Nabii Yusuf (a.s)

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Yusuf)
Bango la filamu ya Nabii Yusuf
Makala hii ni kuhusu Nabii Yusuf (a.s). Ili kufahamu kuhusiana na filamu ya mfululizo yenye jina hili, angalia makala ya Nabii Yusuf (as) (filamu ya mfulilizo).

Yusuf (Kiarabu: النبي یوسُف) ni mmoja wa Mitume anayetokana na Bani wa Israili na mtoto wa Nabii Yakub. Alitawala Misri kwa miaka mingi huku akiwa na nafasi na daraja ya Utume. Ndani ya Qur’an, kuna sura iliyopewa jina la Yusuf na kisa cha maisha yake kimesimuliwa ndani yake.

Yusuf alitupwa kisimani na ndugu zake alipokuwa mtoto; lakini kundi lilimnusuru kutoka kisimani na kumuuza kama mtumwa kwa Azizi wa Misri. Zulaykha, mke wa Azizi wa Misri, alipenda ujamali wa Yusuf, lakini baada ya Yusuf kukataa kuwa na mahusiano naye wa kimapenzi, alimshutumu Yusuf kwa kumsaliti Azizi wa Misri, na akatiwa gerezani.

Baada ya miaka mingi, Yusuf alithibitisha kuwa hana hatia na akatoka gerezani, na kwa kufasiri ndoto ya mfalme wa Misri na kulipatia ufumbuzi tatizo la njaa nchini Misri, akaondokewa kuwa kipenzi na akawa waziri wake.

Kisa cha Yusuf ndani ya Qur'an kina tofauti na kile ambacho Torati inasimulia kuhusiana na jambo hili; kwa mfano, kwa mujibu wa Qur’an, ndugu ndio waliomuomba baba yao Nabii Ya’qub amtume Yusufu pamoja nao jangwani, lakini kwa mujibu wa Torati, Yakobo anamwomba Yusuf aandamane na ndugu zake.

Inasemekana kwamba Nabii Yusuf aliishi kwa miaka 120 na mahali alipozikwa ni Palestina.

Nafasi

Yusuf mwana wa Ya’qub alikuwa mmoja wa Manabii wa Bani Israili, na jina la mama yake ni Rachel. [1] Alikuwa na kaka kumi na mmoja, ambapo miongoni mwao ni Benjamin tu ndiye nduguye waliyechangia baba na mama. [2] Yusuf alikuwa mdogo zaidi kwa kaka zake isipokuwa Benjamin. [3]

Jina la Yusuf limekuja mara 27 katika Qur'an [4] na Sura ya 12 ya Qur'an imeitwa kwa jina lake. Qur’ani imemtambulisha Yusuf kuwa ni mmoja wa waja waaminifu na wenye ikhlasi wa Mwenyezi Mungu [5], ambapo, kwa mujibu wa Allama Tabataba’i, siyo tu kwamba hakukubaliana na ombi la Zulaykha aliyemtaka kimapenzi, bali hata hakuwa na mwelekeo wa fikra hiyo moyoni mwake. [6] Pia katika Qur'ani Yusuf anahesabiwa kuwa miongoni mwa wafanyao wema. [7]

Utume

Yusuf anahesabika kuwa ni miongoni mwa Manabii wakubwa [8] Katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Baqir (a.s) anasema akinukuu Aya za Qur’an kwamba, Yusuf anahesabiwa kuwa Nabii na Mtume. [9] Kwa mujibu wa tafsiri ya Nemooneh, ndoto ya Yusuf ambayo ndani yake mwezi na nyota 11 na jua vilimsujudia, mbali na kutoa habari ya Yusuf kuwa tajiri na kupata mamlaka na uongozi, hilo lilikuwa likibainisha Utume wake katika mustakabali. [10] Allama Muhammad Hussein Tabataba’i pia anasema kuwa, moja ya vielelezo vya kukamilika neema kwa ajili ya Yusuf ambacho kimekuja katika Aya ya 6 ya Surat Yusuf ni kufikia kwake nafasi na daraja ya Utume. [11]

Historia ya maisha yake

Katika Qur'an, kisa cha maisha ya Yusuf kimeelezewa kwa kina katika Surat Yusuf. Qur'an Tukufu ikaita hadithi yake kuwa ni Ahsan al-Qasas (simulizi nzuri kabisa) [12] na ikasimulia kwa maelezo ya kina kabisa na kubainisha kuhusiana na kipindi cha ubarobaro na kuinukia kwake, kutupwa kisimani, kuuzwa kwake kwa Azizi wa Misri, kisa cha Zulaykha na Yusuf, kufungwa gerezani, kukutana na baba yake na ndugu zake, na utawala wake huko Misri. [13]

Kutupwa kisimani na kupelekwa Misri

Kadhalika angalia: Surat Yusuf

Kisa na simulizi ya maisha ya Yusuf imefafanuliwa kwa kina ndani ya Qur'an katika Surat Yusuf. Kwa mujibu wa Qur'an, Yusuf anamwambia: Ewe babaangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja, na jua, na mwezi vinanisujudia. Baba yake akamwambia: Ewe mwanangu! Usiwasimulie nduguzo ndoto yako; kwa sababu wanapanga mpango hatari dhidi yako. [14]

Wafasiri wanasema kuwa, makusudio ya nyota kumi na moja ni ndugu zake Yusuf, na makusudio ya mwezi na jua kuwa ni baba yake na mama yake, ambao baadaye walimfanyia taadhima Yusuf alipofikia hadhi ya kidunia na kimaanawi. [15]

Watoto wa Nabii Ya’qub (a.s) walikuwa wakisema kuwa Yusuf na kaka yake wanapendwa zaidi na baba kuliko sisi. [16] Siku moja walimuomba Yaaqub amruhusu Yusuf aende nyikani kucheza nao na wakaahidi kumlinda. [17] Walikuwa katika jangwa wakati walipomkamata Yusuf na kamtupa kisimani na baada ya kurejea wakamwambia Yaqub kwamba mbwa mwitu amemla. [18] Kwa mujibu wa aya za Quran, Yaqub hakuamini maneno yao. [19]Na baadaye akawa kipofu kutokana na maumivu ya kutengana na kutokana na kumlilia sana Yusuf. [20] Imamu Sadiq (a.s) aliulizwa: Nabii Yaqub, alimhuzunikia Yusuf kiasi gani? Akasema: Kama majonzi ya wanawake sabini ambao watoto wao wamekufa. [21] Msafara ukamuokoa Yusuf kisimani [22] na kumpeleka Misri kama mtumwa na Azizi wa Misri alimnunua na akaingia katika familia ya Azizi na kuwa sehemu ya familia hiyo. [23]

Uzuri wa Yusuf na mkasa wake na Zulaykha

Katika vitabu vya visa vya Qur'an, Yusuf anaelezewa kama kijana mzuri sana. [24] Kwa hiyo, Zulaykha, mwanamke mpendwa wa Kimisri, alimpenda na kumwita mara kwa mara kutenda dhambi, lakini Yusuf alikataa na kuona uthibitisho wa Mola wake kwamba ni kitu katika jinsia ya aelimu na yakini ni kwa ajili ya Waumini. [25] Hakukubali ombi la Zulaykha la kufanya naye kitendo kichafu. [26]

Habari ya mkasa wa Zulaykha kumpenda Yusuf na kumtaka kimapenzi ikaenea na kufika masikioni mwa watu wa mji huo na kundi la wanawake lilimlaumu Zulaykha na walisema, Mke wa Mheshimiwa anamtamani mtumishi wake ! Hakika amesalitika kwa mapenzi. Sisi hakika tunamwona yumo katika upotovu ulio dhaahiri. Kwa mujibu wa Qur’an, Zulaykha alipo sikia masengenyo yao aliwaalika wanawake [40] miongoni mwa wanawake wa familia za kibwanyenye na akawawekea matakia ya kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu na matunda. [28] Akamwambia Yusuf: Tokeza mbele yao. Basi walipo mwona waliathirika na kuvutiwa mno na waliona ni kitu kikubwa kabisa, na wakajikata vibaya mno mikono yao. Wakasema: Hasha Lillahi! Huyu si mwanaadamu. Hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu. [29]

Baada ya tukio hili, na kutokana na kuwa, kila siku wanawake walikuwa wakimtaka Yusuf awe na mahusiano haramu nao, alimwomba Mwenyezi Mungu amtupe gerezani ili aepukane nao pale aliposema: Ee Mola Mlezi wangu! Nastahabu kifungo kuliko haya anayo niitia. Na usipo niondoshea vitimbi vya wanawake mimi nitamili kwao, na nitakuwa katika wajinga. Baada ya muda, alifungwa jela kwa amri ya Zulaykha. [31]

Kufasiri ya ndoto ya mfalme na mheshimiwa wa Misri

Kutokana na Yusuf kujua kufasiri ndoto, alifasiri ndoto ya wafungwa wawili na kutabiri kwamba mmoja wao atauawa na mwingine ataachiliwa huru na kupata cheo kwa mfalme wa Misri.[32] Miaka michache baada ya tukio hili , mfalme wa Misri akaota ng'ombe saba wanene wanaliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu. [33] Na kwa sababu wafasiri wa ndoto walishindwa kufasiri ndoto hiyo ya mfalme, wakati huo yule mfungwa ambaye alikuwa ameachiliwa na alikuwa ndani ya utawala na mmoja wa wafanyakazi wa karibu na mfalme, alisema kwamba Yeye atawaambia tafsiri ya ndoto hiyo. [34]

Alienda gerezani na kusema, Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng'ombe saba wanene kuliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu, ili nirejee kwa watu wapate kujua. Yusuf akasema: Mtakuwa na miaka saba ya maji mengi na katika kipindi hicho mtalima miaka saba kwa juhudi. Halafu akapendekeza kwamba, Mtacho vuna kiwacheni katika mashuke yake, isipo kuwa kidogo mtacho kula. Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayo kula kile mlicho iwekea isipo kuwa kidogo mtacho kihifadhi. Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao katika mwaka huo watu watasaidiwa, na watakamua. [35]

Baada ya Mfalme kupenda tafsiri hii ya ndoto yake iliyotolewa na Yusuf na suluhisho lake la kuokoa Misri kutokana na njaa, aliagiza Yusuf aletwe mbele yake; lakini alimwambia mjumbe wa mfalme amuulize mfalme kuhusu kisa cha kujikata mikono wanawake na kufungwa kwake. Mfalme alichunguza suala hili na kuwaita wanawake wa jiji kwenye mahakama. Wanawake wa Misri walisisitiza kutokuwa na hatia Yusuf na Zulaykha akakiri kile alichofanya. [36]

Baada ya kufasiri ndoto na kuthibitisha kutokuwa na hatia kwa Yusuf, mfalme wa Misri alimtoa gerezani na kumfanya waziri wake na azizi wa Misri. [37]

Kukutana na familia

Wakati wa ukame wa Misri, eneo la Canaan nalo pia lilikumbwa na uhaba wa chakuka. Kwa hiyo Yaqub akawatuma wanawe Misri ili kufuata ngano baada ya kusikia kwamba, huko inapatikana. [38] Yusuf akawatambua alipowaona ndugu zake; lakini wao hawakumtambua [39] Aliwatendea wema ndugu zake [40] na kwa kumpelekea Yaqub kanzu yake, akayafanya macho yake ya upofu yaone [41] Baada ya hapo, Yaqub na watoto wake walikwenda Misri kumtembelea Yusuf. [42]

Kuoa kwake na kupata watoto

Kwa mujibu Masoudi, mwanahistoria Mwislamu wa karne ya nne Hijiria, Yusuf alioa huko Misri na kuruzukiwa watoto wawili wa kiume walioitwa Ephraim, (babu yake Yushau Bin Nun) na Manasseh.[43]

Kufunga ndoa na Zulaykha

Katika baadhi ya hadithi, ndoa ya Yusuf na Zulaykha imetajwa kuwa ilifanyika baada ya Yusuf kufikia cheo cha azizi huko Misri. Kwa mfano, imetajwa katika hadithi ya kwamba Yusuf alimuona mwanamke aliyesema, "Asante Mungu kwa kuwa umewafanya watumwa kuwa wafalme kwa sababu ya utiifu wao na kuwafanya wafalme kuwa watumwa kwa sababu ya uasi wao." Alimuuliza yeye ni nani, akasema mimi ni Zulaykha, na Yusuf akamuoa. [44] Na hata imekuja katika baadhi ya riwaya, imeelezwa kuwa Zulaykha alibadilika na kuwa kijana baada ya kuombewa dua na Yusuf na kisha Yusuf akamuoa. [45] Lakini baadhi baada ya kuzichunguza riwaya husika katika sanadi na mapokezi wamezitilia dosari na hivyo kuzikataa. [46] Imekuja katika baadhi ya nukuu watoto wote wawili wa Yusuf (Manasseh na Ephraim) alizaa na Zulaykha. [47]

Kuacha lililobora

Kadhalika angalia: Kuacha lililo bora
Ramani ya mahali alipozaliwa Nabii Yusuf na kupewa Utume

Kwa mujibu wa Aya ya 42 ya Surat Yusuf, Yusuf alipokuwa gerezani, alimpa mfungwa mmoja habari za kuachiliwa kwake na akamwambia: Nikumbuke kwa bwana wako. Lakini Shetani alimsahaulisha kumtaja kwa bwana wake. Basi Yusuf akakaa gerezani miaka kadhaa. Kuna tofauti ya maoni kati ya wafasiri katika suala hili.Baadhi wamesema makusudio ni kwamba, shetani alimfanya Yusuf amsahau Mungu, na kwa mujibu wa baadhi ya watu wengine, shetani alimfanya mfungwa yule asahau kumwambia mfalme kuhusu kutokuwa na hatia kwa Yusuf. Allama Tabataba’i aliichukulia rai ya kwanza kuwa haiendani na Qur'ani; kwa sababu, kwa upande mmoja, katika Qur’ani, Yusuf anahesabiwa kuwa mmoja wa watu wema na wenye ikhlasi, na kwa upande mwingine, imeelezwa kwamba shetani kamwe hawezi kupenya katika mawazo ya waja wema. [48] Vyovyote itakavyokuwa, wafasiri wametambua kitendo hicho cha Yusuf kuwa ni kuacha lililo bora; kwani kwa Manabii na watu ambao wana daraja ya juu ya tawhidi, kiwango hiki hiki cha kutumia njia za kidunia hakikubaliki. [49]

Katika baadhi ya hadithi kuna kitendo kingine cha “kuacha lililobora” ambacho kinanasibishwa na Yusuf. [50] Kwa mujibu wa hadithi hizi, Nabii Yaqub alipokuja kwa Yusuf baada ya kutengana kwa miaka mingi, Yusuf hakushuka kutoka kwenye kiti chake cha ufalme [51] ili kumheshimu baba yake mzee, akizingatia nafasi yake ya ufalme, na kwa sababu hii, Mwenyezi Mungu akaondoa Unabii kutoka katika kizazi cha Yusuf [52] na akakiweka katika kizazi cha Levi nduguye Yusuf. [53] Jafar Sobhani, mmoja wa wafasiri wa Qur’an wa Kishia, anaamini kwamba, hadithi hizi hazioani na Qur’ani; kwa sababu kwa mujibu wa Aya za Qur'ani Tukufu, Yusuf alimfanyia heshima kubwa baba yake. [54] Muhammad Sadiq Tehran, mwandishi wa tafsiri ya al-Furqan anaamini kuwa, hadithi hizi ni Israiliyat na zina matatizo katika pande mbalimbali. [55]

Tofauti ya kisa cha Yusuf katika Qur’an na Torati

Kwa mujibu wa kile kilichonukuliwa na Allama Tabatabai, kisa cha Yusuf katika torati kina tofauti na kilivyoelezwa katika Qur’an.[56] Imeelezwa kuwa Yusuf alieleza ndoto ya kusujudiwa na nyota, jua na mwezi kwa ndugu zake, wakamwonea husda na wivu na wakaingiwa na wasi wasi kwamba Yusuf atawatawala baadaye. Pia, kwa mujibu wa Torati, alipomuelezea baba yake Yaqub ndoto hiyo, Yaaqub alimkasirikia na akasema: Je, mimi na mama yako na ndugu zako kumi na mmoja tutakusujudia? Tofauti nyingine ni kuwa, kwa mujibu wa Qur’an, nduguze Yusufu walimuomba Ya’qub amruhusu Yusuf aende pamoja nao jangwani, [58] lakini katika ripoti ya torati, ni kwamba, Ya’qub ndiye valiyemtaka Yusuf awafuate ndugu zake jangwani ili aone kama wao na kondoo wako salama. [59]

Kifo na mahali alipozikwa

Kwa mujibu wa Masoudi mwanahistoria wa Kiislamu wa karne ya nne ya Hijria, Nabii Yusuf aliishi kwa miaka 120. Wakati kifo chake kilipowadia Mwenyezi Mungu alimletea Wahyi akimwambia kwamba, nuru na hekima alizonazo ampatie Babarz bin Lewi bin Ya’qub. Kisha Yusuf akamuita Babarz bin Lewi na Aal Ya’qub (ukoo wa Ya’qub) ambao wakati huo ulikuwa na wanaume 80 na kuwaambia kwamba, muda si mrefu kundi fulani litakushindeni na mtakumbwa na adhabu kali, mpaka Mwenyezi Mungu atakapokusaidieni kupitia kwa mmoja wa watoto wa Levi ambaye jina lake ni Mussa. [60] Baada ya kifo cha Nabii Yusuf, kila kundi lilikuwa likitaka azikwe katika eneo lake. Ili kuepusha mzozo usitokee wakamzika katika Nile baada ya kuweka maiti yake katika sanduku la marumaru. Baada ya miaka mingi, Nabii Mussa alikuja kulitoa jeneza hilo [61] na kwa mujibu wa Yaqut Hamawi, mwandishi wa historia wa karne ya 6 na ya 7 Hijria, akamzika huko Palestina. [62]

Yusuf katika athari za kisanaa

Makala asili: Nabii Yusuf (as) (filamu ya mfululizo)

Kisa cha Yusuf kimeakisiwa katika athari za kisanaa na vyombo vya habari kama vile uchoraji, fasihi, sinema na televisheni. Mwaka 2008-9, filamu ya mfululizo ya Nabii Yusuf ilirushwa katika Televisheni ya Iran. [63]

Vyanzo

  • Balāghī Ṣadr al-Dīn, al. Qiṣaṣ-i Qurʾān. 17th edition. Tehran: Amīr Kabīr, 1380 AH.
  • Ḍīyāʾ Ābādī, Muḥammad. Tafsīr Sūra Yusuf. Tehran: Muʾassisa Bunyād Khayrīyya al-Zahrāʾ, 1388 Sh.
  • Chāhār Sāl bā Yusuf Payāmbar. Vista.ir [1].
  • Ibn Tāwūs, Alī b. Mūsā. Al-Mujtanā min al-duʿā al-mujtabā. First edition. Qom: Dār al-Dhakhāʾir, 1411 AH.
  • Ibn Kathīr. Al-Bidāya wa al-nahāya. Beirut: Dār al-Fikr. 1407 AH.
  • Ibn Kathīr. Qiṣaṣ al-anbīyāʾ wa akhbār al-māḍīn. Compiled by Muḥammad b. Aḥmad Kanʿān. 1st Edition. Beirut: Muʾassisa al-Maʿārif, 1416 AH-1996.
  • Jazāʾirī, Niʿmat Allāh al-. Al-Nūr al-mubīn fī qiṣaṣ al-anbīyāʾ wa l-mursalīn. 2nd edition. Beirut: Dār al-Aḍwāʾ, 1423 AH.
  • Jaʿfarī Yaʿqub. Namha-yi payāmbarān dar Qurʾān. [n.p]. Maktab-i Islam, [n.d].
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Ithbāt al-waṣīyya. 3rd edition. Qom: ʿIsmāʿilīyān, 1384 Sh.
  • Maʿārif and others. Barrasī-yi riwāyāt-i tafsīrī-yi farīqayn dar masʾala-yi izdiwāj-i haḍrat-i Yusuf ba Zulaykhā. Dufaṣlnāma-yi Hadīth Pazhūhī, Year, 7. no 13. Spring and Summer 1394.
  • Maqdisī, Muṭahhar b. Ṭāhir al-. Al-Badʾ wa l-tārīkh. Port Said: Maktabat al-Thaqāfa al-Dīnīyya, [n.d].
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1374 Sh.
  • Rāwandī, Saʿīd b. Hibat Allāh al-. Qiṣaṣ al-anbīyāʾ al-hāwī li ahādīth kitāb al-nubuwwah li-shaykh al-Ṣadūq. Qom: Intishārāt-i ʿAllama Majlisī, 1388 Sh.
  • Ṣuḥufī Sayyid Muḥammad. Qiṣṣahā-yi Qurʾān. 2nd edition. Qom: Ahl Bayt, 1379 Sh.
  • Ṭabāṭabāyī, Mūhammad Ḥusayn. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. 5th edition. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.
  • Yāqūt al-Ḥamawī. Muʿjam al-buldān. 2nd edition. Beirut: Dār Ṣādir, 1995.