Nenda kwa yaliyomo

Hafhaf ibn al-Muhannad ar-Rasibi

Kutoka wikishia

Al-Hafhaf ibn al-Muhannad ar-Rasibi (Kiarabu: هفهاف بن المهند الراسبي) (aliyeuawa shahidi 61 Hijria) ni mingoni mwa Mashia wa Basra na ni katika mashahidi wa Karbala ambaye aliuawa shahidi baada ya Imamu Hussein (a.s). Hafhaf ambaye alikuwa na historia ya kuwa katika safu ya masahaba wa Imam Ali (a.s.) katika vita vya Siffin, aliposikia habari ya Imamu Hussein (a.s) kuanza safari ya kuelekea Iraq, alifunga safari na kuelekea kwake. Lakini alifika Karbala siku ya Ashura, baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (a.s). Alipambana na jeshi la Omar bin Sa'd na akauawa shahidi.

Kwa mujibu wa Mamaqani, mmoja wa wasomi wa elimu ya Rijaal wa Kishia (aliyefariki mwaka 1351 Hijiria) ni kwamba, Hafhaf ibn al-Muhannad alikuwa mmoja wa wapanda farasi shupavu na mahiri wa Basra na mmoja wa Mashia waaminifu. [1] Alikuwa mmoja wa masahaba wa Imamu Ali (a.s) katika vita vya Siffin, na kwa mujibu wa nukuu kutoka kwa Imam Ali (a.s), alikuwa kamanda wa Azdian wa Basra katika vita hivi. [2] Anahesabiwa kuwa mmoja wa masahaba wa Imam Hassan (a.s). Hafhaf katika lugha ina maana ya mtu mwembamba. [4]

Fadhl bin Zubayr Kufi (aliyefariki dunia karne ya 2 Hijiria), Al-Murshid Billah mmoja wa wanazuoni wa Zaydiyya, (aliyeaga duni 479 Hijiria) na Humayd bin Ahmad Muhalli mwandishi wa wasifu wa watu wa Kizaydiyya (aliyefariki 652 Hijria) wameripoti kwamba, baada ya Hafhaf kupata habari kwamba, Imamu Hussein (a.s) ameondoka na kuelekea Iraq aliharakisha kuelekea kwa Imamu huyo; lakini aliwasili katika medani ya vita baada ya kuwa Imam Hussein ameshauawa shahidi. Hivyo aliingia vitani kwa ajili ya kupigana na wanajeshi wa Omar bin Sa'd. Alichomoa upanga wake na akawapigia kelele: “Enyi jeshi lililojizatiti kwa silaha! Mimi ni Hafhaf bin Muhannad! Ninaifuata familia ya Muhammad (s.a.w.w)"! Kisha akaenda kupigana na jeshi la Omar Sa'd na akawauwa baadhi yao na hatimaye wakamuua shahidi. [5]

Katika muendelezo wa riwaya hii, Imam Sajjad (a.s) amenukuliwa katika kumsifu Hafhaf: “Watu hawajamuona mpiganaji mpanda farasi shujaa yeyote kama Hafhaf tangu zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w) baada ya Ali bin Abi Talib (a.s)..." [6] Imeelezwa katika ensaiklopidia ya Imamu Hussein kwamba, jina la Hafhaf limetajwa katika maandishi ya zamani tu katika kitabu Tasmiyat man Qutil ma‘a al-Husayn, kilichoandikwa na Fudhayl bin Zubayr. [7] Jina la Hafhaf halijatajwa katika Ziyarat al-Shuhadaa inayonasibishwa na Imam wa Zama (a.s) [8] na Ziyarat Rajabiyyah ya Imam Hussein (a.s). [9]

Rejea

Vyanzo