Nenda kwa yaliyomo

Herufi za mkato

Kutoka wikishia

Herufi za Mkato (Kiarabu: الحروف المقطعة) ni herufi moja au kadhaa ambazo zimeanza katika Sura 29 za Qur'ani Tukufu baada ya Bismillahi al-Rahmani al-Rahim. Herufi hizi husomwa moja moja na kwa kutenganishwa; kwa mfano «الم» iliyokuja mwanzonii mwa Surat al-Baqarah inasomwa: «alif, laam, mim».

Ukiondoa Surat al-Baqarah na Aal Imran, Sura nyingine zote zilizoanza na herufi za mkato ni Makki (zimetaremshwa Makka). Baadhi ya Sura za Qur’ani ambazo zimeanza na herufi za mkato ni: A'raf, Yunus, Hud, Maryam, Taha, Qasas, Ghafir na Qalam.

Wanazuoni na watafiti wa masuala ya Qur'ani, wamebainisha maana na tafsiri tofauti za herufi za mkato na kumeandikwa vitabu vya kujitegemea kuhusiana na maudhui hii. Allama Tabatabai anaamini kwamba, herufi za mkato, ni alama ya siri baina ya Mwenyezi Mungu na Mtume (s.a.w.w) na hakuna anayefahamu maana zake isipokuwa Mtume (s.a.w.w). Tafsiri hii kuhusiana na maana ya herufi za mkato, imekuja pia katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s). Baadhi ya maana zingine zilizotajwa za herufii za mkato ni: Ishara za muujiza wa Qur'ani Tukufu, ni jina kubwa na tukufu zaidi Mwenyezi Mungu.

Utambulisho

Herufi za mkato ni herufi moja au kadhaa ambazo zimekuja mwanzo katika Sura sura 29 za Qur'ani Tukufu baada ya Bismillah husomwa moja moja na kwa kutenganishwa; kwa mfano الم iliyokuja mwanzoni mwa Surat al-Baqarah inasomwa: "alif, laam, miim", Yaa Sin (یس), Swaad (ص). Majina mengine ya herufi hizi ni: Muqattaat [1] na Fawatih al-Suwar (vifungua sura). [2]

Sura ambazo zinaanza na herufi hizi zinajulikana kwa jina la Makki (zimeshuka Makka) isipokuwa Sura mbili za al-Baqara na Al-Imran [3] ambazo zimeshuka katika miaka ya kuanza kipindi cha Madina na zinajulikana kwa jina la Madani (yaani zilizoshuka Madina). [4] Kwa mujibu wa hesabu ya Kufi, ambayo ilinukuliwa kutoka kwa Ali bin Abi Talib (a.s), [5] herufi za mkato zilizokuja katika baadhi ya sura, ikiwa ni pamoja na mwanzo wa Surat Al-Baqarah [6], Al-Imran [7] na Araaf [8], ni Aya inayojitegemea na katika baadhi nyingine, ikiwa ni pamoja na Surat Yunus [9] na Hud [10], ni sehemu ya Aya.

Herufi za Mkato katika Qur'ani
Nambari Jina la Sura Herufi za Mkato Nambari Jina la Sura Herufi za Mkato Nambari Jina la Sura Herufi za Mkato
1 al-Baqara Alif, Lam, Mim 11 Taha Ta Ha! 21 Ghafir Ha, Mim
2 Al Imran Alif, Lam, Mim 12 al-Shu'ara' Ta, Sin, Mim 22 Fussilat Ha, Mim
3 al-A'raf Alif, Lam, Mim, Swad 13 al-Naml Ta, Sin 23 Shura Ha, Mim, ‘Ayn, Sin, Qaf
4 Yunus Alif, Lam, Ra 14 al-Qasas Ta, Sin, Mim 24 al-Zukhruf Ha, Mim
5 Hud Alif, Lam, Ra 15 al-'Ankabut Alif, Lam, Mim 25 al-Dukhan Ha, Mim
6 Yusuf Alif, Lam, Ra 16 al-Rum Alif, Lam, Mim 26 al-Jathiya Ha, Mim
7 al-Ra'd Alif, Lam, Mim, Ra 17 Luqman Alif, Lam, Mim 27 al-Ahqaf Ha, Mim
8 Ibrahim Alif, Lam, Ra 18 al-Sajda Alif, Lam, Mim 28 Qaf Qaf
9 al-Hijr Alif, Lam, Ra 19 Yasin Ya Sin! 29 al-Qalam Nun
10 Maryam Kaf, Ha, Ya, ‘Ayn, Swad 20 Swad Swad

Maana na Tafsiri Tofauti

Wanachuoni na watafitii wa Qur’ani wameeleza maana na tafsiri tofauti za herufi za mkato katika kazi zao, na kwa kuongezea ni kuwa, kuna vitabu vinavyojitegemea vimeandikwa kuhusiana na herufi za mkato. Miongoni mwa vitabu hivyo ni: Al-Huruf al-Muqattaa fil Qur'ani, kilichoandikwa na Abdul-Jabbar Sharara, Awail al-Suwar fil Qur'ani al-Karim, mwandishi Ali Nasuh Tahir, I'jaz Qur'an: Uchambuzi wa takwimu za herufi za mkato, mwandishi: Rashad Khalifa. Pamoja na hayo, kundi la wasomi wa Kiislamu likitegemea baadhi ya hadithi ziilizoko katika athari na vitabu vya Sheikh Tusi, Fakhrurazi na Suyuti [11] linaamini kuwa, herufu hizi ni miongoni mwa siri ambazo azijuaye ni Mwenyezi Mungu tu na matokeo yake wamekataa kutoa mtazamo na maoni yao kuhusiana hili. [12]

Siri baina ya Mwenyezi Mungu na Mtume, Aya za mutashabihat za Qur'ani, majina ya sura, herufi za kiapo, ishara za Qur'ani kuwa muujiza, jina kubwa na tukufu (a'dham) la Mwenyezi Mungu na kutumia kama wenzo wa kumfanya mtu awe makini ni miongoni mwa maana muhimu zaidi zilizotajwa kuhusiana na herufi za mkato. Ibn Hajr al-Asqalani anaaminii kuwa, kutokana na kuwa, hakuna ripoti ya kuaminika kuhusiana na swali la sahaba kwa Mtume kuhusu herufi za mkato, inawezekana kufikia natija hii kwamba, makusudio ya herufi za mkato na maana yake lilikuwa jambo linalofahamika baina ya masahaba na halikuwa jambo la kukanushika. Yaani hakikuwa kitu ambacho hakieleweki baina yao la sivyo kungepatikana maswali kuhusu hili. [13] Pamoja na hayo, Allama Tabatabai anaamini kuwa, maana zilizotajwa kuhusiana na herufi za mkato hazina itibari; kwa sababu hazijavuta matarajio na hakuna hoja ya kuthibitisha usahihi wake. [14]

  • Siri baina ya Mwenyezi Mungu na Mtume: Baadhi ya wanazuoni akiwemo Allama Tabatabai na Sayyid Mahmoud Taleghani, wanaona kuwa, herufi za mkato ni siri baina ya Mwenyezi Mungu na Mtume ambapo Mwenyezi Mungu hajataka mtu mwingine afahamu ghairi ya Mtume. [15] Mtazamo huu umenasibishwa pia na Imamu Ja’far Swadiq (a.s). [16]
Imamu Khomeini amesema

Kuhusiana na herufi za mkato zilizokuja mwanzoni mwa (baadhi ya) sura za Qur’ani kwamba, kuna hitilafu kubwa, na kile ambacho kinaonekana kuwa sahihi zaidi ni kama siri baina ya mpendwa na mpenda na hakuna mwenye elimu juu ya hilo. Sharh Chehel Hadith (Ufafanuzi wa Hadithi Arobaini), uk 351.

  • Aya za Mutashabihat za Qur’ani Tukufu: Fakhrurazi na Suyuti ambao ni miongoni mwa wanazuoni wa Kisuni, wanaamini kwamnba, herufi za mkato ni katika mutashabihat za Qur’ani (Aya ambazo kuna uwezekana kuwa na maana kadhaa) na ni Mwenyezi Mungu tu ndiye anayejua maana zake. [17] Baadhi ya hadithi zilizonukuliwa na wapokezi wa hadithi wa Kishia zinaunga mkono mtazamo huu. [18]
  • Majina ya sura: Sheikh Tusi, Tabarsi na Suyuti, ambao ni wafasiri wa Qur‘ani wa Kishia na Kisuni wanaamini kuwa, herufi za mkato ni majina ya sura na anuani ya kila sura ndio ile herufi ya mkato ambayo inaanza nayo. [19] Sheikh Tusi na Tabarsi, wameitambua kauli hii kuwa mtazamo bora zaidi katika kufasiri maana ya herufi za mkato. [20] Kauli iliyotajwa imenasibishwa na Zayd bin Aslam. [21] Kadhalika Khalil bin Ahmad na Sibaweyh. [22]
  • Herufi za kiapo: Ibn Abbas na Ikrama, wamezitambua herufi za mkato kuwa ni ni herufi za kiapo na wanaamini kwamba, Mwenyezi Mungu ameapa kwa herufi hizi ambazo ni katika majina yake. Suyuti katika kuhalalisha na kuunga mkono nadharia na mtazamo huu ametumia kama hoja hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Ali bin Abi Twalib (a.s) ambaye alisema: «یا کهیعص اغفرلی» “Ewe Kaaf, haa, yaa, ain swaad nighufirie mimi”. [24]
  • Ishara ya muujiza wa Qur’ani: Moja ya nadharia na mtazamo mkongwe na mashuhuri zaidi katika kufasiri na kutoa maana ya herufi za mkato ni hii kwamba, Mwenyezi ameanza na herufi katika sura 29 za Qur’ani ili wazungumzao lugha ya Kiarabu waelewe kwamba, Qur’ani imeundwa kutokana herufi hizo ambazo wanazitumia kuzungumza na kama wanadhani kwamba, Qur’ani sio muujiza basi walete mfano wa Qur’ani kwa kutumia herufi hizo hizo. [25] Mtazamo huu umekuja pia katika baadhi ya maandiko ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ikiwemo tafsiri inayonasibishwa na Imamu Hassan Askary (a.s). [26] Sayyid Qutb, mmoja wa wanazuoni wa Ahlu-Sunna ametosheka tu na kauli hii na kusema kwamba, inastahiki kutajwa. [27]
  • Jina kuu la Mwenyezi Mungu: Ibn Masoud [28] na Ibn Abbas [29], miongoni mwa wafasiri wa Qur’ani mwanzoni mwa Uislamu wamesema kuwa, herufi hizi ni jina kuu la Mwenyezi Mungu. [30] Kadhalika Said bin Jubayr anaamini kwamba, herufi za mkato, ni majina ya Mwenyezi Mungu yaliyoandikwa kwa mkato. [31] Mtazamo unapatikana pia katika nukuu zinazonasibishwa na Maimamu wa Kishia. [32
  • Wenzo wa kuleta umakini: Baadhi wanaamini kwamba, kila herufi miongoni mwa herufi za mkato ni wenzo wa kumfanya mtu awe makini na kuwa tayari kusikiliza kitu fulani kama vile: اَلا، اَما، و هان na kadhalika; kwa msingi huu, kwa kuzingatia kwamba, mushrikina walikuwa wakifanya juhudi za kuipinga na kuikataa Qur'ani na hivyo hawakuwa wakitaka kuisikiliza na wakati Qur’ani ilipokuwa ikisomwa walikuwa wakifanya makelele ili isisikike, [33] Mwenyezi Mungu ameanza maneno yake katika baadhi ya Sura za Qur’ani kwa herufi za mkato ili kuwafanya mushirikina wanyamaze na kuwa na umakini na kuielekea wakiwa na shauku ya kusikiliza. [34] Kwa nini kuhusiana na hili, Mwenyezi Mungu hakutumia nyenzo mashuhuri za kuwafanya watu wanyamaze na kuwa makini kutaka kutegea sikio kitu? Inaeelezwa kuwa, Qur’ani ni maneno ambayo hayafanani na maneno ya mwanadamu; hivyo ni lazima kuanza na nyenzo za kumfanya mtu awe makini ambazo si za kawaida ili maneno mengine yawe yenye balagha na ufasaha zaidi na yenye taathira zaidi. [35]
  • Tafsiri ya idadi: Kundi la wafasiri limezitambua herufi za mkato kuwa siri ziliazoambatana na maana ya kinembo iliyojengeka juu ya msingi wa thamani za idadi za herufi za Kiarabu kama “Adu abi jad au Hisab al-Jumal. [36] Kundi hili ambalo limeathirika na Mayahudi, kwa kufasiri kwa idadi herufi za mkato lilitaka kutabiri wakati wa kuasisiwa tawala na kusambaratika kwake, muda wa kudumu kwake na kuongoza kaumu na makundi na hususan muda wa kudumu na kubakia kwa Umma wa Kiislamu. [37] Ibn Hajr al-Asqalani, akiwa na lengo la kubatilisha tafsiri hii alitegemea mtazamo wa Ibn Abbas na kusema: Ibn Abbas alikataza “Add Abi Jad” na kulihesabu hilo kuwa ni alama na nembo ya uchawi, kwani hilo halina chimbuko lolote la katika sheria za Kiislamu. [38]

Rejea

Vyanzo