Sayyid Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi

Kutoka wikishia
Sayyid Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi

Sayyid Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi (Kiarabu: السيد محمد كاظم الطباطبائي اليزدي) (aliye ishi kati ya mwaka 1248 na 1337 Hijiria) alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kishia na mwandishi wa kitabu maarufu kijulikanacho kwa jina la al-Urwatu al-Wuthqa. Baada ya kifo cha Sayyid Muhammad Hassan Shirazi, Sayyid Muhammad Kadhim alikuwa tayari amesha pevuka kielemu na kufikia daraja ya kushika nafasi ya umarja’a, ambacho ni cheo cha kielemu akifikiacho mwanazuoni na kumpa uwezo wa kutoa fatwa za kidini. Yeye alikuwa ni mmojawapo wa wapinzani wa harakati za kutaka mabadiliko ya katiba (Constitutional Movement). Katika mashambulizi ya Italia dhidi ya Libya, Sayyid Yazdi alitoa fatwa ya ulazima na wajibu inayo wataka Waislamu kutetea nchi yao dhidi ya mashambulizi hayo. Mara kadhaa alionekana kutoa aina kama hiyo ya fatwa, ikiwemo fatwa ya wajibu wa kupigana jihadi dhidi ya Uingereza katika mashambulizi lake dhidi ya Iraq, na katika shambulio la Urusi dhidi ya Iran.

Muhammad Baqir Najafi na Mirza Muhammad Hassan Shirazi, ni miongoni mwa walimu wa Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, na baadhi ya wanafunzi wake ni: Muhammad Hussein Kashif al-Ghitaa, Agha Dhiyaa Iraqi, Sayyid Abdulhussein Sharafuddin, Hassan Ali Nokhodaki Isfahani, Sayyid Muhammad Taqi Khansari, Sayyid Mohsin Amin na Agha Bozorg Tehrani.

Kitabu cha Urwat al-Wuthqa cha Sayyid Yazdi ni mojawapo ya vitabu maarufu zaidi katika seminari (hawza) za kidini, kilichoandikiwa aina mbali mbali za maandishi fafanuzi na chambuzi juu ya muqtadha wa mada zilizomo ndani yake. Kitabu kiitwacho “Faraatar az Rawesh Azmuun wa Khataa wa Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi” ni kitabu makhususi kilicho andikwa kuhusiana na maisha ya Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi.

Wasifu wa Maisha Yake

Sayyid Yazdi akiwa na watoto wake

Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi alizaliwa katika kijiji cha Kisnawiyeh huko Yazd. [1] Baba yake, Sayyid Abdolazim, alikuwa ni mkulima. [2] Nasaba yake inarudi kwa Sayyid wa Tabatabai na hatimae kuishia kwa Imamu Hassan Mojtaba (a.s). Kuna maoni tofauti juu ya mwaka wa kuzaliwa aliozaliwa: katika kitabu kiitwacho Ayan al-Shia, kuna rikodi ioneshayo kuwa alizaliwa mwaka wa 1247 Hijria. [3] Ila Ali Dawani katika kitabu Nehdhat Rohaniyun Iran, baada ya kuelezea familia yake, ameeleza mwaka wa kuzaliwa kwake kuwa ni mwaka wa 1248 Hijria. [4]

Kaburi la Sayyid Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi na mwanawe Sayyid Muhammad katika Haram ya Imam Ali (a.s)

Sayyid Muhammad Kadhim alifariki dunia mwezi 28 Rajabu mwaka 1337 Hijria (1298 Shamsia) kutokana na ugonjwa wa nimonia, na kuzikwa katika msikiti wa Umran bin Shahin ndani ya Haram ya Imamu Ali (a.s). [5] Kifo kiliombolezwa na Waislamu wa pande zote zote mbili Shia pamoja na Sunni nchini Iraq. Kufuatia kifo chake nchini Iran, hata Ahmad Shah (mfalme wa Iran) pia alihudhuria katika mazishi yake. [6] Mtaalamu wa rikodi za nyaraka na vitabu ajulikanaye kwa jina la Sayyid Abdulaziz Tabatabai Yazdi (aliye ishi kati ya mwaka 1308 na 1374 Shamsi), ni mjukuu na matunda ya Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi. [7]

Kaburi la Muhammad Kadhim Yazdi katika Haram ya Imam Ali (a.s) mwaka 1445 Hijiria.

Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi alioa katika mji wa Najaf. Watoto wake ni: Sayyid Ali, Sayyida Zahra, Sayyid Hassan, Sayyid Mahmoud, [8] Sayyid Asadullah, [9] pamoja na Sayyid Muhammad ambaye ni mwandishi wa vitabu "Sahaaif al-Abraar bi Wadhaifi al-Ash-ar" na "Risalatu fi Fadhaili al-Kutubi wa Iqtinaa-iha". [10] Sayyid Mohammad pia aliwahi kuwa na jukumu la uongozi katika vita vya koo za wakazi wa Ahwaz dhidi ya majeshi ya Uingereza katika mji wa Ahwaz mkoani Khuzistan. [11] Baadhi ya watafiti wanaamini kwamba; Sayyid Muhammad, mwana wa mwandishi wa kitabu kiitwacho “Al-Urwat al-Wuthqa”, hakufa kupitia kifo cha kawaida, bali aliuawa kupitia mazingira maalumu. Ila watafiti wengine wanaamini kinyume na hivyo, kwa mfano Aqa Bozorg Tehrani, mwandishi wa Al-Dhari'a, anaamini kwamba; Kifo chake kilikuwa kilikuwa ni cha kawaida, ambapo rikodi zao zaonesha ya kwamba, kifo chake kilitokea mnamo mwezi 13 Jumadu al-Awwal mwaka 1334 Hijria. [12] Sayyid Ali Khamenei anaamini kwamba Sayyid Muhammad alienda vitani dhidi ya Waingereza kwa agizo la baba yake na alikuwa kiongozi mkuu miongoni mwa wanazuoni waliokuwepo vitani, lakini hakufa kishahidi vitani humo, bali alikuja kufariki baadae. [13]

Maisha Yake ya Kielimu

Elimu Yake

Sayyid Muhammad Kadhim alikuwa ni mkulima na akaendelea na shughui hiyo kwa kipindi fulani, ila baadae alijitosa katika mkondo wa kutafuta kielimu. [14] Mnamo mwaka 1256 Hijria, Sayyid Muhammad Kadhim alianza kujifunza masomo ya awali ya kidini katika chuo cha Mohsiniyyeh au Doomanar huko Yazd. [15] Miaka minne baadaye, alihamia Mashhad ili kuendelea na masomo yake na alijifunza masomo ya ngazi ya kati pamoja na elimu ya anga, unajimu (elmu alfalak), na hisabati. Mnamo mwaka 1265 Hijria, alihamia Isfahani [16] na kukaa katika shule ya Sadri, ambapo alihudhuria masomo ya Sheikh Muhammad Baqir Najafi hadi alipompa ruhusa (ijaza) ya ijtihadi. [17]

Mwaka 1281 Hijria, kwa ruhusa na utambulisho wa Muhammad Baqir Najafi Isfahani, alielekea mjini Najaf [18] na akaishi katika shule ya Sadri ilioko mjini Najaf. Kuingia kwake mjini Najaf kulisadifiana na tukio la kifo cha Sheikh Murtadha Ansari, ambapo nafasi ya cheo cha umarja’a (mamlaka ya kutoa fatwa) kilihamia kwa mwanazuoni aitwaye Mirza Shirazi. Baada ya muda fulani, Sayyid Muhammad Kadhim aliteuliwa kuwa ni imamu wa jamaa wa msikiti wa Haram ya Imamu Ali (a.s). [19]

Baada ya Mirza Shirazi kwenda Samarra, Sayyid Kadhim alibaki Najaf na kuanaza kufundisha masomo ya kidini hadi akafikia daraja ya umarja’a. [20]

Hadhi Yake ya Kielimu

Kulingana na ripoti iliopo katika kitabu kiitwacho A’ayanu al-Shi’a, takriban kulikuwa kiasi cha idadi ya watu mia mbili waliokuwa wakihudhuria duru za masomo za Sayyid Yazdi. [21] Mohsen Amin akimsifu Sayyid Yazdi, alimwelezea kuwa yeye alikuwa ni mtaalamu wa lugha na adibu (mwanafasihi) mzuri, akisema kuwa kitabu chake, Urwat al-Wuthqa, kilikuwa na umuhimu mkubwa mno, kiasi kwamba yeyote aliyetaka kufikia daraja ya umarja’a, alilazimika kuandika tasnifu fafanuzi ya kitabu hicho. [22] Muhammad Gharawi, katika kitabu chake Ma’a Ulamaa Najaf al-Ashraf, alimsifu Sayyid Kadhim Yazdi akisema kwamba; Yeye alikuwa ni bahari ya elimu na utafiti, na mtaalamu mzuri mno kwenye sekta sote mbili, sekta ya elimu ya maandiko (manqul) na kiakili (ma’aquul). Akiendelea kumsifu aliandika akisema ya kwamba; Yeye alikuwa na uelewa mpana juu ya matawi yote ya fani fiqhi na maandiko ya Hadithi. [23]

Sayyid Musa Shubeiri, kupitia kwa Aqha Dhiya Iraqi, aliripoti akisema kuwa; Sayyid Mohammad Kadhim Yazdi alikuwa na elimu zaidi kuliko Akhund Khorasani, na sababu ya kufikia daraja hiyo, ilikuwa ni juhudi na umakini mkubwa aliokuwa nao Sayyid Yazdi katika fani ya fiqhi. [24]

Umarjaa

Sayyid Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi alifikia hadhi ya umarja’a mnamo mwaka 1312 Hijria baada ya kifo cha Mirza Shirazi. Katika siku hizo, Akhund Khorasani na Sheikh Muhammad Taha Najaf walikuwa ni miongoni mwa Marja’a (wanazuoni wenye mamalaka ya kutoa fatwa) wa Shia ambao walikuwa hai. Baada ya vifo vya wanazuoni hao, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi alibaki kuwa ndiye Marja’a pekee wa wa zama hizo. [25] Baada ya kifo chake, Nafasi na cheo cha umarja’a kilihamia kwa Mirza Muhammad Taqi Shirazi na Sayyid Ismail Sadr. [26]

Wakufunzi Wake

Wanafunzi

Idadi ya wanafunzi wa Sayyid Muhammad Kazem Yazdi, ni 350 kama ilivyoripotiwa kwenye makala za kongamano la kumbukumbu yake; [36] hata hivyo, utafiti mwingine unaonyesha kuwa wanafunzi wake walifikia idadi ya watu 750. [37] Baadhi ya wanafunzi hao ni:

Baadhi wanamchukulia Sheikh Abdul-Karim Hairiy na Sayyid Hussein Boroujerdiy kama ni wanafunzi wa Sayyid Kadhim Yazdi; lakini kwa mujibu wa maelezo ya Sayyid Mussa Shubairi, ni makosa kuwahisabu wawili hao kuwa ni miongoni mwa wanafunzi wake, kwani wawili hawa walikuwa ni wanafunzi wa Akhund Khorasani. [39]

Kazi Andishi

Kulingana na maelezo ya Abul-Hassani katika kitabu chake “Faaratar az Raveshe Aazmon wa Khata”, ni kwamba; Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi ameandika idadi ya kazi 25 za kifiqhi na usuli al-fiqhi. [40] Kitabu “Al-Urwat al-Wuthqa” ndiyo maarufu na muhimu zaidi miongozi mwa kazi zake hizo andishi ndani ya nyanja mbili hizo. [41] Kitabu hichi kimepata nafasi ya kipekee katika tafiti za kifiqhi, pia kimekuwa na heshima kubwa mno mbele ya wanazuoni na mafaqihi mbali mbali. Kuna tasnifu na tungo andishi kadhaa zilizo andikwa kwa ajili ya kutoa tafsiri na maelezo chambuzi ya kitabu hichi. [42] Umuhimu wake ni mkubwa mno, kiasi ya kwamba imepelekea mwandishi wa kitabu hiki kujulikana kwa jina la kitabu chake kwa kuitwa «Sahib al-Urwa». [43]

Harakati za Kisiasa

Yasemekana kwamba Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, alikuwa na shughuli chache zaidi za kisiasa ikilinganishwa na wanazuoni wengine wa zama zaka, kama vile Akhund Khurasani. Shughuli zake za kisiasa zilikuwa hasa katika kutoa telegramu na kuandika ilani za kisiasa, lakini kutokana na nafasi yake kama kiongozi mkuu wa kidini, shughuli hizo zilikuwa na umuhimu mkubwa juu yake. [44]

Baadhi ya Shughuli za Kisiasa za Sayyid Mohammad Kadhim Yazdi ni kama zifuatazo:

Kuhamasisha na Kuunga Mkono Kampuni ya Kiislamu

Mnamo mwaka wa 1316 Hijria, baadhi ya waumini walianzisha Kampuni ya Kiislamu huko Isfahan kwa lengo la kupambana na ushawishi wa kiuchumi wa wageni. [45] Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi pamoja na wanazuoni wengine kama vile Akhund Khurasani, Mirza Hussein Nouri, Shariat Isfahani, na Sayyid Ismail Sadri, walitoa baraka zao kwa kuandika maoni yao kwenye kitabu cha "Libasu-al-Taqwa," kilicho kuwa na lengo la kuhamasisha jamii kununua bidhaa za ndani. [46]

Fatwa dhidi ya Ukoloni wa Italia, Urusi, na Uingereza

Kufuatia uvamizi wa nchi ya Libya ulio fanywa na vikosi vya Italia, pamoja na pia uvamizi wa vikosi vya Urusi na Uingereza nchini Iran wa mwaka wa 1329, Hijria Sayyid Kadhim Yazdi alisimama na kutoa fatwa ya wajibu kwa Waislamu wote "Waarabu kwa Waajemi" kuinuka na kuwa tayari «kuwafukuza makafiri kutoka kwenye ardhi zao za Kiislamu». [47]

Tangazo la Jihad dhidi ya Uingereza

Maulamaa wa Najaf wakikabiliana na jeshi la Uingereza

Wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na uvamizi wa Iraq na vikosi vya Uingereza, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, pamoja na wanazuoni kama vile Mirza Muhammad Taqi Shirazi na Sheikh Al-Sharia Isfahani, walisimama na kutangaza jihad dhidi ya Uingereza. [48] Mirza Muhammad Taqi Shirazi alipoteza mmoja kati wanawe katika jihad hii, ambaye ni Sayyid Muhammad aliye uawa vitani. [49]

Mwamko wa Kimapinduzi wa Kutaka Mageuzi ya Katiba

Maulamaa wa Najaf wakikabiliana na jeshi la Uingereza

Katika harakati za kimapinduzi dhidi ya katiba, Sayyid Yazdi alishirikiana bega kwa bega na Sheikh Fadhlullah Nouri, alifanya hivyo huku akisisitiza ya kwamba; Uungwaji mkono wa Bunge unapaswa kuwa na masharti ya Bunge hilo kufuata kikamilifu kanuni za Kiislamu. Wakati Sheikh Fazlollah alipingia kwenye Haram ya Shah Abdul-Adhim, na kuamsha mgomo wa kuigomea wito wa kundi la pili la wanamageuzi, ambao hawakuwa wakisisitiza ulazima wa bunge kufuata kanuni za kidini, Sayyid Yazdi alikuwa ni mmoja wa waliomuunga mkono ipaswavyo, ambapo alionekana kumsadia kwa hali namali kwenye mgomo wake huo. [50]

Baada ya wapinzani kupopoa Bunge kwa kutumia mizinga, wakati ambapo Akhund Khurasani alikuwa akifanya juhudi kubwa kurejesha uwanjani harakati za mageuzi ya katiba bila ya sharti ya kufuata kanuni za dini, Sayyid Yazdi alitoa fatwa ya kupinga katiba hiyo ili kuzuia magauzi hayo ya katiba. [51]

Huduma za Kijamii

Muonekano wa shule ya Seyyed Yazdi huko Najaf

Imeelezwa ya kwamba; Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi alikuwa na utashi na dukuduku la kutafuta maendeleo ya ujenzi wa miji pamoja na vijiji, alijitahidi kujenga misikiti, bafu, na nyumba za kupumzikia wageni na wasafiri mbali mbali. Pia alijali sana ujenzi wa majengo ya kielimu. Shule maarufu zaidi ya kidini ilioko huko Najaf, ijulikanayo kwa hivi sasa kama Madrasatu Sayyid, ni miongoni mwa majengo yaliojengwa kwa juhudi zake. [52]

Pia, yeye ndiye aliye anzisha mahali pa kupumzikia wageni katika mtaa wa Al-Amarah huko Najaf, ambapo palikuwa panajulikana kwa jina la «Khanu Al-Zairina», ila mnamo mwaka 1384 Hijria, jengo hilo lilibadilishwa na kuwa madrasa. [53]

Sifa za Kimaadili

Sayyid Musa Shubairi, kiongozi wa kidini wa Shia, anaeleza akisema kuwa; Sayyid Ahmad Khansari, ambaye alikuwa ni mashuhuri kwa uchamungu na uadilifu, aliamini juu ya uchamungu wa kweli aliokuwa nao Sayyid Yazdi. [54] Pia anasema Sayyid Mohammad Kadhim Yazdi alikuwa ni mwangalifu na mwenye tahadhari sana; kiasi ya kwamba alipofariki, alibakisha kiasi cha sala na saumu elfu sita, ambazo zilikuwa zikisubiri kupata waumini wa kweli wa kuzisali kwa niaba ya maiti waliotanguli. Hii ni kwa sababu ya kule yeye kuto kuwa na uhakika juu ya ukweli wa imani za watu wanaostahiki kutekeleza ibada hizo. [55]

Kumbukumbu

Mnamo tarehe 24 Esfand 1391 (kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia), kulifanyika kongamano la kimataifa kwa ajili ya kumuenzi Sayyid Mohammad Kadhim Yazdi. Kongamano hilo lililo fanyika huko Qom, lilipewa jina la "Kongamano la Kimataifa la Sahibu Al-Uruwa". Kongamano hili, lilihudhuriwa na wanazuoni na viongozi kutoka nchi kadhaa, ikiwemo Iran, Iraq, na nchi nyingine mbali mbali. [56]

Bibliografia (Vitabu Vilivyomuhusiana na Maudhui Hii)

  • Kitabu Faraatar az Rawesh «Aazimun wa Khataa», kilichoandikwa na Ali Abulhasani. [57]
  • Kitabu Al-Sayyid Mohammad Kadhim Al-Yazdi, kilichoandikwa na mwandishi wa Kiiraqi aitwaye Kamil Salman Al-Jabouri. Kitabu hichi kinazingatia shughuli za kijamii za Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi huko Iraq. [58]
  • Kitabu Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi Faqiih Darun-Andish, kilichoandikwa na Murtadha Bazri-afshaan. [59]
  • Kitabu Shukuuh Paarisaaiy wa Paayedaariy. Kitabu hichi kilichapishwa na Ofisi ya Gavana wa Yazd kuhusiana na mapambano na urithi ulio achwa na Sayyid Yazdi. [60]

Rejea

Vyanzo