Nenda kwa yaliyomo

Dhima za Kisheria

Kutoka wikishia

Dhima za Kisheria “Kiarabu تکلیف الشرعی”: Ni wajibu na majukumu ya kidini ambayo Uislamu humtaka muumini kuyatekeleza. Kuna masharti maalumu yanayozingatiwa na mafaqihi, ili muumini akabiliwe na majukumu hayo. Masharti hayo ni; akili timamu, kubalehe, pamoja na kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu hayo. Mtu asiyekamilisha moja ya nguzo hizi, hawi ni miongoni mwa wahusika wanaotakiwa kutekeleza majukumu ya kisheria. Taklifa au majukumu ya kisheria zimegawaika katika matawi matano, nayo ni: wajibu (amri ya lazima), haramu (katazo la lazima na la mkato), mustahabu (amri pendekezwa), makruhu (katazo pendekezwa), na mubah (matendo yote yaliokosa amri au katazo maalumu). Baadhi ya mafaqihi hawazingatii Uislamu pamaja na kuelewa haki, kama ni nguzo za asili zinazopelekea mja kukabiliwa na majukumu ya kisheria. Wao katika wakifafanua maoni yao, wanashikilia kuwa; majukumu ya kisheria yanawahusu waja wote bila ubaguzi kati yao. Hata hivyo, iwapo jahili qasir (mjinga aliyekosa hila na njia ya kutambua haki), atatenda makossa fulani kwa ujinga alionao, na kuacha baadhi ya majukumu yake, mjinga huyo hataadhibiwi wala kulaumiwa mbele ya Mola wake. Pia si lazima kwa asiye Muislamu kulipa fidia kutokana na kuacha kutekeleza majukumu yaliyokuwa yakimkabili kabla ya kusilimu kwake. Wanazuoni wa fani ya elmu kalam (theolojia) wanayachukulia majukumu kwa waja, kama ni amri na mafundisho ya Mwenye Ezi Mungu kwa waja wake, wao wanaamini kwamba; kuwa lengo lango msingi la majukumu haya, ni kuwafikisha waja wake kwenye maslahi yao ya kidunia na kiakhera. Baadhi ya familia nchini Iran, huandaa sherehe maalumu zinazojulikana kama ni "maadhimisho ya kukabiliwa na majukumu". Maadhimisho haya huwa ni kwa ajili ya watoto wao waliofikia umri wa kukabiliwa na majukumu ya kisheria. Sherehe hizi hufanyika katika mazingira ya kijamii kama vile maskulini, misikitini, na maeneo mengine matakatifu.

Dhana na Umuhimu wa Dhima za Kisheria katika Fiqhi ya Kiislamu "Dhima za kisheria" au “wajibu wa kisheria”: humaanisha majukumu ya kisheria yaliowekwa na sheria ya Kiislamu. Majukumu haya yanawahusu wale wanaotimiza vigezo vinavyohitajika, ikiwa ni pamoja na; kubalehe, kuwa na akili timamu, na uwezo wa kutekeleza au kuachana na jambo lililokatazwa kisheria. [1] Anayeelekezewa majukumu ya kisheria au maagizo ya lazima ya sheria huitwa "mukallaf". [2] Dhima za kisheria, au majukumu ya lazima (ahkamu al-taklifiyya), yamegawanyika katika makundi matano, nayo ni: wajibu (amri ya lazima), haramu (katazo la lazima na la mkato), mustahabu (amri pendekezwa), makruhu (katazo pendekezwa), na mubah (matendo yote yaliokosa amri au katazo maalumu). [3] Mada kuhusiana na majukumu ya kisheria, hujadiliwa na kutafitiwa katika vyanzo vya fiqhi, usuli al-fiqh, na itikadi. Mafaqihi, hujadili masharti ya kukabiliwa na majukumu haya, katika sehemu mbalimbali vitabuni mwao, iwe ni kuhusiana na masuala ya ibada au mambo yanayohusiana na miamala mbali mbali. [4] Mada hii ya dhima kwa waumini, ni mada inayohusiana moja kwa moja na hukumu zote mbili za kisheria, yaani ahkamu al-taklifiyya (hukumu za wajibu wa kiibada) pamoja na ahkamu al-wadh’iyya, ambazo ni hukumu vamizi au shikamanifu (zinazo mvaa mja kutokana na hali maalumu, kama vile hukumu zinazomvaa baada ya ndoa). Hii ndiyo sababu iliyomepelekea dhima hizi za kisheria, pia kujadiliwa katika elimu ya usuli al-fiqh. [5] Katika fani ya elimu ya kalama (theolojia), dhima hizi hujadiliwa chini ya dhana ya kwamba dhima hizi ni miongoni mwa matendo au viumbe vilivyoumbwa na Mwenye Ezi Mungu, kwa ajili ya maslahi na manufaa ya wanadamu kiduniani na Akhera. [6] Masharti ya Dhima za Kisheria Kuna masharti kadhaa yanazozingatiwa na mafaqihi (wafasiri na wanazuoni wa fiqhi), na namna ya mja anavyoweza kukabiliwa na dhima za kisheria. Masharti hayo ni pamoja na; kumili akili timamu, kubalehe, pamoja na kuwa na uwezo wa dhima na amri hizo zitokazo kwa Mola wake. Hiaya ndio masharti ya jumla ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika dhima zote za kisheria. Masharti haya katika istilahi ya kifiqhi, hujulikana kama ni masharti msingi kuhusiana na dhima za kisheria (shaa’itu aammu li al-taklif). [7] Hivyo basi mtu yeyyote yule anayekidhi masharti matatu haya, huyo atakuwa anawajibika na kulazimika kufuata sheria za dini. [8] Kwa hivyo dhima za kisheria, haziwahusu watoto wadogo wasiobalehe, wendawazimu, au wale wasio na uwezo wa kutekeleza dhima hizo. [9] Wanazuoni wengine wanasema kwamba; “ufahamu” na welewe, pia ni miongoni mwa sharti kuu katika kukabiliwa na dhima za kisheria. [10] Kwa msingi huu, mtu asiye na fahamu, aliyepoteza fahamu au aliyelala, huwa hana wajibu wowote ule wa kisheria hadi aamke na apate fahamu zake kamili. [11] Pia, mafaqihi wanasema kwamba; pia kuna masharti mengine makhususi na ya pekee, yanayotakiwa kuzingatiwa kuhusiana na dhima hizi za kisheria. [12] Kwa mfano, katika amali ya Hija ya lazima, pamoja na masharti ya msingi; kama vile kubalehe, kuwa na akili timamu, na kuwa na uwezo, pia suala la wakati ni miongoni mwa masharti ya ibada hiyo. Hivyo basi mtu anayewajibikiwa na amali ya Hiji pia ni lazima awe na wakati wa kutosha wa kusafiri na kufanya ibada yake ya Hija. Mafaqihi wameteuwa jina maalumu kuhusiana na sharti hii, ambapo katika istilahi za kifiqhi hujulikana kwa jina la "uwezo wa kiwakati". [13]

Je Dhima za Kisheria Pia Zinamhusu Asiyetambua Sheria Hizo (Mjinga)? Kulingana na maelezo ya Muhammad Reza Mudhaffar, mwanazuoni wa Kishia wa karne ya kumi na nne ya Hijiria, ni kwamba; wanazuoni wote wa madhehebu ya Ithna’ashariyyah ni wenye kauli moja juu ya suala hili (wana ijmaa ndani yake). Kwa mujibu wa maelezo yake, wanazuoni wa madhehebu ya Ithna’ashariyyah wanasema kawamba; sheria za Allah ni sawa kwa mwenye elimu na kwa mtu asiyekuwa na elimu. Hivyo basi wote wawili wanalazimika kufuata wajibu wao wa dini. [14] Wao wanatoa mfano wa wa sala wakisema kwamba; sala ni lazima kwa kila mtu, iwe anajua kuwa ni faradhi juu yake au hajuia suala hilo. [15] Lakini wanazuoni hawa wanasema kuwa; mtu asiyejua kwa sababu ya kukosa fursa zinazokubalika kimantiki, mtu huyo iwapo ataacha au kukiuka wajibu wa kihsaria, hatakuwa ni mwa watakaoadhibiwa. [16]

Jee Dhima za Kisheria Pia Inawahusu Wasiokuwa Waislamu? Kulingana na kitabu cha Al-‘Anaawin, wazo linalokubalika zaidi miongoni mwa wanasheria wa madhehebu ya Shia Imamiyyah ni kwamba; Dhima za kisheria zinawahusu wote wawili, Waislamu na wasio Waislamu. [17] Lakini kwa mujibu wa kanuni ya Jabb (kusamehe yaliyopita), si lazima kwa aliyesilimu kulipa ibada ambazo hakuzifanya wakati alipokuwa si Muislamu [18]. Hata hivyo, Sahibu al-Hada’iq na Sayyid Abu al-Qasim al-Khui, wanasema kwamba; baadhi ya wanasheria wa Kishia, wanaamini kwamba, wajibu wa kisheria hauwahusu wasio Waislamu. [19]

Umri wa Taklifa kwa Wavulana na Wasichana katika Fiqhi ya Kishia Kwa maelezo zaidi, angalia pia: Kubalehe na Kubalehe kwa Wasichana. Kulingana na maoni maarufu zaidi miongoni mwa wanazuoni wa Kishia, umri wa kukabiliwa na dhima, au kubalehe kwa mvulana ni miaka kumi na tano kamili, kulingana na kalenda ya mwezi (Hijria), ambayo inalingana takriban na miaka kumi na nne, na miezi sita, na siku kumi na mbili katika kalenda ya jua (Shamsia). [20] Kwa upande wa wasichana, umri wa kukabiliwa na dhima, ni baada ya kutimiza miaka tisa ya kalenda ya mwezi wa Kiislamu (Hijiria), ambayo inalingana takriban na miaka minane, miezi minane, na siku ishirini za kalenda ya jua (Shamsia). [20] Nini Lengo la Dhima za Mwenye Ezi Mungu kwa Wanadamu? Kwa mtazamo wa wanazuoni wa taaluma ya theolojia, ni kwamba; wajibu usio na lengo maalunu ndani yake, ni sawa kitendo cha kupumbaza, cha bure na kisicho thamani, na kitendo cha bure hakiwezi kutoka kwa Mungu Mwenye Hekima. Pia, faida ya lengo la dhima haiwezi kurejea kwa Mungu, bali inarejea moj kwa moja kwa waja wake, na kuna maslahi na manufaa maalumu yanayomrudia mwawajibikiwa peke yake, manufaa ambayo hayawezi kupatikana bila kutekeleza dhima hizo. [21] Kwa sababu hiyo, wanatheolojia wanasema kwamba; dhima kimsingi ni jambo jema (Hasan). [22] Baadhi wameona kuwa lengo la dhima ni kule mukallaf (mwekewa dhima) kufikia thawabu na ujira wa Allah. [23] Wengine vile vile wamesema kuwa; lengo la dhima za kisheria ni inaweza kuhusisha mambo tofauti, ikiwa ni pamoja na: kumtihani mukallaf (mwekewa dhima), kushukuru juu ya neema zilizokithiri, na kujilea malezi mema na ya kiroho. [24] Allama al-Hilli, mutakallim (mwanatheolojia) wa karne ya nane Hijria, katika Kashf al-Murad amesema kwamaba; kutekeleza dhima za kisheria kunampatia mja manufaa matatu, ambayo ni: • Kuilea nafsi na kuizuia na matamanio na shahawa. • Kuizoesha nafsi kutafakari katika masuala yanayhusiana na Mwenye Ezi Mungu, kama vile kutafakari katika mambo yanayohusiana na mwanzo mwanadamu na maisha ya Akhera. • Kujikumbusha kheri na shari za Akhera ambazo sheria imeahidi. [25] Sherehe za Kusheherekea Kubalehe Inasemekana kuwa Sayyid Ibn Tawus alikuwa ndiye mtu wa kwanza kuanzisha desturi ya kusheherekea za sherehe za kubalehe miongoni mwa Waislamu, na kuwahamasisha wengine kuzienzi na kuiheshimu sherehe hizo. [26] Katika kitabu chake kiitwacho Kashfu al-Mahajjati li-Thamarati al-Muhjahti, alimwusia mwanawe kuiheshimu na kuitukuza siku hii adhimu, alimtaka kurikodi tarehe yake, na amshukuru na kumhimidi Mola wake kila mwaka, kama vile afanyavyo katika siku za furaha na sikukuu mbali mbali. Pia alimtaka kutoa sadaka na kuwakirimu wahitaji katika siku hiyo adhimu. [27] Pia Muhammad bin Muhammadi Rayshahri, katika kitabu alichoandika kuhussiana na sherehe za kubalehe, ameipa siku hii jina la "Yawmu-Allah" (Siku ya Mungu), na amechukulia suala la kuienzi siku hii, kuwa ni moja ya matendo ya kuheshimu nembo za Mwenye Ezi Mungu (Sha’a’iru Al-llah). [28] Pia yeye anaamini kwamba; kufanya sherehe za kubalehe, huleta kumbukumbu yenye ladha ya kiroho, na yenye kujenga welewe maalumu ndani ya akili ya binti au mtoto wa kiume, na katu kumbukumbu hii haisahauliki akilini mwake, na inabaki kuwa ni mwongozo wake katika maisha yake ya ibada. [29] Baadhi ya familia za kidini nchi Iran, huwa na kawaida ya kufanya sherehe za kubalehe kwa watoto wao wanaofikia umri wa kukabiliwa dhima za kisheria, na ni kawaida kwa washiriki kumpa zawadi mtu aliyefikia umri huo wa kukabiliwa na dhima hizo. [30] Pia desturi ya kusheherekea sherehe za kubalehe, hufanyika hadharani katika maskuli, misikiti na maeneo matakatifu. [31] Kumwajibishia Mja Kitu Kisichowezekana Makala kuu: Kuwajibisha Kitu Kisichowezekana Kuwajibisha kitu kisichowezekana, ni kumlazimisha mtu kufanya jambo ambalo liko nje ya uwezo wake na nguvu zake. [32] Kuna mitazamo kadhaa kutoka kwa wanazuoni wa taaluma ya theolojia katika suala la kwamba; je Mungu anaweza kuwalazimisha waja wake kufanya jambo lililo nje ya uwezo wao na nguvu zao au la? Kwa mtazamo wa madhehebu ya pamoja na Mu'tazila na Imami, ni kwamba; Kuwajibisha lisilowezekana, ni jambo baya na lisilokubalika, na jambo baya haliwezi kutoka kwa Mungu Mwenye Hekima. [33] Lakini Ash'ari wanaamini kwamba; Mwenye Ezi Mungu anaweza kumlazimisha mtu kufanya jambo ambalo liko nje ya uwezo wake. [34]