Uandishi wa Vyanzo Asilia

Kutoka wikishia

Uandishi wa “Usul” (Vyanzo Mama au Asilia) ni mojawapo ya mbinu na hatua ya kwanza muhimu ya kukusanya na kuhifadhi Hadithi. Neno Aslu kilugha humaanisha asili au chanzo, ila kitaalamu na kwa istilahi za Kishia, humaanisha vitabu maalumu vya Hadithi ambavyo ima mwandishi wake yeye ni mmoja wa waopokea Hadithi moja kutoka kwa Ma’asum (mtoharifu) au ni mwenye kupokea kupitia mpokezi fulani apokeaye moja kwa moja kutoka kwa Ma’asum, kisha kuziandikwa na kuziorodhesha kwa usahihi kabisa kitabuni mwake. Kitabu cha Asil (chanzo asilia) kina thamani maalum ikilinganishwa na vitabu vyengine vya Hadithi, hasa kwa wanazuoni wa Kishia. Kwa mujibu wa imani yao, kuwepo kwa Hadithi katika Asil ndio kigezo muhimu cha kukubalika kwa Hadithi hiyo na kupata hadhi ya usahihi. Hii ni kwa sababu ya kwamba; Hadithi zilizomo ndani ya Asil, ni zenye ukuruba zaidi na chanzo chake asilia, na kwamba, ima baina ya Hadithi na msemaji wake (Ma’asumu) huwa na masafa sifuri au masafa ya ngazi moja (Mpokezi) tu, wala msikivu wa Hadithi hapati tabu ya kuteremka ngazi kadhaa hadi kumfikia msemaji wa Hadithi hizo, jambo ambalo hupunguza uwezekano wa kutokea makosa na upotoshaji ambao unaweza kujitokeza katika mchakato wa usambazaji na uhifadhi wa Hadithi hizo. Kwa mujibu wa maelezo ya wanazuoni wa Kishia, “Vyanzo Asilia” vingi vya Hadithi viliandikwa katika kipindi cha Imamu Ja’far al-Sadiq (a.s) au muda mfupi kabla na baada ya kipindi hico. Inasemekana kuwa, idadi ya vitabu vya “Aslu” vilizoandikwa na Masahaba wa Maimamu, ni kiasi cha vitabu mia nne, na hiyo ndio sababu kupewa jina la "Usulu Arba'am-a". Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wana maoni kwamba idadi halisi ya vitabu hivyo inaweza kuwa ni ndogo zaidi kuliko inavyodhaniwa. Kwa bahati mbaya, idadi kubwa ya Vyanzo Asilia hivi imepotea, na leo hii, ingawa majina yake yameorodheshwa katika vitabu mbalimbali, ila ni Asil kumi na sita tu ya vitabu hivyo ndivyo vilivyopo mikononi mwetu. Vitabu 16 vilivyobaki mikononi mwetu, vimechapishwa katika kitabu mjumuiko wa vitabu uliopewa jina la "Al-Asul al-Sittatu 'Ashar" (Vyanzo Asilia 16). Hata hivyo, inadhaniwa kwamba kulikuwa na Aslu nyingi zilizoko mikononi mwa waandishi wa vitabu vinavyojulikana kama "Kutub al-Arba’a", ambavyo ni miongoni mwa ensaiklopedia muhimu zaidi za Hadithi za Kishia. Kwa hiyo waandishi wa "Kutub al-Arba’a" walinukuu Hadithi kutoka katka vitabu hivyo asilia na kuweka kwenye ensaiklopedia zao hizo.

Utambuzi na Ufafanuzi wa Neno “Aslu” Kuna Ufafanuzi na tafsiri kadhaa juu ya dhana na istilahi ya "Asilu", [1] ila tafsiri ya Agha Bozorg Tehrani inachukuliwa kuwa ndiyo kina na sahihi zaidi kuliko nyengine. [2] Kwa mujibu wa tafsiri yake, neno "Aslu" linamaanisha kitabu cha Hadithi ambacho Hadithi zake zimeandikwa kupita mwandishi ambaye, ima yeye mwenyewe ndiye mpokezi wa Hadithi hizo moja kwa moja kutoka kwa Ma’asumina, au kutoka kwa mpokezi mwaminifu apokeaye uso kwa uso kutoa kwa Ma’asumina. [3] Kwa hiyo yaliyomo ndani ya "Aslu", huwa hayakuchukuliwa kutoka katika vitabu vyengine, bali ni Hadithi zilizo rikodiwa na mwandishi mwenyewe, ambazo ima alizisikia kwa sikio lake kutoa mdomoni mwa Ma’asumina au kapoke kutoka kwa msikivu wa kwanza kabisa aliyezisikia kwa sikio lake, na sio kuHadithiwa na mtu fulani. [4] Kulingana na maelezo ya mwandishi wa kitabu kiitwacho “Dirasatu Hawla al-Usulu al-Arba'a”, matumizi ya neno "asili" yalijitokeza kwa mara ya kwanza mnamo katika karne ya tano Hijiria na yaliendelea kutumika ndani maandiko ya wanazuoni mbali mbali wa Shi'a hadi zama zetu za hivi sasa. [5] Neno hili limeonekana kutumiwa zaidi katika kazi za Sheikh Mufid, Najashi, na Sheikh Tusi, ambao walitoa mchango mkubwa katika tafsiri na matumizi ya dhana hii katika maandiko na fasihi za kidini. [6]

Tofauti Kati ya Asili na Kitabu, Musnad, na Musannaf Katika tafiti mbali mbali za wanazuoni wa upande wa madhehebu ya Shi'a, mara nyingine neno "asili" hutumika kama kinyume na linavyotumika neno "kitabu." Hii inajitokeza pale isemwapo kwamba; mpoke fulani wa Hadithi ana "kitabu" pamoja na "Aslu." [7] Vilevile, baadhi ya vitabu vya Hadithi vya Ahl al-Sunnah hutambuliwa kwa jina la "musnad" au "musannaf." [8] Ili kuelewa tofauti hizi kwa kina, ni muhimu kutofautisha istilahi hizi kama ifuatavyo: • Istilahi ya Kitabu inahusiana na kitabu chenye kujumuisha maandiko yote ya Hadithi, bila kujali kama Hadithi hizo zimeandikwa kwa kufuata kitabu kingine au kama ilivyo katika "Aslu," ambapo Hadithi zake huorodheshwa kitabuni humo bila kutegemea maandiko mengine. [9] Kwa hivyo, "kitabu" ni istilahi pana inayohusiana na hati na nyaraka mbali mbali za Hadithi kwa ujumla. • Istilahi ya Musnad inahusiana na vitabu vya Hadithi ambapo Hadithi zimekusanywa na kuratibiwa kulingana na Masahaba maalum, ambapo kila sehemu ya vitabu hivi inahusiana na sahaba mmoja na Hadithi zake. Mfano wa vitabu mama vya "musnad au Masaaniid" ni Musnad Ahmad ibn Hanbal, ambacho ni kinacho nukuu Hadithi kwa kufuata mtindo huu wa uainishaji. Utaratibu wa Musnad huwa umekusanya Masahaba mbali mbali ndani yake, na kila mlango wa kitabu hicho huwa unahusiana na Sahaba mmoja. [10] • Istilahi ya Musannaf inahusiana na vitabu vya Hadithi ambapo Hadithi zake hupangwa kwa msingi wa mada au kichwa cha habari. [11] Katika vitabu vya aina hii, Hadithi huainishwa kulingana na mada maalum, na hivyo kufanya iwe ni rahisi kwa mtafutaji kupata kwa haraka Hadithi zinazohusiana na mada fulani anayoihitaji. Mfano mzuri wa "musannaf" ni Musannaf wa Abd al-Razzaq ibn Hammam al-San'ani, ambao unafuata mtindo huu katika uandishi wake. [12]

Ukubalikaji wa Vitabu vya "Aslu" Hadithi Kulingana na maelezo ya Aqa Bozorg Tehrani, mabaye ni mtaalamu wa Kishia wa utambuzi wa vitabu, ni kwamba; vitabu vya "Aslu" vinakubalika zaidi kuliko vitabu vyengine, hii ni kutokana na uaminifu wake mkubwa zaidi ikilinganishwa na mikusanyo mingine mbali mbali ya Hadithi. Hii ni kutokana na ukweli wa kwamba; Hadithi zilizomo ndani ya vitabu vya "Aslu", ima huwa zime kusanywa moja kwa moja kutoka chanzo asili (Ma’asumina) kisicho na makosa au kupitia ngazi ya mtu mmoja tu. Kwa hivyo, vitabu vya "Aslu" vinaonekana kuwa na uaminifu zaidi, hasa ikiwa mwandishi wake ni miongoni mwa waandishi wanaokubalika na wenye sifa kamili zinazohitajika kwa ajili ya upokeaji wa Hadithi. Katika hali hii, Hadithi zilizomo ndani yake zinaweza kuaminika kwa kiwango kikubwa. [13] Hii ndiyo sababu iliopelekea pale wanazuoni kuthamini Hadithi za mwandishi wa "Aslu", na pale wanasema kwamba; mwandishi fulani alikuwa ni mwandishi wa “Aslu”, hiyo huchukuliwa kama ni sifa chanya kwa mwandishi huyo, kwani inaonyesha kujitolea kwake katika kuhakikisha usahihi wa kurekodi Hadithi, na kupata maneno halisi kutoka kwa chanzo kisicho na makosa, pamoja na kuepuka sababu zinazoweza kudhoofisha Hadithi ambazo miongoni mwazi ni kusahau au kuteleza katika nukuu. [14] Feidhu Kashani, ambaye ni mtaalamu wa Hadithi wa Kishi'a, anasisitiza kwamba; "Aslu" ilikuwa ni mojawapo ya vigezo muhimu katika kutathmini Hadithi. Wafqihi wa kale walizihukumu na kuzipa hadhi ya usahihi zile Hadithi ambazo ima; zilikuwa zimeandikwa katika vitabu kadhaa vya "Aslu" au zilijumuishwa katika"Aslu" moja au mbili, huku zikiwa na mlolongo wa wapokezi wenye kuaminika. Aidha, walikubali Hadithi kama sahihi ikiwa mwandishi wa "Aslu" alikuwa ni mmoja wa watu waliokubalika kwa Ijma (muwafaka) ya wanazuoni. [15] Inadaiwa kwamba wanazuoni wa Shi'a wanaafikiana wote kwa pamoja ya kwamba; vitabu vya "Aslu" vilikuwa ndio msingi wa kuandika mikusanyo (ensaiklopidia) muhimu zaidi ya Hadithi za Shi'a. Aidha, nyingi ya Hadithi zilizomo katika Vitabu Vinne (Al-Kutubu Al-Arba’a), zinatokana na vitabu vya "Aslu", jambao ambalo linatoa ushahidi juu ya umuhimu na uaminifu wa vitabu hivi katika urithi wa Hadithi za Shi'a. [16]

Historia ya Uandishi wa Aslu Wanazuoni wa madhehebu ya Shi'a wanakubaliana kuwa vitabu vya "Aslu au Usuulu” vvyote vikiandikwa katika kipindi cha Maimamu (a.s), kuanzia enzi za Imamu Ali (a.s.) hadi enzi za Imamu Hassan Askari (a.s.). [17] Hata hivyo, kuna mitazamo miwili maarufu kuhusu kipindi cha mwanzo wa uandishi wa vitabu vya vitabu hivi. Mitazamo miwili kuhusiana na mwanzo wa uandishi wake ni kama ifuatavyo: 1. Mtazamo wa Kwanza: Baadhi ya wanazuoni, ikiwa ni pamoja na Sayyid Mohsin Amin, wanafuata maoni ya Sheikh Mufid na wanaamini kwamba mwanzo wa uandishi wa vitabu vya "Aslu au Usuulu”, ilikuwa ni zama za Imamu Ali (a.s) na kuendelea hadi enzi za Imamu Hassan Askari (a.s). [18] 2. Mtazamo wa Pili: Kundi jengine la wanazuoni, kama vile Shahid Awwal, Muhaqiq Hilli, na Mir Damad, wanadai kwamba; kuandika vitabu kwa vya "Aslu au Usuulu”, kulianza zama za Imamu Sadiq (a.s) na kwamba vitabu hivyo vilikuwa vikiandikwa kabla na baada ya kipindi kidogo cha Imamu Sadiq (a.s). [19] Mwandishi kitabu kiitwacho “Dirasatu Hawla al-Usuli al-Arba’a”, amesisitiza na kuunga mkono usahihi wa mtazamo wa pili. [20] Aqa Bozorg Tehrani, kwa upande wake katika kitabu “Al-Dhari'a”, ameandika akisema kwamba; haijulikani ni tarehe gani hasa halisi yakuanza kuandika kwa vitabu hivi vya "Aslu au Usuulu”. Hata hivyo, ni dhahiri kwamba, vitabu vyote vya " Aslu au Usuulu” viliandikwa na wafuasi wa Imamu Sadiq (a.s.), iwe ni Masahaba wake maalum au Masahaba wake wengine, ambao walikuwa ni wanafunzi wa Imamu Baqir (a.s.) au Imam Kadhim (a.s), isipokuwa kwa idadi ndogo sana, vitabu vya "" Aslu au Usuulu” ndiyo iliandikwa na katika zama za Maimamu wengine (a.s). [21] Kwa upande mwingine, Majiid Ma'arif, katika kitabu chake “Tareekhe Umumie Hadith”, ametoa mtazamo wa tatu ulio nje ya mitazamo miwili iliyo pita, ambao unasema kuwa; vitabu vya "Aslu au Usuulu”, vilikiandikwa wakati wa Imamu Baqir (a.s.), Imamu Sadiq (a.s.), na Imamu Kadhim (a.s.). Ushahidi wake ni kwamba, Hadithi nyingi zilizomo katika vitabu vya "Aslu au Usuulu” zinatoka kwa Maimamu hawa watatu (a.s). [23]

Sababu za Kuenea kwa Kuandishi wa "Aslu au Usuulu” katika Kipindi cha Imamu Sadiq (a.s) Kwa mujibu wa ripoti za Agha Bozorg Tehrani, ni kwamba; kipindi cha uongozi wa Imamu Baqir, Imamu Sadiq, na sehemu ya kipindi cha Imamu Kadhim (a.s) kilikuwa sambamba na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah na hatimae kuanguka kwake, na madaraka kuhamia kwa kwa Bani Abbas. Katika kipindi hichi, watawala walikuwa wakihangaika na migogoro ya kisiasa, na hawakuwa na fursa ya kuwabana na kuwadhibiti sana Maimamu wa Kishia (a.s) pamoja na wafwasi wao. Hivyo basi, hakukuwa na kizuizi kikubwa kwa Maimamu (a.s) katika kueneza mafundisho ya kidini, pia wapokezi wa Kishia no walihudhuria kwa amani katika vikao vyao mbali mbali vya elimu, iwe vikao huria au vya faragha na kuandika Riwaya wanazozipokea kutoka kwao (a.s). [24] Mlingano Biana ya Aslu au Usuulu na Vitabu vya Musnad au Masaaniid Shia na Ahlus-Sunna walichukua mielekeo tofauti katika uandishi wa vitabu vyao vya hazina za Hadithi (Usuulu na Masaaniid), wakitoa mwangaza wa kipekee katika mchakato huu muhimu wa kihistoria. Kwa upande wa Ahlus-Sunna, mfumo wa uandishi wa "Musnad" uliibuka na kupata umaarufu mkubwa, huku ukifuata mkondo wake kurikodi Hadithi za Mtume (s.a.w.w) hatua baada ya hatua. Kwa upande mwingine, Waislamu wa Shia, jambo walilolipa umuhimu mkubwa zaidi, ilikuwa ni uandishi wa "Aslu au Usuulu”. [25] Ingawa kuna mfanano baina "Aslu au Usuulu”, na "Musnad au Masaaniid", katika vipengele kadhaa, ila kuna tofauti muhimu baina ya vyanzo viwili hivi. Katika vyote viwili, kipengele kikuu kinacho viunganisha vyanzo viwili hivi, ni kwamba; msingi wa vyote viwili ni uratibu na mpangilio wa Hadithi, huwa ni kulingana na mpokezi wa hadithi hizo, badala ya mada ya mada yake. Hii ina maana kwamba katika "Aslu au Usuulu”, na "Musnad", mpokezi mmoja anaweza kukusanya Hadithi mbalimbali katika kitabu chake, bila kujali maudhui zake. Mfanano wa pili kati vyanzo hivi, ni kwamba; vitabu vya pande zote mbili (Aslu au Usuulu pamoja na Musnad au Masaaniid), vilitayarishwa kwa kutegemea usikivu wa Hadithi moja kwa moja kutoka kwenye chemuchemu asili ya msemaji wake, bila kutumia vyanzo vyengine vya katika nukuu zake. Pamoja na haya, vitabu vya "Aslu au Usuulu”, vya Shia vilikuwa ndiyo msingi thabiti wa uandishi wa ensaiklopedia kubwa za Hadithi zilizoandikwa baadae. Pia waandishi wa Ahlus-Sunna wa Hadithi na walitumia vitabu mama vya Musnad au Masaaniid kama ni chanzo msingi katika uandishi ensaiklopedia zao za Hadithi. [26] Hata hivyo, kwa mtazamo wa wanazuoni wa Shia vitabu mama vya "Aslu au Usuulu”, vinahisabiwa kuwa na ubora wa juu zaidi kuliko vitabu mama vya"Musnad au Masaaniid". Hii ni kwa sababu Hadithi zilizokusanywa katika vitabu mama vya "Aslu au Usuulu”, zilisikiwa moja kwa moja kutoka kwa Imamu au kupitia ngazi ya mpokezi mmoja tu, hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea makosa au upotoshaji. Kwa upande mwingine, vitabu mama vya"Musnad au Masaaniid", mara nyingi humalizikia kwa bwana Mtume (s.a.w.w) kupitia wapokezi wanne, watano, au sita, hali inayozifanya zisiwe na daraja ya chini ikilinganishwa na vitabu mama vya "Aslu au Usuulu”. [27]

Idadi ya Aslu au Usuulu Maoni maarufu miongoni mwa wanazuoni wa Kishia yanayo onekana katika tafiti mbali mbali za kielimu yanaonyesha kwamba; idadi hasa ya vitabu mama vya “Aslu au Usuulu”, ilikuwa ni jumla ya vitabu mia nne. [28] Hata hivyo, kulingana na kauli ya Agha Bozorg Tehrani, idadi hii inaweza kuwa ni chini ya vitabu mia nne. [29] Wanazuoni wanaounga mkono mtazamo huu ni pamoja na Sheikh Mufid, kama ilivyoelezwa katika ripoti inayopatikana katika kitabu cha “Ma‘alimu al-‘Ulamaa”, ingawa taarifa hii haijarekodiwa katika maandiko yake mwenyewe. Aidha, maoni haya yanakubaliana na baadhi ya wanazuoni wengine, akiwemo; Fadl ibn Hassan Tabarsi, Sheikh Bahai, Hurr Amili, na Mirdamad. [30]

Kwa mfano, kitabu cha “Ma‘alim al-‘Ulama” kinachoripoti kutoka kwa Sheikh Mufid kinasema kuwa, katika mdhehebu ya Imamiyya, kutoka enzi za Imamu Ali (a.s) hadi Imamu Hassan Askari (a.s), Waislamu wa madhehebu haya ya Kishia, walifanikiwa kuandika vitabu mia nne vilivyojulikana kwa jina la “Aslu au Usuulu”. [31] Aidha, Sayyid Mohsin Amin, mwandishi wa “A‘yan al-Shi‘a”, anadai kwamba; Waislamu wa madhehebu ya Shia, kuanzia wakati wa Imamu Ali hadi Imam Hasan Askari (a.s), waliweza kuandika jumla ya vitabu elfu sita, ambapo vitabu mia nne kati ya yake vilipata umaarufu wa kipekee miongoni mwa Shia, na kujulikana kwa jina la "Usuulu Arba’a Mi-a". [32]

Mtazamo wa Kinyume na Maoni Maarufu Ingawa maoni maarufu miongoni mwa wanazuoni wa madhehebu ya Shia yanaonyesha kuwa; idadi ya vitabu mama vy “Aslu au Usuulu”, ilikuwa ni jumla ya vitabu mia nne, ila Sayyid Muhammad Hussein Hosseiniy Jalaliy, katika kitabu chake “Dirasatu Hawla al-Usuli al-Arba’i mi-a”, anatoa mtazamo kinyume na ule ulio zoeleka. Katika kitabu chake Hosseiniy Jalaliy anadai kwamba; idadi halisi ya vitabu mama vya “Aslu au Usuulu” ilikuwa si zaidi ya vitabu mia moja. [33] Moja ya sababu zilizozaa mtazamo huu, ni matokeo ya utafiti wa kina uliofanywa na Sayyid Muhammad Hussein Hosseini Jalali. Katika kitabu chake “Dirasatu Hawla al-Usuli al-Arba’i mi-a”, Jalali alibaini kuwa; katika uchambuzi wa maandiko ya Sheikh Tusi na Najashi, hakuna vitabu mama vya “Aslu au Usuulu” ndani ya maandiko hayo isipokuwa vitabu sabini na kitu. Hii ni licha ya jukumu muhimu walilokuwa nalo wawili hawa (Sheikh Tusi na Najashi) katika kuorodhesha vitabu vya Shia, ambapo Sheikh Tusi alitoa kauli akisema kwamba yeye hakuacha hata kitabu kimoja cha Kishia katika orodha yake ya vitabu. [34]

Kwa maoni yake, tofauti ya tafsiri iliopo juu ya welewa wa neno "Aslu" ndiyo chanzo cha kukubaliana kwa wanazuoni juu ya kuwepo kwa "Usulu" mia nne. Miongoni mwa wanazuoni, kuna waliokuwa na mawazo ya kulipa neno "Aslu" ya kitabu chochote kile kilichokuwa na Hadithi zinazokubalika, wakati baadhi yao walikifikiria kwamba "Aslu" ni kitabu ambacho hakikuwa na Hadithi zilizo chukuliwa kutoka katika vyanzo vingine. Hivyo basi, wanaposema kuwa Waislamu wa Shia waliandika vitabu elfu sita, na mia nne kati yake ni “Aslu au Usuulu”, walikuwa wanaashiria kuwa; idadi hii (mia nne) ya vitabu ilikuwa na hadhi ya kuaminika zaidi ikilinganishwa na vitabu vyengine vilivyo bakia. [35]

Mtazamo Unaounga Mkono Majiid Ma'arif, mwandishi wa kitabu kiitwacho “Taariikh ‘Umuumi Hadith”, anaunga mkono mtazamo mashuhuri juu ya idadi ya hazina za Hadithi za “Aslu au Usuulu”, na amejaribu amenatoa kutoa mifano ya hoja na ushahidi inayo thibitisha mtazamo huo. Mojawapo ya ushahidi huo ni kwamba katika maandiko ya Najashi na Sheikh Tusi, kuna zaidi ya watu mia tano kutoka kwa Masahaba wa Imamu Baqir (a.s) hadi Imamu Kadhim (a.s) walio orodheshwa, wakitambulishwa kama ni wapokezi walio kuwa wakinukuu Hadithi moja kwa moja au uso kwa uso kutoka kwao. [36] Kitabu hiki (Taariikh ‘Umuumi Hadith) kinaeleza kuwa; Sheikh Tusi alikusanya na kuorodhesha "Aslu au Usuulu" pamoja na maandiko mengine kdhaa mbali mbali ya Mashia, katika kitabu chake kiitwacho Al-Fahrist. Hata hivyo, hakuna uthibitisho wala ushahidi wa wazi ya kwamba, Sheikh Tusi alifanikiwa kutambua na kuorodhesha vitabu vyote vya "Aslu au Usuulu". [37]

Hali ya Sasa ya Asili

Inasemekana kwamba Mashia walikuwa jitihada kubwa katika kuhifadhi na kutunza vitabu hivi vya "Aslu au Usuulu", vyenye hazina muhimu ya Hadithi za Kishia ndani yake. [38] Hata hivyo, hali ya sasa inaonyesha kwamba; ni idadi ndogo tu ya vitabu vya "Aslu au Usuulu" vimeweza kudumu hadi leo, huku vingi vikidhaniwa kuwa vilipotea kutokana na sababu mbalimbali za kihistoria na kiutamaduni. Ingawa baadhi ya vitabu hivi mama vya "Aslu au Usuulu" vilikuwepo wakati wa kuandikwa kwa vitabu vya vinne maafuru kwa jina la “Kutub Arba‘a”, ambavyo ni ensaiklopedia muhimu za Hadithi za Shia. [39] Haidhuru kwa hivi sasa idadi kubwa ya vitabu hivi imepotea na haipo tena mikononi mwetu. Ila Hadithi zimetajwa na kuorodheshwa ndani ya ensaiklopea hizo ziitwazo “Kutub Arba‘a”. [40]

Bwana Kadhim Mudir Shanechi, mtafiti wa Hadithi, anaeleza kwamba sababu kuu ya kupotea kwa vitabu hivi mama vya Hadithi (Aslu au Usuulu) ni kwamba; Baada ya kuanzishwa kwa ensaiklopedia za Hadithi, Waislamu wa madhehebu ya Kishia walijisahau na kulipa kisogo suala la kulinda na kuhifadhi vitabu vitabu hivyo vya "Aslu au Usuulu". Shanechi katika maelezo yake anabainisha kwamba; mara tu baada ya kuundwa kwa ensaiklopedia hizo, kulizuka mtindo wa kupuuzilia mbali umuhimu wa vitabu vya  "Aslu au Usuulu" kama vyanzo asili vya Hadithi za Kishia. Hii ikapelekea kupungua kwa jitihada za kulinda na kutunza vitabu hivyo muhimu, hivyo kusababisha kupotea kwa sehemu kubwa ya ""Aslu au Usuulu",  vitabu ambazo vilikuwa na thamani ya kihistoria na kiakademia. 

Hali ya Sasa ya Vitabu Mama vya Usuulu Katika orodha kuu ya vitabu vya "Aslu au Usuulu", kuna idadi ya vitabu kumi na sita vilivyobaki hadi sasa. Pamoja na kuwepo kwa nakala za maandiko ya vitabu hivi, pia kwa jitihada za Hassan Mustafawiy, vitabu hivi vimeweza kuchapishwa kama ni ensaiklopedia ya kitabu kiitwacho “Al-Usul al-Sittatu ‘Ashar”. Vitabu hivi vya asili ni sehemu muhimu ya urithi wa Kishia na vina mchango mkubwa katika tafiti za kihistoria na kidini. Orodha ya vitabu vilivyo chapishwa kwa jina la “Al-Usulu al-Sittatu ‘Ashar”, ni kama ifuatavyo: 1. Kitabu Asili cha Zaid Zarad al-Kufi 2. Kitabu Asili cha Abu Said Abbad Usfuri 3. Kitabu Asili cha Asim ibn Humaid Hammad al-Kufi 4. Kitabu Asili cha Zaid Narsi al-Kufi 5. Kitabu Asili cha Ja'afar ibn Muhammad ibn Shuraih Hadrami 6. Kitabu Asili cha Muhammad ibn Muthnna Hadrami 7. Kitabu Asili cha Abdulmalik ibn Hakim Khath’ami 8. Kitabu Asili cha Mithna ibn Waleed Hannaat 9. Kitabu Asili cha Khallad Sindi 10. Kitabu Asili cha Hussein ibn Uthman Amiri 11. Kitabu Asili cha Abdullah ibn Yahya Kahili 12. Kitabu Asili cha Sallaam ibn Abi Umrah 13. Kitabu Asili cha Nawadir Ali ibn Asbat al-Kufi 14. Dondoo za Kitabu Asili cha ‘Alaa-u ibn Razin al-Qala 15. Kitabu Asili cha Darust ibn Abi Mansur Muhammad Waasiti 16. Kitabu Asili cha Abdullah ibn Jabr kilichojulikana kama “Kitabu Diyyaat Dharif ibn Nasih alKufi”