Nenda kwa yaliyomo

Siqayat al-Hajj

Kutoka wikishia
Makala hii inahusiana na cheo cha kuwanywesha maji mahujaji. Ili kujua kuhusiana na Aya yenye jina kama hii, angalia makala ya Aya ya Siqayatu al-Hajji.

Siqayat al-Hajj (Kiarabu: سقاية الحاج ina maana ya kuwanywesha maji mahujaji ambapo hili lilikuwa moja ya majukumu na vyeo muhimu katika kipindi cha kabla ya Uislamu na mwanzoni mwa Uislamu pamoja na kushikilia na kutunza funguo za Kaaba. Kuwanywesha maji mahujaji kawaida kulikuwa bi kwa kuwapatia maji ya zamzam.

Inaelezwa kuwa, kabla ya Makka kutekwa na kukombolewa na Waislamu katika mwaka wa 8 wa Hijria, mahujaji wakati mwingine walikuwa wakipatiwa mvinyo badala ya maji. Sambamba na ujio wa Uislamu, Abbas, ami yake Mtume, alichukua jukumu la kuwanywesha maji mahujaji, na Mtume akamuachia aendelee na jukumu hilo.

Nafasi ya imani na jihadi inatajwa katika Qur'ani kuwa ni ya juu kuliko kuwahudumia mahujaji kwa kuwanywesha maji.

Utambulisho

Siqayat al-Hajj ina maana ya kuwanywesha maji mahujaji. [1] Kutokana na ukame na uhaba mkubwa wa maji uliokuwa katika ardhi ya Makka katika zama hizo, kazi hiyo sambamba na ile ya utunzaji wa funguo za Kaaba yalikuwa mambo na majukumu yenye umuhimu mkubwa sana na kazi ya kuwahudumia mahujaji kwa kuwapatia maji ya kunywa ilikuwa ikimpatia msimamizi wake nafasi na daraja maalumu baina ya watu. [2]

Kuwanywesha mahujaji maji hakukuwa kukitimia kupitia maji ya kisima cha zamzam tu, kwani kwa mujibu wa vyanzo, kwa kipindi kirefu kisima hicho hakikuwa kikitambulika na hatimaye, Abdul-Muttalib akafanikiwa kugundua kisima hicho baada ya kuota ndoto na kisha akakihuisha. [3]

Kabla ya Fat-h Makka katika mwaka wa 8 Hijria, kuwanywesha maji mahujaji wakati mwingine mbali na maji, kulikuwa kukitolewa pombe pia. [4]

Waliokuwa na Jukumu la Kuwanywesha Maji Mahujaji

Sambamba na kudhihiri Uislamu mjini Makka, jukumu la kuwanywesha maji mahujaji na wakati wa kushuka Aya ya Siqayatu al-Hajji [5] lilikuwa mikononi mwa Abbas bin Abdul-Muttalib, ami yake Bwana Mtume (s.a.w.w). [6] Kabla yake Abu Talib ndiye aliyekuwa na jukumu hilo. Lakini baada ya muda kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha alilikabidhi jukumu hilo kwa Abbas. [7] Pamoja na hayo, Ibn Hisham katika kitabu chake cha Sirat al-Nabawiyyah amemtaja Abbas kuwa ndiye aliyekuwa na jukumu la kuwanywesha maji mahujaji baada ya Abdul-Muttalib na hajataja jina la Abu Talib. [8] Imetajwa katika kitabu cha Ansab al-Ashraf kwamba, huduma ya kuwanywesha maji mahujaji, ni miongoni mwa vyeo vilivyokuwa mikononi mwa watoto wa Abdul-Manaf; kwa msingi huo cheo hicho kikamfikia Hashim bin Abdul-Manaf na baada yake kwa utaratibu kikamfikia Muttalib bin Abdul-Manaf, Zubeyr bin Abdul-Muttalib na kisha Abu Talib. [9]

Baada ya Fat'h Makka Mtume (s.a.w.w) hakufanyia mabadiliko vyeo viwili tu ambavyo ni kazi ya kuwanywesha maji mahujaji na utunzaji wa funguo za Kaaba [10] na hivyo kazi hizo ziliendelea kushikiliwa na watu wale wale waliokuwa wakihudumu katika nyadhifa hizo kabla ya kukombolewa Makka. [11]

Imani na Jihadi ni Bora Kuliko Kuwanywesha Maji Mahujaji

Makala Asili: Aya ya Siqayatu al-Hajji

Nafasi na daraja ya imani na jihadi katika Qur'ani imetambuliwa kuwa bora kuliko kunywesha maji mahujaji. [12] Fakhrurazi, mmoja wa wafasiri mahiri wa Kisuni anaamini kuwa, Aya hii haionyeshi kutokuwa na maana au kutokuwa na umuhimu kitendo cha kuwanywesha maji mahujaji, bali inalihesabu suala la kuwanywesha maji mahujaji, kuwa karibu na daraja ya imani na jihadi na ndio maana ikakitaja pamoja na imani na jihadi. [13] Wapokezi wa hadithi [14] na baadhi ya wafasiri wa Qur'ani wa Kishia kama Sheikh Tabarsi na Sheikh Makarim Shirazi wameashiria hadithi za kufasiri Qur'ani ambazo zinabainisha sifa ya imani ya Imamu Ali (a.s) kuhusiana na kushuka Aya hiyo. [15]

Wafasiri wa Kisuni pia kama Fakhru-Razi (606 H), [16] Muhammad bin Jarir bin Yazid Tabari (aliaga dunia 310 H), [17] Ahmad bin Muhammad Qurtubi (aliaga dunia 761 H), [18] Abdu-Rahman Suyuti (aliaga dunia 911 H), [19] Ahmad bin Muhammad Tha'labi, [20] na Ibn Abi Hatim (aliaga dunia 327 H) [21] wameashiria hadithi zinazobainisha sababu ya kushuka Aya ya Siqayat al-Hajj na ambazo zinaonyesha kuwa juu na bora imani ya Imamu Ali (a.s) kwa kazi ya Abbas bin Abdul-Muttalib na kazi ya Shaybah bin Othman ya kuamirisha msikiti wa Makka; [22] kiasi kwamba, Hakim Askani, mmoja wa wapokezi wa hadithi wa Ahlu-Sunna wa karne ya 5 Hijria ameorodhesaha katika kitabu chake cha Shawahid al-Tanzil zaidi ya hadithi 10 kuhusiana na maudhui hii. [23]

Rejea

Vyanzo