Nenda kwa yaliyomo

Ugeuzaji umbo

Kutoka wikishia

Metamofosisi au Ugeuzwaji Umbo (Kiarabu: المَسْخ) ni aina ya adhabu ambapo katika hilo, mwanadamu anabadilishwa na kuwa na sura na umbo la mnyama. Hata hivyo katika hali ya kugeuzwa, mwanadamu hapotezi utambulisho wake. Bali umbo lake la kidhahiri tu ndilo ambalo huonekana kwa sura ya mnyama. Katika vyanzo vya kiislamu kumetajwa matukio tofauti ya kugeuzwa watu na kuwa katika maumbo ya wanyama. Tukio mashuhuri zaidi miongoni mwayo ni kisa cha As’hab al-Sabt (watu wa Sabt).

Katika tukio hilo, baada ya maonyo ya siku chache, watu hao wapotofu walipokithiri katika kutotii amri ya Allah, waliteremshiwa adhabu kutoka kwa Allah kwamba nyuso zao ziligeuka kuwa za wanyama na baada ya kupita siku tatu, Allah (s.w.t) aliwateremshia adhabu kali kiasi kwamba wote kwa pamoja wakateketea.

Kwa mujibu wa Aya za Qur’an As’hab al-Sabt (watu wa Sabt) ambao ni katika kundi la Banu-israel waligeuzwa manyani baada ya kuasi amri ya Allah iliyowataka wasivue samaki siku ya Jumamosi. Kwa mujibu wa hadithi za Kiislamu, katika siku ya kiyama pia kutakuwa na metamofosisi (kugeuzwa) ambapo baadhi ya watenda dhambi watageuzwa na kuonekana katika sura na umbo la wanyama kama nyani na nguruwe.

Baadhi ya wafasiri wa Qur’an tukufu wanaamini kuwa, ugeuzwaji wa umbo unaozungumziwa katika Qura’n ni neno la ufananishaji kwa maana hii kwamba; baadhi ya watu kutokana na kutenda dhambi huwa na hali na tabia ya kinyama; hata hivyo wafasiri wengi hawakubaliani na tafsiri na maana hii na wanasema kwamba, watu wa namna hiyo sura na umbo lao la kidhahiri pia hubadilika.

Maana ya Metamofosisi au Ugeuzwaji (المَسْخ) na Tofauti Yake na Ufutwaji (التناسخ)

Metamofosisi maana yake ni kubadilishwa sura ya kidhahiri na kuwa na umbo baya na lisilofaa. [1] Ugeuzwaji (المَسْخ) una tofauti na ufutwaji (التناسخ). Ufutwaji una maana ya roho kutoka katika mwili fulani na kwenda katika mwili mwingine, lakini katika ugeuzwaji ni kwamba roho haitengani na mwili; bali ni umbo la dhahiri tu ndilo linalobadilika na kuwa na katika sura ya mnyama. [2]

Kubakishwa Utambulisho wa Mtu katika Metamofosisi

Wanazuoni wa Kiislamu wanasema kuwa, kubadilishwa umbo la dhahiri la mtu haina maana kwamba, uhalisia wa mwanadamu huyu pia imegeuka na kubadilika. [3]. Kwa msingi huo, metamofosisi (maskh) haina maana ya kuangamia mtu na kuja mtu mwingine au kuumbwa mtu mwingine katika umbo la nyani na wala roho haihamishwi na kuingizwa katika mwili wa mnyama. [4] Bali kimsingi metamofosisi au mabadiliko hayo yanahusiana na umbo la dhahiri la mwanadamu huyo na sio kubadilika utambuslisho wake halisi. Kwa maana kwamba, anaonekana katika sura ya mnyama lakini wakati huo huo sura yake kama binadamu inabakia pia. Katika hali kama hii mtu huyu anapaswa kupewa anuani ya mwanadamu mnyama. [5]

Shahidi Mutahhari anatoa ufafanuzi wa jambo hili kwa kusema: “Siku ya Kiyama kwa umbo lolote nitakalokuwa nalo, niwe na mwili huu huu au mwili mwingine, mia kwa mia ni mimi yule yule; isipokuwa yumkini umbo langu likawa limebadilika. Hata kama mimi siku ya kiyama nitafufuliwa katika sura ya mnyama, bado ni mimi yule yule, lakini nipo katika umbo la mnyama.” [6]

Kugeuzwa Watu kwa Mujibu wa Qur’an

Kadhalika angalia: As’hab al-Sabt

Katika Aya za Qur'an tukufu kumezungumziwa kugeuzwa baadhi ya watu. Kwa maana kwamba, kumesimuliwa visa na matukio ya watu waliogeuzwa. Katika Surat al-Maidah Aya ya 60 kimezungumziwa kisa cha kubadilishwa watu na kuwa nyani na nguruwe. [7]Aya hiyo inasema:Sema: Je! Nikwambieni yule ambaye ni mwenye malipo mabaya zaidi kuliko hayo mbele ya Mwenyezi Mungu? Ni yule ambaye Mwenyezi Mungu amemlaani na amemkasirikia, na amewafanya miongoni mwao manyani na nguruwe, na wakamuabudu Shet'ani. Hao ndio wenye mahali pabaya na wamepotea zaidi njia iliyo sawa.

Kadhalika Aya ya 65 ya Surat al-Baqarah, Mwenyezi Mungu anasimulia kisa cha watu wa Sabt kutoka Bani Israel ambao kutokana na kuasi amri ya Allah ya kutovua samaki siku ya Jumamaosi walibadilishwa na kuwa manyani. [8] Aya hiyo inasema:(Na hakika mlikwishayajua ya wale miongoni mwenu walio ivunja Sabato, (siku ya mapumziko, Jumamosi) na tukawaambia: Kuweni manyani wadhalilifu). [9]

Kubadilishwa Baadhi ya Hawariyyun (Wanafunzi wa Nabii Issa)

Kwa mujibu wa Aya za Qur’an tukufu, Hawariyyun (wanafunzi) wa Nabii Issa (a.s) walimuomba Mwenyezi Mungu ashushe chakula kutoka mbinguni [10] na Mwenyezi katika kujibu ombi la alisema: Kama baada ya kushushwa chakula hicho mtu akakufuru, nitampa adhabu ambayo sijawahi kumuadhibu nayo mtu yoyote yule. [11]. Aya za 114 na 115 za Surat al-Maida zinazungumzia kisa hiki:(Akasema Isa bin Maryamu: Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshia chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanao ruzuku. Mwenyezi Mungu akasema: Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakaye kanya baadae, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu.) Baadhi ya wafasiri wameandika chini ya Aya hizi kwamba, idadi kadhaa ya Hawariyyun licha ya kushushwa chakula walifanya khiyana na Mwenyezi Mungu akawabadilisha, [12], lakini baadhi ya wafasiri wengine kama Allama Tabatabai, amepinga suala la kubadilishwa watu hao na kulitambua jambo hilo kuwa ni lenye kupingana na Qur'an. [13]

Kubadilishwa Watu Siku ya Kiyama

Kwa mujibu wa hadithi mbalimbali za Kiislamu, siku ya kiyama kuna watu ambao watafufuliwa hali ya kuwa wamegeuzwa na kuwa katika sura ya wanyama. Kwa mfano kuna hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Muadh ibn Jabal ambapo anasema, Mtume (s.a.w.w) aliulizwa kuhusiana na Aya isemayo: (یوْمَ ینْفَخُ فِی الصُّورِ فَتَأْتُونَ أَفْواجاً ; Siku litapo pulizwa barugumu, nanyi mtakuja kwa makundi). [ 13] Mtume alijibu kwa kusema: Baadhi yao watafufuliwa wakiwa katika umbo la nyani na wengine watafufuliwa wakiwa katika sura ya nguruwe… [13]

Kuna hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Baqir (a.s) inayosema: Watafufuliwa wanaokadhibisha kadari ya Mwenyezi Mungu kutoka katika makaburi yao hali ya kuwa wamegeuzwa manyani na nguruwe. [14]

Kugeuzwa Kiroho

Katika fikra za baadhi ya wahakikiki wa Kiislamu ni kwamba, yumkini mwanadamu akageuzwa kiroho na kimwili na kuwa mnyama. Baadhi ya wafasiri wa Qur'an tukufu wanaizungumzia Aya ya 179 ya Surat al-A'raf kwamba, inaashiria hilo. Aya hiyo inasema: (أُولئِک کالْأَنْعامِ بَلْ هُمْ أَضَل ; Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi).

Mifano ya Metamofosisi katika Hadithi

Katika baadhi ya vitabu vya hadith vya Kishia na Kisuni, kumenukuliwa kuhusiana na metamofosisi na kugeuzwa umbo mtu au watu tofauti na kile kilichoelezwa katika Qur'an. Kwa mfano kuna hadithi inayopatikana katika kitabu cha al-Khisal cha Sheikh Swaduq ambapo kuna wanyama 13 wakiwemo nge, popo na dubu ambao awali walikuwa binadamu na kisha baadaye wakabadilishwa na kuwa katika maumbo haya. [15] Kadhalika al-Tabarani, mmoja wa wanazuoni wa Kisuni wa karne ya 3 na 4 Hijria, amenukuu hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ambayo kwa mujibu wake, katika mustakabali baadhi ya Waislamu watageuzwa na kubadilishwa na kuwa katika umbo la manyani na nguruwe. [15]

Hatima ya Watu Waliobadilishwa

Kwa mujibu wa hadithi za kiislamu ni kwamba, watu ambao kugeuzwa kwao kumezungumziwa katika Qur'an, wataishi kwa muda wa siku tatu tu na hakutabakia kizazi kutoka kwao. [16] Sadr al-Mutaalihin ameandika, Waislamu wamefikia ijmaa na kauli moja kwamba, wanyama wa leo hawatokani na kizazi Adam na watu ambao walibadilishwa walikufa baada ya siku tatu bila ya kuacha kizazi katika kipindi chao cha kuwa wanyama. [17].

Rejea

Vyanzo