Nenda kwa yaliyomo

As’hab al-Sabt

Kutoka wikishia

As’hab al-Sabt (Kiarabu: أصحاب السبت) (Watu wa Sabt au watu wa Sabato) ni kundi miongoni mwa Bani Israil ambalo kwa mujibu wa Aya za Qur’an baada ya kutotii amri ya Allah (s.w.t), ya kutovua samaki siku ya Jumamosi (sabato) waliteremshiwa adhabu kutoka kwa Allah na nyuso zao ziligeuka kuwa za wanyama na baada ya kupita siku tatu, Allah aliwateremshia adhabu kali kiasi kwamba wote kwa pamoja wakateketea. Aghalabu ya hadithi zinaonyesha kuwa, tukio la watu wa Sabt lilitokea katika zama za Nabii Daud na ilikuwa ni katika mji wa Eyla ambao hii leo unapatiakna katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na unajulikana kwa jina la Eilat.

Allama Muhammad Hussein Tabatabai amesema katika Tafsir al-Mizan: Watu pekee waliookoka miongoni mwa watu wa Sabt ni wale waliokuwa wakikataza maovu na watu waliofanya makosa na ambao walinyamaza kimya mkabala wao walikumbwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Utambuzi wa Maana

Watu wa Sabt ni kundi miongoni mwa kaumu ya Bani Israil ambalo baada ya kutotii amri ya Allah ya kutovua samaki siku ya Jumamosi waliteremshiwa adhabu. [1] Watu hao walikuwa wakiishi katika zama za Nabii Daud na idadi yao inakadiriwa takribani 12,000 au 70,000. [2] Ibara ya “As’hab Sabt” (Watu wa Sabt au Jumamosi) imekuja mara moja tu kwa uwazi katika Qur’an katika Aya ya 47 ya Surat al-Nisaa., lakini Aya zingine za Qur’an pia zimebainisha na kusimulia kisa cha kaumu hiyo na hatima iliyokumbwa nayo. [3]

Sabt ambayo ina maana ya kuacha kufanya jambo [4] na katika lugha ya Kiebrania inajulikana kwa jina la Sabbath, [5] ambayo ni siku ya Jumamosi baina ya Mayahudi yaani sabato [6] na ina maana ya kupumzika. [7] Kwa mujibu wa utamaduni wa Kiyahudi, kaumu ya Yahud ilipaswa kupumzika siku ya Jumamosi na kuacha kufanya kazi zao. [8] Kulinda heshima ya siku ya Jumamosi na kutofanya kazi ilikuwa ni katika amri kumi za Nabii Mussa (a.s). [9]

Mkasa Wenyewe

Kwa mujibu wa Qur’ani tukufu, watu wa Sabt walishushiwa adhabu kutokana na kukiuka sheria za Mwenyezi Mungu ya kutovua samaki siku ya Jumamosi. [10] Ilikuwa marufuku kuvua samaki siku hiyo na waligeuzwa ili waone natija ya kazi yao na iwe ibra na funzo kwa wacha Mungu. [11]

Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s) ni kuwa: Watu wa Sabt ni kundi lililokuwa likiishi kando ya bahari na Mwenyezi Mungu aliwakataza kuvua samaki siku ya Jumamosi. [12] Wakati uvuaji wa samaki ulipokuwa umepigiwa marufuku katika siku za Jumamosi, samaki walibuni njia yao, walikuwa wakijitokeza kwa wingi ufuoni mwa bahari katika siku hizo na kwa siku zilizobakia walikuwa wakiondoka kwenda mbali kabisa katika maji mengi ili wasiweze kuvuliwa na wavuvi. Watu wa Bani Isra’il ambao walikuwa wakitilia maanani maslahi yao ya kidunia, walikusanyika na kulizungumzia suala hili na kutoa kauli yao: Sisi hatuna budi kubuni mikakati ya kuweza kudhibiti suala hili la uvuaji wa samaki. Katika siku za Jumamosi, samaki wengi mno huonekana ufuoni kuliko siku zinginezo. Hivyo itatuwia rahisi mno kuvua samaki siku hiyo kwani siku zingine tunaambulia kapa kwani wao wanakwenda katika maji yenye kina kirefu mno hivyo kutuwia vigumu uvuvi.Katika kikao hicho kuliafikiwa kuwa wabuni taratibu za kuvulia samaki. Hivyo wakaafikiana kuchimba mito na mifereji midogo midogo ili samaki wanapokuja ufuoni katika siku za Jumamosi waweze kupitiliza katika mifereji hiyo, hivyo kuwawia rahisi katika kuwanasa. [13] Hivyo wao walitekeleza mpango wao huo na wakachimba mito kutokea baharini. Katika siku za Jumamosi samaki wengi mno walikuwa wakiogelea kwa furaha hadi ukingoni mwa bahari na kupenya katika mito hiyo. Katika nyakati za usiku wakati samaki hao walipokuwa wakitaka kurudi baharini, wao walikuwa wakiziba midomo ya mito hiyo ili samaki hao wasiweze kurudi baharini na badala yake wabakie katika mito hiyo. Siku iliyofuatia yaani Jumapili wao walikuwa wakiwanasa samaki wote waliokuwa katika mito hiyo. [14] Kwa njia na mbinu hiyo, watu wa sabt wakawa wakijilimbikizia mali nyingi na kupata neema nyingi. [15] Kwa mujibu wa hadithi, watu hao idadi yao ilikuwa 80,000 na waliopopuuza amri ya kutovua samaki siku ya Jumamosi walikuwa 70,000. [16]

Kugeuzwa Umbo Watu wa Sabt

Makala Asili: kugeuzwa

As’hab Sabt hatimaye walikumbwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Inaelezwa kuwa, katika tukio hilo, baada ya maonyo ya mara kadhaa, watu hao wapotofu walipokithiri katika kutotii amri ya Allah, waliteremshiwa adhabu kutoka kwa Allah ambapo nyuso zao ziligeuka kuwa za wanyama. [17] Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi, baada ya kupita siku tatu, Allah (s.w.t) aliwateremshia adhabu kali kiasi kwamba wote kwa pamoja wakateketea. [18]

Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai ameandika katika Tafsir al-Mizan: Kwa mujibu wa Aya ya 165 ya Sura Al-A'raf, wale waliokataza maovu miongoni mwao waliokolewa, lakini makundi mawili mengine, yaani waliofanya kosa na walionyamazia hilo walikumbwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu [19].

Baadhi yao, akiwemo Mujahid bin Jabr, mfasiri wa Shia (aliyefariki mwaka 104 Hijiria) na Muhammad Abduh, mfasiri wa Kisunni, wanaamini kwamba mabadiliko ya kimwili kwa watu wa Sabato hayakutokea na kwamba, yale yaliyotajwa katika aya ya 65 ya Surah Al-Baqarah ni ushabihishaji na hekaya ya kugeuzwa mioyo ya As’hab Sabt. [20]

Sehemu na Zama

Kwa mujibu wa Aya za Qur’an As’hab al-Sabt (watu wa Sabt) walikuwa wakiishi kando ya bahari. [21] Katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Muhammad Baqir (a.s), mji wa watu wa Sabt ni Eyla (Eilat). [22] Fakhrurazi pia ametambua eneo walilokuwa wakiishi As’hab Sabt kuwa ni Eyla. [23] Mji wa Eyla kuna uwezekano ndio mji wa Eilat hivi leo unaopatikana kando ya Bahari Nyekundu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. [24] Allama Tabatabai ameitaja miji ya Madyan na Tabariya pia kwamba, yalikuwa makazi ya kuishi ya As’hab Sabt. [25]

Akthari ya hadithi zimekitaja kisa cha As’hab Sabt kwamba, kilitokea katika zama za Nabii Daud (a.s). [26]

Rejea

Vyanzo

  • Al-Qurʾān al-Karīm.
  • Fakhr al-Rāzī, Muḥammad b. al-ʿUmar al-. Mafātīḥ al-ghayb. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1420 AH.
  • Majlisī, Muḥammad Bāqir. Ḥayāt al-qulūb. Qom: Surūr 1384 Sh.
  • Mughnīya, Muḥammad Jawād al-. Tafsīr al-Kāshif. Qom: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1424 AH.
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1374 Sh.
  • Qurashī Bunābī, ʿAlī Akbar. Qāmūs-i Qurʾān. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1371 Sh.
  • Rūḥī, Abu l-Faḍl. Asḥāb-i sibt dar aʿlām-i Qurʾān az Dāʾirat al-maʿārif Qurʾān-i karīm. volume 2. Qom: Muʾassisa-i Būstān-i Kitāb, 1385 Sh.
  • Tafsīr al-Imām al-Ḥasan al-ʿAskarī (a). Qom: Madrasa al-Imām al-Mahdī, 1409 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islāmī, 1417 AH.
  • Ṭabrisī, Faḍl b. al-Ḥasan al-. Majmaʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Tehran: Intishārāt-i Nāṣir Khusraw, 1372 Sh.