Ammaar bin Hassaan Ta'i

Kutoka wikishia

Ammaar bin Hassaan Ta'i (Kiarabu: عمار بن حسان الطائي) alikuwa ni miongoni mwa wafuasi waaminifu wa Imamu Hussein (a.s) na ni mmoja kati ya mashujaa waliouawa pamoja na Imamu Hussein (a.s) katika tukio la Karbala. Jina lake ni miongongoni mwa majina yalio orodheshwa katika matini maalumu yanayohusiana na namna ya kuwasalia na kuwatakia rehema mahashidi wa Kiislamu (Ziara Nahiye Muqaddasa). Kulingana na vyanzo vya kihistoria, Ammaar bin Hassaan alisafiri kutoka Makka akiwa pamoja na Imamu Hussein (a.s) mnamo mwaka wa 61 Hijria, na hatimae kufariki akiwa katika njia ya haki katika tukio la kihistoria la Karbala, lililokamilika mnamo siku ya Ashura (mwezi 10 Muharram).

Jina na Nasaba Yake

Ammaar bin Hassaan ni Muislamu atokaye katika kabila la Tai, [1] naye ni mmoja wa Mashia waaminifu wa karne ya kwanza Hijria, aliye shikamana bega kwa bega na Imamu Hussein (a.s), hadi kupoteza roho yake katika tukio la Karbala. [2] Katika baadhi ya vyanzo, yeye ametwa kwa jina la «Aamir bin Hassaan». Watafiti wengine wanakisia kuwa; tofauti hii kuhusiana na jina lake, inatokana na kufanana kwa jina lake na bwana Aamir bin Muslim, shahidi mwingine aliye poteza roho yake katika tukio la Ashura, ambaye huenda alikuwa ni mpwa wa Aamir bin Hassaan. Au pia inawezekana kuwa; haya ni majina mawili yanayo mrejelea mtu mmoja, ambapo tofauti za kimaandishi ndizo zilizo pelekea utata huu. [3] Kwa kuongezea, Muhammad Taqi Shushtari, katika kitabu chake Qamus al-Rijal, anasema kwamba; huenda jina la «Aamir bin Hassaan» na «Ammar bin Abi Salaama» likawa linahusiana na mtu mmoja tu aliyekufa shahidi katika tukio la Ashura. [4]

Baba wa Ammar, ambaye ni «Hassan bin Sharih», naye pia alikuwa ni miongoni mwa wafuasi waminifu wa Imamu Ali (a.s), aliye hudumu katika jeshi la Imamu Ali (a.s) katika vita vya Jamal na Siffin, ambapo hatimae alikufa shahidi katika vita vya Siffin. [5] Abdullah bin Ahmad, msimulizi wa Hadithi za Kishia na mwandishi wa kitabu «Qadhaya Amir al-Mu'minin», ni miongoni mwa matunda yatokayo kwa Ammaar, kwani yeye ni miongoni mwa wajukuu wa bwana Ammaar. [6]

Kufariki kwake Kishujaa Katika Tukio la Karbala

Kwa mujibu wa riwaya za Najashi, Ammaar bin Hassaan ni mmoja wa mashujaa waaminifu waliouawa katika tukio la Ashura, lililotokea mnamo mwaka wa 61 Hijria huko Karbala nchini Iraq. [7] Watafiti wanakubaliana ya kwamba; Ammar alikuwa miongoni mwa wale waliofuatana na kushikamana na Imamu Hussein (a.s) katika safari yake ya kutoka Makka hadi Karbala. Katika tukio hili muhimu, Imamu Hussein (a.s) alitoa hotuba akilihutubia Jeshi la Omar bin Sa’d, kwa lengo la kuwashauri kuachana na mapigano yao haramu. Hata hivyo, nasaha zake zilipuuzwa na kubaki bila ya mafanikio. Baada ya hotuba hiyo, Shimru akiwa na kundi la wapiganaji wake, alianzisha mashambulizi dhidi ya kambi ya Imamu Hussein (a.s) kutoka pande kadhaa, huku wakimimina mishale yao kama mvua. Shambulio hili katika maandiko ya kihistoria, linajulikana kwa jila la «Shambulio la Awali», ambalo lilipelekea Ammar bin Hassaan kuuawa shahidi katika uwanja huo wa vita vya Karbala. [11]

Kwa heshima ya kujitolea kwake, jina la Ammar bin Hassan limeorodheshwa na kutajwa kwa salamu maalum katika matini ya ziara za Mashahidi, huku akipewa salamu zisemazo: «اَلسّلامُ عَلَی عَمّار بنِ حَسّان» “Amani iwe juu yako, ewe Ammaar bin Hassaan.” [12]

Rejea

Vyanzo