Malkia wa Sheba

Kutoka wikishia

Malkia wa Sheba (Kiarabu: ملكة سبأ) ni mtawala pekee wa kike ambaye ametajwa katika Qur’an na katika vitabu viwili vya maagano mawili. Jina la Malkia wa Sheba ni Bilqis. Yeye alikuwa msimamizi wa ufalme wa eneo la Sheba (Yemen ya leo), hapo awali alikuwa mwabudu jua; lakini baada ya kukutana na Nabii Suleiman, aliamini na akawa mwana tawhidi. Leo, baadhi ya watafiti wanatumia utendaji chanya wa Qur’an kuhusiana na uongozi wa Malkia wa Sheba kama hoja kuhusu nafasi na uwepo hai wa wanawake katika jamii.

Kisa cha kufahamu Nabii Suleiman juu ya watu wa Sheba na malkia wao, kuhamishwa kwa kiti cha enzi cha Malkia wa Sheba kwa mtukufu Nabii Suleiman chini ya muda wa kupepesa kwa jicho, na uwepo wa Malkia wa Sheba kwenye kasri yake ni miongoni mwa visa na simulizi za Qur’an. Taarifa ya kukutana kwa Malkia wa Sheba na Suleiman katika Quran na Agano la Kale zinashirikiana katika baadhi ya matukio; lakini kwa mujibu wa watafiti wa Kiislamu, kuna tofauti muhimu kati ya ripoti hizi mbili, muhimu zaidi ni kwamba ripoti ya Qur'an ina mwelekeo wa mwongozo.

Watafiti wanasema kwamba kisa cha Malkia wa Sheba kimefafanuliwa katika vyanzo vya Kiislamu, kutegemea vyanzo vya Israiliyat.

Katika fasihi ya Kiarabu na Kiajemi, kicha cha Malkia wa Sheba kimeashiriwa sana. Katika mashairi, Malkia wa Sheba anatajwa kuwa nembo ya hekima, akili na utajiri. Vitabu mbalimbali vimeandikwa juu ya mada ya Malkia wa Sheba, miongoni mwao ni Al-Malikat Bilqis; Al-Tarikh, Al-Asturah, wal-Ramz kilichoandikwa na Bilqis Ebrahim Al-Hadharani.

Umuhimu

Malkia wa Sheba alikuwa mfalme wa eneo la Sheba, na kisa cha kukutana kwake na Nabii Suleiman kimetajwa katika Qur’an, katika Surat Naml [1] na pia katika Biblia Takatifu [2] Malkia wa Sheba ametajwa kuwa mtawala pekee wa kike mwenye uwezo maalumu aliyetajwa ndani ya Qur'an. [3] Anahesabiwa kuwa mmoja wa wanawake wenye hekima. [4] Kulingana na kisa cha Malkia wa Sheba katika Qur'an, kumeandikwa makala kwa ajili ya kuchunguza mtazamo wa Qur'an kuhusu uongozi na usimamizi wa wanawake na kuthibitisha nafasi na uwepo hai wa wanawake katika jamii. [5] Inasemekana kwamba wakati wa kuandikwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baadhi ya wajumbe walitumia kama hoja kisa cha Malkia wa Sheba kwenye Qur'ani ili kueleza nafasi ya uongozi wa wanawake. [6] Kulingana na utafiti, kisa cha Malkia wa Sheba kimefafanuliwa na na kubainishwa kwa mapana na marefu katika vyanzo vya Kiislamu na baadhi ya nukta zake zimetajwa kuwa zimechukuliwa kutoka Israiliyat (hadithi za kutunga). [7]

Jina, nasaba na utawala wa Malkia wa Sheba

Jina la Malkia wa Sheba halijatajwa katika Qur’ani na katika agano la kale; [8] lakini akthari ya wafasiri na wanahistoria wamesema kuwa, jina lake ni Bilqis. [9] Katika hadithi mbalimbali zilizonukuliwa na Waislamu wa Kishia pia jina hili hili limekuja. [10] Hata hivyo, katika vyanzo vingine, majina mengine yamesajiliwa na kutajwa kuwa ni ya Malkia wa Sheba, kama vile Yalmaqah. [11] Wanasema kwamba Malkia wa Sheba alizaliwa katika eneo la Marib. [12] Majina mbalimbali kama vile Sharh [13] na Haddad bin Sharahil yametajwa kuwa ni ya baba yake. [14] Katika baadhi ya vyanzo, inasemekana kwamba alikuwa ni dhuria wa Sam bin Nuh. [15] Pia inasemekana kwamba mama yake alitokana na majini; hata hivyo mtazamo huo umekataliwa. [17]

Bilqis ametambulishwa kuwa anatokana na kabila la Himyar [18] na ikasemekana kwamba alikuwa na serikali yenye nguvu na katika ardhi ya Sheba (Yemen ya leo), [20] na mji mkuu wa serikali yake ulikuwa Marib. [21] Kwa mujibu wa ripoti ya Ibn Asakir, msomi wa elimu ya hadithi wa karne ya 6 Hijria ni kwamba, kabla Malkia wa Sheba kukutana na Nabii Suleiman, alitawala Yemen kwa miaka tisa na baada ya hapo kwa miaka minne kwa niaba yake. [22] Bila shaka, miaka mingine imetajwa kwa muda wa utawala wake. [23] Kwa mujibu wa ripoti na nukuu ya Abul-Futuh al-Razi, mwandishi wa kitabu cha Rawdhat al-Jinan ni kwamba, Malkia wa Sheba alijenga Bwawa la Ari na baadaye likasambaratika katika mafururiko ya Arim. [24] Kuna watu wengine pia waliotajwa kuwa ndio waliojenga bwawa hilo. [25]

Baadhi ya waandishi, kwa kuzingatia ukweli kwamba Malkia wa Sheba alikuwa katika zama moja na Nabii Sulemani, wameutambua utawala wa Bilqis kwamba, ulikuwa katikati ya karne ya 10 Miladia. [26] Ni kwa msingi huo ndio maana, shaka juu ya kuwepo kwa Malkia wa Sheba kutokana na kutokuwepo kwa jina la mfalme yeyote wa kike katika maandishi yaliyogunduliwa Yemen si sahihi; kwa sababu maandishi haya yanahusiana na karne ya 8 Miladia. [27] Kulingana na baadhi ya watafiti, katika umbali wa kilomita 120 mashariki mwa Sana'a, kuna mabaki ya nguzo za Jumba la ufalme la Bilqis. [28] Jawad Ali, mtafiti wa masuala ya historia wa karne ya 14, ameandika kwamba Wahabeshi wwanajitambua kuwa, wanatokana na kizazi cha Bilqis Malkia wa Sheba. [29]

Kumuamini Nabii Suleimani na kuolewa naye

Kulingana na Aya za Qur'an, Malkia wa Sheba mwanzoni alikuwa akiabudu jua, [30] lakini baada ya kukutana na Suleiman, alimwamini Mwenyezi Mungu. [31] Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo vya tafsiri, Bilqis alifunga ndoa na Nabii Suleiman. [32] Kwa mujibu wa kile kilichokuja katika Dairat al-Maarif (Ensaiklopidia) ya Kifarsi, imenukuliwa kutoka katika baadhi ya vyanzo vya Mayahudi kwamba, Nabii Suleiman na Bilqis walifanikiwa kuzaa mtoto aliyejulikana kwa jina la Nebuchadnezzar; [33] lakini kwa mujibu wa baadhi Bilqis aliolewa na mtu mwingine asiyekuwa Suleiman [34] na kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, hakuolewa kamwe. [35]

Riporti ya Qur’an na maagano mawili kuhusu kukutana Suleiman na Malkia wa Sheba

Qur’ani imesimulia kisa cha kukutana kwa Nabiii Suleiman na Balqis. [36] Hadhrat Suleiman alifahamishwa na ndege aitwaye Hud Hud kuhusu ardhi iliyokuwa inatawaliwa na mwanamke ambaye alikuwa na nguvu, ambaye aliabudu jua pamoja na watu wake. [37] Suleiman alimwandikia barua Malkia wa Sheba na kumwalika. [38] Kwa kujibu barua hiyo, malkia alimtumia zawadi Suleiman ili kuzuia ufisadi na kuua watu. Lakini Suleiman hakukubali zawadi hiyo. [39] Malkia alikwenda kwake kuzungumza na Suleiman, na Hadhrat Suleiman aliwasilisha kiti cha enzi cha malkia katika muda wa chini ya kupepesa macho, kupitia kwa mtu ambaye "alijua sehemu ya kitabu. Alifanya hivyo kabla ya kuwasili kwa malkia, ". [40] Malkia alikuja katika makao ya Sulemani na kumwamini Mungu. [41] Inasemekana kwamba kiti chake cha enzi kilikuwa cha utukufu sana na kikubwa na kilikuwa na vito vingi. [42]

Kulingana na ripoti ya Agano la Kale, Malkia wa Sheba, ambaye alikuwa amesikia mengi kuhusu Sulemani, alikuja kwake na kuuliza maswali na kusikia majibu ya kufaa kutoka kwa Sulemani. [43] Kadhalika mbali na hilo, kuona kasri zuri, vyakula vya kifalme, huduma mbalimbali, na utumishi wenye nidhamu watumishi na wanyweshaji, na dhabihu zilizotolewa katika nyumba ya Mungu, zikamshtua.” [44] Mwishowe, Malkia wa Sheba akamsifu Suleiman na Mungu wake. Pande zote mbili zilipeana zawadi za thamani sana na Malkia wa Sheba akarudi katika nchi yake. [46] Malkia wa Sheba pia ameashiriwa katika sehemu za Agano Jipya. [47]

Kwa mujibu wa utafiti, ripoti ya Qur'an na ripoti ya Agano la Kale kuna baadhi ya matukio yanashirikiana na kufanana; lakini pia kuna tofauti muhimu. [48] Miongoni mwa tofauti hizi, ni ripoti ya Qur’an kuwa na maelezo mapana na ya kina zaidi ikilinganishwa na ripoti ya Agano la Kale na utendaji wa Qur’an kuwa ni wa kimuongozo. [49] Pia, katika Qur'ani Tukufu mahali walipokutana Nabii Suleiman na Bilqis hapajatajwa. [50] Lakini katika Agano la Kale, pametajwa kuwa ni Baytul Muqaddas (Jerusalemu). [51] pamoja na hayo, kwa mujibu wa kile kilichokuja katika vyanzo vya Kiislamu ni kwamba, wawili hawa hawakukutana Baytul-Muqaddas (Jerusalem) bali walikutana katika safari ya Hadhrat Suleiman huko Makka. [52]

Kuaga dunia na mahali alipozikwa

Kulingana na baadhi ya vyanzo vya kihistoria, Bilqis alikufa miaka saba na miezi michache baada ya kukutana na Suleiman na akazikwa katika mji wa Tadmur (Palmyra) huko Syria. [53] Hakuna mtu aliyekuwa na taarifa kuhusiana na mahali lilipo kaburi lake mpaka katika zama za utawala wa Walid bin Abdul-Malik ambaye alidhihirisha na kufichua kaburi lake na kwa amri yake likajengewa. [54]

Kuakisiwa kisa cha Malkia wa Sheba katika fasihi

Kisa cha Malkia wa Sheba kimeakisiwa pakubwa katika fasihi za lugha ya Kiarabu na Kifarsi. [55] Katika mashairi Bilqis anatajwa kuwa nembo ya utajiri, hekima na akili. [56]

Bibliografia

Kumeandikwa vitabu mbalimbali kuhusiana na kisa cha Malkia wa Sheba na baadhi yavyo ni:

  • Al-Malikat Bilqis; Al-Tarikh, Al-Asturah, wal-Ramz kilichoandikwa na Bilqis Ebrahim Al-Hadharani. [59]
  • Bilqis; Imraat al-Alghaz Washaitanat al-Jins; mwabndishi Ziyad Muna. Ndani ya kitabu hiki mwandishi anabainisha na kueleza shakhsia ya Malkia wa Sheba katika historia, Uislamu, Ukristo na Uyahudi. [61] Kitabu hiki kilichapishwa na Taasisi ya Uchapishaji na Usambazaji ya Riyadh al-Raisi ya Beirut mwaka 1998. [62]

Vyanzo

  • Ayāzī, Muḥammad ʿAlī. Dāstān-i Sulaymān wa belqis wa istinād-i bi ān dar jahād-i ibtidāyī. Pazhūhishhā-yi Qurāni Magazine. Year 19, no 1, Spring 1392 Sh.
  • Ibn Ḥabīb Baghdādī, Muḥammad b. Ḥabīb. Al-Muḥabbar. Edited by Shititer Ilza Likhtin. Beirut: Dār al-Āfāq al-Jadīda, [n.d].
  • Ibn Ṣāʿid Andulusī, Ṣāʿid b. Aḥmad. Al-Taʿrīf bi ṭabaqāt al-umam. Edited by Ghulāmriḍā Jamshīdnizhād. Tehran: Markaz-i Pazhūhishī-yi Mīrāth-i Maktūb, 1376 Sh.
  • Ibn ʿAsākir, ʿAlī b. al-Ḥasan. Tārīkh madīnat Dimashq. Beirut: Dār al-Fikr, 1415 AH.
  • Ibn Kalbī, Hisham b. Muḥammad. Nasab al-muʿid wa Yaman al-kabīr. Edited by Ḥasan Nājī. Lebanon: ʿĀlam al-Kutub, 1425 AH.
  • Khaṭīb ʿAmrī, Yāsīn. Al-Rawḍat al-fīḥāʾ fī tawārīkh al-nisāʾ. Edited by ʿAbd al-Ḥakīm Ḥisām Riyāḍ. Lebanon: Muʾassisat al-Kutub al-Thiqāfīyya, 1420 AH.
  • Nūwī, Yaḥyā b. Sharaf. Tahdhīb al-asmāʾ wa al-lughāt. Edited by Ghazbān ʿĀmir; Murshid ʿĀdil. Damascus: Dār al-Risāla al-ʿĀlamīyya, 1430 AH.
  • Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Edited by Ṭayyib Mūsawī Jazāʾrī. Qom: Dār al-Kitāb, 1404 AH.
  • Riʿāīyī, Fahīma. Gulāb-bakhsh Maryam. Belqis ishāratī bar zan az dīdgāh-i Qurān. Ḥikmat-i Sīnawī Magazine. No 4, Spring 1377 Sh.
  • Rūḥānīmanish, Maʿṣūma. Olgūhā-yi mudīrīyat-i zanān dar Qurān. Faṣlnāma Taḥqīqāt-i Āmūzishī. Year 5, No 3, Spring 1393 Sh.
  • ʿUtibī Ṣaḥārī, Salma b. Muslim. Al-Ansāb.Edited by Muḥammad Iḥsān. Oman: Salṭanat Oman: Wizārat al-Turāth al-Qawmī wa al-Thiqāfa, 1427 AH.