Istibra

Kutoka wikishia

Istibra (Kiarabu: الاستبراء (فقه)) ni kitendo cha mustahabu ambacho kinapendekezwa kufanywa na wanaume baada ya kutoka manii au mkojo, ili kwa njia hiyo kusafisha na kuondoa mabaki ya mkojo au manii katika njia ya mkojo. Istibra maana yake ni kusafisha kitu, kuondokana na kitu. Hapa ina maana ya kuondokana na matone ya mkojo kutoka kwenye uume. Kwa mujibu wa hukumu za fiq'h, kama mtu ambaye amefanya istibra' kisha baadaye akaona unyenyevu na umajimaji usioeleweka na wa kutia shaka ambao umetoka katika njia ya mkojo, basi anauhesabu kuwa ni msafi na tohara na haubatilishi udhu au ghusli (josho).

Miongoni mwa baadhi ya faida na matumizi mengine ya istibra katika Fiqhi ni: Kumfanyia istibra mnyama (ambaye nyama yake inaliwa) anayekula najisi (kumzuilia na kumshikilia kwa muda mnyama ambaye nyama yake ni halali kuliwa ambaye amezoea kula kinyesi, kwa ajili ya kuifanya nyama na maziwa yake kuwa masafi na kuondokana na najisi) na istibra ya hedhi (kuchunguza uke baada ya kukatika damu ya hedhi).

Utambuzi wa maana na matumizi

Aghalabu istibra huitwa kile kitendo ambacho ni mustahabu na ambacho hufanywa na mwanaume (cha kukamua uume wake) baada ya kutoka manii au mkojo ili kusafisha mabaki ya mkojo au manii katika njia ya mkojo. [1] Neno istibra katika fikihi lina matumzi mengine pia kama: Kumfanyia istibra' mnyama (ambaye nyama yake inaliwa) anayekula najisi (kumzuilia na kumshikilia kwa muda mnyama ambaye nyama yake ni halali kuliwa ambaye amezoea kula kinyesi, kwa ajili ya kuifanya nyama na maziwa yake kuwa masafi na kuondokana na najisi) na istibra' ya hedhi (kuchunguza uke baada ya kukatika hedhi).

Namna ya kufanya istibra

Namna ya kufanya istibra: Ni kukamua kwa kidole cha kati cha mkono wa kushoto kuanzia njia ya haja kubwa mpaka kinapoanzia kiungo cha mkojo mara tatu; kisha unashikilia kiungo cha mkojo kati ya dole gumba na vidole vya mbele, kamua mara tatu kuanzia kinapoanzia kiungo cha mkojo mpaka kwenye kichwa; na kamua kichwa chenyewe mara tatu. [2]

Kufanya istibra ya manii ni kama istibra ya mkojo hakuna tofauti katika ufanyaji wake. Hata hivyo istibra ya manii inapaswa kufanyika baada ya kukojoa (mkojo). Kwa maana kwamba, aliyefanya tendo la ndoa au ametokwa na manii, kabla ya kufanya istibra anapaswa kukojoa kwanza. Pamoja na hayo baadhi ya mafaqihi wanaamini kwamba, kukojoa mkojo baada ya kutokwa na manii inatosha na hakuna haja ya kufanya istibra ya manii. [3]

Kuwa tohara umajimaji wa kutia shaka baada ya istibra

Kwa mujibu wa fat'wa ya kifiq'h ni kwamba, kama umajimaji au unyevunyevu utatoka kwenye kiungo cha mkojo cha mtu baada ya kukojoa, na akatia shaka iwapo huo ni mkojo au kitu kingine, basi anaweza akachukulia kuwa ni tohara kama amefanya istibra, na hivyo udhu au ghusl yake haviwezi kubatilika; [4] lakini kama hakufanya istibra basi lazima auchukulie unyevunyevu huo kuwa ni najisi na unabatilisha udhu wake. [5] Kwa mujibu wa fat'wa mashuhuri, kama mtu ataoga janaba baada ya kutokwa na manii, lakini bila ya kufanya istibra na kisha baadaye ukatoka umajimaji katika njia ya mkojo na asifahamu kwamba, ni manii au kitu kingine anapaswa kuoga tena janaba. [6]

Je, wanawake wanapaswa kufanya istibra' pia?

Wanazuoni na mafakihi wamehitalifiana kimtazamo kuhusiana na je wanawake nao wanapaswa kufanya istibra au la. Hata hivyo wengi miongoni mwao wanaamini kwamba, kuwa mustahabu istibra ni makhsusi kwa wanaume tu. [7] Majimaji yanayotoka katika njia ya mkojo ya mwanamke baada ya kukojoa au kutokwa na manii hata kama hakutakuwa kumefanyika istibra ni masafi na tohara. [8] Pamoja na hayo, imeelezwa kwamba, ni bora kwa mwanamke baada ya kukojoa asubiri kidogo kisha ajikoholeshe na kukandamiza uuke wake. [9] Allama Hilli anaamini kwamba, istibra ipo pia kwa wanawake, [10] hata hivyo hakubainisha namna ya ufanyikaji wake. [11]

Kumfanyia istibra mnyama anayekula najisi

Istibra inafanyika pia kwa mnyama ambaye nyama yake ni halali kuliwa lakini amezoea kula najisi; kwa msingi huo ili kuhalalisha maziwa na nyama ya mnyama ambaye nyama yake ni halali kuliwa ambaye amezoea kinyesi cha binadamu, ni lazima kumzuia kufanya hivyo kwa muda fulani. [13] kwa maana kwamba, utamfungia sehemu mnyama huyo na kumzuia kula kinyesi kwa muuda fulani. Muda wa istibra kwa wanyama unatofautiana kulingana na aina ya mnyama wenyewe; Sheikh Tusi anasema kuwa, muda wa istibra kwa ngamia ni siku 40, ng'ombe ni siku 20, kondoo ni siku 10 au 7 na kuku ni siku tatu. [13]

Istibra ya damu ya hedhi

Kuchunguza uke baada ya kukatika damu ya ada ya mwezi (hedhi): Kwa mujibu hukumu za fiq'h, ikiwa damu ya hedhi itakoma kabla ya siku kumi na mwanamke akashuku kuwa damu imesalia kwenye uterasi (mji wa mimba) yake, anapaswa kuingiza pamba kwenye uke wake, [14] kisha aitoe. Ikiwa pamba haijachafuliwa na damu, basi mwanamke huyo ni msafi kutokana na hedhi, vinginevyo angoje mpaka iwe safi. [15]

Rejea

Vyanzo

  • Ḥakīm, Muḥsin. Mustamsak al-ʿUrwat al-wuthqā. Qom: Muʾassisat Dār al-Tafāsīr, 1416 AH.
  • Ḥillī, al-Ḥasan b. Yūsuf al-. Muntahā l-maṭlab fī taḥqīq al-madhhab. Mashhad: Majmaʿ al-Buḥūth al-Islāmīyya, 1412 AH.
  • Najafī, Muḥammad al-Ḥasan al-. Jawāhir al-kalām fī sharḥ sharāʾiʿ al-Islām. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1404 AH.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Man lā yaḥḍuruh al-faqīh. Edited by Ali Akbar Ghaffari. Qom:, Intishīrīt-i Islāmī, 1413 AH.
  • Shahīd al-Thānī, Zayn al-Dīn b. ʿAlī. Rawḍ al-jinān fī sharḥ Irshād al-adhhān. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt , [n.d.].
  • Ṭabāṭabāʾī Yazdī, Muḥammad Kāẓim al-. Al-ʿUrwat al-wuthqā. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn, 1419 AH.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥaasn al-. Al-Khilāf. Edited by ʿAlī Khurāsānī et.al. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1407 AH.