Nenda kwa yaliyomo

Sala ni bora kuliko usingizi

Kutoka wikishia

Sala ni Bora Kuliko Usingizi (Kiarabu: الصَّلاةُ خَيرٌ مِنَ النَّوم) ni tamko na ibara inayotumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Ahlu-Sunna, ambayo huitamka mara mbili katika Adhana ya Sala ya Alfajiri baada ya kumaliza kipengele cha Adhana kisemacho: «Haya ala al-Falah ; حی علی الفلاح» Hadithi mbalimbali, hulihisabu tamko hili kuwa ni mustahabu lenye nia ya kuhimiza watu kuhudhuria Sala ya Alfajiri. Kwa mujibu wa masimulizi ya upande wa madhehebu ya Kisunni, tamko hili lina nafasi maalum ya kiibada katika kutekeleza wito wa kuamsha waumini kwa ajili ya ibada ya Sala katika wakati mgumu wa alfajiri. Hata hivyo, mtazamo wa wanazuoni wa madhehebu ya Imamiyya (Shia) unapingana na dhana hii. Kwa mujibu wa mtazamo wa wanazuoni wa Kishia, haijuzu kuongeza ibara hii katika Adhana, bali ni haramu endapo nyongeza hii itaongezwa kwa nia ya kuanzisha kipengele kipya cha sheria. Kwa mtazamo wa madhehebu ya Shia Imamiyya, hakuna ithibati yoyote ile ya kisheria, si kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w) wala Maimamu (a.s) inayo onesha kuidhinishwa kwa ibara hii katika adhana, hivyo basi, kufanya hivyo ni sawa na kwenda kinyume na taratibu za ibada kama zilivyowekwa na Mwenye Ezi Mungu mwenyewe.

Kuna simulizi tofauti zinazopatikana katika vyanzo vya Hadithi vya Ahlus-Sunna kuhusiana na asili ya tamko hili. Katika moja ya simulizi maarufu inadaiwa kuwa Bilal, mwadhini maarufu wa bwana Mtume (s.a.w.w), aliongeza tamko hili katika adhana ya alfajiri, na bwana Mtume (s.a.w.w) akaliridhia na kuidhinisha jambo hilo. Pia, kuna masimulizi mengine yanayodai kuwa; bwana Mtume (s.a.w.w) alimfundisha Abu-mahdhura kutumia maneno hayo. Aidha, kuna vyanzo vingine vinavyosema kuwa; Sa’ad bin Aidh aliyekuwa mwadhini wa msikiti wa Quba katika zama za bwana Mtume (s.a.w.w), ndiye mtu wa kwanza kabisa aliye anzisha matumizi ya ibara hiyo katika kipindi cha ukhalifa wa Omar bin Khattab. Kwa mujibu wa riwaya iliyonukuliwa na Malik bin Anas katika kitabu chake kiitwacho Al-Muwatta, tamko hili liliongezwa rasmi kwenye adhana kwa idhini ya Omar bin Khattab wakati zama za ukhalifa wake.

Kutamka ibara ya «Sala ni bora kuliko usingizi ; الصَّلاَةُ خَیْرٌ مِنَ النَّوْمِ» kunajulikana kwa jina la tathwib. Kulingana na wanazuoni wa fiqhi, tathwib inamaanisha kurudi tena kwenye wito asili wa Adhana baada ya ya kutowa wito usemao «Sala bora usingizi» uliofuata baada ya kipengele kisemacho «Haya ala al-Swala». Kwa hiyo ile hali ya yeye kurudi tena kwenye adhana ndiyo tathwib, jambo ambalo hufanyika katika adhana ya alfajiri. Aidha, kwa upande wa madhehebu ya Kisunni, tathwib huchukuliwa kama ni njia ya kuongeza msisitizo wa ibada kwa waumini ambao wanaweza kuwa na uzito wa kuamka alfajiri kwa ajili ya sala. Hata hivyo, tathwib inachukuliwa kujumuisha ibara zaidi ya moja, na baadhi ya wanazuoni wa fiq’hi wanasema kwamba; ni kitendo kinachojumuisha ziada ndani ya Adhana. Baadhi ya ibara za tathwib ni kutamka maneno kama vile; «Sala rehema za Mwenye Ezi Mungu ziwe juu yenu ; الصلاةَ، رَحِمَکُمُ اللهُ» au kuongeza neno sala ndani ya Adhana na Iqama, au kurudia kusema Haya ala al-Sala na "Haya ala al-Falah" mara kadhaa kwa ajili ya kuhamasisha watu zaidi kuhudhuria sala, hasa katika sala ya alfajiri.

Tafiti za Dhana Tathwib na Nafasi yake

Ibara ya «Sala ni bora kuliko usingizi ; الصلاة خیر من النوم» ni sehemu ya wito wa Adhana ya Alfajiri inayotumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Ahlus-Sunna, ambapo tamko hili hufuatia baaya ya kipengele cha Adhana kisemacho «Haya ala al-Falah» (Njoo kwenye kufuzu). Tamko hili linalonesha umuhimu wa sala juu ya usingizi, hasa katika muda mgumu wa alfajiri wakati ambapo watu wengi wapo katika usingizi mzito, hukaririwa mara mbila katika Adha hiyo. [1] Jina jengine la ibara hiyo ni Tathwib, [2] Kulingana na Ahlus-Sunna, tathwib, yaani kutamka "Swala ni bora kuliko usingizi", ni desturi inayokubalika na kutambulika kama sunna katika Adhana ya sala ya Alfajiri, ikihimiza waumini kujitahidi kuamka kwa ajili ya ibada hiyo. Tathwib inachukuliwa kama wito wa pili, ambapo baada ya kuwaita waumini kwenye sala kwa kutumia ibara isemayo Haya ala al-Sala (Hima Elekeeni Kwenye Ibada ya Sala), mwadhini huongeza msisitizo wa wito wake kwa kusema: Sala ni bora kuliko usingizi, akiwakumbusha waumini umuhimu wa ibada hiyo juu ya starehe ya usingizi. [3] Lengo la tamko hili ni kuhamasisha waumini kuacha usingizi na kuelekea kwenye sala, ikijulikana kuwa kipindi cha alfajiri ni kipindi ambacho mwili wa mwanadamu unakuwa ni zaidi, lakini sala inapaswa kupewa kipaumbele. Hii ni mbinu ya Wasunni katika kuimarisha Sala ya Alfajiri.

Baadhi ya wanazuoni wamehusisha matamko ya ibara nyengi katika hukumu yah ii ya Tathwib. Kwa mtazamo wao kusema: «Sala rehema za Mwenye Ezi Mungu ziwe juu yenu ; الصلاةَ، رَحِمَکُمُ اللهُ» au kuongeza neno sala (kati ya ibara za Adhana na Iqama, kisha kuendelea na Adhana, ni miongoni mwa mifano ya tathwib. [4] Pia, imeelezwa kuwa baadhi ya wanazuoni wa madhehebu ya Hanafiyya huko mjini Kufa wameona kuwa; suala la kurudia mara mbili ibara ya «Haya ala al-Swala» na «Haya ala al-Falah» ndani ya Adhana au Iqama ya Sala ya Alfajiri, ni aina nyengine ya tathwib. [5]

Mada hii imejadiliwa vya kutosha katika vitabu vya fiqhi, hasa katika mlango unaohusiana na sala, [6] pia ni miongoni mwa masuala yaliyotumbukia katika uwanja wa mijadala ya kitheolojia iliopo kati ya Sunni na Shia. [7]

Mtazamo wa Shia Imamiyya Kuhusu Ubid'a  (Uzushi) wa Ibara ya «Sala ni Bora Kuliko Usingizi»

Wanazuoni wa madhehebu ya Shia Imamiyya wameafikiana kwa kauli moja ya kwamba: ni bid’a (uzushi) kutamka ibara isemayo: «Swala ni bora kuliko usingizi ; Kigezo:Araabic» katika Adhana, na ni haramu kuongeza tamko hili kwa nia ya kuanzisha au kuhalalisha ibada ya bid’a (uzushi) katika dini. [8] Imamiyya wanaamini kuwa hakuna ushahidi wa wenye ithibati za kisheria, unaothibitisha uhalali wa kutumia tathwib katika Adhana, na kuongeza ibara hii, kunahisabiwa ni kujenga msingi mpya katika sheria ya Kiislamu. [9] Ingawa kuna baadhi ya riwaya zinazodai kuwa Maimamu (a.s) walikuwa wakikubaliana na tathwib katika adhana, [10] ila wanazuoni wa Imamiyya wanapinga uthibitisho wa Hadithi hizo kwa kueleza kuwa Hadithi hizo ni Hadithi shaadhun (zilizokosa umashuhuri), [11] wala nguvu za kutosha kisheria, kwani ni zenye kukinzana na Hadithi sahihi kutoka kwa Ahlul Bait zenye kupinga tathwib. [12] Wanazuoni wa Kishia wamekubaliana ya kwamba Riwaya hizo si za kuaminika, hasa kwa kuwa zinakinzana na Riwaya nyingine sahihi ambazo zinakataa moja kwa moja uwepo na uhalali wa tathwib. Zaidi ya hayo, wanazuoni wa Imamiyya wanaamini kuwa Riwaya zinazotetea tathwib zilitamkwa katika hali ya taqiyyah (kitendo cha kuficha msimamo wa kweli wa kidini ili kulinda dini au maisha wakati wa hatari). [13] Hivyo, matamko hayo hayawezi kuchukuliwa kama ni msingi wa kisheria wa kuhalalisha tathwib katika Adhana. Hii ni kwa sababu ya kwamba; katika misingi ya imani za Imamiyya, kuthibitisha jambo lolote la ibada, huwa kunategemea uwepo wa dalili wazi ima; kutoka katika Qur’ani, Sunna za bwana Mtume (s.a.w.w) au Ahlul Bait (a.s). Hivyo basi wanapinga vikali dhana ya kuongeza tamko la "Sala ni bora kuliko usingizi" kwenye Adhana.

Inasemekana kwa wanazuoni wote wa madhehebu ya Shia Imamiyya wamekubali kwa kauli moja   ya kwamba; kutamka ibara ya Swala ni bora kuliko usingizi katika Adhana kunaruhusiwa masharti ya kwamba ibara hiyo iwe ni kwa nia ya kuwakumbusha waumini muda wa sala au kutokana na hali ya taqiyyah, ambacho ni kitendo cha kujicha imani kwa ajili ya kulinda dini (au madhehebu) yako katika mazingira ya hatari. [14] Katika hali hizi mbili maalum, kutamka tathwib kunaweza kuchukuliwa kuwa ni halali, ambapo wakati mwengine pi kutofanya hivyo, kunaweza kuzusha mizozo ya kiitikadi na kisheria. Hata hivyo, tatizo hujitokeza pale tathwib inapotekelezwa bila nia ya taqiyya au pasipo na lengo la kukumbusha sala. Katika hali kama hii, kuna mvutano mkubwa miongoni mwa wanazuoni wa Kishia kuhusiana na uhalali wa tendo hilo. [15] Baadhi ya wanazuoni mashuhuri kama vile Fadhil Hindi [16] na Faidh Kashani [17] wanaamini kuwa; tathwib ni makruhu (yaani jambo lenye kuchukiza). Kwa maoni yao ni kwamba; haidhuru halifai mtu kutekeleza jambo hilo, ila katazo la utendaji waki halifikii kiwango cha uharamu. Kwa mtazamo wao ni bora kuepuka utaratibu huo, lakini sio lazima tendo hilo kuingizwa katiko kundi la matendo ya haramu. Kwa upande mwingine, wanazuoni wakubwa kama vile Sahibu Al-Jawahir [18] na Kashif al-Ghita [19] wameshikilia msimamo mkali zaidi, wakisisitiza kuwa; ni haramu kabisa kabisa mtu kufanya tathwib, au kutoa tamko la Swala ni bora kuliko usingizi katika adhana, na wala hakuna kitu kinacho weza kuhalalisha jambo hili, kwahiyo halipaswi kutekelezwa katika hali yoyote ile.

Kashif al-Ghita, ambaye ni miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kishia, amekuwa wazi kabisa akieleza kuwa tathwib ni moja ya aina za ubid’a (uzushi wa kidini ambao kimsingi hauna chanzo katika Qur’ani wala Sunna). Hivyo anaamini kuwa hakuna ushahidi wowote wa kisheria unaoweza kuhalalisha tathwib, na kuongeza tamko hili katika adhana ni kinyume na desturi na nyenendo asili za bwana Mtume (s.a.w.w). Kwa mtazamo wake, kufanya hivyo ni kuvuka mipaka ya ibada sahihi na kuzua jambo lisilo na msingi katika sheria ya Kiislamu. [20]

Mtazamo wa Wanazuoni wa Ahlu-Sunna Kuhusu Kauli ya «Swala ni Bora Kuliko Usingizi»

Kulingana na maoni yanayokubalika miongoni mwa wanazuoni maarufu wa fiqhi wa Ahlus-Sunna, ni Sunna kwa mwadhini katika adhana ya Sala ya Asubuhi kutamka kauli isemayo: "Swala ni bora kuliko usingizi" baada ya kauli ya ya kumaliza kipengele kisemacho: "Hayya 'ala al-falaah". [21] Hii inamaanisha kwamba sio faradhi wala jambo la lazima, bali ni tendo linalopendekezwa kwa wale wanaofuata madhehebu haya. Hata hivyo, kuna ushahidi wa maandiko na maelezo tofauti juu ya suala hili katika madhehebu ya Ahlu-Sunna. Kwa mfano, inasemekana kuwa Imamu Muhammad bin Idris al-Shafi'i, mwanachuoni maarufu wa fiqhi na kiongozi wa madhehebu ya Kishafi, katika baadhi ya maandiko yake alikubali kuwa ni mustahabu mtu kutamka kauli hiyo. Hata hivyo, katika maandiko yake mengine, alionekana kulishutumu tendo hili na kuliona kama ni jambo ni makruhu, yaani ni jambo ambalo lisilo pendeza. [22] Hali hii inadhihirisha kwamba hata ndani ya madhehebu ya Kisunni, pia kuna mitazamo tofauti kuhusiana na suala hili. Kwa upande mwingine, wanazuoni wa madhehebu ya Hanafiyya, miongoni mwa madhehebu manne makubwa ya Ahlu-Sunna, kuna wanazuoni wanaokubali kuwa; ni halali kutamka ibara ya "Swala ni bora kuliko usingizi" katika Adhana. Zaidi ya hayo, wao pia wanaruhusu kutamka kauli hii hata baada ya kumalizika kwa Adhana ya Sala ya Asubuhi, kama njia ya kuendelea kuhimiza waumini juu ya umuhimu wa sala. [23]

Kwa mujibu wa maoni maarufu ya wanazuoni wa Ahlus-Sunna, tathwib au kutamka ibara isemayo: "Swala ni bora kuliko usingizi" inahusishwa katika adhana ya Sala ya Asubuhi tu. [24]

Nembo ya Ahlu-Sunna

Kwa muda mrefu, kutamka kauli (Swala ni bora kuliko usingizi ; الصلاة خیر من النوم) katika Adhana imekuwa ikichukuliwa kuwa ni alama na nembo muhimu ya utambulisho wa Ahlu-Sunna. Katika tawala zilizokuwa chini ya watawala wa Kisunni, kauli hii iliamrishwa rasmi na kufanywa kuwa ni sehemu ya Adhana, ikisisitiza nguvu za kiutawala wa madhehebu ya Kisunni. [25] Kwa mfano, kitabu cha Siratu Al-Halabiyya kinaeleza kuwa; katika kipindi cha utawala wa Bani Buwaih huko Baghdad, tamko la Hayya 'ala khayr al-'amal lilikuwa ni sehemu ya Adhana. Hata hivyo, hali hii ilibadilika pale Waseljuqi (Seljuks) walipochukua madaraka mnamo mwaka 448 Hijiria, ambapo kulitoka amri ya kuacha kutamka kauli hiyo. Badala yake, ikamuliwa kwamba tamko "Swala ni bora kuliko usingizi" ndilo lisheke nafasi ya ibara ya "Hayya 'ala khayr al-'amal". [26]

Mabadiliko haya yanaonekana kuwa ni mkakati wa makusudi wa kisiasa na kidini, ambao ulilenga kuimarisha utambulisho wa madhehebu ya Kisunni na kupunguza ushawishi wa Kishia. Katika kipindi hichi, ibada za kidini kama Adhana zilitumiwa kama nyenzo za kuonyesha mamlaka na kujenga mshikamano wa kijamii chini ya mfumo wa kisiasa na kimadhehebu.

Tofauti ya Maoni Kuhusu Wakati na Namna ya Kauli «Sala ni Bora Kuliko Usingizi» Ilivyoongezwa katika Adhana

Kuna mitazamo tofauti kuhusu wakati na nani aiye ongeza kauli ya «Swala ni bora kuliko usingizi ; الصلاة خیر من النوم» kwenye adhana ya Sala ya Alfajiri.

Wakati wa Ukhalifa wa Omar bin Khattab

Sayyid Ali Shahrastani katika kitabu chake chenye jina la «الصلاة خیر من النوم فی الاذان ; Swala ni Bora Kuliko Usingizi katika Adhana», ameandika akisema kwamba; wanazuoni wa madhehebu makuu matatu, yaani ya Shia Imamiyyah, Ismailiyya na Zaidiyya, wanasema kuwa kauli hii iliongezwa katika Adhana wakati wa utawala wa Omar bin Khattab na kupitia amri yake yeye mwenyewe. [27] Malik bin Anas pia amenukuu katika kitabu chake kiitwacho Al-Muwatta akisema kwamba; siku moja mwadhini alimwendea Omar bin Khattab akimwita kwa ajili ya Sala ya Asubuhi, ila alimkuta akiwa amelala, hapo mwadhini aliinua sauti yake akisema: "Swala ni bora kuliko usingizi". Baada ya tukio hilo, Omar akatoa amri rasmi kwamba kauli hii itamkwe katika Adhana ya Alfajiri. [28] Pia, baadhi ya wanazuoni wanasema kwamba Omar bin Khattab ndiye aliye toa amri ya kuondolewa kwa kauli ya Hayya 'ala khayr al-'amal kutoka kwenye adhana na badala yake kuwekwa kauli «Swala ni bora kuliko usingizi ; الصلاة خیر من النوم». [29]

Kwa mujibu wa simulizi nyingine, kauli «Swala ni bora kuliko usingizi» kwa mara ya kwanza iliongezwa na Sa’ad bin Aa-idh, ambaye alikuwa ni mwadhini wa Msikiti wa Quba wakati wa zam za bwana Mtume (s.a.w.w). Inasemekana kuwa nyongeza hiyo aliingiza kwenye Ahana katika zama za ukhalifa wa Omar bin Khattab, kitendo ambacho wanazuoni wengine wamekitaja kama bid'ah (uzushi wa kidini). [30] Hata hivyo, kuna Riwaya nyingine kutoka kwa Imamu Kadhim (a.s), ambayo inayo sema kuwa, kauli hii iliongezwa kwenye Adhana wakati wa utawala wa Bani Umayyah. [31] Riwaya hii inaashiria kuwa; mabadiliko haya yaliletwa na watawala wa ukoo wa Bani Umayyah ili kuimarisha utawala wao wa Kisunni na kudhibiti ushawishi wa madhehebu mengine, hususan Shia, katika masuala ya ibada.

Wakati wa Uhai wa Mtume (s.a.w.w)

Kuna simulizi mbalimbali na zinazokinzana zilizoripotiwa katika vyanzo vya Hadithi za Ahlu-Sunna, kuhusiana na suala la kuongezwa kwa kauli ya «Swala ni bora kuliko usingizi» katika adhana wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w.w). Katika baadhi ya Hadithi hizo, inasemekana kwamba; siku moja Bilal alimwendea bwana Mtume (s.a.w.w) ili kumwita kwa ajili ya Sala ya Alfajiri, lakini alipofika akamkuta amelala, akapaza sauti na kusema: «Swala ni bora kuliko usingizi». Baada ya tukio hilo, bwana Mtume (s.a.w.w) aliunga mkono kauli hiyo ana akatoa amri ya kuingizwa rasmi kauli hiyo katika Adhana ya Sala ya Asubuhi. [32] Aidha, kuna Riwaya nyingine zinazoeleza kwamba bwana Mtume (s.a.w.w) ndiye aliye mfundisha Abu-Mahdhura kauli hii, akiashiria umuhimu wa kuamka kwa ajili ya ibada na kuchukua hatua ya kuimarisha utekelezaji wa Sala ya Alfajiri. [33]

Kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh Ja'far Subhani, Riwaya zinazohusu kuongezwa kwa kauli "Swala ni bora kuliko usingizi" katika Adhana, zinaopatikana ndani ya vyanzo vya Ahlu-Sunna, zikiwa katika hali ya kutofautiana na kukinzana, jambo ambalo linazidhoofisha Hadithi hizo na kuzifanya zipoteze thamani, kwahiyo haziwezi kuchukuliwa katika kujenga msingi wa hukumu za kidini. Subhani anasisitiza kuwa jambo hili linagusa masuala nyeti kati ya mustahabu na bid'ah, ambao ni uzushi au jambo lililoongezwa katika dini, ambalo kisheria na ni jambo haramu. Kwa hivyo, anapendekeza kuwa ni bora kauli hii iachwe na kuondolewa kabisa kabisa katika Adhana, kwani hata kama itakwa ni sunna, basi kuiacha kwake hakutaleta madhara yoyote misingi ya kisheria; lakini ikiwa ni bid'a (uszushi), basi kuitamka kwake kutahesabika kuwa ni jambo haramu na linaweza kustahiki adhabu. [34]

Baadhi ya wanazuoni wa wa upande wa Ahlu-Sunna pia wamekubali kwamba kauli hii haikuwa ni sehemu ya Adhana wakati wa uhai wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), bali iliongezwa baadae yaani baada ya kifo chake, kwa hivyo inachukuliwa kama bid'a (uzushi). [35]

Msimamo huu unaungwa mkono na hoja isemayo kwamba; jambo lolote lililoingizwa katika ibada za Kiislamu bila msingi wa kisheria linaweza kuathiri uhalali wa ibada hizo, na hivyo inashauriwa kutoitumia kauli hiyo katika Adhana ili kuepuka kuingia kwenye eneo la bid'a (uzushi), ambalo ni haramu na ni lenye madhara kwa waumini.

Monografia

Kuhusu suala la kauli «Swala ni bora kuliko usingizi» katika Adhana na uhalali wake, kuna kazi kadhaa za kimaandishi zilizo andikwa ambazo zinaweza kutoa mwanga wa kutosha kuhusiana na mada hii. Miongoni mwa kazi hizo ni:

  • «Swala ni bora kuliko usingizi ; الصلاة خیر من النوم فی الاذان». Hichi ni kitabu kilichoandikwa na Sayyid Ali Shahristani na kuchapishwa mwaka wa 1433 Hijria kupitia Taasisi ya Uchapishaji ya Al-Rafid huko Baghdad. Kitabu hichi kinajadili kwa kina suala la kuongezwa kwa kauli hii katika Adhana, kikitathmini uhalali na uhalisia wa kauli hii kupitia maoni ya wanazuoni mbali mbali katika uwanja wa historia. [36]
  • Kadhia ya «Sala ni Bora Kuliko Usingizi ; مسألة، الصلاة خیر من النوم». Kitabu hichi kiliandikwa na kikundi cha watafiti wa Jumuia ya Dunia ya Ahlul-Bait (a.s), na kuchapishwa katika juzuu ya ishirini na nne katika mlolongo wa mijalada ya mfululizo wa jarida liitwalo "Fi Rahab Ahlul-Bayt". Kitabu hichi baadae kilikuja kufasiriwa kwa lugha ya Kifarsi. [37]

Rejea

Vyanzo