Mauaji yanayotokana na huruma

- Makala hii inahusiana na wasifu kuhusu mafuhumu na maana ya kifikihi na hivyo haiwezi kuwa kigezo cha amali na matendo ya kidini. Kwa ajili ya amali za kidini, rejea katika vyanzo vingine.
Mauaji Yanayotokana na Huruma (Euthanasia) (Kiarabu: القتل الرحيم أو الموت الرحيم) ni kitendo cha kuondoa maisha ya mtu kutokana na kumhurumia, kwa sababu ya ugonjwa usiotibika unaomletea mateso makali. Kitendo hichi kinaweza kufanyika kwa kutumia dawa ya kuua isiyo na maumivu, au kwa kuacha kutoa huduma msingi za matibabu. Njia ya kwanza katika zoezi hili inajulikana kwa jina la «active euthanasia» (mauaji ya haraka), huku njia ya pili ikiitwa «passive euthanasia» (mauaji taratibu). Zaidi ya hayo, kuna hali ambapo dawa huwekwa karibu na mgonjwa ili ajimalizie maisha yake yeye mwenyewe; hii inajulikana kama euthanasia isiyo ya moja kwa moja (indirect euthanasia). Euthanasia ni miongoni mwa masuala mapya yanayochukua nafasi katika mijadala ya fiqh (sheria za Kiislamu).
Kulingana na maelezo ya wanazuoni wa fiqh, «active euthanasia» (mauaji ya haraka), ni haramu kabisa kabisa. Wao wanasisitiza kwamba; ikiwa kitendo hicho kimefanywa bila idhini ya mgonjwa, basi msimamizi wake (walii wake), ana haki ya kudai kisasi (ulipizi wa kisasi) au kuchukua diya (fidia ya kifedha). Hata hivyo, kuna maoni yanayotofautiana kuhusiana na hali ambapo mgonjwa mwenyewe ameridhia kutentewa zoezi hilo la euthanasia: baadhi ya wanazuoni wanaamini kwamba; msimamizi bado ana haki ya kufanya kisasi au kutaka malipo ya diya, ilhali wengine wanakataa dhana hiyo, na wanasema kwamba, katika hali kama hiyo walii hatakuwa na haki ya diya wala kisasi. Kuhusiana na «passive euthanasia», pia kuna khitilafu za maoni ndani yake: wengi wanatoa fat’wa ya uharamu wa tendo hilo, lakini baadhi yao wanasema kwamba ikiwa mgonjwa ana ugonjwa usiotibika na mateso yake yanaendelea bila ya nafuu, si wajibu wa kidini kumpa huduma za matibabu mgonjwa kama huyo.
Aidha, wanazuoni wa fiqhi wanakubaliana kwamba; euthanasia isiyo ya moja kwa moja, ambapo mgonjwa yeye mwenyewe hutumia dawa ya kuua, huwa ni sawa na tendo la kujiua (qatlu an-nafs), kwa hivyo wanakataza tendo hilo kwa kutoa ya fatwa juu ya tendo hilo haramu.
Dhana ya Euthanasia na Nafasi Yake
«Euthanasia» inamaanisha kumwua mtu mwenye ugonjwa usiotibika na unaomsababishia mateso.[1] Kitendo hichi hufanywa kwa njia ya kuhurumia mgonjwa na kwa njia isiyo na maumivu,[2] kwa kutumia dawa ya kuua au kwa kuacha kutoa huduma muhimu na za lazima.[3] Euthanasia hufanywa kwa njia tatu: «active euthanasia» (mauaji ya haraka), «passive euthanasia» (mauaji taratibu), na kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Ikiwa patatumika dawa ya kusababisha kifo cha mgonjwa, hiyo inaitwa «active euthanasia».[4]Ikiwa mgonjwa ataacha bila ya matibabu, ili mgonjwa huyo afe kwa njia hiyo, hiyo huitwa «passive euthanasia».[5] Katika euthanasia isiyo ya moja kwa moja, dawa huwekwa karibu na mgonjwa, ili yeye mwenyewe amalize maisha yake mwenyewe kwa kutumia dawa hizo.[6]
Katika maandiko ya kale ya kisheria za fiqhi ya Kishia (wakati wa uhai wa Sheikh Tusi na kabla yake), kunapatikana maandiko yanayohusiana na uharamu wa kumwua mtu aliyeridhia yeye mwenyewe kuuliwa; lakini hakujakuwa na mjadala wala maandiko kuhusiana na hukumu za zoezi la euthanasia.[7] Kwa msingi huu, suala hili linachukuliwa kuwa, ni miongoni mwa masuala mapya ya kisheria (figh).[8] Mjadala wa kisheria kuhusu euthanasia ni tofauti na mada ya kifo cha ubongo (brain death); kwa njia hii, inawezekana kwa mwanachuoni wa sheria (faqih) kuona inafaa kuondoa mashine kwa mgonjwa aliyekufa ubongo, au mgonjwa ambaye yuko katika hali ya kupoteza fahamu (koma) na hakuna matumaini ya kumponya; lakini mwanachuoni huyo huyo anaweza kuona «passive euthanasia», yaani, kuacha matibabu kwa aliji ya kumua mgonjwa, kuwa ni miongoni mwa matendo ya haramu.[9]
Hukumu za Kisheria (Ahkamu Taklifiyya) za Euthanasia katika Fiqh ya Kishia
Mtazamo wa wanazuoni wa sheria wa Kishia kuhusiana na uhalali na uharamu wa euthanasia umegawanyika katika vifungu vifuatavyo:
- Active Euthanasia: inahusisha kumpa mgonjwa dawa au kuchukua hatua za moja kwa moja za kumaliza maisha yake. Kulingana na fatwa za wanazuoni wa sasa wa Kishia, hii inachukuliwa kuwa ni zoezi la mauaji, na ni haramu kabisa moja kwa moja.[10] Ridhaa au ruhusa ya mgonjwa haiwezi kubadilishi hukumu hii, kwani uharamu huu unadumu bila kujali matakwa yake.[11]
- Passive euthanasia: inarejelea kukataa au kuacha kutoa matibabu kwa mgonjwa. Hapa kuna maoni ya aina mbili:
- Wanazuoni kama Lutfullah Safi Golpayegani na Hussein-Ali Muntadhari wanaona kuwa tendo hilo ni haramu, na hairuhusiwi kuacha kutoa matibabu kwa mgonjwa asiyetibika na anayeteseka.[12]
- Kinyume chake, wanazuoni kama Mirza Jawad Tabrizi, Sayyid Abul-Qasim Khui na Sayyid Ali Khamenei wametoa fatwa isemayo kwamba; si wajibu wa kisheria kuendeleza matibabu hayo, iwapo mgonjwa huyo yuko katika hali isiyowezakana kumponya.[13]
- Euthanasia Isiyo ya Moja kwa Moja: Hii inahusisha mgonjwa mwenyewe kutumia dawa au njia za kumaliza maisha yake. Kulingana na fatwa za wanazuoni wa Kishia, kitendo hichi kinachukuliwa kuwa ni kujiua na ni haramu.[14]
Hukumu za Kisheria (Ahkamu Wadh’iyya) Kuhusu Euthanasia
Hukumu za Kisheria (Ahkamu Wadh’iyya) Kuhusiaana na Euthanasia: zinahusu masuala ya kisheria yanayohusiana na adhabu (kifo) au fidia ambayo inaweza kuwepo kwa mtu anayehusika na zoezi la euthanasia katika fiqh ya Kiislamu. Hapa, euthanasia imegawanywa katika aina mbili: Active euthanasia na Passive euthanasia. Wanazuoni wa taaluma ya fiqhi wametoa fatwa tofauti kulingana na hali zinazozunguka kila moja ya aina mbili hizi, hasa kuhusiana na wajibu wa kulipiza kisasi (qisas) au kulipa fidia (diya). Maelezo ya hukumu hizi ni kama ifuatavyo:
Active Euthanasia
Active euthanasia inarejelea kitendo cha mtu, kama daktari, kumuua mgonjwa asiyetibika kwa makusudi ili kumwondolea mateso yake. Hukumu inategemea ikiwa mgonjwa huyo aliruhusu kitendo hicho au la:
- Bila Ruhusa ya Mgonjwa: Ikiwa daktari au mtu mwingine anamuua mgonjwa bila idhini yake, kitendo hicho kinachukuliwa kama ni mauaji ya kukusudia. Hivyo, msimamizi wa mgonjwa (walii) ana haki ya:
- Kulipiza kisasi (qisas), yaani kuomba hukumu ya kifo kwa muuaji, au
- Kupokea fidia (diya), ambayo ni malipo ya kifedha kwa ajili ya mauaji hayo.
Hii inatumika hata kama muuaji alikuwa na nia ya huruma au rehma, kwa sababu kitendo chenyewe kinavunja sheria ya Kiislamu inayolinda maisha.[15]
- Ikiwa Mgonjwa Aliruhusu: Kuna maoni tofauti kati ya wanazuoni wa sheria kuhusiana na yule mgonjwa aliyekubali mwenyewe alikubali au aliomba kufanyiwa euthanasia:
- Maoni ya Kwanza: Hakuna Haki ya Qisas Wala Diya, wanazuoni kama Sayyid Abdul-A'la Sabzewari, Imamu Khomeini na Sayyid Muhammad Sadiq Ruhani wanasema kuwa; ridhaa ya mgonjwa huondoa haki ya kulipiza kisasi au kulipwa fidia. Hii ni kwa sababu mgonjwa alikubali kifo chake, hivyo hakuna lawama ya kisheria kwa yule aliyefanya kitendo hicho.[16]
- Maoni ya Pili: Haki ya Qisas au Diya Inabaki, wanazuoni kama Sayyid Abul-Qasim Khui, Mirza Jawad Tabrizi, na Ja'far Subhani wanaamini kuwa; haki ya kulipiza kisasi au kulipwa fidia haiondoki, hata kama mgonjwa aliruhusu tendo hilo. Wao wanasema kwamba;[17] kulingana na sheria ya Kiislamu, haruhusiwi mtu kujiangamiza, kwa hivyo ridhaa yake haibadilishi uhalifu wa kitendo hicho.[18]
Passive Euthanasia
Passive euthanasia inahusu hali ambapo mtu ana uwezo wa kumtibu mgonjwa, au kumsaidia mtu anayeteketea, lakini akaacha kumwokoa na kumpa matibabu, na mgonjwa huyo akakafa kutokana na hali hiyo. Hukumu yake hapa ni kama ifuatavyo:
- Ikiwa daktari au mtu mwingine anaweza kumtibu mgonjwa fulani, lakini haamui kufanya hivyo, kitendo chake kinahisabiwa ni dhambi kwa sababu yeye anavunja wajibu wa kuokoa maisha.[19]
- Hata hivyo, hakuna adhabu ya kulipiza kisasi (qisas) wala kulipa fidia (diya) dhidi yake, kwa sababu hakukuwa na kitendo cha moja kwa moja cha mauaji kilichopita takita tukio hilo.[20]
Rejea
- ↑ Anwari, Farhang Rouz Sokhan, 1383 S, uk. 38.
- ↑ Anwari, Farhang Rouz Sokhan, 1383 S, uk. 38-39.
- ↑ Yazdanifar, Atanazy Az Mandhure Fiqh wa Huquq, 1395 S, uk. 28.
- ↑ Qasimi, Daneshname Fiqh Pezeshki, 1395 S, juz. 3, uk. 323.
- ↑ Qasimi, Daneshname Fiqh Pezeshk, 1395 S, juz. 3, uk. 323.
- ↑ Qasimi, Daneshname Fiqh Pezeshk, 1395 S, juz. 3, uk. 323.
- ↑ Tizama Muhaqiq Hilli, Sharay' al-Islam, 1408 AH, juz. 4, uk. 180.
- ↑ Khodayar, Saadi, «Istanad Be Qaideh Idhin Baraye Mashruiyat Atanazy Dotalaban Faal» uk. 36.
- ↑ Tizama Makarim Shirazi, Istifta'at Jadid, 1427 AH, juz. 1, uk. 479-480; Khui Tabrizi, Ahkam Jamii Masail Pezeshki, 1432 AH, uk. 280; Khui, Fiqh al-Aadhar al-Sharia wa al-Masal al-Tibiya, 1422 AH, uk. 198.
- ↑ Muntadhiri, Ahkam Pezeshki, 1381 S, uk. 122; Fadhil Lankarani, Ahkam Bimaran wa Pezeshkan, 1427 AH, uk. 152; Makarim Shirazi, Istiftaat Jadid, 1427 AH, juz. 1, uk. 479; Makarim Shirazi, Ahkam Pezeshki, 1429 AH, uk. 116; Khui na Tabrizi, Ahkam Jamii Masail Pezeshki, 1432 AH, uk. 280-281; Safi Golpayegani, Istiftaat Pezeshki, 1395 AH, uk. 100; Alawi Gorgani, Istiftaat Pezeshki, 1396 S, uk. 40; Qasimi, Daneshname Fiqh Pezeshki, 1395 S, juz. 3, uk. 305.
- ↑ Fadhil Lankarani, Ahkam Bimaran wa Pezeshkan, 1427 AH, uk. 152; Makarim Shirazi, Istiftaat Jadid, 1427 AH, juz. 1, uk. 479; Muntadhiri, Ahkam Pezeshki, 1381 S, uk. 122.
- ↑ Safi Golpayegani, Istiftaat Pezeshki, 1395 AH, uk. 100; Makarim Shirazi, Istiftaat Jadid, 1427 AH, juz. 1, uk. 479; Muntadhiri, Ahkam Pezeshki, 1381 S, uk. 122.
- ↑ Tizama Khui, Fiqh al-Aa'dhar al-Shari'a wa al-Masa'il al-Tibbiyah, 1422 AH, uk. 198; Khui na Tabrizi, Ahkam Jamii Masail Pezeshki, 1432 AH, uk. 281.
- ↑ Tizama Muntadhiri, Ahkam Pezeshki, 1381 S, uk. 123; Qasimi, Daneshname Fiqh Pezeshki, 1395 S, juz. 3, uk. 303.
- ↑ Safi Golpayegani, Istiftaat Pezeshki, 1395 S, uk. 100; Ansari Qomi, «Qatl Az Rouye Tarahum», uk. 138.
- ↑ Sabzevari, Mahdhab Al-Ahkam, Dar Al-Tafsir, juz. 28, uk. 199; Imamu Khomeini, Tahrir al-Wasilah, 1434 AH, juz. 2, uk. 489; Rouhani, Fiqh al-Sadiq, juz. 26, uk. 34.
- ↑ Khui, Mabani Takmulat al-Manahij, Muasasat Ihyai Athar al-Imamu al-Khui, juz. 42, uk. 18; Tabrizi, Tanqih Mabaani al-Ahkam, 1429 AH, uk. 47-48; Subhani, Ahkam al-Qisas Fi al-Shari al-Islamiyah Bil Gharaa, uk. 93.
- ↑ Khui, Mabani Takmulat al-Manahij, Muasasat Ihyai Athar al-Imamu al-Khui, juz. 42, uk. 18; Tabrizi, Tanqih Mabaani al-Ahkam, 1429 AH, uk. 47-48; Subhani, Ahkam al-Qisas Fi al-Shari al-Islamiyah Bil Gharaa, uk. 93.
- ↑ Tizama; Allamah Hilli, Tahrir al-Ahkam, juz. 5, uk. 551; Najafi, Jawahir al-Kalam, juz. 43, uk. 153.
- ↑ Ansari Qomi, «Qatl Az Rouye Tarahum», uk. 141
Vyanzo
- Imamu Khomeini, Sayyid Ruhullah, Tahrir al-Wasilah, Tehran, Markaz Tandhim wa Nashri Athar Imamu Khomeini, 1434.
- Ansari, Muhammad Ridha, «Qatl Az Rouye Tarahum», Dar Majaleh Fiqh Ahlul-Bayt (a.s), Sh.43, Payiz 1384S.
- Anwari, Hassan. Farhang Rouze Sokhan, Tehran, Sokhan, Chapa ya 24, 1383 S.
- Fadhil Lankarani, Muhammad, Ahkam Bimarane wa Atibba', Qom, Markaz Fiqhi A'imeh At-har (a.s), Chapa ya Kwanza, 1427 AH.
- Imam Khomeini, Sayid Ruhullah. Tahrir al-Wasilah. Tehran, Markaz Tanzhim wa Nashr Athar Imam Khomeini, 1434 AH.
- Khu'i, Sayyid Abu al-Qasim, Fiqh al-As'dhar al-Shar'iyyah wa Masail al-Tibbiyyah, Qom: Dar al-Sayyidah al-Shahidah, 1422 AH.
- Khu'i, Sayyid Abu al-Qasim, Mabani Takmilah al-Minhaj, Qom, Muassasah Ihya' Athar al-Imam Khu'i, Bi-ta.
- Khu'i, Sayyid Abu al-Qasim; Tabrizi, Mirza Jawad, Ahkam Jamii Masail Tibby, Qom, Dar al-Sayyidah al-Shahidah, Chapa ya Kwanza, 1432 AH.
- Khudayar, Hussein wa Hussein-Ali Sa'di, «Istinad be Qaideh Idhin Baraye Mashru'iyyat Atanazy Dotalabaneh fa'al», Fiqh Pezeshki, Shomareh 5-6, 1390 S.
- Makarim Shirazi, Nashir, Ahkam Tibbiyyah, Qom, Madrase Imamu Ali bin Abi Talib (a.s), 1429H.
- Makarim Shirazi, Nashir, Istifta'at Jadid, Qom, Madrase Imamu Ali bin Abi Talib (a.s), Chapa ya Pili, 1427H.
- Muhaqqiq Hilli, Ja'far bin Hasan, Sharai' al-Islam, Qom, Muasase Ismailiyan, Chapa ya Pili, 1408 AH.
- Muntadhiri, Hussein-Ali, Ahkam Tibbiyyah, Tehran, Nashr Sayeh, 1381 S.
- Murtadhawi, Sayyid Muhsin, Qatl Az Rouye Tarahum (Eutanasia) Dar Ayneh Fiqh, Qom, Muassase Imamu Khomeini, 1395 S.
- Najafi, Muhammad Hassan, Jawahir al-Kalam, Beirut, Dar Ihya' al-Turath al-Arabi, Chapa ya 8, 1362 S.
- Qasimi, Muhammad Ali, Daneshnameh Fiqh Tibbi, Qom, Markaz Fiqhi A'imah At-har (a.s), 1395 S.
- Rouhani, Sayyid Muhammad Sadiq, Fiqh al-Sadiq, Qom, Intisharat al-Ijtihad, Bi-ta.
- Sabzewari, Sayyid Abdul-A'la. Mahdhab al-Ahkam, Qom, Dar al-Tafsir, Bi-ta.
- Sadiqi, Muhammad Hadi, «Barresi Fiqhi wa Huquqi Atanazy», Mutala'at Huquqi, Shomareh 2, Shahrivar 1394 S.
- Safi Golpaygani, Lutfullah, Istifta'at Pezeshki, Qom, Daftar Tandhim wa Nashr Athar Ayatullah Safi Gulpaygani, 1395 S.
- Alawi Gurgani, Sayyid Muhammad Ali, Istifta'at Pezeshkan, Qom, Faqih Ahlul-Bayt (a.s), 1396 S.
- Allamah Hilli, Hassan bin Yusuf, Tahrir al-Ahkam, Qom, Muassase Imamu Sadiq (a.s), 142 H.
- Subhani, Ja'far, Ahkam al-Qisas fi al-Shariah al-Islamiyyah al-Gharra', Qom, Muassase Imamu Sadiq (a.s), Bi-ta.
- Tabrizi, Mirza-Jawad, Tanqih Mabani al-Ahkam (Qisas Shara'i al-Islam), Qom, Dar al-Sayyidah al-Shahidah, Chapa ya Tatu, 1429 AH.
- YazdaniFur, Saliheh, Atanazy Az Mandhur Fiqh wa Huquq, Qom, Daftar Nashr Ma'arif, 1393 S.
- «Ahkam Atanazy (Qatl Az Rouye Tarhum)», Paygah I'tilaf-Risani Daftar Maqam A'la Rahbari, Tarikh Bazard: 30 Mehr 1401 S.