Kutothamini Wazazi

Kutoka wikishia

Kutothamini wazazi (Kiarabu: عقوق الوالدين) ni katika madhambi makubwa na ni katika tabia na maadili mabaya kabisa ambayo yamekemewa na kukatazwa katika mafundisho ya Uislamu. Hali inaelezwa kuwa, kuwaudhi baba na mama au mmoja wao kwa ulimi na kauli au kwa vitendo. Kwa maana kwamba, kuwatolea kauli chafu na mbaya, au kuwafanyia kitendo kibaya. Katika hadithi imekuja kuwa, kuasi amri zao, kuwatazama kwa hasira, kutowashimu, kuwaambia ah, (kuonyesha kukereka na kauli au agizo lao) na kuwakemea kwamba, ni mifano kuwaudhi baba na mama. Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu Mwenyezi Mungu amekataza wazazi kujibiwa hata kwa kauli ya ah’ ambayo mtoto anaonyesha kutoridhishwa na alichoambiwa na mmoja wa wazazi wake. Inaelezwa kuwa, lau kungekuwa na kitu cha chini zaidi ya ah, basi Mwenyezi Mungu angekataza kufanyiwa au kuambiwa wazazi. Miongoni mwa matokeo mabaya ya kuwaudhi wazazi ambayo yameelezwa na kubainishwa katika riwaya na hadithi mbalimbali ni mhusika kuharamishiwa pepo, kuingizwa mtoni, kutokubaliwa Swala na hata kutojibiwa dua za mtoto mwenye kuwaudhi wazazi wake. Baadhi ya wanazuoni wa elimu ya akhlaqi na maadili wanasema, kupungua umri, kupata maumivu na uchungu shadidi wakati wa kutoka roho ni miongoni mwa athari za hapa duniani za kuwaudhi na kuwakera wazazi.

Maana

Kuwaudhi wazazi maana yake ni mtoto kumfanyia kitendo cha maudhi baba na mama au mmoja wao kwa ulimi na kauli au kwa vitendo. [1] Hata hivyo neno Uquuq katika lugha lina maana ya kukata. Katika hali hii makusudio ya Aaq Walidain itakuwa ni kukata uhusiano na maingiliano nao. [2] Mullah Mahdi Naraqi anasema, Aaq Walidain (kuwaudhi na kukata uhusiano nao) ni aina mbaya kabisa ya kukata uhusiano na ndugu na anaamini kuwa, kila ambacho kina ishara za lawama kuhusu kukata uhusiano na ndugu kina ishara pia katika lawama za kuwaudhi wazazi. Kadhalika anatambua kuwaudhi wazazi kuwa ni katika uchafu wa maadili na tabia mbaya ambayo inahusiana na nguvu ya ghadhabu na matamanio ya kinafsi na chimbuko lake ni chuki, hasira au ubakhili na kupenda dunia. [3]

Mifano

Kuwaudhi wazazi inaelezwa kuwa ni kutowaheshimu na kuwafanyia aina yoyote ile ya maudhi na kuwafanya wasiwe radhi. Katika hadithi imeelezwa kuwa, kuwatazama kwa jicho kali, [4] kukanyaga haki zao, [5] kutowatekelezea matakwa yao, kutotii amri zao na kutowaheshimu [6] ni mifano ya wazi kuwaudhi wazazi wawili. Mullah Ahmad Naraqi amesema: Kila ambacho kinapelekea wazazi kuudhika, kuchukia na kutokuwa radhi kinahesabiwa kuwa ni maudhi dhidi ya wazazi wawili. [7] Katika hadithi iliyopekewa kutoka kwa imam Ja’afar Swadiq (as) inaelezwa kuwa, kuwaambia au kuwajibu wazazi kwa neno ah (kuonyesha kutoridhishwa au kuchoshwa na mambo yao au kukereka) ni mfano mdogo kabisa wa kuwaudhi wazazi wawili ambao umetajwa na kuelezwa kwamba, hakukuwa na kitu kingine kidogo chini ya hapo kwani kama kingekuweko basi Mwenyezi Mungu angekikataza. [8]

Kuwatendea Wema Wazazi

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameikutanisha shukrani ya wazazi wawili na yake na akawajibisha kuwatendea wema na kuwafanyia hisani; sawa na alivyowajibisha kuabudiwa kwake. Aya ya 23 katika Surat al-Israai inasema: Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. Kuanzia hapa ndio mafakihi wamesema kwa kauli moja kwamba kuwaasi wazazi wawili ni katika madhambi makubwa, na kwamba mwenye kuwaasi ni fasiki hauwezi kukubaliwa ushahidi wake. Hadith tukufu inasema: “Hakika mwenye kuwaudhi wazazi wawili hatapata harufu ya pepo”. Makusudio ya kuwatendea wema wazazi wawili ni kuwatii na kuwachukulia upole. Kuna kisa cha mwanamke mmoja aliyembeba baba yake mgongoni kutoka Yemen mpaka Makka. Akatufu naye katika Al-Ka’aba. Mtu mmoja akamwambia “Mwenyezi Mungu akulipe heri, umetekeleza haki yake.” Akasema: “Hapana sijatekeleza; yeye alikuwa akinibeba huku akinitakia uhai (niishi) na mimi hivi sasa ninambeba huku nikimtakia mauti (afe).”

Matokeo ya Kuwaudhi Wazazi

Kuwaudhi wazazi ni katika katika tabia mbaya za kimaadili na imeelezwa bayana [9] katika hadithi kwamba, ni miongoni mwa madhambi makubwa na kuna matokeo ambayo yametajwa kwa mwenye kutenda jambo hili baya la kimaadili:

  • Kuharamishiwa pepo na kutopata harufu yake; [10] na kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imamu Ja’afar Swadiq (as) ni kwamba: Siku ya Kiyama pazia miongoni mwa mapazia ya peponi litafunguliwa na kisha harufu yake kumfikia kila kiumbe hata aliyeko umbali wa miaka 500, isipokuwa watu ambao walikuwa wakiwaudhi wazazi. [11] Kadhalika imekuja katika hadithi mbalimbali zikionyesha kwamba, mwenye kuwaudhi wazazi hataingia peponi. [12]
  • Kuingia motoni. [13]
  • Kutokubaliwa Swala; imekuja katika hadithi ya kwamba mtu ambaye anamuangalia mama au baba yake kwa jicho la dhalimu wake (kwamba anamdhulumu), Mwenyezi Mungu hakubali Swala zake. [14]
  • Kutotakabaliwa dua. [15]
  • Adhabu duniani; imekuja katika hadithi na riwaya mbalimbali kutoka kwa Bwana Mtume (saww) ambazo zimelitambua suala la kuwafanyia maudhi wazazi kwamba, ni katika madhambi ambayo mtu adhabu yake ataishuhudia hapa hapa duniani. [16] Mullah Ahmad Naraqi anasema: Tajiriba na uzoefu umethibitisha kwamba, kuwafanyia maudhi wazazi kunasababisha kupungua umri, machungu maishani, umasikini, kutokuwa na utulivu, kutokwa na roho kwa shida na kupata maumivu wakati wa kukata roho. [17]
  • Adhabu ya kaburi; kwa mujibu wa Mullla Mahdi Naraqi ni kuwa, mtu ambaye mama yake hayuko radhi naye atakabiliwa na ugumu wakati wa kuaga dunia na adhabu kali kaburini. [18]

Kuwaudhi Wazazi Baada ya Kifo Chao

Kwa mujibu wa hadithi ni kwamba, maudhui kwa wazazi ni suala ambalo haliishi tu katika kipindi cha uhai wao, bali hata baada ya kufariki kwao. Kama ambavyo kuwatendea wema na hisani hakuishi tu katika zama za uhai wao. Inawezekana mtu akawa mwema na mwema huruma, huba na mapenzi kwa wazazi wake wakati wa uhai wao, lakini baada ya baba na mama yake kufariki dunia akawafanyia maudhi. Mifano ya hilo ni kama kutowalipia deni au kutowaombea maghufira. Kadhalika yumkini mtoto akawafanyia maudhi wazazi wake duniani, lakini baada ya baada ya kifo chao asifanye hivyo. [19] Mullah Ahmad Naraqi anakumbusha taabu na usumbufu waliopata wazazi kama vile, kuhangaika na kusumbukia watoto, wakati mwingine kushindwa kulala ili kumshughulikia mtoto wao, kuwaonyesha huba na mapenzi, kuwahudumia watoto wao, kujinyima kwa ajili ya watoto wao na kujibiwa dua mbaya ya baba na mama kwa mtoto kama moja ya njia za kuondokana na suala la kuwaudhi wazazi.[20]

Rejea

Vyanzo