Nenda kwa yaliyomo

Ayat al-Isti’adha

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Aya ya Istiadha)
Makala hii inahusiana na Ayat al-Isti’adha (Aya ya kuomba kinga na hifadhi). Ili kujua kuhusu istilahi yenye jina kama hili angalia makala ya Isti’adha.
Ayat al-Isti’adha

Ayat al-Isti’adha (Kiarabu: آية الاستعاذة ) (Aya ya kuomba kinga na hifadhi) ambayo ni Aya ya 98 ya Surat al-Nahl inabainisha nukta hii kwamba, wakati wa kusoma Qur'an inapasa kumuomba Mwenyezi Mungu akulinde na vishawishi vya shetani ili kulindwa na kuepushwa na kuteleza na kukosea. Isti’adha ni kuomba hifadhi na ulinzi na huku kuomba hifadhi kumetambuliwa kuwa ni hifadhi ya kimoyo; kwa maana kwamba, mwanadamu anapaswa kuhisi ndani ya moyo wake kwamba, ameomba hifadhi na kinga kwa Mwenyezi Mungu. (رجیم) ina maana mwenye kufukuzwa na inakumbusha kuwa, shetani alitimuliwa na kufukuzwa katika rehema za Mwenyezi Mungu kutokana na taasubi na kiburi chake.

Mafakihi wakitumia Aya hii wanasema kuwa, kabla ya kusoma Qur'an na kabla ya kuanza kisomo katika Salam ni mustahabu kuanza na: ((اَعوذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیمِ ; Naomba hifadhi kwa Allah dhidi ya shetani aliyefukuzwa)). Katika baadhi ya hadithi kumenukuliwa lafudhi zingine za Isti’adha (kuomba hifadhi na kinga) kama ((أَعُوذُ بِاللَّهِ السَّمِیعِ الْعَلِیمِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیم‏))

Andiko na tarjumi ya Aya

Aya ya 98 ya Surat al-Nahl ambayo inatajwa kama Ayat al-Isti’adha (Aya ya kuomba kinga na ulinzi), [1] inabainisha nukta hii kwamba, kuna ulazima wa kuomba hifadhi kwa Mwenyezi Mungu wakati wa kusoma Qur'an. Waislamu wakitumia Aya hii huanza kufanya baadhi ya kazi zao kwa kuomba hifadhi kwa Allah dhidi ya shetani aliyefukuzwa.

فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ

Unaposoma Qur'ani muombe Mwenyezi Mungu akulinde na shetani mwenye kufukuzwa



Tafsiri

Sheikh Tabarsi (aliaga dunia: 548 Hijiria) anasema kuwa, Isti’adha ni kuomba hifadhi na ulinzi mtu aliye na daraja ya chini kwa aliye na daraja ya juu zaidi kwa sura ya unyenyekevu. Makusudio ya Isti’adha katika Aya hii ni kwamba, wakati wa kusoma Qur'an inapasa kumuomba Mwenyezi Mungu akulinde na vishawishi vya shetani ili kulindwa na kuepushwa na hali ya kuteleza na kukosea. [2] Allama Tabatabai (1281-1360 Hijiria Shamsia) anakutambua huku kuomba hifadhi na ulinzi kuwa ni kwa kimoyo; [3] kwa maana kwamba, mwanadamu anapaswa kuhisi ndani ya moyo wake ameomba hifadhi na ulinzi kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, anajitenga na hawaa na matamanio ya nafsi ambayo yanamzuia kuwa na ufahamu sahihi na sio kwamba, atamke tu hilo kwa ulimi. [4] Hata hivyo Isti’adha ya ulimi imetambuliwa kuwa ni utangulizi wa kuleta hali ya kimoyo. [5]

Baadhi ya wafasiri wa Qur’an tukufu wanasema kuwa, sababu ya kuleta sifa ya “Rajim” (mwenye kufukuzwa) kwa ajili ya shetani ni kukumbuka kiburi na kuasi kwake amri ya Mwenyezi Mungu; kwa maana kwamba, wakati wa kusoma Qur’an, tunapaswa kujiweka mbali na kiburi, ghururi na taasubi ili tusije kukumbwa na hatima ya shetani mlaaniwa. [6]

Isti’adha ni wajibu au mustahabu?

Maulamaa wa Kiislamu wamekichukulia kitendo cha kuamrisha kilichotumika katika Aya yaani “Istaidh” (omba hifadhi) katika hali ya mustahabu na kwa msingi huo wamesema kuwa, ni mustahabu kutamka: ((اَعوذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیمِ)) wakati wa kuanza kusoma Qur’an. [7] Muqaddas Ardabili (aliaga dunia: 993 Hijiria) mmoja wa mafakihi wa karne ya 10 Hijiria anasema kuwa, mtazamo wa akthari ya Maulamaa ni kutokuwa wajibu na kutokuweko hadithi zinazoonyesha wajibu wa Isti’adha na hivyo wameona kuwa, Aya hii inaonyesha juu ya kuwa mustahabu suala la kuomba hifadhi kwa Allah dhidi ya shetani. [8] Pamoja na hayo, baadhi wakitumia dhahiri ya kitendo cha kuamrisha (Istaidh), wanaamini juu ya kuwa wajibu suala la kuomba hifadhi kwa Allah dhidi ya shetani wakati wa kusoma Qur’an. [9]

Sheikh Tusi [10] (385-460 H) na Allama Hilli [11] (648-726 H), wanasema kuwa, mafakihi wa Kishia na Kisunni wakitegemea Aya hii wanaona kuwa, ni mustahabu kutamka: ((اَعوذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیمِ)), katika rakaa ya kwanza ya Sala (baada ya Takbira ya kuhirimia na kabla ya kisomo). Imenukuliwa kwamba, miongoni mwa mafakihi wa Imamiya ni Abu Ali mtoto wa Sheikh Tusi tu, ndiye aliyekuwa akiamini wajibu wa Isti’adha [12] na Malik bin Anas yeye anaona kuwa inajuzu kuanza na ((اَعوذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیمِ)) kwenye Sala za Sunna tu. [13] Kuchunga kusoma kimya kimya katika kutamka: ((اَعوذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیمِ)) katika Sala kunahesabiwa kuwa ni mustahabu. [14]

Lafudhi za Isti’adha

Kumenukuliwa ibara na lafudhi mbalimbali za Isti’adha (kuomba hifadhi na kinga); [15] Allama Majlisi (1037-1110 H) anaona kuwa, mashuhuri zaidi miongoni mwazo ni: ((اَعوذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیمِ)) na ((أَعُوذُ بِاللَّهِ السَّمِیعِ الْعَلِیمِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیم‏)) [16] Katika baadhi ya hadithi kumenukuliwa pia ibara zingine za kuomba kinga na hifadhi kwa Allah dhidi ya shetani. Miongoni mwazo ni: ((أَسْتَعِیذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیم‏)) '((أَعُوذُ بِاللَّهِ السَّمِیعِ الْعَلِیمِ مِنَ الشَّیْطَانِ الرَّجِیمِ‏)) ((أَعُوذُ بِاللَّهِ أَنْ یَحْضُرُونِ‏))[18] ((أعوذ بِالله مِن الشیطان الرجیم إن الله هُوَ الْفَتّٰاحُ الْعَلِیمُ)). [19]

Licha ya kuwa katika Ayat al-Isti’adha Mwenyezi Mungu anasema: ((فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ ; Unaposoma Qur'ani muombe Mwenyezi Mungu akulinde na Shetani mwenye kufukuzwa)), lakini makusudio yake yamefahamiwa kuwa ni wakati unapotaka kusoma Qur’an, basi soma Audhubillahm…; [20] kama ilivyo katika Aya isemayo: ((إِذا قُمْتُمْ إِلَی الصَّلاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَکُمْ ; Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu)), kwa maana kwamba, wakati mnapotaka kusali basi tieni udhu. [21]

Rejea

Vyanzo

  • ʿAbd, Zakariyā. Al-Mīzān fī aḥkām tajwīd al-Qurʾān. Cairo: Dār al-Īmān, 2005.
  • ʿĀmilī, Sayyid Jawād. Miftāḥ al-karāma fī sharḥ qawāʿid al-ʿallāma. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d].
  • Ardabīlī, Aḥmad b. Muḥammad. Zubdat al-bayān fī aḥkām al-Qurʾān. Edited by Muḥammad Bāqir Bihbūdī. Tehran: al-Maktaba al-Murtaḍawiyya, [n.d].
  • Fayḍ al-Kāshānī, Muḥsin. Kitāb al-Wāfī. Edited by Ḍīyāʾ al-Dīn ʿAllāma Iṣfahānī. Isfahan: Kitābkhāna-yi Amīr al-Muʾminīn (a), 1406 AH.
  • Ḥillī, al-Ḥasan b. Yūsuf al-. Tadhkirat al-fuqahāʾ. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt (a), 1414 AH.
  • Ḥimyarī, ʿAbd Allāh b. Jaʿfar al-. Qurb al-isnād. Qom: Muʾassisat Āl al-Bayt (a), 1413 AH.
  • Ibn ʿĀshūr, Muḥammad b. al-Ṭāhir. Al-Taḥrīr wa l-tanwīr. Beirut: Muʾassisat al-Tārīkh, [n.d].
  • Jaʿfarī, Yaʿqub. Tafsīr kawthar. Qom: Muʾassisat Intishārāt-i Hijrat, 1376 Sh.
  • Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir al-. Biḥār al-anwār. Beirut: Muʾassisat al-Ṭabʿ wa l-Nashr, 1410 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1374 Sh.
  • Najafī Khomeinī, Muḥammad Jawād. Tafsīr-i āsān. Tehran: Intishārāt-i Islāmīyyah, 1398 AH.
  • Shahīd al-Awwal, Muḥammad b. Makkī. Al-Durūs al-sharʿīyya fī fiqh al-imāmiyya. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.
  • Suyūṭī, ʿAbd al-Raḥmān b. Abī Bakr al-. al-Itqān fī ʿulūm al-Qurʾān. Cairo: al-Hayʾat al-Miṣrīyya al-ʿĀmma li l-Kitāb, 1394 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Tehran: Naṣir Khusruw, 1372 Sh.
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥaasn al-. Al-Khilāf. Edited by ʿAlī Khurāsānī et.al. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1407 AH.