Adi ibn Hatim al-Tai

Kutoka wikishia

Adi ibn Hatim al-Tai (Kiarabu: عَديّ بن حاتِم الطائي) (aliaga dunia 67 Hijiria) ni mmoja wa masahaba wa Bwana Mtume (s.a.w.w) na pia ni katika masahaba wa Imam Ali ibn Abi Twalib (a.s). Adi alishiriki katika vita vya Jamal, Siffin na Nahrawan na alikuwa akipigana upande wa Imam Ali (a.s). Aidha katika zama za Uimamu wa Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib (a.s) alikuwa akiwamahasisha na kuwashajiisha watu wajiunge na jeshi lake kwa ajili ya kupigana vita na Muawiya bin Abi Sufyan. Adi ibn Hatim al-Tai alisisitiza wazi kabisa mbele ya Muawiiya mapenzi yake kwa Imam Ali (a.s) na kumtetea.

Adi ibn Hatim al-Tai ni mtoto wa malenga na mshairi Hatim Tai aliyekuwa shakhsia mkubwa na kiongozi wa kabila la Tayy. Adi hakushiriki katika mapinduzii na harakati ya Mukhtar ibn Abi Ubayd al-Thaqafi lakini hakupingana naye.

Nasaba na nafasi yake

Adi alikuwa mmoja wa masahaba wa Bwana Mtume (s.a.w.w). Baba yake ni Hatim Tai ambaye katika zama za ujahilia alikuwa akipigiwa mfano kwa ukarimu. [1] Adi alitanmbulika kama mtu mwenye hekima na busara, khatibu, asiyekosa majibu na kiongozi wa kaumu yake. [2]

Adi aliaga dunia mwaka 67 Hijiria katika utawala wa Mukhtar huko Kufa. [3] Kuna kauli zinazosema pia kuwa, alifarikii dunia mwaka wa 68 na 69 Hijiria. [4] Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80 au 120. [5]

Imenuukuliwa kutoka kwa Adi ibn Hatim Tai ya kwamba, kila mara nilipokuwa nikiingia Mtume (s.a.w.w) alikuwa akipanua nafasi kwa ajili ya mimi kukaa. [6] Mtume alimpa jukumu la kukusanya sadaka (Zaka) katika kabila la Tayy na Bani Asad. [7]

Kisa cha kusilimu kwake

Kabla ya Adi ibn Hatim Tai kusilimu na kuingia katika dini tukufu ya Kiislamu alikuwa Mkristo na alikuwa kiongozi wa kabila la Tayy. [8] Tarehe 18 Rabiu Thani; mwaka wa 9 Hijiria, Mtume (s.a.w.w) alimtuma Imam Ali (a.s) na jeshi aende katika ardhii ya Tayy. [9] Wakati Adi alipopata habari ya hilo, aliituma familia yake Sham pamoja na mali zake. Hata hivyo dada yake alikamatwa mateka na jeshi la Uislamu na akahamishiwa Madina. Dada yake Adi alimuomba Bwana Mtume (s.a.w.w) amtendee wema kwa kumuachilia huru. Mtume alikubali ombi lake na akamuachilia huru pamoja na kafila na msafara wa kaumu ya Tayy na hivyo akaelekea Sham. [10] Alipofika kwa kaka yake, Adi alimuuliza mtazamo wake kuhusiana na Mtume. Dada yake Adi alimtaka ndugu aende kwa Mtume haraka zaidi, kwani kama itakuwa kweli ni Mtume basi kila atakayejiunga naye na kumuamini ana fadhila kubwa na kama ni mfalme basi hakuna kitakachopungua katika izza na heshima yako. Adi alikubaliana na mtazamo wa dada yake, hivyo akafunga safari na kwenda Madina. Baada ya kukutana na Mtume na kufanya naye mazungumzo akagundua kwamba, ni kweli ni Mtume wa Allah, hivyo akaamua kusilimu. [11] Inaelezwa katika historia kwamba, Adi alisilimu na kuingia katika Uislamu katika mwaka wa 9 Hijiria au 10 Hijiria.

Kushiriki katika vita mbalimbali katika zama za makhalifa

Katika tukio la kuritadi watu na kutoka katika Uislamu baada ya kuaga dunia Bwana Mtume (s.a.w.w) Adi yeye alibakia katika Uislamu na alizuia pia kaumu yake kuritadi na kutoka katika Uislamu. [13] Alipeleka sadaka za kabila la Tayy kwa Khalifa Abu Bakr. [14] Alishiriki katika vita vya Ridda vilivyotokea katika zama za Khalifa wa kwanza [15). Katika vita na Tulayha aliyekuwa akidai Utume [16], Adi alikuwa kamanda wa mrengo wa kulia. [17. Kadhalika kama zama za Khalifa wa pili alishiriki katika kuyakomboa maeneo mengi na kuyaweka chini ya udhibiti wa Uislamu (Iran na Iraq) [18]. Katika kipindi cha ukhalifa wa Othman bin Affan, Adi alijiunga na wapinzani wa khalifa huyu na Ibn A'tham al-Kufi anamhesabu Adi bin Hatim kuwa miongoni mwa waliomuua Othman bin Affan. [19]

Kuwa kwake pamoja na Imam Ali (a.s) na Imam Hassan (a.s)

Adi alikuwa pamoja na Imam Ali (a.s) katika zama za ukhalifa wake. [20]

  • Vita vya Jamal

Kwa mujibu wa nukuu ya Qutaybah (aliyeaga dunia) 276 Hijiria), Adi bin Hatim Tai aliandaa wapiganaji 13,000 waliokuwa katika vipando wa kabila lake la Tayy kwa ajili ya kwenda kumsaidia Imam Ali (a.s). [21] Wakati wa kujiri vita pia, Imam Ali (a.s) alimtaka Adi na watu wengine kadhaa kumfuatilia ngamia aliyekuwa amependa bibi Aisha. [22] Inasemekana kuwa, Adi alijeruhiwa jicho lake katika vita vya Jamal [23] na kauli nyingine ikisema alijeruhiwa katika vita vya Siffin. [24] Turayf mtoto wa Adi aliuawa katika vita hivi vya Jamal. [25]

  • Vita vya Siffin

Katika vita vya Siffin kulikuwa na ushindani baina ya Adi bin Hatim Tai na Bwana mmoja kutoka katika kabila la Bani Hazmar wa kubeba bendera ya jeshi la Waislamu. Hata hivyo, Imam Ali (a.s) alikabidhi bendera hiyo kwa Adi bin Hatim. [26] Kadhalika katika vita hivi, Imam Ali alimteua Adi na watu wengine kadhaa na kuwatuma kwa Muawiya ili wakamlinganie Mwenyezi na kitabu chake (Qur'ani). [27] Katika vita hivi, mwanawe Zayd alikuwa katika jeshi la Imam Ali (a.s), lakini wakati alipoona jeneza la mjomba wake Habis bin Sa'ad Tai ambaye alikuwa katika jeshi la Muawiya, alijitenga na jeshi la Imam Ali (a.s) na kujiunga na jeshi la Muawiya. [28]

  • Vita vya Nahrawan

Katika vita vya Nahrawan pia, Adi alikuwa katika jeshi la Imam Ali (a.s) [29] na mwanawe Turfa aliuawa pia katika vita hivi. [30]

Baada ya kuuawa shahidi Imam Ali (a.s)

Katika zama za ukhalifa na uongozi wa Imam Hassan al-Mujtaba (a.s), Adi bin Hatim Tai alikuwa akiwahamasisha na kuwashajiisha watu pia wajiunge na jeshi la Imam Hassan kwa ajili ya kupigana jihadi na Muawiya. [31] Kwa mujibu wa nuukuu ya Abul-Faraj Isfahani ni kwamba, wakati Adi alipoona udhaifu na kulegalega watu kuhusu kujiunga na jeshi la Imam Hassan aliwahutubu kwa kuwaambia: Subhanallah! (ametakasika Mwenyezi Mungu) ni kwa namna gani kitendo chenu hiki ni kibaya! Kwa nini hamuitikii mwito wa Imam wenu?!... Je, hamuogopi ghadhabu za Mwenyezi Mungu?! [32]

Kumtetea Imam Ali (a.s) mbele ya Muawiya

Ali bin Hussein Mas'oudi, mwandishi wa historia wa Kishia anasema: Muawiya alimuuliza Adi: Wanao kimewapata nini? Adi akajibu kwa kusema: Waliuawa wakiwa katika jeshi la Imam Ali (a.s). Muawiya akasema: Kwa hakika Ali hakuamiliana nawe kwa insafu na uadilifu, kwani aliwaacha watoto wake na akawatuma watoto wako vitani. Adi akasema: "Hapana; Naapa kwa Mwenyezi Mungu, mimi sikufanya muamala wa kiinsafu, kwani Ali ameuawa na mimi ningali hai!" [33]

Kadhalika Adi alimuonya Muawiiya kuhusiana na kuumsema vibaya Imam Ali (a.s) na kusema: Naapa kwa Mungu wa Muawiya! Chuki niliyokuwa nayo moyoni mwangu dhidi yako, hadi sasa ingalipo, na panga ambazo zilipigana na wewe zikiwa katika safu ya Ali zina nafasi katika mabega yangu. Kama utatukaribia sisi kwa kiwango cha umbali wa vidole viwili ukitumia ubaya na hila, basi sisi tutakuja karibu nawe, na kwa hakika ni rahisi kwetu kukata koo zetu na kukosa pumzi kuliko kusikia kashfa na maneno mabaya kumhusu Ali." [34]

Ibrahim Muhammad Bayhaqi, mwanafasihi wa karne ya tatu Hijria amenukuu mazungumzo mengine yaliyojiri baina ya Muawiya na Adi katika kitabu cha al-Mahasin wal-Musawa. Katika mazungumzo haya, Muawiya alimtaka Adi ampe wasifu kuhusiana na Ali (a.s). Adi alisema: Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, yeye alikuuwa mwenye upeo wa mbali na mwenye nguvu, na alikuwa akizungumza kwa uhakika kabisa, alikuwa akiwasaidia watawala waliokwama (hapa inaashiriwa msaada katika utoaji hukumu)…." Muawiya alilia kwa kusikia maneno haya ya Adi na kusema: Subira yako ya kutengana naye iko kwa namna gani? Adi akajibu kwa kusema: Ni mfano wa subira ya mwanamke ambaye mwanawe amekatwa kichwa mikononi mwake; si machozi yake yanakauka wala kilio chake kina mwisho." [35] Sheikh Abbas Qomi (aliaga dunia) 1359 Hijiria), naye ameyaandika haya katika kitabu chake cha Safinat al-Bihar. [36]

Mazungumzo haya katika baadhi ya vyanzo yamenasibishwa na Dhirar bin Dhamrah. [37]

Kuwaombea watu kwa Mukhtar

Muhammad Hadi Yusuf Gharawi (alizaliwa 1327 Hijiria Shamsia), mtafiti wa historia ya Kiislamu anasema, Adi bin Hatim wakati wa harakati ya Mukhtar hakuwa miongoni mwa waungaji mkono wale wapinzani wake. [38] Katika vita vya Jabbâna as-Sabî' vilivyotokea baina ya Mukhtar al-Thaqi na wapinzani wake, kundii miongoni mwa kabila la Tayy ambalo lilikuwa wapinzani wa Mukhtar lilichukuliwa mateka, [39] Adi bin Hatim alikwenda kwa Mukhtar na kuwaombea na Mukhtar akwaachilia huru. [40] Kadhalika familia ya Hakim bin Tufayl al-Tai mmoja wa wanajeshi wa Omar bin Sa'ad katika tukio la Karbala, ilimtakka Adi bin Hatim aende kuwaombea kwa Mukhtar. Wakati Adi alipomuombea, Mukhtar alisema: Vipi unaona inafaa kumuombea msamaha mmoja wa wauaji wa Hussein?! Adi alisema, wamemsingizia uongo. Mukhtar akasema, kama ni hivyo, ninamkabidhi kwako. Hata hivyo kabla ya hapo, watu wa Mukhtar ambao walikuwa wakihofia Mukhtar kukubali uombezi wa Adi walimuua Hakim bin Tufayl.[41]

Nafasi yake katika hadithi

Sheikh Tusi amemhesabu Adi bin Hatim kuwa ni miongoni mwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w) [42] na katika masahaba wa Imam Ali (a.s). [43] Adi amepokea hadithi kutoka kwa Imam Ali (a.s). [44] Kadhalika baadhi ya hadithi zake zimenukuliwa katika kitabu cha Sahih Bukhari. [45]

Vyanzo

  • Balādhurī, Aḥmad b. Yaḥyā al-. Jumal min ansāb al-ashrāf. Edited by Suhayl Zakār & Riyāḍ al-Ziriklī. volume 1. Beirut: Dār al-Fikr, 1996.
  • Bayhaqī, Ibrāhīm b. Muḥammad. Al-Maḥāsin wa al-masāwī. Beirut: Dar al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1420 AH.
  • Bukhārī, Muḥammad b. Ismāʿīl al-. Ṣaḥīḥ al-Bukhārī. [n.p]. [n.d].
  • Dhahabī, Muḥammad b. al-Aḥmad al-. Tārīkh al-Islām wa wafayāt al-mashāhīr wa l-aʿlām. [n.p]. [n.d].
  • Dīyārbakrī, Ḥusayn b. Muḥammad. Tārīkh al-khamīs fī aḥwāl ʾanfas al-nafīs. [n.p]. [n.d].
  • Ibn al-Athīr al-Jazarī, ʿAlī b. Abī l-Karam. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār Ṣādir, 1385 AH-1965.
  • Ibn Ḥazm al-Andulīsī, ʿAlī b. Aḥmad b. Saʿīd. Jamharat ansāb al-ʿarab. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1997.
  • Ibn Saʿd, Muḥammad. Al-Ṭabaqāt al-kubrā. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Qādir ʿAṭā. Beirut: Dar al-Kutub al-ʿIlmiyya, 1997.
  • Ibn ʿAbd al-Barr, Yūsuf b. ʿAbd Allāh. Al-Istīʿāb fī maʿrifat al-aṣḥāb. Edited by ʿAlī Muḥammad al-Bajāwī. Beirut: Dār al-Jīl, 1412 AH.
  • Ibn Qutayba al-Dīnawarī, ʿAbd Allah b. Muslim . Al-Imāma wa l-sīyāsa. Qom: Intishārāt-i al-Sharīf al-Raḍī, 1413 AH.
  • Ibn Kathīr al-Dimashqī, Ismāʿīl b. ʿUmar. Al-Bidāya wa l-nihāya. Beirut: Dār al-Fikr, 1407 AH-1986.
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik. Al-Sīra al-nabawīyya. Edited by Muṣṭafā al-Saqā and others. volume 2. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
  • Khoei, Sayyid Abū l-Qāsim al-. Muʿjam rijāl al-ḥadīth. [n.p]. [n.d].
  • Muslim Nayshābūrī. Ṣaḥīḥ Muslim. [n.p]. [n.d].
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Murūj al-dhahab wa maʿadin al-jawhar. Edited by Asʿad Dāghir. Qom: Dār al-Hijra, 1409 AH.
  • Nuwayrī, Aḥmad b. ʿAbd al-Wahhāb. Nihāyat al-ʾarab fī funūn al-ʾadab. Cairo: Dār al-Kutub wa al-Wathāʾiq al-Qawmiyya, 1423 AH.
  • Qummī, Shaykh ʿAbbās. Safīnat al-biḥār. Tehran: Farāhānī, [n.d].
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-Ṭabarī. volume 11. Beirut: Dar al-Turāth, 1967.
  • Wāqidī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Al-Radda maʿ nabadhat min futūḥ al-Irāq wa dhikr al-Muthannā b. Ḥāritha al-Shaybānī. Edited by Yaḥyā al-Jabūrī. Beirut: Dār al-Gharb al-Islāmī, 1410 AH.
  • Wāqidī, Muḥammad b. ʿUmar al-. Al-Maghāzī. volume 3. Beirut: Muʾassisa al-Aʿlamī, 1409 AH.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Beirut: Dār Ṣādir, [n.p].
  • Yūsufī Gharawī, Muḥammad Hādī. Mawsaūʿa al-tārīkh al-Islāmī. 1st edition. Qom: Majmaʿ Andīsha-yi Islāmī, 1417 AH.