Nenda kwa yaliyomo

Kamari

Kutoka wikishia

Kamari au Kucheza kamari (Kiarabu: القمار) ni aina ya mchezo ambao ndani yake kuna sharti la atakayeshindwa anapaswa kumlipa hela mshindi. Mafakihi wote wametoa fat’wa ya kuharamisha kamari; lakini hawauhesabu mchezo wa kubeti katika mashindano ya soka, kupanda farasi, ulengaji shabaha na mchezo wa kushindana kwa kutumia vitara (fencing) kuwa sio kamari. Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihi, kucheza na vifaa vya kuchezea kamari iwe ni kwa kubeti au siyo kubeti ni haramu.

Mafakihi wakiwa na lengo la kutoa fa’twa ya kuharamisha mchezo wa kamari, wametumia hoja mbalimbali ikiwemo Aya ya 90 ya Surat al-Maida ambayo ndani yake inautaja mchezo wa kamari kama uchafu katika kazi za shetani. Mafakihi wanasema kuwa, ni haramu kula chakula ambacho kimepatikana kutokana na njia ya kamari na wanaamini kwamba, ushahidi wa mcheza kamari haukubaliki. Kwa mujibu wa nadharia na mtazamo wa mafakihi, fedha na mali ambayo imepatikana kupitia kamari inapaswa kurejeshwa kwa mwenyewe.

Utambuzi wa Maana

Katika vitabu vya Fiqhi kumetolewa fasili na maana tofauti kuhusiana na kamari. Sheikh Murtadha Ansari anasema, kamari ni kucheza kwa kutumia vifaa maalumu ambapo ndani yake kunawekwa kitu ambacho ni dau ili aje kulipwa atayeshinda. [1]

Baadhi ya mafakihi wengine wanaona mchezo wowote unaochezwa kwa kutumia vifaa vya kuchezea kamari kuwa ni kamari, iwe ni kwa njia ya kubeti au kwa njia nyingine. [2] Ali Mishkini katika kitabu chake Mustalahat al-Fiqh amefafanua kamari kama mchezo ambao mshindwa huweka dau kitu kwa ajili ya kumlipa mshindi. [3]

Hata hivyo, mafaqihi hawatambui kubeti kama kamari. Kwa mujibu wa fat’wa yao, kubeti kwenye mashindano ya kupanda farasi, kulenga shabaha na mchezo wa kushindana kwa kutumia vitara (fencing) sio kamari. Ni kwa msingi huo, ndio maana katika fiq’h kuna michezo inayotajwa kwa jina la Sabq (mashindano ya kupanda farasi) na Remayah (mashindano ya kulenga shabaha). [4]

Hukumu ya Fiq’h

Kwa mujibu wa Sheikh Murtadha Ansari na Sahib Jawahar ni kwamba, mafaqihi wamekubaliana kwa kauli moja juu ya uharamu (wa kucheza) kamari, na Qur'an na hadithi mutawatir (zilizopokewa kwa wingi) zinaonyesha na kuashiria uharamu wake. [5]

Aya ambayo inatumiwa kama hoja katika uwanja huu ni ya 90 katika Surat al-Maida ambapo ndani yake Maisir imetambuliwa kuwa ni uchafu katika kazi za shetani:

((إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالأَنصَابُ وَالأَزْلامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ))
((Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani)).[6]

Kwa mujibu wa hadithi makusudio ya neno Maisir ni kamari. Kwa mfano katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imamu Muhammad Baqir(a.s) na ambayo imenukuliwa katika kitabu cha Kafi, wakati Aya hii iliposhuka, Mtume (s.a.w.w) aliulizwa: Makusudio ya Maisir ni nini: Mtume akajibu: Kila kitu ambacho kupitia kwacho kunachezwa kamari. [7] Kadhalika Sheikh Kulayni katika kitabu hiki hiki, amenukuu kutoka kwa Imamu Ridha (a.s) kwamba, maisir ni kamari. [8]

Nyenzo za Kamari

Makala Asili: Nyenzo za Kamari

Nyenzo za kamari aghalabu ni suhula ambazo hutumiwa kwa ajili ya kuchezea kamari. [9] Katika vitabu vya fiq’h kunajadiliwa masuala kama shataranji (chesi), [10] backgammon (mchezo unaofanana na chesi), [11] karata na biliadi (aina ya mchezo wa kugonganisha mipira midogo kwenye meza maalumu) kama nyenzo na suhula za kamari. [12]

Kwa mujibu wa fat’wa ya mafakihi walio wengi, ni haramu kucheza na nyenzo za kamari iwe ni kwa kubeti au pasi na kubeti. [13] Kadhalika wanasema kuwa ni haramu kutengeneza nyenzo za kamari, kuuza, kununua au kukodisha. [14]

Tofauti ya Kamati na Kubeti

Wengi wa mafaqihi wa zamani, akiwemo Sheikh Sadouq, walichukulia kucheza chess kuwa ni haram; Lakini baadhi ya mafaqihi wa zama hizi, akiwemo Imamu Khomeini, wanaamini kwamba kama chess haitambuliwi kama chombo cha kamari, kucheza nacho si haram.

Mafakihi hawaoni kama hukumu ya Fiqhi ya kamari inajumuisha pia kubeti katika mashindano ya upandaji farasi na ngamia, na vilevile mashindano ya ulengaji shabaha na mchezo wa kushindana kwa kutumia vitara (fencing). [15] Wakitegemea hadithi mbalimbali wanasema, michezo licha ya kuwa ina kubeti lakini haihesabiwi kuwa ni kamari. [16]

Hukumu za Kucheza Kamari

Kwa mujibu wa kile kilichokuja katika vitabu vya Fiqhi baadhi ya hukumu za kucheza kamari ni:

  • Ni haramu kula chakula kilichopatikana kwa njia ya kamari. [17]
  • Ushahidi wa mcheza kamari hakubaliwi. [18]
  • Ni haramu kujifunza kamari. [19]
  • Fedha na mali ambayo imepatikana kwa njia ya kamari, sio halali na lazima irejeshwe kwa mwenyewe. [20]

Falsafa ya Kuharamishwa Kamari

Mwenyezi Mungu anautambulisha mchezo wa kamari kuwa ni uchafu katika kazi za shetani na shetani anataka kutia uadui kati ya waumini na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali.

((إِنَّما يُريدُ الشَّيْطانُ أَنْ يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَداوَةَ وَ الْبَغْضاءَ فِي الْخَمْرِ وَ الْمَيْسِرِ وَ يَصُدَّكُمْ عَنْ ذِكْرِ اللَّهِ وَ عَنِ الصَّلاةِ فَهَلْ أَنْتُمْ مُنْتَهُونَ))
((Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha?))

Kubeti Katika Sheria za Kiraia

Kwa mujibu wa kifungu cha 654 cha sheria ya kiraia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kubeti hakuna itibari na hakuna hatua ya kisheria ambayo inaweza kuchukuliwa kwa mujibu wake. [21] Katika kifungu hicho ni kuwa, maeneo ambayo Fiqhi haijahesabu kuwa ni kamari kama kubeti katika mashindano ya upandaji farasi, ulengaji shabaha na mchezo wa kushindana kwa kutumia vitara (fencing) imeondolewa katika hukumu ya kifungu cha 654. [22]

Rejea

Vyanzo