Hadithi ya Makarimu al-Akhlaqi
Innamaa bu’ith-tu liutammima makaarima al-akhlaaqi (Kifarsi: انما بعثت لاتمم مکارم الاخلاق) (Hakika mimi nimetumwa kwa ajili ya kukamilisha maadili ya juu ya tabia njema): Ibara hii ni Hadithi itokayo kwa bwana Mtume (s.a.w.w), ambayo inafafanua kuwa; Malengo ya kutumwa kwa bwana Mtume (s.a.w.w), ni kukamilisha tabia njema. Kulingana na Hadithi hii, bwana Mtume (s.a.w.w) amesema ya kwamba: Mimi nimetumwa kwa lengo la kukamilisha tabia njema. Hadithi hii inajulikana kwa jina la «Hadithi ya Makarim al- Akhlaqi». Kwa mujibu wa Hadithi hii, maadili yanachukuliwa kuwa ni miongoni mwa masuala muhimu katika dini ya Kiislamu, na kufundisha maadili mema pamoja na kuyaboresha hadi kufikia kileleni mwake, kunazingatiwa kuwa ndio malengo makuu ya utume wa Mtume (s.a.w.w).
Hadithi hii imenukuliwa katika vyanzo vya Kishia pamoja na Kisunni. Pia kuna Riwaya nyingine kadhaa zenye maudhui sawa na Riwaya hii, ingawa maneno ya ibara zake yana tofauti kwa kiasi fulani na Riwaya hii katika vyanzo hivyo vya Hadithi. Baadhi ya watafiti, kwa kuzingatia wingi wa Riwaya zinazohusiana na maudhui ya Hadithi hii, wamesihisabu Riwaya hizo kuwa ni zenye maudhui sawa na Riwaya hii, kwa kusema kwamba; Riwaya zote hizo ni sisitizo la Riwaya hiyo moja. Kwa hiyo wao wameihisabu Riwaya hii kuwa ni Riwaya mutawatir maanawiy, yaani ni Riwaya iliyopokewa na wapokezi tofauti kwa ibara tofauti, ila zote ni zenye maana moja, hata kama ibara zake ni tofauti.
Inasemekana kuwa; neno Makarimu al-Akhlaqi linatofautiana kimaana na tabia njema za kawaida, na kwamba neno hili lina maana ya maadili yalio bora kuliko hayo yaliozoeleka katika maisha ya kila siku. Katika Hadithi kuna sifa kadhaa zilizo hisabiwa kuwa ni miongoni mwa Makarimu al-Akhlaqi, miongoni mwazo ni: subira, shukrani, uaminifu, kuridhika (kutosheka), ujasiri (ushujaa), kuunga udugu,hayaa pamoja na kuwa na tabia njema.
Hadhi Yake
Hadithi isemayo hii isemayo «إِنَّمَا بُعِثْتُ لِأُتَمِّمَ مَکَارِمَ الْاَخْلَاق» ina maana isemayo kwamba: Kwa hakika mimi nimetumwa ili kukamilisha maadili ya juu ya tabia njema. [1] Hadithi hii inajulikana kama Hadithi ya Makarimu al-Akhlaqi [2] au Hadithi ya Tatmiimu [3] na imepokewa moja kwa moja kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w) [4]. Kwa mujibu wa Hadithi hii; moja ya malengo makuu ya utume wa Mtume (s.a.w.w) ni kukamilisha na kufundisha maadili mema, ili kuyafikisha kileleni mwake [5] na Hadithi hii inaonesha umuhimu na nafasi ya masuala ya maadili katika dini ya Uislamu. [6]
Welewa Tofauti wa Hadithi ya Makarimu al-Akhlaqi
Kumekuwa na tafsiri tofauti kuhusiana na Hadithi ya Makarimu al-Akhlaqi:
Murtadha Mutahhari, mtafiti wa Kiislamu na mwandishi wa Kishia, ameandika akisema kuwa; Hadithi hii inaonyesha kwamba, utume wa Mtume (s.a.w.w), unahusiana na Nyanja za kiroho na kimaadili, una lengo la kuwapa watu malezi bora. Ambapo umekuja kuamsha ns kuhamasisha hisia, na na haukuwa na malengo ya kisayansi, kiufundi, na kadhalika. Na mfumo wake ni tofauti na mfumo wa maadili ya Sokrati (Socrates), ambao unategemea misngi ya kimaadili kupitia misingi ya akili, ambapo huzingatia tu upande wa misingi ya kiakili. Kwa sababu hiyo basi, misingi ya Sokrati (Socrates) ni misingi mikavu isiyo endelevu. [7]
Kulingana na mawazo ya Ibn Arabi, mwanairfani (mwenye itikati za kisufi) na mfasiri wa upande wa Kisunni (aliye ishi baina ya mwaka 560 na 638 Hijiria), ni kwamba; Kila mmoja kati ya mitume, ambaye alikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kupokea fadhila mbali mbali za Mwenye Ezi Mungu, [8] na ambaye ametanguliwa na mitume wengine kabla yake, kiuhalsia, yeye huwa amebeba sifa zote za ukamilifu wa mitume waliomtangulia kabla yake. Hivyo basi, Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) amepata hadhi uhalali wa kuzikweza sifa zote za maadili mema. [9]
Baadhi ya watafiti pia wanaamini kwamba; Lengo la Hadithi ya Makarimu al-Akhlaqi, sio kukamilisha maadili mema tu, [10] kwani pia kuna malengo mengine kadhaa yaliotajwa kuwa ni miongoni mwa malengo ya kutumwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w), ambapo miongoni mwayo ni kama vile; siasa na uongozi wa jamii na kukamilisha hoja mbele ya wanadamu. [11] Kutokana mawazo kadhaa juu ya maana ya Hadithi hii, wanazuoni wametoa tafsiri nyengine kadhaa, kuhusiana na maana ya Hadithi hii, ambazo zawezekana kuwa ndio tafsiri sahihi ya Hadithi hii, nazo ni kama ifuatavyo:
- Hadithi hii inaonesha kuwa kukamilisha maadili ya juu ya tabia njema, ni jukumu pekee la Mtume wa Uislamu; yaani, kati ya mitume wote, yeye pekee ndiye aliye tumwa kwa ajili ya kukamilisha maadili ya juu ya tabia njema. [12]
- Hadihti hii inamaanisha kuwa; maadili mema yalio kusudiwa katika Haithi hii, yanatofautiana na maadili ya kawaida; yaani, bwana Mtume (s.a.w.w), ametumwa kwa ajili ya kukamilisha maadili mema maalumu yenye sifa za juu kabisa za tabia njema. [13]
- Sababu na lengo kuu la utume wa bwana Mtume (s.a.w.w), ni kukamilisha maadili ya juu ya tambia njema, na lengo hili ndiyo msingi wa kusimama kwa malengo na vipengele vingine vya kidini. [14]
Ithibati za Uhalali wa Hati za Hadithi Hii
Hadithi ya Makarimu al-Akhlai imepokewa katika vyanzo vya Shia pamoja na vyanzo vya Sunni:
Kutoka kwa vyanzo vya Shia, Hidithi hii inapatikana katika kitabu cha Al-Risalatu Al-Alawiyyah [15] kilichoandikwa na Muhammad bin Ali Karajaki (aliyefariki: mwaka 449 Hijiria) na pia inapatikana katika tafsiri ya Majma’u al-Bayani [16] iliyoandikwa na Fadhlu bin Hassan Tabarsi (aliyefariki: mwaka 548 Hijiria). vyanzo hivi vinahisabiwa kuwa ndio vyanzo vya zamani zaidi vilivyo nukuu Hadithi ya Makarimu al-Akhlaqi. [17] Pia, Hassan bin Fadhlu Tabarsi ameinukuu Hadithi hii katika utangulizi wa kitabu chake kiitwacho Makarim Al-Akhlaq bila kutoa marejeo ya sanad yake (hati na ithibati yake). [18]
Hata hivyo, Hadithi hii pia imekuja katika vyanzo vingine kwa maneno na ibara tofauti: Katika Fiqh al-Ridha imeandikwa:«بُعِثتُ بِمَکارِمِ الاَخلاق ; Nimetumwa nikiwa na maadili ya juu ya tabia njema», [19] na katika kitabu cha Aamali kilichoandikwa na Sheikh Tusi (aliye ishi baina ya mwaka 385 na 460 Hijiria) imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwa maneno yasemayo: «بُعِثتُ بِمَکارِمِ الاَخلاقِ و مَحَاسِنِها ; Nimetumwa nikiwa na maadili ya juu tabia njema na mapambo yake». [20]
Kati ya vyanzo vya Sunni, Baihaqi (aliyefariki: mwaka 458 Hijiria) ameiandika Riwaya hii katika kitabu chake Sunan al-Kubra akirejelea sanad (mlolongo wa wapokezi ulio egemea), kutoka kwa Abu Huraira, aliyepokea kutoka kwa bwana Mtume (s.a.w.w). [21] Pia, Malik bin Anas (aliye ishi: kati ya mwaka 93 na 179 Hijiria), [22] Ahmad bin Hanbal (aliye ishi: kati ya mwaka 164 na 241 Hijiria), [23] na Muhammad bin Ismail Bukhari (aliye ishi: kati ya mwaka 194 na 256 Hijiria), [24] wameiandika Hadithi hii kwa maneno na ibara zinayofanana katika vitabu vyao. Baadhi ya watafiti, kwa kuzingatia wingi wa Riwaya zenye maudhui sawa na Hadithi, hii katika vyanzo vya Shia na Sunni, wameichukulia Hadithi hii kuwa; ni Hadithi mutawatiru maanawiy. Yaani wao wamezihisabu Riwaya hizo zote kuwa ni sawa na Riwaya moja tu, ambazo zinaungana kimaana, hata kama zinatofautiana kiibara. [25]
Mifano Hai ya Makarimu Akhlaqi (Maadili ya Juu ya Tabia Njema)
Neno Makarimu ni wingi wa makramah «مَکرَمة» lenye maana ya adhimu na tukufu, [26] na wanazuoni wameifasiri ibara ya Makarimu Akhlaqi kama ni maadili adhimu. [27] Kuna Riwaya nyingi katika vyanzo vya Hadithi kutoka kwa Maasumina (Maimamu watukufu) (a.s), kuhusiana na Makarimu Akhlaq, [28] na baadhi ya Hadithi hizo zimetaja sifa kadhaa, kama ni mifano hai ya Makarimu Akhlaqi. Kulayni katika kitabu chake cha al-Kafi amenukuu Hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s), ambayo inaeleza ya kwamba; Makarim Akhlaq ni mapambo ya Mitume, Hadithi ambayo pia inawahimiza watu kuwa kushikamana na mapambo hayo. Kisha akataja sifa kumi za mifano ya maadili ya Makarimu Akhlaqi kama ifuatavyo: Kuwa na yakini, Qana'ah (kuridhika), subira, shukrani, kujidhibiti (kutokana na matamanio haramu ya nafsi), kuwa na tabia njema, ukarimu, heshima, ujasiri (ushujaa), na uadilifu. [29] Katika Pia Hadithi nyingine katika kitabu hicho hicho, imetaja sifa nyingine kadhaa za mifano ya maadili ya Makarimu Akhlaqi, nazo ni: kutokuwa na tamaa (neema walizo nazo watu wengine), kusema ukweli, kua mwaminifu juu ya amana, kuunga udugu, kuwakirimu wageni, kuwalisha wenye mahitaji, kufidia na kulipa mema yaliopita, kuheshimu haki za jirani, na kuheshimu haki za rafiki. Kisha ikaelezwa katika Hadithi hiyo ya kwamba; msingi wa Makarimu al-Akhlaqi, ni kuwa na uso wenye hayaa. [30]
Tofauti kati ya Maadili ya Juu ya Tabia Njema (Makarimu al-Akhlaqi) na Mahasinu al-Akhlaqi (Mapambo ya Maadili)
Katika baadhi ya nukuu za Hadithi za maadili ya juu ya tabia njema (Makarimu al-Akhlaqi), maadili ya juu ya tabia njema, yamewekwa sambamba na mapambo ya maadili, jambo ambalo pia linaonekana katika riwaya iliyo nukuliwa na Sheikh Tusi. [31] Kulingana na maelezo ya Muhammad Taqi Falasafi (Aliye zaliwa: mwaka 1286 na kufariki 1377 Shamsia), ambaye ni mmoja wa wahadhiri wa kidini, ni kwamba; katika Riwaya hizo, hakuna kigezo cha kutofautisha kati ya “Makarimu al-Akhlaqi” (maadili ya juu ya tabia njema) na “Mahasinu al-Akhlaqi” mapambo ya maadili. [32] lakini kwa kuzingatia mifano iliyotajwa katika Hadithi kwa ajili ya aina mbili mbili hizi za maadili, tunaweza kusema kuwa; kuwa na bashasha na watu, jambao ambalo linasisitizwa na kuthaminiwa na sharia za Kiislamu, ambalo pia halipingani na matamanio ya nafsi, [33] na ni miongoni mwa mambo yanayo husiana zaidi na uhusiano wa kijamii na jinsi ya kuishi na wengine, [34] ni miongoni mwa mapambo ya maadili. Na kwa upande wa pili; kuna sifa maalumu za kimaadili kama vile: kudhibiti hasira, si miongoni mwa mambo rahisi, na ni lazima mtu kupambane na matamanio ya nafsi yake au angalau kuipuuza, kwa yule mwenye nia ya kuzingatia jambo hilo. Aina hii ya maadili zinajumuishwa katika kategoria ya “Makarimu al-Akhlaqi” (maadili ya juu ya tabia njema). [35]
Maudhui Zinazo Fungamana
- Hadhi na Heshima ya Mwanadamu
- Aya ya Karama (Heshima)
Rejea
Vyanzo