Nenda kwa yaliyomo

Istidraj

Kutoka wikishia

Istidraj au Emlaa au Imhal (Kiarabu: الاستدراج أو الإملاء أو الإمهال) Ni dhana muhimu katika mtindo na desturi adilifu za Mwenyezi Mungu, ikimaanisha taratibu ya kumfikisha kiumbe au viumbe wake katika adhabu taratibu na hatua kwa hatua. Ni adhabu maalum inayowapata makafiri na wale wanaotenda dhambi ambao wamekuwa na tabia ya kutokushukuru neema za Mwenye Ezi Mungu. Katika hali hii, kwa kadiri wanavyo endelea na kupiga hatua katika dhambi zao, ndivyo Mwenye Ezi Mungu anavyozidi kuwabariki, ili tu kuongeza jeuri na uzembe wao, jambo ambalo mwishowe hupelekea adhabu kali iumizayo. Kwa mujibu wa tafiti za baadhi ya wataalamu, Qur'ani hakutaja tu istidraj ya mtu mmoja mmoja, bali pia istidraj ya kijamii. Kwa mfano, katika Aya ya 48 ya Surat Hajj, Mwenye Ezi Mungu anazungumzia kuhusu kuwapa muhula watu wa mji fulani ambao hawakuwa waadilifu. Hapa, Mwenye Ezi Mungu aliwacheleweshea adhabu yao ili kuongeza kiwango cha dhambi zao, na hatimae walipokea mwisho mbaya na adhabu kali.

Kuneemeshwa kama kuneemeshwa, huwa hakumaanishi istidraj, au ikawa ndiyo kisingizio cha mtu fulani mwenye neema kuambiwa kuwa yupo katika kipindi cha istidraj. Kinachoweza kutupa ishara juu ya istidraj ni yale matendo ya aliyefadhiliwa na Mola wake.Iwapo mja ataneemeshwa kisha akatumia neema hizo kinyuma na matakwa ya Mola wake, kisha bado akawa anazidi kuneemeka, huyo atakuwa amesha ingia katika mtego wa istidraj ya Mwenye Ezi Mungu. Pia imesemwa kwamba; kule watu waovu kuwa na aina fulani za makarama ya kichawi, ni miongoni mwa aina za mitego ya istidraj. Moja ya vitabu muhimu kuhusiana na mada hii, kitabu kiitwacho “Istidraj Suquut Gam be Gam”, ambacho kinatafiti mitego ya istidraj kilicho chapishwa na taasisi ya uchapishaji ya Farhang wa Maarfe Qur’an.

Istidraj, Kuiendea Taratibu Adhabu ya Mwenye Ezi Mungu

«Istidraj» ni neno la kitaalamu ambalo istilahi yake imchukuliwa moja kwa moja kutoka katika Qur'ani. [1] Neno sitidraj lina maana ya kukaribia kitu fulani hatua kwa hatua. [2] Katika mila za Kiislamu, ni miongoni mwa mitindo na desturi adilifu za Mwenye Ezi Mungu, kwa maana ya Mwenye Ezi Mungu kuwafikisha wale wasio tahadhari kutenda makosa na wavukao mipaka, taratibu kwenye adhabu yake. Hii ni kwamba, kila wao wanapozidi kukiuka mipaka ndipo Mwenye Ezi Mungu anapo waneemesha zaidi. Jmabo ambalo huwalevya na kukoleza zaidi maovu yao, hatimae hukubwa na wimbi la adhabu kali ya Mola wao bila kufikiria. [3]

Dhana ya istidraj imekuja mara mbili katika Qur'ani, na mara zote mbili imekuja kwa mfumo wa kitenzi. Moja ni katika Surat Al-A’araaf, ambayo ni Aya ya 182, na ya pili ipo kwenye Surat Qalam ambayo ni Aya ya 44, na zote mbili zimekuja kwa ibara moja isemayo: «سَنَسْتَدْرِجُهُم» “tutawapurusia”. Aya zote mbili zimekuja kuwatahadharisha makafiri, [4] ambapo Aya ya 182 Surat Al-A’araaf imekuja kwa ibara yenye maelezo yasemayo: «Wale wanaozikanusha Aya zetu, tutawapurusia kamba katika njia wasio itambua, na hatimae tutawafikisha kwenye adhabu wanazostahiki».

Mafundisho ya Qur'ani Yanayoeleza Dhana ya Istidraj

Kuna Aya kadhaa za Qur'ani zilizo kuja kuhusiana na suala la istidraj, bila ya kutumia neno «Istidraj», huku zikijadili dhana hii kwa kina na kwa na kwa ufafanuzi wa kutosha. [5] Dhana nyengine zilizo kuja katika Qur'ani, zikiwa na maana sambamba na neno istidraj, ni dhana ya «imlaa» (kupewa muda) pamoja na «imhaal» (kuchelewesha). [6]

Kwa mujibu wa maoni ya Allama Tabatabai katika tafsiri ya Al-Mizan, miongoni mwa Aya zilizokuja kuhusiana nadesturi ya istidraj, ni Aya ya 178 ya Surat Al-Imran, ambapo Allah ndani yake anasema: [7] «Wala wale walio kufuru wasidhani kwamba kupewa kwao muda ni miongoni mwa kheri kwa ajili yao; bali tunawapa muda ili waongeze dhambi zao, na mwishowe wataadhibiwa adhabu idhalilishayo». [8]

Istidraj (Kupuruziwa Kamba) Kijamii

Kulingana na maoni ya baadhi ya watafiti, ni kwamba; pamoja na Qur'ani kuelezea suala la istidraj binafsi, pia imejadili dhana kijamii katika Aya zake mbali mbali. Miongoni mwa ushahidi unaotolewa kwa aina hii ya istidraj, ni Aya ya 48 ya Surat Al-Hajj, [9] Mwenye Ezi Mungu katika Aya hii anasema: «Na ni mara ni mara ngapi niliupa muda mmoja kati ya miji, hali wakiwa ni madhalimu, kisha nikautia mkononi, na hatima yao ni kwangu mimi». [10]

Alama na Dalili za Istidraj

Kulingana na baadhi ya Riwaya katika vyanzo mbali mbali, ni dhahiri kwamba; mara nyingine neema zinaweza kuwa ni dalili za istidraj. Kuleini anamnukuu Imam Ja'far al-Sadiq (a.s) akisema kwamba; “Mtu anayefanya dhambi, kisha Mungu akampuruzishia kamba na kumpa muda pamoja na kuendelea kumneemesha, hadi akajisahau na kuto kuomba msamaha, basi elewa ya kwamba mtu huyo tayari amekwisha nasa kwenye mshipi wa istidraj. [11] Pia, Nahjul Balagha inaeleza kwamba iwapoMungu atampa dhalimu muda wa siku chache, hiyo kamwe haimaanishi kuwa mtu huyo keshateleza na kutoka mikonono mwa Mungu, na wala isidhaniwe kwamba yeye tayari keshaepukika na adhabu za Mwenye Ezi Mungu. [12] [Maelezo 1]

Pia kuna moja ya Hadithi iliyo pokewa kutoka katika Kitabu cha Al-Kafi, isemayo kwamba: “Mtu mmoja alikwenda kwa Imam Ja'afar al-Sadiq (a.s) huku akiwa na hofu moyoni mwake, akisema: "Ewe Mjukuu wa Mtume (s.a.w.w), nilimwomba Mwenye Ezi Mungu anijalie mali, naye kwa rehema zake akaniruzuku mali nyingi. Nikamwomba anibariki kwa kunipa mtoto, naye akanikidhia ombi langu kwa kunijaalia kupata mtoto. Kisha, nikamwomba nyumba, na kwa uweza wake akaniwezesha kupata nyumba. Lakini sasa, nina hofu kubwa kwamba kujibiwa kwa maombi haya yote, kwani huenda hii ikawa ni dalili ya istidraj". Imam al-Sadiq, kwa hekima zake, alimjibu kwa utulivu kabisa akisema: "Ewe mja wa Mwenyezi Mungu, ikiwa utaweza kutekeleza shukrani kutokana na neema hizi ulizo jaaliwa na Mwenye Ezi Mungu, basi jua kwamba hii siyo dalili ya istidraj. [13]

Fakhr al-Razi, mfasiri na mwanatheolojia wa kutoka upande wa Ahlu-Sunna wa Karne ya Sita Hijria, anatambulika sana kwa mchango wake mkubwa katika tafsiri ya Qur'ani na teolojia ya Kiislamu. Katika maoni yake, al-Razi anaamini kwamba; ule uwezo wa baadhi watu watendao dhambi kufanya mambo ya maajabu na yasiyo ya kawaida, ni moja ya mifano halisi ya dhana ya istidraj. [14] al-Razi anasisitiza kwamba; kupitia uwezo huu wa kufanya mambo ya maajabu, mtu huyo hapati chochote zaidi ya kuongezeka kwa kiburi chake, majivuno, na kujiona bora kuliko wengine. Hali hii, kwa mujibu wa al-Razi, inamfanya mtu huyo kutumbukia zaidi katika upotovu na kujiweka mbali na njia sahihi ya Mwenye Ezi Mungu. Kwa hivyo, istidraj, kama inavyoelezwa na al-Razi, ni mchakato wa Kimungu unao wawezesha watenda dhambi kuendelea katika njia zao potofu kwa kupewa fursa za kufanya mambo makubwa makbwa, lakini mwisho wake ni kuangamia kwao kutokana na kiburi na upotovu wao. [15]

Kulingana na Murtadha Mutahhari, mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu wa upande wa madhehebu ya Kishia, ana mtazamo wa kipekee kuhusiana na dhana hii ya istidraj. Kwa mujibu maoni wake; kupata neema na baraka kwa upande mmoja hakuwezi kuchukuliwa kama dalili ya kuingia katika istidraj. Hii ni kwa sababu kile kinachobainisha kuwa mtu fulani yuko katika hali ya istidraj au la, ni jinsi ya yeye anavyo kabiliana neema hizo alizo jaaliwa na Mola wake. Mutahhari anaeleza kwamba endapo mneemeshwa atashukuru kutokana na neema hizo na kuzitumia katika njia inayompendeza Mwenye Ezi Mungu, basi hatakuwa kwenye hatari ya istidraj. Shukrani na matumizi sahihi ya neema ni njia ya kumridhisha Mwenye Ezi Mungu, na ndiyo dalili ya ioneshayo kwamba tuko kwenye njia sahihi. Hata hivyo, anatoa onyo kwamba ikiwa tutajivuna kwa sababu ya neema tulizopewa, au tutaendekeza matamanio yetu na kuhadalika kwa matendo mabaya, ubadhirifu au kuzitumia neema hizo katika njia zisizompendeza Mungu, basi tuelewe kwamba tayari tumeshaingia kwenye mtego wa istidraj. Katika hali hii, neema hizo zinaweza kuwa ndiyo sababu ya kuanguka kwetu, kwa kuwa zinatufanya tuzidi kupotoka na kujiweka mbali na njia ya haki. [16]

Monografia

Kitabu «Istidraj Suquut Gam be Gam» "Kupuruziwa kamba Kuanguka Polepole" ni utafiti wa kina na wa kipekee kuhusiana na dhana ya istidraj, uliofanywa na Taasisi ya Farhang wa Maarife Islamiy/ Kituo cha Utamaduni na Maarifa ya Qur'ani, na kuchapishwa mwaka 1386 Hijria (2007 Miladia). [17] Kitabu hichi kinajadili mada mbalimbali ndani yake, ikiwa ni pamoja na maana ya istidraj, ugumu wa adhabu ya istidraj, sababu na dalili au alama za istidraj. [18]

Maelezo

  1. لَئِنْ أَمْهَلَ [اللَّهُ] الظَّالِمَ فَلَنْ يَفُوتَ أَخْذُهُ وَ هُوَ لَهُ بِالْمِرْصَادِ

Rejea

Vyanzo