Hifdh al-Qur’an

Kutoka wikishia

Hifdh al-Qur’an (Kiarabu: حفظ القرآن / استظهار القرآن) ni kuhifadhi kwa moyo Aya za Qur’an Tukufu. Jambo hili lina thawabu nyingi na thawabu zimeahidiwa katika hadithi. Katika hadithi, Mtume (s.a.w.w) ametambulisha hadhi na daraja ya hafidh al-Qur’an (aliyehifadhi Qur’an) kwa watu kama hadhi yake juu ya wanadamu wengine. Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria na hadithi, mtu wa kwanza kuhifadhi Qur'an alikuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Idadi ya mahafidhi wa Qur'an katika zama za Mtume haijulikani. Hata hivyo, katika baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, idadi ya mahafidhi wa Qur'an katika mwaka wa nne wa Hijiria ilikuwa zaidi ya watu 70.

Kuna njia mbalimbali za kuhifadhi Qur'ani, bora zaidi ni kuhifadhi taswira ya Aya. Nchi za Kiislamu kama vile Iran, Malaysia, Misri, Jordan, Libya na Saudi Arabia hufanya mashindano ya kila mwaka kupima mahafidhi wa Qur'ani. Mnamo mwaka 2013, Sayyid Ali Khamenei, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliziomba mamlaka za masuala ya kiutamaduni nchini Iran kulea na kuandaa mahafidhi milioni 10 wa Qur'an.

Utambuzi wa maana

Hifdh al-Qur’an ni kuhifadhi kwa moyo Aya za Qur’an Tukufu. [1] Baadhi ya wahakiki wakitegemea ripoti za historia wanasema historia ya kutumiwa neno Hifdh al-Qura’n kwa maana hii inarejea katika nusu ya karne ya pili Hijiria. [2] Kulingana na mwandishi wa makala ya kuhifadhi Qur'an katika Ensaiklopidia ya Ushia, mwanzoni mwa Uislamu, wale waliohifadhi Qur'an walikuwa wakijulikana kwa majina kama ya Jamma'a Al-Qur'an na Hamalat al-Qur'an. [3] Neno hifdh yaani hifadhi katika lugha ya Kiarabu lina maaana mbili ambapo ya kwanza ni kutunza na kuhifadhi na ya pili ni kukumbuka na kusoma kwa moyo kitu bila ya kuangalia. [4]

Katika istilahi ya sayansi ya Quran (Ulum al-Qur’an) mtu anayesoma Qur'an kwa tajweed, tartil na kanuni nyinginezo anaitwa hafidh; vile vile, mtu ambaye anafahamu Sunnah za Mtume (s.a.w.w) na hali na wasifu wa wapokezi wa hadithi pamoja na daraja za masheikh pia huitwa Hafidh.[5]

Nafasi

Baadhi ya watafiti kwa kuzingatia mlengwa na mhutubiwa katika Aya za mwanzo za Surah Al-Alaq ambapo Aya ya kwanza inasema: ((Iqra; yaani Soma)), wanaamini kuwa, usomaji wa Qur'an kwa moyo ni hatua ya kwanza ya usomaji, na kuandika Qur'an ni hatua inayofuata. [7] Kwa msingi huu, katika historia ya Qur’an Ramiyar ametambuliwa kuwa hafidhi wa kwanza wa Qur’an. [8] Tabatabai, mfasiri wa zama zetu hizi wa Qur'an, amezingatia maana ya dhikr (kukumbuka) katika Aya ya 34 ya Surah Al-Ahzab kuwa ni kuhifadhi Qur'an, [9] pia Tabarsi ameorodhesha maana ya kuifanya Qur'an kuwa nyepesi kufahamika iliyozungumziwa katika Aya ya 17 ya Surat al-Qamar kuwa ni kuhifadhi Qur'an. [10]

Kwa mujibu wa mwandishi wa makala ya kuhifadhi Qur'ani katika Ensaiklopidia ya Ulimwengu wa Kiislamu, kuhifadhi Qur'an kulizingatiwa kuwa ni aina ya ubora na upendeleo mwanzoni mwa Uislamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana, wakati mwingine vijana walikuwa wakitangulizwa na kufanywa Maimamu wa Sala ya Jamaa mbele ya wengine kutokana na kuwa ni mahafidhi wa Qur'an au katika vita vya Uhud, mashahidi waliohifadhi Qur'an walizikwa karibu na Hamza, ami yake Mtume (s.a.w.w). [11]

Kwa mujibu wa Shahidi Thani (aliyefariki dunia: 965 AH), wanazuoni wa zamani waliamini kwamba “kuhifadhi Qur’an” ni elimu inayopaswa kutangulizwa mbele ya elimu zote. Walifundisha fiqhi na hadithi kwa wale tu waliohifadhi Qur'an. [12]

Kuna njia mbalimbali za kuhifadhi Qur'an, bora zaidi ni kuhifadhi taswira ya Aya. Nchi za Kiislamu kama vile Iran, Malaysia, Misri, Jordan, Libya na Saudi Arabia hufanya mashindano ya kila mwaka kupima mahafidhi wa Qur'an. [13]

Sayyid Ali Khamenei, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliziomba mamlaka za kiutamaduni nchini Iran kulea na kuandaa mahafidhi milioni 10 wa Qur'an. [14] Kwa mujibu wa Mehdi Qarasheikhlou, mmoja wa maafisa wa Mradi wa Kitaifa wa Kuhifadhi Qur'an Tukufu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hadi mnamo mwaka 1400, hakukuwa takwimu sahihi za idadi ya mahafidhi wa Qur'an nchini Iran. [15] Hata hivyo, baadhi wamekadiria idadi ya mahahifidhi wa Qur'ani nchini Iran kuwa karibu 20,000 au 30,000. [16]

Fadhila za kuhifadhi Qur’an

Kulayni, mmoja wa wafasiri mashuhuri wa Kishia, amekusanya hadithi zinazohusu ubora wa kuhifadhi Qur’an katika sura inayojitegemea. [17] Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, haifai kwa hafidhi wa Qur’an kudhani kwamba Mwenyezi Mungu amempatia mtu mwingine kitu bora kuuliko alichompatia yeye (yaani hifdh al-Qur’an). [18] Mtume aliwatambulisha mahafidhi wa Qur'an kuwa ni viongozi wa umma wake na akawaweka katika nafasi na daraja ya baada ya Mitume na wanachuoni.[19] Kulingana naye, wale wanaowalaumu au kuwavunjia heshima wabebaji wa Qur'an watalaaniwa na Mwenyezi Mungu, [20] na uombezi wa mahafidhi wa Qur'an utakubaliwa kwa watu kumi wa familia zao ambao wameandikiwa moto. [21]

Kwa mujibu wa kile ambacho Kulayni akinukuu kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s), anasema, idadi ya daraja za mbinguni ni sawa na Aya za Quran, na Siku ya Kiyama, hafidhi wa Qur'an ataitwa kuisoma Qur'an na kwenda juu kadiri anavyosoma Qur’an na daraja ya juu kabisa ya pepo ni ya mahafidhi wa Qur’an. [22] Kwa mujibu wa Jawadi Amoli, mwanafalsafa na mfasiri wa Qur’an, kuhifadhi na kusoma Qur’an kidhahiri peke yake hakutoshi kufikia daraja na fadhila hizi; bali, kwa mujibu wa riwaya nyinginezo, kuzifuata Aya za Mwenyezi Mungu ndilo sharti kuu la kukubaliwa amali yake. Anaamini kwamba katika Siku ya Kiyama, mtu atakuwa na uwezo wa kusoma tu Aya ambazo amezifanyia kazi. [23]

Licha ya hadithi hizi, Imamu Swadiq (a.s) aliona kusoma Aya za Qur’an juu ya msahafu (kwa kuangalia) kuwa ni bora na yenye thawabu zaidi kuliko kuhifadhi. Ameeleza sababu ya msemo huu ni faida ya macho kwa kuangalia Aya za Qur'an. [24]

Hifdh zilizosahaulika

Kwa mujibu wa baadhi ya mafaqihi, kuhifadhi Qur'an ni mustahabu. [25] Hata hivyo, baadhi ya hadithi zinakumbusha matokeo machungu kwa wale wanaohifadhi Qur’an au sura kisha wakaisahau. Kwa hivyo, riwaya hizi zimewafanya baadhi ya mafaqihi kuhukumu juu ya uharamu [26] au makuruhhu ya kuisahau Qur'an baada ya kuihifadhi, au juu ya kuwa mustahabu au wajibu juu ya kuendelea katika kuisoma Qur'an ili kutoisoma kupelekee kusahau. [27] Kwa upande mwingine, baadhi, wakirejelea riwaya zinazokinzana, hawakuona maana ya kusahaulika katika kundi hili la riwaya kuwa ni kusahau maneno ya dhahiri ya Qur’an; bali wameiona kuwa ni dalili ya kuacha tabia na kuacha mafundisho ya mwongozo ya Qur'an, kwa namna ambayo inasahaulika kwa sababu ya uzembe na kusababisha Qur'an kuachwa na kuhamwa. [28]

Njia mbalimbali za kuhifadhi Qur'an

Ili kuhifadhi Qur'an kuna njia na mbinu mbalimbali zilizozoeleka kama kuhifadhi kwa kusikiliza, kimafuhumu na kitaswira. [29] Idadi ya mbinu za kuhifadhi Qur'an zimetajwa kuwa zaidi ya 20 [30] na njia bora kabisa ya kuhifadhi Qur'an ni kukumbuka Aya zake kwa taswira. [31] Katika mbinu hii, baada ya kusoma Aya, mhusika hufanya hima ya kuhifadhi na kuweka katika kumbukumbu yake nafasi ya kijiografia ya Aya katika ukurasa mmoja, namna ya kuandikwa maneno na herufi na kadhalika kwa sura makini. [32]

Idadi ya mahafidhi wa Qur'an

Watafiti wanaamini kuwa, mwanzoni mwa Uislamu mahafidhhi wa Qur'an walikuwa wengi sana lakini hakuna idadi kamili inayofahamika. [33] Syuti akiwa na lengo la kuthibitisha ukweli wa madai haya, ametumia idadi ya waliouawa katika vita vya Uhud, vita vya Bi'r Mauna na vita vya Yamama kama hoja. [34] Akitegemea nukuu za waandishi wa historia amesema kuwa, katika vita vya Uhud waliuawa shahidi masahaba 74 ambao wengi wao walikuwa mahafidhi wa Qur'an. Kadhalika katika mwezi Safar mwaka wa nne Hijiria kulitokea vita vya Bi'r Mauna ambapo waliuawa shahidi takribani mahafidhi 40 au 70 wa Qur'an. Baada ya kuaga dunia Bwana Mtume (s.a.w.w), katika vita vya Yamama pia Waislamu 1200 waliuawa ambapo inaelezwa kuwa miongoni mwao walikuwemo masahaba 450 au 700 na mahafidhi wa Qur'an. [35]

Suyuti anasema kuwa, miongoni mwa wanaume ambao walikuwa mahafidhi mashuhuri katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) ni Imamu Ali (a.s), Ubayy bin Kaab, Abu al-Dardar, Muadh bin Jabal, Zayd bin Thabit, Abdallah bin Masoud n.k na kwa upande wa wanawake mahahafidhi mashuhuri walikuwa Fatima Zahra (a.s), Fidhah, Aisha na Hafsa. [36]

Baadhi wakitegemea baadhi ya nyaraka wamemtambulisha Hafidh Shirazi kuwa hafidhi wa Qur'an yote. Wanaamini kwamba, hata kutambulika kwake zaidi kwa jina la Hafidh kulitokana na kuhifadhi kwake Qur'an. [37] Kadhalika inaelezwa kuwa, Karbalai Kadhim Saruqi, mzee mkulima na ambaye hakusoma (hakuwa akijua kusoma wala kuuandika) alikuwa akiishi katika eneo la Saruq katika mji wa Arak nchini Iran ambapo kutokana na kuwa na unyeti maalumu na kuzingatia mno suala la kutoa Zaka na kuchuma mali ya halali aliondokea kuwa hafidhi wa Qur'an kimuujiza. [38]

Abul-Qassim Khaz'ali (aliaga dunia: 1394 Hijiria Shamsia) Sheikh na mwanazuoni wa Kishia na Muhammad Taqi Bahlul (aliaga dunia: 1384 Hijiria Shamsia) wanahesabiwa kuwa na mahafidhi wengine wa Qur'an Tukufu. [39]

Monografia

Kumeandikwa vitabu vingi kuhusiana na mahafidhi na mbinu mbalimbali za kuhifadhi Qur'an Tukufu. Baadhi ya vitabu hivyo ni:

  • Mu'jam Hhuffadh al-Qur'an Abr al-Tarikh, mwandishi Muhammad Salim Muhaysin: Katika kitabu hiki mwandishi anataja na kueleza maisha ya makumi ya mahafidhi na maqarii (wasomaji) wa Qur'an.
  • Ma'arifat al-Qurra al-Kibar Aal al-Tabaqat Wal-Asar au Tabaqat al-Qurra, mwandishi wa kitabu hiki ni Shamsuddin Muhammad bin Ahmad bin Othman Dhahabi: Katika kitabu hiki mwandishi amekusanya majina ya maqarii na mahafidhi wa Qur'an kwa sura ya mafungu mafungu.
  • Usul va Raveshihay Hifz Qur'an, mwandishi Sayyid Ali Mirdamad Najafabadi: Kitabu hiki kimechapishwa na Kituo cha Kimataifa cha Tarjuma na Usambazaji cha al-Mustafa. Katika kitabu hiki mwandishi mbali na kueleza umuhimu wa kuhifadhi Qur'an anabainisha misingi na utangulizi wa kuhifadhi Qur'an.

Masuala yanayo fungamana