Ubatilifu wa Matendo Kutokana na Dhambi
Ubatilifu na uharibikaji wa matendo (Kiarabu: الإحباط) unahusisha kupotea au kufutwa kwa thamani ya matendo mema kutokana na kutenda dhambi, na ni moja ya mijadala muhimu ndani ya elimu ya teolojia ya Kiislamu. Kwa ujumla, Waislamu wote wanakubaliana kuwa matendo mema yanaweza kupoteza malipo yake kutokana na dhambi za mja mwenyewe. Hata hivyo mitazamo ya wanazuoni inatofautiana juu ya namna matendo hayo yanavyo poteza thamani yake. Kwa mujibu wa wanazuoni wengi wa Shia, kufutwa kwa matendo mema, ni kinyume na mafundisho ya Qur’ani na mantiki (akili); hivyo basi wao wanatoa tafsiri nyengine inayolingana na misingi ya Qur’ani na akili juu ya dhana hii.
Kwa mujibu wa mtazamo huo mashuhuri, matendo mema ya mja fulani, hayawezi kupata malipo bila ya kufuata masharti maalumu ndani ya uanzilishi wa matendo hayo. Moja ya mashariti muhimu ya kujuzu na kupata thamani kwa matendo hayo, ni kutofwatilishwa kwa matendo maovu baada ya tendo jema. Kwa hiyo iwapo mtu atatenda dhambi baada kutenda matendo mema, hii ina maana ya kwamba yeye hakutimiza masharti yanayo takiwa, na hivyo tendo hilo hilo halistahili malipo. Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wa Shia wanaamini kwamba, katika baadhi ya hali, matendo mema yanaweza kufutwa au kubatilishwa kwa namna inayoshabihiana na mambo ya kidunia, wakikubali kwamba matendo yanaweza kuwa batili katika hali fulani, kwani hakuna hoja za Hadithi wala hoja za kiakili zinazojenga kizuizi cha kukataa uwezekano wa kutokea kwa hali hilo.
Miongoni mwa Ahlu-Sunna, kundi la Ash’ari lina msimamo unaofanana na ule wa Kishia, wakipinga uhalali wa kufutwa kwa matendo mema (Habt). Kinyume chake, kundi la Mu’utazila linaamini kuwa Habt (الحبط) ni tokeo sahihi lisilo na pingamizi. Kwa mtazamo wao, matendo yote mabaya na mema yatahisabiwa katika Siku ya Kiyama, ambapo dhambi kubwa zinaweza kufuta sehemu ya matendo mema au kuharibu malipo ya matendo hayo.
Jambo lililo kubaliwa na Waislamu wote duniani ni kwamba; kuritadi (kuasi dini) kunapelekea kufutwa na kuharibika kwa matendo mema yote ya yule aliyeritadi. Mfano wa hili ni Ibilisi, ambaye aliye haribu ibada zake za miaka elfu sita kutokana na kiburi chake. Aidha, katika Qur’ani na Hadithi, kuna sababu nyengine zilizotajwa kutika vyanzo hivyo, ambazo zina uweza wa kubatilisha matendo mema, miongoni mwazo ni kama vile; kupaza sauti mbele ya Mtume, unafiki, kukataa uongozi wa Imamu Ali (a.s), na kufanya mama kwa ajili ya kujionesha mbele za watu badala ya kutafuta radhi za Mwenye Ezi Mungu.
Ufahamu na Hadhi ya Neno Ubatilifu (الحبط)
Neno Habt (الحبط) au Ihbaat (الاحْباط) ni istilahi inayotumika katika Qur'ani [1] na ni dhana muhimu katika elimu ya itikadi (kalam au theoloji), [2] ikimaanisha kupotea kwa thamani ya matendo mema na malipo yake kutokana na utendaji wa dhambi ufanywao na mtenda wa matendo mema huyo. [3] Abu al-Hassan Sha'arani, mfasiri mashuhuri wa Kishia, anatoa maoni yasemayo kwamba; Habt inayozungumziwa katika Qur'ani inahusisha matendo ya makafiri peke yao, ambayo hayakufanywa kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenye Ezi Mungu. Hata hivyo, katika elimu ya itikadi (theolojia), dhana ya Habt inahusiana na matendo mema yaliyofanywa kwa nia sahihi na kwa ajili ya kupata ukuruba na Mwenye Ezi Mungu, ila yanapoteza malipo yake kwa sababu ya dhambi maalum zilizotendwa na mja aliyetenda mema hayo.
[4] Istilahi ya Habt na matawi yake imetumika mara kumi na sita katika Qur'ani [5], ikionesha umuhimu wa dhana hii. Kinyume cha Habt ni Takfiri, inayomaanisha kufutwa kwa dhambi kutokana na kutenda matendo mema baada ya dhambi zilizo tangulia. [6]
Suala la Habt limejadiliwa kwa undani kabisa katika taaluma ya fani ya itikadi (kalam au theolojia), na kuna mitazamo kadhaa iliyo tolewa kuhusiana na dhana hii. [7] Kwa mujibu wa wanazuoni wa elimu ya kalam (theolojia), dhana ya Habt linahusiana na waumini ambao wakati mwingine hufanya matendo mema na wakati mwingine hujikwaa kwa kufanya dhambi na matendo maovu, nalo ndio kundi kubwa miongoni mwa wanajamii ya jamii ya Kiislamu. [8] Hata hivyo, makafiri wasiotubu hadi mwisho wa maisha yao na waumini wasiojihusisha na dhambi kabisa hawajumuishwi katika mijadala inayojadili dhana hii ya Habt. Katika taaluma ya itikadi (theolojia), dhana hii inaonekana kuhusishwa na mijadala kadhaa ikiwemo; ufufuo, malipo ya thawabu, adhabu, maonyo pamoja na bishara. [9]
Habt ni dhana muhimu inayopasa kueleka kwa kina mno, kwani matende mema na maovu ni yenye athari ya moja kwa moja katika hatima ya mwanadamu duniani na Akhera. [10] Uelewa wa dhana hii unawatahadharisha waumini na kuwafanya waelewe ya kwamba; matendo yao mema yanaweza kuharibiwa na matendo waliyo yafanya kwa hiari zao wenyewe. [11] Watafiti wanasema kwamba; dhana isiyo sahihi kuhusiana na welewa wa Habt na athari yake, inaweza kusababisha hali ya kukata tamaa au majivuno, na kuondoa hali ya hofu na matumaini kwa mwanadamu. [12] Hii inaweza kumfanya mtu kudhani kuwa matendo yake yote yamefutwa, hivyo kuacha kufanya matendo mema, au kudhani kwamba, dhambi zake zote zimesamehewa, na hivyo kujivuna na kuendelea na dhambi kwa ujasiri kwa tamaa ya kupata msamaha. Kulingana na hotuba ya Imamu Ali (a.s) katika moja ya hotuba zake iitwayo “Khutbatul-Qasi'a / خطبۀ قاصِعه”, ni kwamba; ibada za miaka elfu sita za Ibilisi zilifutwa kutokana na jeuri zake. [13] Aidha, Aya ya 65 ya Suratu Al-Zumar inaonesha kuwa dhana ya Habt ya yenye maana ya kubatilika kwa matendo ya waja, ni miongoni mwa dhana zilizokuwepo katika dini zilizo tangulia kabla ya Uislamu.
Je, Dhana ya Habt Ina Maana ya kupotea kwa Amali Zote Njema?
Kulingana na mitazamo ya wafwasi wa madhehebu yote ya Kiislamu, ikiwa ni pamoja na Shi'a, ni kwamba; baadhi ya dhambi zinaweza kusababisha kufutwa kwa matendo mema yam ja fulani. [14] Kwa mfano, kwa mujibu wa wanazuoni wote wa Kiislamu, matendo yote mema ya muumini yanaweza kufutwa kwa kuasi dini (kubadili dini), iwapo mtu huyo hatatubu baada ya kuritadi (kubadili dini) kwake. [15] Abdullah Jawadi Amuli, katika tafsiri yake ya Tasnim, anabainisha kwa kusema kuwa; kuna aina mbili za kuharibika au kubatilika kwa matendo: kubatilika kwa matendo mema kiukamilifu na kubatilika kwa kwa matendo kufutwa kwa matendo sio kiukamilifu. Katika ufafanuzi wake, anasema kwamba; matendo kama vile kuasi dini (kuritadi) ni miongoni mwa sababu zenye kuondoa matendo mema yote kwa jumla, wakati baadhi ya dhambi kama vile kiburi, zinaweza kuondoa baadhi ya matendo hayo, yaani, husababisha kufutwa kwa yale matendo yaliyo fanyika kwa njia ya jeuri, na hayafuti matendo yote mengine kwa ujumla. [16] Kwa mujibu wa Allama Majlisi, mwandishi wa kitabu Bihar al-Anwar, si kila dhambi inaweza kuchukuliwa kama sababu ya kufutwa kwa matendo mema, bali ni vyema kusimama kwa msimamo wa Qur’ani na Hadithi. Kwa kila dhambi iliyo orodheshwa na Qur’ani na Hadithi, ndiyo twatakiwa kuihisabu kuwa ni dhambi ifutayo amali njema, na hatutakiwi kukiuka mipaka na kuingiza dhambi nyengine katika orodha hiyo. [17] Baadhi ya wanazuoni wa Kishia wanaamini kwamba; kufutwa kwa athari za matendo mema kunahusiana tu na ukafiri, unafiki, na kuasi imani (kuritadi). [18]
Wanazuoni wa Kishia wana nadharia tofauti katika kutoa uchambuzi wa namna ya dhambi zinavyo weza kuondoa na kufuta amali njema. Nadharia za wanazuoni wa madhehebu haya ni kwma ifuatavyo:
Kupinga Dhana ya Kufutwa kwa Matendo Mema Yote kwa ujumla
Kwa mujibu wa maoni ya Sheikh Tusi, mwanatheolojia maarufu wa Kishia wa karne ya nne, ni kwamba: dhana ya kufutwa kwa matendo mema kama inavyoelezwa katika baadhi ya Aya za Qur’ani inahitaji kufasiriwa kwa uangalifu. Sheikh Tusi anapinga tafsiri ya kawaida inayofwata dhahiri ya lugha kama ilivyo kuja katika Aya hizo bila kujali mantiki, akieleza kuwa imani na theolojia ya Kiislamu inategemea misingi ya mantiki na akili, hivyo haiwezekani kukubali kwa ujumla kwamba matendo yote mema yanaweza kufutwa kwa dhambi zinazofwata baadae. Kwa hivyo ni vyema Aya hizi zikafasiriwa kulingana na mantiki salama iendayo na akili za wanadamu na misngi ya kitheolojia. [19] Ili kujenga uwiano kati ya imani yenye kufwata mantiki na Aya hizi, imeelezwa ya kamba; Hadithi zilizozungumzia dhana ya Ihbat, hazimaanisha kufutwa kwa matendo kabisa kabisa, bali zinaashiria kwamba, utendaji wa matendo mema unahitaji kufwata masharti maalumu ili matendo hayo yakubalike mbele ya Mwenye Ezi Mungu, na miongoni mwa masharti hayo ni kutotenda dhambi fulani katika nyakati zijazo. Katika muktadha huu, Sheikh Tusi anaeleza kwamba; dhambi zinazotajwa katika Qur’ani na Hadithi, hazifuti matendo mema moja kwa moja, bali zinaonyesha kwamba muumini hakuwa ametimiza masharti kamili tangu mwanzoni mwa utendaji wa amali zake njema. Kwa hivyo, muumini huyo hakuwa na haki ya kupata thawabu, kwani masharti ya matendo hayo hayakukamilika ipasavyo. [20]
Katika hatua hii, ufafanuzi wa kiakili unaunga mkono hoja ya kwamba; kukubalika kwa tendo jema kunategemea kuepuka baadhi ya dhambi zinazoweza kuathiri matendo hayo katika siku zijazo. Kwa maneno mengine, dhambi inafichua udhaifu wa kiroho uliokuwepo tangu awali ambao ulifanya tendo hilo jema lisikubalike.
Allama Majlisi, mwanafalsafa na mwanazuoni maarufu wa Shi’a, anauthibitisha msimamo huu na kusema kwamba; ndiyo maoni yanayokubalika na wengi miongoni mwa wanazuoni wa Kishia. [21]
Baadhi ya wanazuoni wametumia hoja za kiakili na Aya za Qur’ani katika kupinga uwepo wa dhana ya kufutwa kwa matendo mema. Hoja hizo ni kama ifuatavyo:
Hoja za kiakili: Kukubali dhana isemayo kwamba; matendo mema yanaweza kufutwa kwa kupitia dhambi za baadae, kunaweza kuonekana kama ni aina ya kupuuza ahadi za Mwenye Ezi Mungu katika kutoa malipo ya amali za waja wakena unyanyasaji, na kwa kuwa Mwenye Ezi Mungu hafanyi dhuluma, basi si haki kufuta matendo mema ya mwanadamu kutokana na dhambi zake za baadae. [23] Katika mtazamo huu, dhana ya kufutwa kwa matendo mema kwa sababu ya dhambi za baadae, unaonekana kukinzana na ahadi za Mwenye Ezi Mungu, ambaye anajali usawa na haki wa kila mmoja. Hata hivyo, ikiwa tangu mwanzo kutakuwa na masharti ya kwamba; kukubaliwa kwa matendo mema kunategemea kutojihusisha na baadhi ya dhambi, basi kwa kutenda dhambi, mtu atakuwa hana haki ya thawabu kwa kuwa yeye amefanya tendo jema bila kufwata masharti kamili. Katika hali hii, dhambi zinaweza kuonesha kwamba; tokea mwanzo matendo mema hayo hayakukubalika kutokana na kutotimiza masharti muhimu yaliyowekwa na Mwenye Ezi Mungu, na hivyo kutostahiki thawabu juu ya matendo. [24]
Hoja za Qur’ani: Qur’ani inatoa mwongozo wa wazi kuhusiana na matokeo ya matendo ya mwanadamu katika Siku ya Kiyama. Kuna Aya katika Qur’ani kuhusiana na jambo hili, miongoni mwazo ni pamoja na Aya kama Aya ya 7 ya Suratu Al-Zilzal na Aya ya 40 ya Suratu Al-Najm, zinazo eleza kwamba; Siku ya Kiama, kilamtu ataona matokeo ya matendo yake aliyoyatenda duniani humu. Aya hizi zinathibitisha kwamba katika Siku ya Kiyama, matendo yote mema na maovu yatadhihiri kwa haki na uadilifu. Kwa hiyo matokeo ya kila tendo yataonekana wazi wazi. Aya hizi zinasisitiza kwamba hakuna kitacho futwa, si matendo mema wala si matendo maovu. Na hii inaonesha kwamba; Mwenye Ezi Mungu atatoa hukumu sahihi kwa matendo yote, bila kubagua kati yake. Kwa hiyo, mtazamo huu unaonekana kuleta picha ya sahihi katika utoaji wa thawabu na adhabu, kulingana na hali halisi ya matendo hayo. [25]
Uthibitisho wa Kufutwa kwa Baadh ya Matendo Mema
Baadhi ya wanazuoni wa Kishia wana imani ya kwamba; kufutwa kwa matendo mema kunaweza kuyasibu baadhi ya matendo mema. Wao hawaamini kuwepo kwa ushahidi wa kiakili au maandiko yanayo thibitisha ufanyaji kazi wa dhana katika amali zote. [26] Nasser Makarem Shirazi, mwandishi maarufu wa “Tafsiri Namune”, anatoa mfano kutoka katika maisha ya kidunia ili kuunga mkono mtazamo huu. Katika mfano huo anasema kuwa; Kama vile kosa dogo linavyoweza kusababisha mtu kupoteza ghafla mali yote aliyojitahidi kuipata kwa bidii maishani mwake, vivyo hivyo, dhambi moja inaweza kusababisha kupotea kwa matendo mema ya mtu. Yeye anauchukulia mzozo ulipo kuhusiana na suala hili, kuwa ni mzozo wa maneno na matumizi ya lugha, ambao hauathiri welewa wa dhana hii. [27]
Tofauti za Maoni kati ya Ash'ariyya, Mu'tazila, na Shi'a
Kama tulivyo ashiria hapo awali, katika ulimwengu wa fikra za Kiislamu, kuna tofauti za maoni kuhusiana na dhana ya kufutwa kwa matendo mema yanayofuatiwa na dhambi za baadae. Kwa mujibu wa mtazamo wa Ash'ariyya, ambao unashabihiana na kwenda sambamba na mtazamo maarufu wa Kishi'a, ni kwamba; dhana ya kufutwa kwa matendo ni dhana batili isiyokubalika katika imani ya kidini. [28] Wanazuoni wa Ash'ariyya wanaamini kwamba; haiwezekani kabsa mtu kufutiwa amali zake njema kutokana na dhambi zake za baadae. Mtazamo huu unajikita katika kuzingatia ahadi na uadilifu wa Mwenye Ezi Mungu, ambaye ametangaza kuweka wazi matendo yote ya mwanadamu Siku ya Kiama.
Kwa upande mwingine, Mu'utazila, ambao wanajulikana kwa msimamo wao mkali juu ya dhidi ya matumizi ya akili, wanaiona kuwa dhana hii ni sahihi isiyo na mashaka yoyote ndani yake. Wao wanadai kuwa; dhambi zinaweza kufuta matendo mema ya muumini. [29] Ja'far Subhani, mwanatheolojia mashuhuri wa Kishia wa karne ya kumi na tano, anaeleza kuwa; chanzo cha mtazamo wa Mu'utazila kinatokana na imani yao kuhusiana na dhambi kubwa. Hii ni kwa sababu, kwa mtazamo wa Mu'utazila; mtenda dhambi kubwa ambaye amekufa bila ya kutubia, yeye hataweza kuepukana na Moto wa Jahanna, naye ataendelea kubaki humo milele na milele. [30]
Mu'tazila hawana mtazamo wenye mwelekeo mmoja kuhusu suala na hili, hivyo wao wana nadharia tatu kuu katika vipimo vya kuungua kwa amali njema. Mitazamo hii ni kama ifuatavyo:
1- Kipimo cha ulinganishaji wa jumla ya thamani ya matendo mema na jumla ya maovu (dhambai): Katika nadharia hii, matendo mema ya mtu fulani na dhambi zake vinazingatiwa kwa ujumla. Iwapothamani ya matendo mema itakuwa kubwa kuliko dhambi zake, hapo matendo yake mema yatapewa kipaumbele zaidi, na hayataathiriwa na dhambi zake, hivyo maovu yake hayatapunguzwa kiwango chochote kile cha mema yake. [31] Hii inatoa msisitizo kwamba wingi wa matendo mema unaweza kumwokoa mtu kutokana na athari za dhambi zake Siku ya Kiama.
2- Kipimo cha muwazana (upimaji) kati ya matendo mema na maovu: Nadharia ya pili inahusisha zingatio la uwiano wa moja kwa moja kati ya matendo mema na dhambi. Katika mtazamo huu, kila dhambi inakabiliana na tendo moja jema, yawezekana thamani ya jema moja ikawa ni kubwa na kusafisha zaidi ya dhambi moja. Kwa hiyo iwapo idadi ya dhambi zake zilizobakia itakuwa ni ndogo kuliko mema yake, hapo matendo mema yatamwokoa, na ikiwa dhambi zake zilizobaki zitakuwa ni nyingi zaidi ya mema yake, hapo itakuwa ni khasara kwake. [32] Muqaddas Ardabili, mwanazuoni maarufu wa Kishia wa karne ya kumi, anasema kwamba; mtazamo huu hauko mbali na ukweli na hakuna ushahidi wa kiakili au maandiko yanayo pinga na mtazamo huu. [33]
Kipimo cha zingatio la tendo la mwisho: Katika nadharia hii, tendo la mwisho analofanya mja fulani, ndilo lihapo matendo yote mema aliyoyafanya kabla yake yataungua na kupoteza thamani yake. [34] Nadharia hii inaweka uzito na thamani mkubwa kwenye tendo la mwisho la maisha ya mwanadamu, ambalo kwa nadharia hii, ni lenye uwezo wa kufuta historia ya matendo yake yote ya mema.
Wanazuoni wa Mu'utazila wametumia hoja za kiakili kuthibitisha madai haya, kwa kuangazia mantiki ya ahadi ya kiungu na uhalisia wa toba. [35] Hata hivyo, wanazuoni wa Kishia na Ash'ariyya wamejibu hoja hizi kwa kutumia hoja mbali mbali. [36]
Sababu za Kufutwa kwa Matendo Mema
Kwa mujibu wa nadharia za Waislamu wa madhehebu tofauti, yaonesha kuwepo kwa mawafikiano baina ya Waislamu wote duniani ywa kwamba; muumini anaye ritadi (yaani, anaye ikana imani ya Uislamu) atakuwa amepoteza matendo yake yote mema yaliyotangila kabla ya kuritadi kwake. [37] Kuna sababu kadhaa zilizo orodheshwa katika Qur’an, kama ni sababu za kufutwa kwa matendo mema. Sababu hizo zinajumuisha mambo tofauti ikiwa ni pamoja na; kuasi baada ya imani, [38] kuwaua wanaoamrisha mema na kukataza maovu, [39] kukataa Siku ya Kiyama pamoja na kuzikataa Aya za Mwenye Ezi Mungu, [40] na kuwa na tabia ya unafiki. [41] [42]
Katika hadithi za Kishia, kuna ya orodha ya dhambi kadhaa zinazoweza kufuta matendo mema ya mwanadamu. Miongoni mwa dhambi hizo ni kukanusha Uimamu wa Imamu Ali (a.s), jambo ambalo linachukuliwa kuwa ni miongoni mwa dhambi kubwa, kwa suala la Uimamu ni lenye nafasi muhimu katika ya Kishia. [43] Dhambi nyingine zinazotajwa katika vyanzo vya Hadithi za Kishia, ni kukosa subira wakati wa msiba. [44] Ambapo kukosa subira mbele ya mitihani ya Mwenye Ezi Mungu huchukuliwa kama ishara ya upungufu wa imani. Jengine ni kumpachika mtu asiye na hatia tuhuma aa zinaa, iwe ni mume ndiye atoaye tuhuma kwa mkewe au mke kwa mumewe, kwa hiyo kosa la kumtuhumu mtu kwa tuhuma za uzinifu ni dhambi inayosababisha kufutika kwa matendo mema. [45]
Pia, kuwadhania watu dhana mbaya, [46] kuwa na ria (yaani kufanya jambo kwa lengo la kuonekana na watu na sio kwa nia ya kumridhisha Mwenyezi Mungu), [47] na ubishi wa kupindukia, [48] ni miongoni mwa dhambi zilizo orodhesha ndani ya vyanzo vya Hadithi, na kutambuliwa kama kuwa ni sababu za kufuta na kuteketeza matendo mema.
Kuinua Sauti Mbele ya Bwana Mtume (S.AW.W):
Katika Aya ya pili ya suratu Al-Hujuraat, waumini wamepewa onyo kali la kuepuka kuinua sauti zao juu ya sauti ya Bwana Mtume (s.aw.w) au kuzungumza kwa sauti kubwa mbele yake (s.aw.w), ili kuepuka hatari ya kuangamia kwa matendo yao mema. Onyo hili linaonesha uzito wa kumheshimu bwana Mtume (s.aw.w) katika kila hali, suala ambalo lina athari moja kwa moja juu ya imani za waumini. Wanazuoni wa fani ya tafsiri wa Kishia, wamejaribu kufafanua kwa undani jinsi kitendo cha kuinua sauti mbele ya bwana Mtume (s.aw.w). Na wametoa jawabu za kamili juu ya swali la kwambe je ni vipi kitendo hicho amacho si ukafiri wala ushirikina kinaweza kusababisha kufutwa kwa matendo ya mja fulani. Majibu yao yamegawanywa katika sehemu tatu zifwatazo: [49]
1. Kuinua sauti juu na kupindukia sauti ya Mtume au kusema kwa sauti kubwa mbele yake kwa nia ya dharau: Kitendo hichi, kwa mujibu wa mitazamo ya wanazuoni, ni kwamba; ikiwa kitafanyika kwa nia ya dharau kwa bwana Mtume (s.aw.w), ambaye ni kipenzi cha Mwenye Ezi Mungu ambaye ni kiongozi nembo wa Waislamu hadi Siku ya Kiama, katika hali kama hiyo kitahisabiwa kuwa ni kufuru na dhambi kubwa inayopelekea kufutwa kwa matendo yote ya mfanyaji wa kitendo hicho. Na hili linaungwa mkono na maoni ya Waislamu wote duniani. Kwani Dhihaka au dharau kwa bwana Mtume (s.aw.w), ni sawa na kukanusha utume wake, jambo ambalo lina athari ya moja kwa moja kwenye matendo mema. [50]
2. Kuhudhuria mbele ya Mtume (s.aw.w) ni miongoni mwa amali zenye thawabu: Wanazuoni wanaeleza kuwa kila mara muumini anapokuwa mbele ya bwana Mtume (s.aw.w), kufanya hivyo peke yake kunahisabiwa kuwa ni kitendo chema chenye thawabu na thamani kubwa mbele ya Alla, kwa sababu hupelekea kupatikana kwa ukaribu baina yake na kiongozi wa dini yake. Hata hivyo, ikiwa mtu atazungumza kwa sauti kubwa au kwa njia ya dharau mbele ya bwana Mtume (s.aw.w), kitendo hicho kitasababisha thawabu za kuhudhuria kwake mbele Yake (s.aw.w) zipotee moja kwa moja. [51]
3. Kufutwa kwa matendo yote mema kutokana na kuvunja heshima ya bwana Mtume (s.aw.w): Wanazuoni wa Kishia wanaamini kuwa kumvujia heshiam bwana Mtume (s.aw.w) inaweza kusababisha kufutwa kwa matendo yote mema ya mtu fulani, hata kama jambo hilo halioneshi ukafiri wa moja kwa moja. Wao wansema kwamba; hakuna hoja ya kiakili ipingayo kutokea kwa jambo hili. Hii ni kwa kuwa matendo mema ya muumini yana uhusiano wa moja kwa moja na imani yake kwa bwana Mtume (s.aw.w). Kwa hiyo, kumdharau Mtume kunaweza kuonekana kama kuvunja uhusiano huo wa kiimani, na hivyo kufuta matendo mema yam ja fulani.