Dua ya thelathini na saba ya Sahifa Sajjadiyya
Dua ya thelathini na saba ya Sahifa Sajjadiyya: ni miongoni mwa dua zilizopokewa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s). Nayo ni maalumu kuhusiana na udhaifu na mapungufu ya mwanadamu katika kumshukuru Mwenye Ezi Mungu. Katika dua hii, Imamu Sajjad (a.s) anatukumbusha kwamba; hakuna mje mwenye uwezo wa kutoa shukrani kamilifu juu ya neema alizoneemeshwa na Mwenye Ezi Mungu. Kupitia dua hii, Imamu Sajjad (a.s) anatutanabahisha ya kwamba; neema tuzipatazo kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu, ni matunda ya fadhila na ukarimu Wake, (na si kwa sababu ya juhudi zetu). Dua hii pia inafundisha kwamba Mwenyezi Mungu hacheleweshi adhabu kwa watenda maovu kwa matumaini kuwa watatubu na kurejea katika uongofu. Hatimaye, Imam Zainul Abidin (a.s.) anadokeza kuhusu uadilifu wa Mungu katika kuamiliana na waja Wake na anaeleza kuwa kupotoka kutoka kwa njia nyoofu ni kwa sababu ya hadaa za Shetani. Kuna kazi andishi kadhaa zilizoandikwa kwa lugha mbali mbali, kwa ajili ya kutoa tafsiri chambuzi za Dua ya thelathini na saba samba na dua nyengine zilizomu ndani ya kitabu cha Sahifa Sajjadiya. Miongoni mwa vitabu vya Kifarsi viliovyoshugulikia kazi hiyo ni pamoja na; 'Diar-e Asheghan', kitabu kilichoandikwa na Hussein Ansarian, pamoja na 'Shuhud wa Shinakht', kazi ya Hassan Mamduhi Kermanshahi. Ama kwa upande wa lugha ya Kiarabu, katika mashuhuri kilichutumikia kazi hiyo, ni kitabu kiitwacho 'Riadhu as-Salikin', kilichoandikwa na Sayyid Ali Khan Madani. Mafunzo ya Dua ya Thalathini na Saba Dua ya thelathini na saba, kutoka katika kitabu cha Sahifa Sajjadiya, ni dua maalumu inatupa welewa wa kutambua kwamba; katu mwanadamu hawezi kumshukuru Mwenye Ezi Mungu kikamilifu (ipaswavyo). Katika dua hii, Imamu Sajjad (a.s) anaonesha jinsi ya mwanadamu alivyo na mapungufu katika kutoa shukrani stahiki kwa Mola wake. [1] Kwa mujibu wa maoni ya Mamduhi Kermanshahi (mmoja wa wafasiri na wachambuzi wa Sahifa Sajjadiyya), ni kwamba; Miongoni mwa vyeo vya kiroho vilivyo juu zaidi mno, ambacho hakiwezi kufikiwa na watu wa kawaida, isipokuwa ni maalumu kwa wateule na waliotakaswa na Mwenye Ezi Mungu, ni kile cheo cha mtu kuweza kufikia hatua ya kutambua kwamba katu yeye hana uwezo wa kuzishukuru neema za Mungu ipasavyo. [2]
Mafunzo Yaliyomo Ndani ya Dua ya Thalathini na Sabu Yamebainishwa katika vipengele vifuatavyo: • Udhaifu wa mja katika kumshukuru Mola wake juu ya mfululizo wa fadhila na neema Zake endelevu. • Mapungufu ya mja katika kumtii na kumwabudu Mola wake ipasavyo. • Kuishukuru neema ni jambo adhimu (ni neema kubwa zaidi) kuliko neema yenyewe. • Umuhali wa mja wa kuteweza kutoa shukrani kamilifu juu ya neema alizopewa na Mwenye Ezi Mungu. • Kutowepo uwezekano wa kutoaji amri au hukumu dhidi ya Mungu, kunatokana na kutowepo kwa kiumbe mwenye mamlaka dhidi Yake. • Fadhila za Mwenye Ezi Mungu ndio chimbuko la kupata radhi na maghufira Yake. • Uwezo wa mja wa kumshukuru Mola wake, ni taufiki maalumu itokanayo na fadhila za Mwenye Ezi Mungu. • Wema, ukarimu na msamaha ni miongoni mwa desturi na tabia ya Mwenye Ezi Mungu. • Ukarimu wa Mwenye Ezi Mungu wa kutoa thawabu kubwa kwa matendo machache ya waja wake. • Uhakika wa msamaha wa Mwenye Ezi Mungu kwa wake, hata kama waja hao hawastahili kupata msamaha huo. • Umuhimu kujipamba kwa tabia za Mwenye Ezi Mungu, ili kupata taufiki ya kushukuru neema zake. • Viumbe wote ni wenye kukiri uadilifu na fadhila za Mwenye Ezi Mungu katika muamala wake nao. • Udanganyifu wa Shetani ndiyo sababu kuu ya kupotea na kutengana na njia ya Mwenye Ezi Mungu. • Udanganyifu wa Shetani kupitia njia ya kuijenga batili katika sura ya haki. • Uvumilivu wa Mwenye Ezi Mungu katika kuchelewesha waasi adhabu Yake. • Mwenendo wa ukarimu wa Mwnye Ezi Mungu katika kuamiliana na watiifu na mwenye dhambi. • Utiifu wa kumtii Mwenye Ezi Mungu ni natija ya uwezeshaji wa kiroho utokao Kwake. • Ueneaji wa Rehema ya Kimungu unaowakumbatia waja wote kwa jumla. • Dhana ya kwamba; thawabu za matendo mema si haki halisi inayomstahikia yeye kutokana na matendo yake, bali ni hisani ya Mwenye Ezi Mungu. • Utoaji wa Mwenye wa riziki isiyo na kipimo, usiambatane na matarajio ya shukrani wala malipo. • Hadhi ya utukufu wa Mwenye Ezi Mungu isiyo na ukomo inayojidhihirisha katika muamala wake na waasi. • Sifa ya ukubwa wa uasi wa mja inayosimama mbele ya upana usio na kifani wa rehema na subira ya Mwenye Ezi Mungu. • Uadilifu wa Mwenye Ezi Mungu, ndicho chanzo pekee cha kumkhofu Yeye. • Kuhifadhiwa kwa wenye dhambi kutokana na kufikwa na Dhulma itokayo kwa Mwenye Ezi Mungu (kwa kuwa Allah si mwenye kudhulumu). • Ucheleweshaji wa adhabu ya waja kwa matumaini ya toba na kurudi kwenye uongofu wa Mwenye Ezi Mungu. • Kupata mafanikio ni matokeo ya kuwa chini ya uongozi wa Mungu. • Uhakika wa malipo ya Mwenye Ezi Mungu kwa wale wanaomtii. • Uthibitisho na ungamo la kuamini uadilifu mkuu wa Mwenye Ezi Mungu.
Maelezo Kuna wanzuoni wengi walijitahidi kufasiri dua za Sahifa Sajjadiyya, ikiwemo dua ya thelathini na saba ya kitabu hicho. Miongoni mwa vitabu chambuzi vilivyofasiri na kuchambua dua hizo kwa lugha ya Kifarsi ni pamoja na; kitabu Diare Asheqan, kilichoandikwa na Hossein Ansarian, [4] Shuhud wa Shenakht, kilichoandikwa na Muhammad-Hassan Mamduhi Kermanshahi, [5] na Sharhe wa Tarjomeh Sahifat Sajjadiyya, kilichoandikwa na Sayyid Ahmad Fahri. [6] Aidha Dua hii imefasiriwa na kufafanuliwa kwa Kiarabu sambamba na dua nyengine za kitabu cha Sahifa sajjadiyya kupitia kazi maridadi za wanazuoni waliotenga muda wao kwa ajili ya kazi hiyo. Miongoni kazi hizo zlizoandikwa kwa lugha ya Kiarabu ni pamoja na; Riyadh as-Salikin, kazi ya Sayyid Ali Khan Madani, [7] Fi Dhilal as-Sahifat as-Sajjadiyya, kazi ya Muhammad Jawad Mughniyah, [8] kitabu Riadhu al-Arifina, kilioandikwa na Muhammad bin Muhammad Darabi [9] na Afaqi ar-Ruh, kazi iliyofanywa na Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah. [10]. Aidha, kuna wanazuoni maalumu waliokusanya maneno na msamiati uliyotumika katika dua hii sambamba na dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya, na kuufafanuliwa kwa mfumo wa kilugha ili kurahisisha welewa wa maana za zilizomo ndani ya Sahifa Sjjadiyya. Miongoni matunda ya kazi ni pamoja na; Ta'aliqati 'ala as-Sahifat as-Sajjadiyya, kazi ya Fadhu Kashani [11] na Sharhu as-Sahifat as-Sajjadiyya, kazi iliyofanywa na Izzu al-Din al-Jazairi. [12] Matini ya Dua Pamoja na Maelezo Yake kwa Kisdwahili
وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ عَلَيْهِ السَّلَامُ إِذَا اعْتَرَفَ بِالتَّقْصِيرِ عَنْ تَأْدِيَةِ الشُكْرِ Na ifuatayo ilikuwa miongoni mwa dua zake, (amani iwe juu yake), aliyokuwa (akiitumia) kwa ajili ya kukikiri upungufu yake katika kutoa shukrani (za Mwenye Ezi Mungu) ipasavyo. اللَّهُمَّ إِنَّ أَحَداً لَا يَبْلُغُ مِنْ شُكْرِكَ غَايَةً إِلَّا حَصَلَ عَلَيْهِ مِنْ إِحْسَانِكَ مَا يُلْزِمُهُ شُكْراً. Ewe Mwenyezi Mungu, ni dhahiri kwa hakuna kiumbe yeyote yule anayeweza kufikia ukomo wa kukushukuru (ukomo wa kushukuru neema Zako), kwani kila hatua ya moja ya shukrani zake huambatana na fadhila nyengi mpya kutoka Kwako, inayomlazimisha mja kuanzisha tena upya mzunguko wa shukuru zake juu ya neema hizo. وَ لَا يَبْلُغُ مَبْلَغاً مِنْ طَاعَتِكَ وَ إِنِ اجْتَهَدَ إِلَّا كَانَ مُقَصِّراً دُونَ اسْتِحْقَاقِكَ بِفَضْلِكَ Na kamwe hakuna mja awezaye kutimiza haki ya utiifu kwa Mola wake, hata kama atafanya juhudi kubwa namna gani. Siku zote atabakia kuwa ni mpungufu katika kukutii Wewe kama unavyostahiki kutokana na zile fahdila Zako (kwa waja Wako). فَأَشْكَرُ عِبَادِكَ عَاجِزٌ عَنْ شُكْرِكَ، وَ أَعْبَدُهُمْ مُقَصِّرٌ عَنْ طَاعَتِكَ Basi mshukurivu zaidi wa waja wako ni mshindwa wa kutimiza shukrani Zako ipaswavyo, na mchamungu wao zaidi kati ya waja wako, ni mpungufu wa kukutii ipaseavyo. لَا يَجِبُ لِأَحَدٍ أَنْ تَغْفِرَ لَهُ بِاسْتِحْقَاقِهِ، وَ لَا أَنْ تَرْضَى عَنْهُ بِاسْتِيجَابِهِ Hakuna hata mmoja anayewajibikiwa kumghufiria (dhambi zake), na wala hakuna hata mmoja (kati ya waja Wako) anayestahiki kuridhiwa Nawe (anayewajibikiwa kupata radhi Zako kutokana na juhudi zake mwenyewe) فَمَنْ غَفَرْتَ لَهُ فَبِطَوْلِكَ، وَ مَنْ رَضِيتَ عَنْهُ فَبِفَضْلِكَ Basi yeyote yule uliyemghufiria, huwa umemghufiria kwa hisani Yako, na yeyote uliyemridhia, huwa umemridhia kwa fadhila (hisani) Zako. تَشْكُرُ يَسِيرَ مَا شَكَرْتَهُ، وَ تُثِيبُ عَلَى قَلِيلِ مَا تُطَاعُ فِيهِ حَتَّى كَأَنَّ شُكْرَ عِبَادِكَ الَّذِي أَوْجَبْتَ عَلَيْهِ ثَوَابَهُمْ وَ أَعْظَمْتَ عَنْهُ جَزَاءَهُمْ أَمْرٌ مَلَكُوا اسْتِطَاعَةَ الِامْتِنَاعِ مِنْهُ دُونَكَ فَكَافَيْتَهُمْ، أَوْ لَمْ يَكُنْ سَبَبُهُ بِيَدِكَ فَجَازَيْتَهُمْ Wewe ni mwenye kuthamini shukrani chache upewazo, na unalipa thawabu (kadhaa) kwa utiifu mdogo unaotendewa. Hali hii inafikia kiasi ambapo inakuwa ni kana kwamba ile shukrani ya waja Wako—ambayo Wewe Mwenyewe ameifanya iwe ni lazima kuilipia thawabu, na ukaitukuza jazaa (malipo) yake—ni jambo ambalo waja hao walikuwa na uwezo kamili wa kulikataa pasipo Nawe kuwazuia, hivyo unawalipa kama ni fidia. Au, ni kana kwamba chanzo cha shukrani hiyo hakikutoka Kwako, hivyo unawalipa kama malipo ya kazi yao. بَلْ مَلَكْتَ يَا إِلَهِي أَمْرَهُمْ قَبْلَ أَنْ يَمْلِكُوا عِبَادَتَكَ، وَ أَعْدَدْتَ ثَوَابَهُمْ قَبْلَ أَنْ يُفِيضُوا فِي طَاعَتِكَ، وَ ذَلِكَ أَنَّ سُنَّتَكَ الْإِفْضَالُ، وَ عَادَتَكَ الاحسان، وَ سَبِيلَكَ الْعَفْوُ Bali, (Ewe Mola wangu), ulikwishayatawala majaaliwa yao kabla ya wao kumudu kuitimiza ibada yako; na ukaandaa ujira wao kabla ya wao kujitosa kwa kina katika utiifu kwako. Na hakika hili linatokana na kwamba; Mfumo wako ni mfumo wa ukarimu, na ada yako ni ihsani, na sira Yako (mwenendo Wako) ni msamaha (na msamaha ndiyo mwnendo Wako). فَكُلُّ الْبَرِيَّةِ مُعْتَرِفَةٌ بِأَنَّكَ غَيْرُ ظَالِمٍ لِمَنْ عَاقَبْتَ، وَ شَاهِدَةٌ بِأَنَّكَ مُتَفَضَّلٌ عَلَى مَنْ عَافَيْتَ، وَ كُلٌّ مُقِرٌّ عَلَى نَفْسِهِ بِالتَّقْصِيرِ عَمَّا اسْتَوْجَبْتَ Kwa kweli, viumbe vyote vinakiri kwamba Wewe si dhalimu kwa yeyote yule umwadhibuye, na vinashuhudia kwamba Wewe ni mwenye kufanyia hisani yule unayemsamehe. Na kila mmoja wao, anakiri binafsi mapungufu yake mbele ya yale unayostahiki. فَلَوْ لَا أَنَّ الشَّيْطَانَ يَخْتَدِعُهُمْ عَنْ طَاعَتِكَ مَا عَصَاكَ عَاصٍ، وَ لَوْ لاَ أَنَّهُ صَوَّرَ لَهُمُ الْبَاطِلَ فِي مِثَالِ الْحَقِّ مَا ضَلَّ عَنْ طَرِيقِكَ ضَالٌّ Basi kama si Shetani kuwaghilibu na kuwatoa (waja wako) katika misingi ya utiifu kwako, basi katu kusingepatikana muasi wa kukuasi. Vivyo hivyo, isingekuwa ni yeye kuidhihirisha (kuipamba) batili mbele ya macho yao kwa ruwaza (picha) ya haki, basi katu kusingetokea mpotofu atakayepotea na kutengana na yako. فَسُبْحَانَكَ مَا أَبْيَنَ كَرَمَكَ فِي مُعَامَلَةِ مَنْ أَطَاعَكَ أَوْ عَصَاكَ تَشْكُرُ لِلْمُطِيعِ مَا أَنْتَ تَوَلَّيْتَهُ لَهُ، وَ تُمْلِي لِلْعَاصِي فِيما تَمْلِكُ مُعَاجَلَتَهُ فِيهِ. Basi, Umetukuka (umetakasika) Ewe Mungu! Ni jinsi ulivyo wazi ukarimu wako katika kuamiliana na wale wanaokutii na wale wanaokukaidi (wakukadhibishao/ wakupingao). Unampa zawadi (unamlipa) yule anayekutii kwa jambo ambalo Wewe Mwenyewe ulimsaidia kulitekeleza, na unamvumilia yule anayekukaidi (akupingaye), japokuwa una uwezo kamili wa kumwadhibu mara moja bila ya kumpa muda. أَعْطَيْتَ كُلًّا مِنْهُمَا مَا لَمْ يَجِبْ لَهُ، وَ تَفَضَّلْتَ عَلَى كُلٍّ مِنْهُمَا بِمَا يَقْصُرُ عَمَلُهُ عَنْهُ. Ulimpa kila mmoja kati ya wawili hao, kile ambacho hakikumwajibikia kuwa nacho (hakikumstahikia), na ukamfadhili kila mmoja wa wawili hao, kwa kile ambacho kimepindukia juhudi (thamani) ya tendo lake. وَ لَوْ كَافَأْتَ الْمُطِيعَ عَلَى مَا أَنْتَ تَوَلَّيْتَهُ لَأَوْشَكَ أَنْ يَفْقِدَ ثَوَابَكَ، وَ أَنْ تَزُولَ عَنْهُ نِعْمَتُكَ، وَ لَكِنَّكَ بِكَرَمِكَ جَازَيْتَهُ عَلَى الْمُدَّةِ الْقَصِيرَةِ الْفَانِيَةِ بِالْمُدَّةِ الطَّوِيلَةِ الْخَالِدَةِ، وَ عَلَى الْغَايَةِ الْقَرِيبَةِ الزَّائِلَةِ بِالْغَايَةِ الْمَدِيدَةِ الْبَاقِيَةِ. Na iwapo ungelimuhisabu mtiifu (Wako) kulingana na kile ambacho Wewe Mwenyewe ulisimamia kumwezesha katika utendaji wake, basi angelikaribia mno kupoteza thawabu Zako (malipo ya tendo hilo), na bila shaka angeliepukwa naneema Yako. Hata hivyo, Wewe kwa ukarimu Wako, umemlipa kutokana na kipindi chake kifupi chenye ukomo, kwa malipo ya kipindi kirefu cha umilele; na (ukamlipa) kwa amali zake zenye mipaka ya muda mfupi yenye kutoweka, kwa malipo yenye mipaka mirefu yenye kudumu. ثُمَّ لَمْ تَسُمْهُ الْقِصَاصَ فِيما أَكَلَ مِنْ رِزْقِكَ الَّذِي يَقْوَى بِهِ عَلَى طَاعَتِكَ، وَ لَمْ تَحْمِلْهُ عَلَى الْمُنَاقَشَاتِ فِي الآْلَاتِ الَّتِي تَسَبَّبَ بِاسْتِعْمَالِهَا إِلَى مَغْفِرَتِكَ، وَ لَوْ فَعَلْتَ ذَلِكَ بِهِ لَذَهَبَ بِجَمِيعِ مَا كَدَحَ لَهُ وَ جُمْلَةِ مَا سَعَى فِيهِ جَزَاءً لِلصُّغْرَى مِنْ أَيَادِيكَ وَ مِنَنِكَ، وَ لَبَقِيَ رَهِيناً بَيْنَ يَدَيْكَ بِسَائِرِ نِعَمِكَ، فَمَتَى كَانَ يَسْتَحِقُّ شَيْئاً مِنْ ثَوَابِكَ لَا مَتَي Zaidi ya hayo, wala Wewe hukumdai fidia (hukupunguza malipo yake) kwa ajili ya riziki (Yako) aliyoitumia, ambayo ndiyo iliyompa nguvu za kukutii. Wala hukumfanyia hesabu kali kwa vile vyombo (kama vile viungo vya mwili wake) ambavyo, ndiyo alivyovitumia katika tafuta msamaha wako (yaani hukumfanyia ugumu katika kuikubali toba yake kutokana na mapungufu yake). Na kama ungemfanyia hivyo, basi juhudi zake zote, na kila alichokifanyia kazi (katika ibada yake) kingeishia kuwa ni malipo ile neema Yako ndogo kabisa kati ya zile neema nyinge zisizohisabika. Na bado angesalia kuwa na deni kubwa mno mbele Yako, kutokana na neema Zako nyingine zisizohisabika. Basi, ni wakati gani hasa angeweza kustahili kupata japo kiwango kidogo cha thawabu zako? Kamwe, (hata kidogo asingewaze kupata hadhi kama hiyo)! هَذَا يَا إِلَهِي حَالُ مَنْ أَطَاعَكَ، وَ سَبِيلُ مَنْ تَعَبَّدَ لَكَ، فَأَمَّا الْعَاصِي أَمْرَكَ وَ الْمُوَاقِعُ نَهْيَكَ فَلَمْ تُعَاجِلْهُ بِنَقِمَتِكَ لِكَيْ يَسْتَبْدِلَ بِحَالِهِ فِي مَعْصِيَتِكَ حَالَ الْإِنَابَةِ إِلَى طَاعَتِكَ، وَ لَقَدْ كَانَ يَسْتَحِقُّ فِي أَوَّلِ مَا هَمَّ بِعِصْيَانِكَ كُلَّ مَا أَعْدَدْتَ لِجَمِيعِ خَلْقِكَ مِنْ عُقُوبَتِكَ. Hii, Ee Mungu wangu, ndiyo hali ya yule aliyekutii, na njia ya yule aliyekuabudu. Ama yule mwenye kuasi amri Yako na mwenye kuingia katika makatazo Yako, basi hukumfanyia haraka kwa adhabu Yako, (ulimpa muhula) ili abadilishe hali yake kukuasi, iwe ni hali ya kurejea kwenye utiifu Wako. Na kwa hakika tokea hatua yake ya mwanzo pale alipotia nia ya kukuasi, alikuwa anastahiki kupata kila ulichokiandaa kwa ajili ya kila mmoja kati ya viumbe Vyako miongoni mwa adhabu Yako. فَجَمِيعُ مَا أَخَّرْتَ عَنْهُ مِنَ الْعَذَابِ وَ أَبْطَأْتَ بِهِ عَلَيْهِ مِنْ سَطَوَاتِ النَّقِمَةِ وَ الْعِقَابِ تَرْكٌ مِنْ حَقِّكَ، وَ رِضًى بِدُونِ وَاجِبِكَ Basi kila adhabu uliyoiahirisha juu yake, na kila pigo la Ghadhabu angamizi ulilolichelewesha, ni msamaha utokanao na kutotenda kwa mujibu wa Haki Yako tukufu (ya kuwaadhibu waasi), na ni kuridhika na kiwango cha chini mno cha wajibu ulio thabiti kwako. فَمَنْ أَكْرَمُ يَا إِلَهِي مِنْكَ، وَ مَنْ أَشْقَى مِمَّنْ هَلَكَ عَلَيْكَ لَا مَنْ فَتَبَارَكْتَ أَنْ تُوصَفَ إِلَّا بِالْإِحْسَانِ، وَ كَرُمْتَ أَنْ يُخَافَ مِنْكَ إِلَّا الْعَدْلُ، لَا يُخْشَى جَوْرُكَ عَلَى مَنْ عَصَاكَ، وَ لَا يُخَافُ إِغْفَالُكَ ثَوَابَ مَنْ أَرْضَاكَ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ هَبْ لِي أَمَلِي، وَ زِدْنِي مِنْ هُدَاكَ مَا أَصِلُ بِهِ إِلَي التَّوْفِيقِ فِي عَمَلِي، إِنَّكَ مَنَّانٌ كَرِيمٌ. Basi, ni nani aliye mkarimu zaidi kuliko Wewe, Ewe Mola wangu? Na ni nani mwenye hasara kubwa zaidi kuliko yule anayeangamia kwa kukuasi Wewe (hakuna aliyeangamia zaidi yake, wakati fursa ya rehema ilikuwepo)? Hakika, Utukufu wako ni mkuu mno kiasi kwamba hauwezi kusifiwa kwa sifa nyengine yoyote ile isipokuwa kwa wema wako, na hadhi yako ni ya juu mno kiasi kwamba hakuna kinachopaswa kuogopwa kutoka kwako isipokuwa Uadilifu wako. Kamwe haiogopwi dhuluma kutoka kwako dhidi ya anayekuasi, wala haihofiwi kuwa utasahau kumlipa yule anayekuridhisha. Basi, mshushie rehema Zako Muhammad na Aali zake, na unijalie mafanikio katika tumaini langu (maombi yangu), na uniongezee nyongeza ya uongofu Wako, nyongeza ambayo itaniwezesha kupata mafanikio ya matendo yangu. Hakika Wewe ni Mwingi wa kutoa na Mkarimu.