Ayyamullah

Kutoka wikishia

Ayyamullah (Kiarabu: أيّام اللّه ) maana yake ni siku za Mwenyezi Mungu. Siku za Mwenyezi Mungu ni ashirio la wakati na kipindi ambacho ndani yake kumetokea matukio muhimu na kudhihirisha zaidi nguvu za Mwenyezi Mungu. Wafasiri wa Qur'ani wamesema katika maelezo yao chini ya Aya zenye neno hili kwamba, Ayyamullah (Siku za Mwenyezi Mungu) ni masiku ya wokozi wa Mwenyezi Mungu na siku za Mwenyezi Mungu kuwapatia waumini neema, siku za adhabu kwa Washirikina na vilevile ni siku za neema na adhabu na lengo la ukumbusho huu ni kuwazindua na kuwafanya wanadamu wawe macho.

Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Baqir (a.s) ni kwamba: Siku za kuanzisha harakati Imam Mahdi (a.t.f.s), rajaa na Kiyama ni mifano na vielelezo vya Ayyamullah (siku za Mwenyezi Mungu). Katika baadhi ya hadithi siku ya Ashura pia imetambuliwa kuwa miongoni mwa siku za Mwenyezi Mungu.

Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran, amezitaja na kuzitambua baadhi ya siku muhimu katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa ni katika siku za Mwenyezi Mungu. Moja ya siku hizo ni 22 Bahman 1357 Hijria Shamsia/Februari 1979 siku ambayo mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi na kuhitimisha utawala wa kidhalimu wa Shah. Kwa mujibu wa mtazamo wake ni kwamba, mambo yaliyotokea katika Ayyamullah (siku za Mwenyezi Mungu) ni jambo la kuamsha, ibra na funzo kwa wanadamu katika kipindi chote cha historia; na ni kuutokana na sababu hii ndio maana siku hizi zinapaswa kuhuishwa.


Utambuzi wa maana

Siku za Mwenyezi Mungu ni ashirio la wakati na kipindi ambacho ndani yake kumetokea matukio muhimu. [1] na kudhihirisha zaidi nguvu za Mwenyezi Mungu. [2] Neno hili limekuja mara mbili katika Qur'an. [3] Katika Surat Ibrahim, Nabii Mussa alitakiwa aikumbushe Qaumu yake kuuhusiana na siku za Mwenyezi Mungu, kwani katika ukumbusho huu kuna ibra, mafunzo na mazingatio. [4] Kadhalika imekuja katika Surat al-Jathiyah ambapo watu walioamini wawasamehe wasio zitaraji (waliokata tamaa) siku za Mwenyezi Mungu ili ailipe kila kaumu kwa mujibu wa kile ilichochuma. [5] Allama Tabatabai anasema, siku ya kufa, barzakhi, siku ya Kiyama na siku ya kutokea adhabu ya kuangamizwa kaumu (kuangamizwa kaumu fulani kutokana na kuasi na kutotii amari za Allah ambapo hakuna nasaha yoyote iliyowazindua) ni mifano na vielelezo vya wazi vya Ayyamullah (siku za Mwenyezi Mungu. [6] Katika tafsiri ya nemooneh imeelezwa kuwa, lengo la kukumbushwa siku za Mwenyezi Mungu na kunukuliwa matukio yanayohusiana nazo ni kutoa nasaha na kuwafanya watu wawe macho. [7] Imam Ali (a.s) katika barua yake kwa Qutham bin Abbas aliyekuwa gavana wake wa Makka alimtaka autumie msimu wa Hija kuwakumbusha watu siku za Mwenyezi Mungu. [8]


Tafsiri

Wafasiri wana mitazamo tofauti katika tafsiri ya siku za Mwenyezi Mungu:

  • Siku za neema: Siku ambazo ndani yake Mitume wa Allah na wafuasi wao wamejumuishwa katika neema za Mwenyezi Mungu; kama kuokolewa kaumu ya Nabii Mussa (a.s) kutoka kwa mafirauni, kutoka kaumu ya Nabii Nuhu (a.s) katika safina ya Nuhu na kuokolewa Nabii Ibrahim (a.s) na moto. [9]
  • Siku za adhabu: Siku ambazo kulishushwa adhabu kwa Qaumu zilizoasi kama Qaumu Aadi na Thamudi. [10]
  • Siku za adhabu na siku za neema: Kila siku ambayo ndani yake amri za Mwenyezi Mungu zimeng’ara kiasi cha kufunika mambo mengine. [11]

Imekuja katika tafsiri ya Nemooneh kwamba, kila siku ambayo ndani yake kunafunguliwa ukurasa mpya katika maisha ya wanadamu na kutolewa somo na mazingatio kwao, kama vile kudhihiri na kuja Mtume au kuangamia mfalme dhalimu na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, ni katika siku za Mwenyezi Mungu. [12] Kadhalika kwa mujibu wa hadithi iliyokuja katika kitabu cha Amali cha Sheikh Swaduq ambayo imenukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ni kwamba, makusudio ya siku za Mwenyezi, ni siku ya kushuka neema, balaa na adhabu za Mwenyezi Mungu. [13]

Feyz Kashani anasema, hakuna hitilafu baina ya mitazamo hii, kwani kumpatia neema muumini katika hukumu ni mithili ya kumpa adhabu kafiri na siku hizi ni neema kwa Qaumu na ni adhabu kwa kaumu nyingine. [14]

Vielelezo na mifano hai

Katika hadithi kumebainishwa mifano na vielelezo vya Ayyamullah (siku za Mwenyezi Mungu). Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir (a.s) ni kwamba, siku za Mwenyezi Mungu ni tatu: Siku ya harakati ya Imam Mahdi (a.t.f.s), siku ya rajaa na siku ya Kiyama. [15] Hata hivyo, Ali bin Ibrahim bin Hashim Qumi, yeye ametaja siku ya kifo badala ya siku ya rajaa. [16] Baadhi ya hadithi zimeitaja siku ya Ashura (siku aliyouawa shahidi Imam Hussein katika jangwa la Karba mwaka 61 Hijria) kuwa ni katika siku za Mwenyezi Mungu. [17]

Kadhalika Imam Khomeini ametambua hijra ya Mtume, siku ya kukombolewa Makka, siku ya vita vya Siffin na siku ambazo kunatokea tetemeko la ardhi, mafuriko na balaa zingine za kimaumbile ambapo ndani yake kuna tanbihi na ukumbusho kwa wanadamu kuwa ni katika siku za Mwenyezi Mungu. [18] Pamoja na hayo imeelezwa kwamba, siku za Mwenyezi Mungu haziishi katika mifano hii tu iliyotolewa bali kuna vielelezo vingine. [19]


Siku za Mwenyezi Mungu za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Imam Ruhullah Khomeini, mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezitaja na kuzitambua baadhi ya siku katika historia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, ni katika siku za Mwenyezi Mungu. Tarehe 22 Bahman 1357/Februari 1979 ambapo mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi, [20] 8 Septemba 1978 tukio ambalo lilipelekea kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo siku hii ya 17 Shahrivar inajulikana katika kalenda ya Kiirani kwa jina la Ijumaa Nyeusi, na tarehe 15 Khordad 1342/Juni 5 1963 ambapo kulitokea Harakati ya tarehe 15 Khordad kuwa ni miongoni mwa hizi siku za Mwenyezi Mungu. [21] Kwa mujibu wa Imam Khomeini ni kwamba, mambo yaliyotokea katika Ayyamullah (siku za Mwenyezi Mungu) ni jambo la kuamsha na kuzindua, mazingatio na funzo kwa wanadamu katika kipindi chote cha historia; na ni kutokana na sababu hii siku hizi zinapaswa kuhuishwa. [22]


Vyanzo

  • Fayḍ al-Kāshānī, Muḥammad b. al-Murtaḍā al-. Tafsīr al-Ṣāfī. Tehran: Maktabat al-Ṣadr, 1373 Sh.
  • Imām Khomeinī, Sayyid Rūḥ Allāh. Ṣaḥīfa-yi nūr. Tehran: Intishārāt-i Surūsh, 1369 Sh.
  • Ibn Abi al-Jumhūr, Muḥammad b. ʿAlī. ʿAwālī al-liʾālī al-ʿazīzīyya fī al-aḥādīth al-dīnīyya. Edited by Mujtabā Irāqī. Qom: Dār Sayyid al-Shuhadāʾ, 1405 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1373 Sh.
  • Qurashī Bunābī, ʿAlī Akbar. Qāmūs-i Qurān. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1412 AH.
  • Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Qom: Dār al-Kitāb, 1404 AH.
  • Sayyid Raḍī, Muḥammad Ḥusayn. Nahj al-balāgha. Edited by Ṣubḥī Ṣaliḥ. Beirut: Dār al-Kutub al-Lubnānī, 1414 AH.
  • Shaʾrānī, Abu l-Ḥasan. Nathr-i ṭūba. Collected by Qarīb, Muḥammad. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1380 Sh.
  • Ṣadūq, Muḥammad b. ʿAlī al-. Al-Khiṣāl. Qom: Jāmiʿat al-Mudarrisīn, 1362 Sh.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Amālī. [n.p], [n.d].
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Tibyān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d].
  • Ṭabrasī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Maʿrifa, 1406 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Jāmiʾ al-bayān fi tafsīr al-Qurʾān. [n.p]: Dār al-Risāla, 1420 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Muʾassisat al-Aʿlamī, 1439 AH.