Ya'la bin Muniyah

Kutoka wikishia

Ya'la bin Muniyah au Ya’la bin Umayah (Kiarabu: يعلى بن أمية أو يعلى بن منية) ni mmoja wa maswaha wa Mtume (s.a.w.w) na alikuwa mmoja wa viongozi wa kundi la Nakithina (wavunja ahadi/mkataba). Ya’la alisilimu wakati wa Fat’h Makka (kukombolewa mji wa Makka) na alishiriki katika baadhi ya vita vya Mtume (s.a.w.w). Zimenukuliwa hadithi kutoka kwake alizonukuu kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). Ya’la alikuwa mmoja wa matajiri wa Makka na mtu aliyekuwa mkarimu na baadhi wanaamini kwamba, utajiri wake huo mkubwa ulitokana na ukarimu wa Othman bin Affan kwake.

Alishirikiana na makhalifa watatu (Abu Bakr, Omar na Othman). Alitumwa na Abu Bakr katika baadhi ya maeneo kwa ajili ya kwenda kukabiliana na As’hab Riddah (kundi la walioritadi). Ya’la alikuwa mshauri wa Othman bin Affan na alikuwa na nafasi muhimu kwake. Katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) na vilevile katika kipindi cha makhalifa watatu, Ya'la alikuwa mtawala wa maeneo mbalimbali ya Yemen. Baada ya Imam Ali (a.s) kuingia madarakani na kushika hatamu za ukhalifa alimuuzulu kutoka katika uongozi wa Yemen. Katika radiamali yake ya kuuzuliwa kutoka uongozini, Ya’la alichukua ushuru na kodi zilizokuwa zimetolewa na kwenda nazo Makka na kisha kujiunga na waasi waliokuwa wameanzisha harakati kwa kisingizio cha kutaka kulipiza kisasi cha damu ya Othman bin Affan. Alitoa pesa na mali nyingi kwa jeshi hilo la waasi.

Ya’la alitoroka baada ya kushindwa katika Vita vya Jamal na alibakia hai mpaka katika kipindi cha mwishoni mwa utawala wa Mu’awiyah; ingawa baadhi wanaamini kwamba, aliuawa shahidi katika Vita vya Siffin akipigana upande wa Imamu Ali (a.s)

Jina, Nasaba na Kuniya

Ya'la bin Muniyah au Ya’la bin Umayah bin Abi Ubaidah [1] alitokana na kabila la Bani Tamim [2] na alifahamika kwa lakabu ya Abu Saf’wan [3] na kuniya yake ilikuwa Abu Khalid. [4] Sababu ya kunasibishwa na majina haya mawili ni hii kwamba, katika baadhi ya wakati alikuwa akinasibishwa na baba yake na wakati mwingine alikuwa akinasibishwa na mama au babu yake Muniyah. [5] Hata hivyo, kunasiubishwa kwake na mama au babu yake kulikuwa mashuhuri zaidi. [6] Kutokana na tofauti za vyanzo katika kusajili jina lake, hilo lilipelekea wakati mwingine atajwe kama Ya'la bin Muniyah. [7]

Katika zama za ujahilia, Ya’la na baba yake walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wamefunga mkataba na kabila la Kureshi [8] ambapo hata hivyo baadhi wametambua mkataba huu kuwa ulikuwa na familia ya Abdul-Muttalib, [9] au Naufal bin Abdul-Manaf [10] au Abdul-Shams. [11] Ya’la alikuwa na nasaba ya sababu pia na Makureshi; kwa sababu alikuwa mkwe wa Zubeir bin Awam. [12]

Sahaba wa Mtume

Ya'la bin Muniyah alidiriki zama za uhai wa Bwana Mtume (s.a.w.w) na alisilimu na kuingia katika Uislamu wakati wa Fat’h Makka (kukombolewa Makka). [13] Kwa mujibu wa nukuu, alikwenda kwa Mtume (s.a.w.w) akiwa pamoja na baba na kaka yake [14] na dada yake [15] na akasilimu; na ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana familia yake yaani kaka zake Salama [16] na Abdul-Rahman [17] na dada yake Nafisa wanahesabiwa kuwa ni miongoni mwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w). [18]

Kwa mujibu wa ripoti ya Abdul-Barr katika kitabu cha Al-Isti’ab fi Ma'rifati al-As’hab, ni kuwa, Mtume (s.a.w.w) alikataa ombi la Ya’la bin Muniyah na baba yake la kuhesabiwa kuwa miongoni mwa Muhajirina; [19] pamoja na hayo, Baladhuri katika kitabu chake cha Ansab al-Ashraf amenukuu hadithi ya kukubaliwa ombi lao kwa uombezi wa Abbas bin Abdul-Muttalib ami yake Mtume (s.a.w.w) [20] na Ibn Athir pia amemhesabu Ya’la na baba yake kuwa ni katika Muhajirina. [21] Ya’la alikuwa mmoja wa masahaba [22] mashuhuri wa Bwana Mtume (s.a.w.w) [23] ambapo inaelezwa kuwa, umashuhuri wa kuwa kwake sahaba ni zaidi ya umashuhuri wa baba yake. [24]

Ya’ala alikuwa miongoni mwa wapokezi wa hadithi [25] na kumenukuliwa hadithi za Mtume (s.a.w.w) kupitia kwake [26] ambazo idadi yake inasemekana zinafikia 28 na hadithi tatu kati ya hizo zinapatikana katika vitabu vya Sahihi Muslim na Sahih Bukhari, miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi na vyenye itibari kwa Waislamu wa Ahlu-Sunna. [27] Kuna wapokezi tofauti wa hadithi pia wamepokea hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w) kupitia kwa Ya’la bin Umayah. [28].

Sheikh Tusi, mmoja wa watalaamu wa elimu ya hadithi wa Kishia aliyeishi katika karne ya 5 Hijria, amemhesabu Ya’la bin Umayyah kuwa miongoni mwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w, ingawa hakutoa maelezo kuhusiana naye, [29] lakini katika vyanzo vilivyofuata vimemtaja kuwa ni: “mwovu miongoni mwa masahaba wa Mtume”. [30] Katika kitabu cha Sharaf al-Nabi, kuna hadithi inayoeleza kwamba, alishuhudia muujiza wa Mtume (s.a.w.w). [31]

Kushiriki Vita

Ya’la bin Muniyah alitambuliwa kuwa mmoja wa mujahidina katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w) [32] na alishiriki katika Vita vya Tabuk, [33] Hunayn na Taif akiwa katika jeshi la Mtume (s.a.w.w). [34] Ya’la anaamini kwamba, kuwa kwake pamoja na Mtume katika vita vya Tabuk, ndio amali yake bora zaidi; [35] kiasi kwamba, kumenukuliwa visa na matukio yanayohusiana na uwepo wake katika vita hivi na maswali yake ya kisheria (kifikihi) aliyomuuliza Mtume (s.a.w.w). [36] Ibn Athir ambaye amemhesabu Ya’la kuwa ni katika Muhajrina anaamini kwamba, sahaba huyu alikuweko pia katika Vita vya Badr. [37]

Kushirikiana na Makhalifa Watatu na Kutawala Yemen

Baada ya kifo cha Badhan, Ya'la bin Muniyah alichukua utawala wa sehemu ya Yemen kwa amri ya Mtume (s.a.w.w) [38] Katika zama za Khalifa wa kwanza Abu Bakr Ya’ala alikuwa gavana na kiongozi wa eneo la Kholan. [39] Alitumwa katika eneo la Hulwan [40] kwa ajili ya kwenda kukabiliana na As’hab Riddah na baada ya kuwashinda, alipata ghawira na mateka.

Utawala wake uliendelea wakati wa zama za ukhalifa wa Omar bin Khattab, Khalifa wa pili [41], na katika kipindi hiki akawa gavana wa maeneo kama vile Najran, [42] Taif, [43] Sana'a, [44] au maeneo mengine ya Yemen [45] na hata yeye amechukuliwa kama mmoja watu waliofuatana na khalifa wa pili katika safari yake ya kwenda Sham [46]; ingawa mwisho wa ukhalifa wa Omar alikumbwa na ghadhabu za Omar na akauzuliwa uongozi, na Omar alimtaka arejee Madina kutoka Yemen kwa kutembea kwa miguu, ambapo baada ya kutembea kwa siku tano au sita hivi kwa miguu, alipata habari ya kifo cha Omar, na hivyo akapanda farasi na akaenda kwa Othman bin Affan huko Madina.[47]

Wakati wa ukhalifa wa Othman bin Affan, Y’ala alikuwa pia Gavana wa Sana'a [48] huko Yemen [49]. Pia alikuwa miongoni mwa washauri wa Othman [50] na alikuwa na nafasi ya juu kwake. [51] Lakini Imam Ali (a.s) alimuondoa kutoka katika utawala na ugavana wa Yemen, na badala yake akamteua Ubaidullah bin Abbas kuwa gavana wa Yemen. [52]

Wanahistoria wanaamini kwamba, katika kipindi cha kutawala kwake Yemen [53], Ya'la bin Muniyah alikuwa mtu wa kwanza kutumia tarehe ya Hijria katika barua zake. [54] Pia alikuwa na wadhifa wa kadhi huko Yemen. [55]

Nafasi ya Kijamii

Ya'la bin Muniyah ana daraja na cheo kikubwa [56] na hata ametambuliwa kuwa mtoa fat'wa huko Makka [57]. Pia, alikuwa mmoja wa wakazi matajiri wa Makka [58] ambaye mali yake wakati ameaga duni ilitajwa kuwa ni dinari elfu hamsini na kumetajwa mali na milki nyingine ambapo thamani ya sehemu ya mali imeripotiwa kufikia hadi dirihamu laki tatu. [55] Na kwa kutumia mali hii, aliwapa na kuwasaidia wengine; [60] kiasi kwamba Ya’la alitambuliwa kuwa mmoja wa watu wakarimu sana katika zama zake [61], na hata kulikuwa na ripoti kuhusu matumizi yake mabaya ya hazina ya dola [62]. Baadhi ya watu waamini kwamba mali hii ilipatikana kutokana na yeye kuwa pamoja na kuwa karibu na Othman bin Affan [63] na kwa hiyo amejumuishwa katika orodha ya masahaba waliopata utajiri mkubwa wakati wa utawala wa Othman. [64]

Kuwasaidia Watu wa Jamal

Ya’la bin Muniyah alikuwa miongoni mwa shakhsia wa asili na wakuu wa vita vya Jamal [65] na alikuwa pamoja na Talha bin Abdallah, Zubeir bin Awam, Abdallah bin Amir, Said bin A’as, Walid bin Aqabah na shakhsia wengine wa Bani Umayyah ambao walianzisha vita kwa kisingizio cha kutaka kulipiza damu ya Othman, [66] na kutokana na watu wa Basra kuwa na mapenzi makubwa kwa Othman khalifa aliyeuawa, [67] baada ya mashauriano mengi walianzisha fitina ya Jamal huko Basra. [68]

Ya'la alikuwa amewaahidi wale waliosimama kulipiza kisasi cha damu ya Othman kwamba atawapatia silaha [69]. Alikuwa na jukumu la kumtia moyo na kumchochea Aisha kuwaondoa na hatia wauaji wa Othman na kujiunga na waasi [70], na akiwa pamoja na Abdullah bin Amir, alichukua jukumu la usaidizi wa kifedha kwa Jeshi la Jamal. [71] Ya'la bin Muniyah alinufaika katika hili na fedha za kodi na ushuru alizokuwa amekusanya huko Yemen. [72] Baada ya kuondolewa kwenye utawala Yemen na Imam Ali (a.s.), Ya'la alichukua ushuru aliokuwa ameukusanywa na kwenda nao Makka [73], ambao unakadiriwa kuwa ulikuwa kama ngamia 400 [74] hadi 600, na kiasi cha fedha taslimu kilikuwa kikikadiriwa kufikia dirihamu 600,000. [75] Kwa mali hii, alitumia mali nyingi kwa ajili ya jeshi [76] na akawapa vifaa na zana za kijeshi watu sabini kutoka kwa Makureshi [77] na akatoa dirihamu laki nne kwa Talha na Zubair [78] na akadhamini na kutayarisha silaha na vifaa kwa ajili ya wapiganaji wa Jamal [79], kwa namna ambayo alimpa kila shujaa silaha na farasi na zaidi ya hayo alilipa dinari 30 kwa kila shujaa kama malipo ya wajibu [81]. Ngamia wa Aisha pia katika vita hivi ambaye alikuwa mashuhuri kwa jina la Askari alinunuliwa na Ya’la bin Muniyah kwa dinari 80 [81] au 200. [82]

Ni kutokana na sababu hii, ndio maana katika baadhi ya riwaya zilizopokelewa kutoka kwa Imam Ali (a.s), zinamtambulisha Ya’la kama mtu msaliti na mfanya khiana [83], na kwamba, alikuwa na kasi zaidi miongoni mwa watu katika kuchochea fitna [84] na msaidizi wa kifedha wa waasi; [85] kama ambavyo Imam Ali (a.s.) katika hadithi nyingine inayohusiana na Vita vya Jamal amemtaja Ya'la na kumuelezea kuwa ni miongoni mwa watu matajiri zaidi, na suala hili, pamoja na ushujaa wa Zubair bin Awam na ukarimu au ibada ya Talha bin Ubaidullah na bila shaka umaarufu wa Aisha, ndio mambo yaliyopelekea akabiliwe na hali ngumu katika vita vya Jamal. [86]

Kifo Chake

Ya'la ibn Muniyah alikimbia baada ya kushindwa katika Vita vya Jamal, na kwa mujibu wa baadhi, kama vile Dhahabi, mwandishi wa Tarikh al-Islam, alikuwa hai hadi mwisho wa ukhalifa wa Mu'awiya ibn Abi Sufyan. [87] Ibn Abd al-Barr katika al-Istiyab ameleta hadithi ambayo inaeleaza kuwa, licha ya kwamba, Ya’la alipigana pamoja na Aisha dhidi ya Imam Ali (a.s) katika Vita vya Jamal, lakini katika Vita vya Siffin alipigana bega kwa bega na pamoja na Imam Ali (a.s), [88] na mwaka 37 Hijiria [89] au 38 Hijiria [90] aliuawa akiwa anapigana upande wa Imam Ali (a.s). [91] Kwa msingi huu, baadhi akiwemo Abdallah Mamaqani, amemtambulisha Ya’la kuwa alipata hatima njema. [92] Pamoja na hayo kuna nukuu pia zinazoonesha kuwa, Ya’la bin Muniyah alikuwa hai mpaka mwaka 49 Hijiria. [93]

Rejea

Vyanzo