujibu wa maelezo ya mtafiti wa kihistoria Rasool Jafarian, jamii ya Kiislamu haikuwa dhaifu kiasi hicho, kiasi ya kwamba uasi dhidi ya khalifa wa Kiislamu ufanywe na Myahudi ambaye ndiyo kwanza ameiingia katika Uslamu. [59]

Utendaji wa Maswahaba

Taha Hossein ambaye ni mmoja wa watafiti wa Kisunni, (aliyefariki mwaka 1973 Miladia), anaamini ya kwamba; Hakuna hata mmoja miongoni mwa Masahaba Muhajirina na Answari aliyehusika katika kumuua Othman; Ingawaje baadhi yao walikuwa wakipingana na namna ya Othman alivyokuwa akiamiliana na watu, ila walilazimika kukaa kimya kutokana na khofu, wengine hawakuingilia kati suala lolote lile katika siasa za utawala wake, na wengine wakauhama mji Madinah. [60] Pia Taha Hussein anaamini kwamba yale yaliyoripotiwa katika vyanzo vya historia kuhusu nafasi ya Masahaba katika suala la kuizunguka nyumba ya Othman na kumuua ni dhaifu. [61] Mwelekeo wa utatiti huu unaohusiana na nafasi ya Masahaba katika tukio la kuuwawa kwa Othman, umejikita zaidi katika msingi wa itikadi ya Kisunni kuhusiana na uadilifu wa Maswahaba. Yaani kupitia itikadi hiyo, haitokuwa sahihi kuwahusisha Masahaba katika tukio hilo la jinai. [62] Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, baadhi ya Masahaba wanahusika moja kwa moja katika uasi dhidi ya Othman. Kwa mfano, Hashim bin Utbah aliwatambulisha wauaji wa Othman kuwa ni Maswahaba wa Muhammad pamoja na watoto wao, n.k. [63] Pia, mke wa Othman, alimwandikia barua Mu'awiah baada ya kuuawa Othman, ambapo ndani barua hiyo aliwataja watu wa Madina kuwa ndio walioizunguka nyumba yake na kumuuwa Othman. [64]

Imamu Ali (a.s)

Kwa upande mmoja, Imam Ali (a.s) alimwita Othman kwa jina la «حَمَّالُ الْخَطَایا» “Mbeba Madhambi”, jian ambalo linamaanisha “mtu mwenye makosa mengi”, [65] wale yeye hakuitakidi kuwa Othman aliuawa bila ya hatia. [66] Kwa upande mwingine, yeye alipingana na tendo la kumuuwa Othman, naye alionesha wazi wazi kuwa yeye hahusiki kabisa na hatia za kuuwawa kwa Othman. [67] Pia, Imam Ali (AS) aliwanasihi waasi walioinuka dhidi ya Othamn na akawaashiria dosari na makosa yao katika mrengo walioshikamana nao. [68] Pia kulikuwa na watu walimtaka Imamu Ali (a.s) aondoke mjini Madina, na endapo Othamn atauwawa, basi yeye awe hayupo mjini humo, ila Imamu Ali (a.s) hakukubaliana na mapendekezo yao. [69] Imam (a.s) akijibu tuhuma za Muawiah katika barua aliyomuandikia akimtuhumu kuhusiana na mauwaji ya Othman, Imamu Ali (a.s) katika kujibu tuhuma hizo alimwandikia kwa kusema; 'Wewe uanitumuhumu juu ya jambo ambalo si ulimi wala mkono wangu unahusiana na tuhuma hizo, wewe (Muawiah) pamoja na wafuasi wako wa Sham (Syria), mmepata kisingizio cha kunisakama kwa kunihusisha na tukio hili (la kuuwawa kwa Othman), kiasi ya kwamba wale wanaelewa ukweli wanawatomeza walio wajinga, na wale wenye nyadhifa wanawatomeza wasiokuwa na nyadhifa (ili wauwashe moto dhidi yangu). [70] [Maelezo 1]

Talha

Mwanahistoria wa Misri, Taha Hussein (aliyefariki mwaka 1973 Miladia), anamhisabu Talha kuwa ni mmoja wa watu ambao hawakuficha mrengo wao katika tukio la uasi dhidi ya Othman, badala yake alililiunga mkono kwa mali yake. [71] Kulingana na baadhi ya nukuu ni kwamba; Hata suala la karantini dhidi ya Othman ya kuzui maji na chakula, ilikuwa ni pendekezo la Talha. [72] Kwa mujibu wa maelezo ya Ibn Abi al-Hadiid Mu'tazili katika kitabu cha tafsiri ya Nahj al-Balaghah ni kwamba; Kabla ya kuanza kwa Vita vya Jamal, Imam Ali (a.s), ambapo alionana na Zubeir, alimsemeza Zubeir kwa kumwambia: "Wewe (Zubeir) na Talha ndio watuhumiwa wakuu katika mauaji ya Othman, na mnapaswa kujisalimisha wenyewe mikoni mwa warithi wa Othman. [73]

Muawiah

Pale Othman alipozingiwa na nyumba yake kuzungukwa na waasi, alimwandikia barua Muawiah na kumwomba msaada. Mu'awiah naye alituma jeshi la watu elfu kumi na mbili, ambalo aliliamrisha kukaa katika mipaka ya Shamu (Syria) hadi amri amri ya pili itakapotolewa [74] Jeshi hili lilizorota katika kuingia Madina na kumsaidia khalifa, na pale mjumbe wa Shamu alipokwenda kukutana na Othman, yeye alimkabili mjumbe huyo kwa kumwambia; Nyinyi mnasubiri niuwawe ili mujifanye kuwa ndiyo wadai na wasimamizi wa kulipiza kisasi juu ya damu yangu. [75]

Imam Ali (a.s) alimlaumu na kumshutumu Mu'awiah katika tukio la kuuwawa kwa Othman. Pale Mu'awiah alipomtuhumu Imamu Ali (a.s) katika mauwaji ya Othman, Imamu Ali (a.s) alimkumbusha Mu'awiah katika kuzorotesha kumpelekea msaada Othman, pale Othman alipukuwa amezungukwa na waasi, huku akisubiri msaada kutoka kwa Mu'awiah. [76] Pia Baadhi ya Masahaba wengine walimzungumzia Mu'awiyah kuwa ni miongoni mwa sababu za kuuwawa kwa Othman, kwani yeye hakuharakisha himaya yake ya kulinda na kumtetea Othman wakati ambao yeye alikuwa amezungukwa na kundi la waasi. [78]

Aisha

Kwa mujibu wa maandishi ya Muhammad bin Jarir Tabari; Aisha alikuwa na usemi maarufu dhidi ya Othamni, yeye alimnadi Othman akisema: «اُقْتُلُوا نَعْثَلا فَقَدْ کفَر» "Muuweni Na'athala [Maelezo 2] kwa hakika yeye ameshakufuru." [79] Neno "نَعْثَلا" alilolitumia Aisha, lilikuwa ima limaanisha naana ya kumnanga Othman kwa sababu yeye alikuwa akimfananisha na mzee wa Kiyahudi aliyejulikana kwa jina hilo, au akimfananisha na mzee wa Kimisri ambaye alikuwa na ndevu refu, au pia kuna wengine wamesema kuwa, neno jina hili lilikuwa na maana ya kizee ambaye ni mjinga asiyejuwa kitu. [79]

Wakati waasi walipokuwa Madina, Marwan bin Hakam alimwomba Aisha awe mpatanishi kati ya Khalifa na waasi. Aisha akatoa kisingizio cha safari ya Hijja, na akasema kwamba; Yeye mwenyewe (Aisha) alitamani kumkatakata vipande Othman na kumtupa baharini. [80] Baada tu ya kifo cha Othman, Aisha akabadili maoni yake na kudai kutaka kulipiza kisasa juu ya kuuwawa kwa Othman. [81] Katika barua ya Saad bin Abi Waqas kwa Ibn 'Aas, alielezea baruani humo ya kwamba; Othman aliuawa kwa upanga uliochomolewa na Aisha kutoka alani mwake, kuung'arishwa (kunolewa) na Talha. [82] Hata hivyo, baada ya kuuwawa kwa Othman na watu wakala kiapo cha utiifu kwa Ali (a.s), Aisha alirejea Makka, kisha akawahutubia watu na kwa namna fulani akaashiria kuwa Imamu Ali (a.s) kuwa ndiye mhusika wa mauwaji ya Othman. [83] Kwa namna hiyo ya Aisha kubadilisha mwelekeo wake, jambo hilo lilipelekea Umm Al-Salamah, ambaye ni mke wa Mtume (s.a.w.w), kumhukumu Aisha, na akamwambia; "wewe uliwachochea watu wamuue Othman kisha leo tena unageuka na kusema maneno haya. [84] Aisha akimjibu Ummu Al-Salamah akasema: “Ninachosema sasa ni bora zaidi kuliko nilichokisema wakati ule.” [85]

Matukio

Mauaji ya Othman yalifuatiwa na matokeo kadhaa, baadhi yake ni:

  • Msingi wa kuanzishwa kwa vita mbali mbali katika zama za ukhalifa wa Imam Ali (a.s): Kwa mujibu wa maoni ya wanahistoria, Vita vya Jamal vilianzishwa na Aisha, Talha na Zubair. Misingi hasa wa kuanzishwa kwa vita hivyo, ni kisingizio cha kutaka kulipiza kisasi juu ya damu ya Othman iliyomwagwa. [86] Imamu Ali (a.s) katika moja ya barua zake alizowatumia wao, aliwahakikishia na kuwathibitishia kuwa yeye hakuhusika kamwe na mauwaji ya Othman, nao pia hawana aina yoyote ile ya haki katika kusimamia damu ya Othman iliyomwagwa katika mauwaji hayo. [87] Kuhusiana na Talha na Zubeir, Imam Ali (a.s) alisema kwamba; Wao wanadai haki ambayo waliiachana nayo (hawaitetea hapo alipokuwa yuhai), bali wao ndio wamwagaji wa damu hiyo ya Othman. [88]
  • Kuripuka upya kwa mzozo baina ya Bani Umayyah na Bani Hashim: Bani Umayyah walitumia mauaji ya Uthman kama ni nafasi na njia ya kurejesha na kuhuisha tena ukuu (ushikaji hatamu) na mamlaka yao miongoni mwa Waarabu. [89] wao Walijitambulisha kama ni wadai wakuu katika suala la damu ya Othman, huku wakimtambulisha Ali (a.s) kuwa ndiye mhusika wa uhalifu katika umwagaji damu ya Othman. [90] Kwa mujibu wa maelezo ya Rasuli Jafarian; Kifo cha Othman kilikuwa ni chenye manufaa zaidi kwa upande wa Muawia. [91] Baada tu ya Othman kuuwawa, Muawia alipanda mimbari na kujidhihirisha kam ni mtetezi na mdai mkuu wa damu ya Othman. [92] Vidole vya mkwewe Othman (Naila) pamoja na kanzu ya Othman iliyojaa damu iligeka kuwa ni kisingizio alichoshikamana nacho Muawiya katika kuwachochea watu wa Sham (Syria) dhidi ya Imamu Ali (a.s). [93]
  • Kuundwa kwa Mrengo wa Unasibi (Chuki Dhidi ya Ahlul-Bait): Inasemekana kwamba Unasibi (Chuki Dhidi ya Ahlul-Bait), ulianza baada ya mauaji ya Othman na ulirasimishwa katika utawala wa Bani Umayyah. [94]

Masuala yanayo husiana

Vyanzo

  • Balādhurī, Aḥmad b. Yaḥyā al-. Ansāb al-ashrāf. Edited by Suhayl Zakār & Riyāḍ al-Ziriklī. Beirut: Dār al-Fikr, 1417 AH.
  • Bakhtiyārī, Shahlā. Sakhtār-i siyāsī hukūmat-i ʿUthmān. Kayhān-i Andīsha, No 77, Spring 1377 Sh.
  • Dīnawarī, Aḥmad b. Dāwūd al-. al-Akhbār al-ṭiwāl. Qom: Manshūrāt al-Sharīf al-Raḍī, 1368 Sh.
  • Dhahabī, Muḥammad b. al-Aḥmad al-. Tārīkh al-Islām. Edited by ʿUmar ʿAbd al-Salām al-Tadmurī. 2nd edition. Beirut: Dār al-Kitāb al-ʿArabī, 1409 AH.
  • Ghabbān, Muḥammad b. ʿAbd Allāh al-. Fitna maqtal ʿUthmān b. ʿAffān. Medina: al-Jāmiʿat al-Islāmiya, 1419 AH.
  • Gharīb, Maʾmūn. Khilāfat ʿUthmān b. ʿAffān. Cairo: Markaz al-Kitāb li-Nashr, [n.d].
  • Ḥusayn Ṭāhā. Al-Fitnat al-kubrā. Cairo: Hindāwī, 2012.
  • Ḥusayn Ṭāhā. ʿAlī wa fitna-yi buzurg-i qatl-i ʿUthmān. Translated to Farsi by Riḍā Rādī. Gulistān-i Qurʾān, No 10, Spring 1379 Sh.
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Muḥammad. Usd al-ghāba fī maʿrifat al-ṣaḥāba. Beirut: Dār al-Fikr, 1409 AH.
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Abī l-Karam. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār Ṣādir, 1385 AH-1965.
  • Ibn Aʿtham al-Kūfī, Aḥmad b. Aʿtham. Kitāb al-Futūḥ. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār al-Aḍwaʾ, 1411 AH-1991.
  • Ibn Ṭaqṭaqī, Muḥammad b. ʿAlī b. Ṭabāṭabā. Al-Fakhrī fī ādāb al-sulṭānīya wa al-duwal al-islāmīya. Edited by ʿAbd al-Qādir Muḥammad Māyu. 1st edition. Beirut: Dār al-ʿIlm al-ʿArabī, 1418 AH.
  • Ibn al-Jawzī, ʿAbd al-Raḥmān b. ʿAlī. Al-Muntaẓam fī tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Qādir ʿAṭāʾ and Musṭafā ʿAbd al-Qādir ʿAṭāʾ. 1st edition. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1412 AH.
  • Ibn Ḥajar al-ʿAsqalānī, Aḥmad b. ʿAlī. Al-Iṣāba fī tamyīz al-ṣaḥāba. Edited by ʿĀdil Aḥmad ʿAbd al-Mawjūd and ʿAlī Muḥammad Muʿawwaḍ. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1415 AH.
  • Ibn Khaldūn, ʿAbd l-Raḥmān b. Muḥammad. Tārīkh Ibn Khaldūn. Edited by Khalīl Shaḥāda. Second edition. Beirut: Dār al-Fikr, 1408 AH-1988.
  • Ibn Saʿd, Muḥammad. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Qādir ʿAṭā. 1st edition. Beirut: Dar al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1410 AH-1990.
  • Ibn ʿAbd al-Barr, Yūsuf b. ʿAbd Allāh. Al-Istīʿāb fī maʿrifat al-aṣḥāb. Edited by ʿAlī Muḥammad al-Bajāwī. Beirut: Dār al-Jīl, 1412 AH.
  • Ibn al-ʿIbrī, Ghirīghurīyūs b. Hārūn. Tārīkh mukhtaṣar al-duwal. Beirut: Dār al-Sharq, 1992.
  • Ibn Qutayba al-Dīnawarī, ʿAbd Allāh b. Muslim . Al-Imāma wa l-sīyāsa. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār al-Awḍāʾ. 1410 AH-1990.
  • Ibn Kathīr al-Dimashqī, Ismāʿīl b. ʿUmar. Al-Bidāya wa l-nihāya. Beirut: Dār al-Fikr, 1407 AH-1986.
  • Jaʿfarīyān, Rasūl. Tārīkh-i khulafā. Qom: Intishārāt-i Dalīl-i Mā, 1380 Sh.
  • Khalīfa b. Khayyāṭ. Tārīkh-i Khalīfa b. Khayyāṭ. Edited by Muṣṭafā Najīb Fawwāz. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1415 AH.
  • Mufīd, Muḥammad b. Muḥammad al-. Al-Ikhtiṣāṣ. Qom: Kungira-yi Shaykh al-Mufīd, 1413 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Second edition. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1403 AH.
  • Maqdisī, Muṭahhar b. Ṭāhir al-. Al-Badʾ wa l-tārīkh. Port Said: Maktabat al-Thaqāfa al-Dīniyya, [n.d].
  • Naṣr b. Muzāhim Minqarī. Waqʿat Ṣiffīn. Edited by ʿAbd al-Salām Muḥammad Hārūn. Qom: Maktabat Āyatullāh Marʿashī al-Najafī, 1404 AH.
  • Sayyid Raḍī, Muḥammad Ḥusayn. Nahj al-balāgha. Edited by Ṣubḥī Ṣaliḥ. 1st edition. Qom: Hijrat, 1414 AH.
  • Shaykh ʿAbd al-Munʿim. Asbāb al-fitna fī ʿahd-i ʿUthmān. al-Azhar, No 22, 1370 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-Ṭabarī. Edited by Muḥammad Abu l-faḍl Ibrāhīm. 2nd edition. Beirut: Dar al-Turāth, 1387 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Amālī. 1st edition. Qom: Dār al-Thiqāfa, 1414 AH.
  • Thaqafī al-Kūfī, Ibrāhīm b. Muḥammad. Al-Ghārāt. Edited by Mīr Jalāl al-Dīn Ḥusaynī Armawī. Tehran: Intishārāt-i Anjuman-i Āthār-i Millī, 1395 AH.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. 1st edition. Beirut: Dār Ṣādir, [n.p].