Dua ya thelathini na nane (38) ya kitabu cha Sahifa Sajjadiyya
Nakala ya Sahifa al-Sajjadiyah, katika hati ya Naskh ya Abdullah Yazdi, Iliyoandikwa Mnamo Sha'ban 1102 AH. | |
| Mtoaji / Mwandishi | Imamu Sajjad (a.s) |
|---|---|
| Lugha | Kiarabu |
| Msimulizi / Mpokezi | Mutawakkil ibn Harun |
| Mada | Dua ya kumwomba msamaha Mwenyezi Mungu kwa mapungufu yanayotokea katika utekelezaji wa haki za binadamu (Haqq al-Nas). |
| Chanzo | Sahifa Sajjadiyah |
| Tafsiri kwa Lugha ya | Kifarsi |
Dua ya Thelathini na Nane (38) ya Kitabu cha Sahifa Sajjadiyya (Kiarabu: الدعاء الثامن والثلاثون من الصحيفة السجادية) ni miongoni mwa dua zilizopekea kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s). Madhumuni ya dua hii ni kuwasilisha toba kwa mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji wa haki za watu mbali mbali, na kuomba ukombozi kutokana na adhabu ya moto wa Jahannam. Lengo kuu la Imamu (a.s) katika dua hii, ni kuomba radhi kwa yafuatayo: kutothamini na kutoonesha shukrani kwa hisani alizotendewa na wengine; kushindwa kumtetea mja aliyedhulumiwa mbele ya umma (mbele yake); kutowapa kipaumbele wenye shida walioomba usaidizi, na badala yake kutanguliza mahitaji binafsi; kutostiri aibu na mapungufu ya wanadamu wengine; kutokubali ombi la msamaha aliloombwa na wengine; na uzembe wa jumla katika kutimiza wajibu na haki za watu.
Dua ya Thelathini na Nane ya Sahifa Sajjadiya imeshereshwa (imefasiriwa na kufafanuliwa) katika vitabu mbalimbali vilivyofasiri dua za kitabu cha Sahifa Sajjadiyya kupitia lugha tofauti. Miongoni mwa tafsiri fafanuzi hizo zilizofanya kazi yake kwa lugha ya Kifarsi (Kiajemi), ni kitabu kiitwacho Shuhud wa Shenakht, kilichoandikwa na Hassan Mamduhi Kermanshahi. Ama kitabu maarufu katika kazi hiyo kilichoandikwa lugha ya Kiarabu, ni kitabu kijulikanacho kwa jina la Riyad as-Salikin, kazi maridadi ya Sayyid Ali-Khan Madani.
Mafunzo ya Dua Hii
Katika dua ya thelathini na nane ya Sahifa Sajjadiyya, Imamu Sajjad (a.s), anawasilisha ombi la msamaha kwa Mola wake kutokana na mapungufu yanayotokea katika utekelezaji wa haki za binadamu (Haqq al-Nas). Aidha, anabainisha nukta za msingi kuhusu mienendo bora ya mahusiano ya kijamii.[1]
Mafundisho ya dua hii yameorodheshwa katika vipengele vifuatavyo:
- Umuhimu wa kuwalinda na kuwatetea watu wanaodhulumiwa na kunyanyaswa.
- Umuhimu wa kutoa shukrani kwa wahisani na watenda wema.
- Umuhimu wa kukubali maombi ya msamaha kutoka kwa wengine.
- Uhalifu (uharamu) wa kuanika siri za wenza wa kiitikadi.
- Ulazima wa kuzuia vitendo viovu katika mazingira ya uasi (vikao vinavyoasiwa Mungu ndani yake).
- Umuhimu wa kutekeleza wajibu wa kuwapa wengine stahiki zao bila kuchelewa.
- Uombaji radhi wa kweli kutokana na kosa fulani, hujumuisha kujifunza kutokana na kosa hilo na kuahidi kutolirudia utendaji wa kosa hilo.
- Ulazima wa kukidhi mahitaji na maombi ya watu wengine (kwa kadiri ya uwezo wako).
- Kuomba kuwezeshwa kufanya maamuzi madhubuti ya kuachana na vitendo vya dhambi.
- Kuomba toba ya kweli (taubatu al-nasuha), itakayosababisha kupata upendo na radhi mbele za Mwenye Ezi Mungu.
- Kumuomba Mwenye Ezi Mungu aipandikize hisia ya kuchukia dhambi moyoni mwa Wake, baada ya mja huyo kutubia dhambi zake.
- Uhakika wa kwamba; Mwenye Ezi Mungu anawapenda wenye kutubia (At-Tawwabina).
- Dhana ya Toba ianajumuisha mchakato wa kujutia makosa ya awali na kuwa tayari kupambana na vishawishi vya makosa yajayo.[2]
Tafsiri Chambuzi za Dua ya Thalathini na Nane
Kuna kazi nyingi zilizoandikwa kwa lugha mbali mbali kwa ajili ya kutoa tafsiri sahihi za Dua ya thelathini na nane sambamba na dua nyengine za kitabu cha Sahifa Sajjadiya. Miongoni mwa kazi zilizoandikwa kwa lugha ya Kifarsi, ni ile inayopatikana katika kitabu kiitwacho Shuhud wa Shenakht, kilichoandikwa na mwanachuoni aitwaye Muhammad-Hasan Mamduhi Kermanshahi,[3]pamoja na kitabu kiitwacho Sharh wa Tarjomeh Sahifa Sajjadiya, kazi ya Sayyid Ahmad Fahri.[4]
Aidha kuna wanazuoni kadhaa wilijitahidi kuichambua Dua hii sambamba na dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya kwa lugha ya Kiarabu, ili kuwarahisishia waumini ufahamu na welewa wa dua hizo. Miongoni mwa wanazuoni waliutmia muda wao kwa ajili ya kazi hiyo ni pamoja na; Maulana Sayyid Ali Khan Madani katika kitabu chake Riadhu as-Salikin,[5] Sheikh Muhammad Jawad Mughniyyah katika kitabu chake Fi Dhilali as-Sahifat as-Sajjadiyya,[6] Muhammad bin Muhammad Darabi katika kitabu chake Riyadh al-Arifin,[7] na Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah katika kitabu chake kiitwacho Afaq al-Ruh.[8] Vilevile, kuna baadhi ya wanazuoni waliofanya kazi ya kutoa maana za maneno na msamiati wa dua hii sambamba na dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya, wakiuchambua msamiati wake kupitia mfumo wa kilugha. Miongo mwa vitabu vilitomikia kazi hiyo ni kama vile; Ta'aliqat 'ala as-Sahifat as-Sajjadiyya, kazi ya Mwanazuoni ajulikanaye kwa jina la Faidhu Kashani,[9] na Sharhu as-Sahifat as-Sajjadiyya, kazi ya Sheikh Izzu al-Din al-Jaza'iri.[10]
Matini ya Kiarabu na Maelezo ya Kiswahili ya Dua ya Thalathini na Nane
وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ عَلَيْهِ السَّلَامُ فِي الِاعْتِذَارِ مِنْ تَبِعَاتِ الْعِبَادِ وَ مِنَ التَّقْصِيرِ فِي حُقُوقِهِمْ وَ فِي فَكَاكِ رَقَبَتِهِ مِنَ النَّارِ
اللَّهُمَّ إِنِّي أَعْتَذِرُ إِلَيْكَ مِنْ مَظْلُومٍ ظُلِمَ بِحَضْرَتِي فَلَمْ أَنْصُرْهُ، وَ مِنْ مَعْرُوفٍ أُسْدِيَ إِلَيَّ فَلَمْ أَشْكُرْهُ، وَ مِنْ مُسِيءٍ اعْتَذَرَ إِلَيَّ فَلَمْ أَعْذِرْهُ، وَ مِنْ ذِي فَاقَةٍ سَأَلَنِي فَلَمْ أُوثِرْهُ، وَ مِنْ حَقِّ ذِي حَقٍّ لَزِمَنِي لِمُؤْمِنٍ فَلَمْ أُوَفِّرْهُ، وَ مِنْ عَيْبِ مُؤْمِنٍ ظَهَرَ لِي فَلَمْ أَسْتُرْهُ، وَ مِنْ كُلِّ إِثْمٍ عَرَضَ لِي فَلَمْ أَهْجُرْهُ.
أَعْتَذِرُ إِلَيْكَ -يَا إِلَهِي- مِنْهُنَّ وَ مِنْ نَظَائِرِهِنَّ اعْتِذَارَ نَدَامَةٍ يَكُونُ وَاعِظاً لِمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنْ أَشْبَاهِهِنَّ.
فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ اجْعَلْ نَدَامَتِي عَلَى مَا وَقَعْتُ فِيهِ مِنَ الزَّلَّاتِ، وَ عَزْمِي عَلَى تَرْكِ مَا يَعْرِضُ لِي مِنَ السَّيِّئَاتِ، تَوْبَةً تُوجِبُ لِي مَحَبَّتَكَ، يَا مُحِبَّ التَّوَّابِينَ.
Na miongoni mwa dua zake (amani iwe juu yake) ilikuwa ni ile aliyoitumia katika kuomba radhi kutokana na madhara ya dhima zitokanazo na haki za watu, mapungufu yatokanayo na majukumu ya kuwatekelezea haki zao, pamaoja kuomba ukombozi wa kuikomboa nafsi yake kutokana na Moto wa Jahannam.
Ewe Mola, ninawasilisha kwako maombi yangu ya msamaha: kutokana na haki ya mnyonge aliyekandamizwa mbele yangu, nami nikashindwa kumnusuru (mnyonge huyo), na (ninaomba mshamaha Wako) kutokana na fadhila nilizotendewa, nami nikaacha kutoa shukrani (juu ya fadhila hizo), na kutokana na mkosaji aliyewasilisha kwangu maombi ya kunitaka radhi, nami nikakataa kumpa msamaha, na kwa yule mwenye uhitaji aliyenielekezea ombi lake, nami nikashindwa kumfadhilisha (mtanguliza yeye) badala ya nafsi yangu, na kutokana na ile haki ya muumini ambayo ilikuwa ni wajibu wangu (kuitekeleza haki hiyo), nami nikazembea katika kuitekeleza kikamilifu,na (ninaomba mshamaha Wako) kwa dosari (aibu) ya muumini fulani iliyonidhihirikia, nami nikaacha kuisitiri, na kwa kila tendo la uasi lililojitokeza mbele yangu, nami nikashindwa kuliepuka.
Ewe Mungu wangu, nakuomba msamaha kutokana na makosa hayo na yale yanayofanana nayo. Ni msamaha (ni toba) unaotokana na majuto ya kweli, ambao utakuwa onyo (somo) kwangu dhidi ya makosa kama hayo katika siku za usoni.
Hivyo basi, mrehemu (mbariki) Muhammad na Aali zake. Na ijaalie nadama yangu juu ya mapungufu (makosa) niliyoangukia ndani yake, pamoja na dhamira yangu madhubuti ya kuviacha vitendo viovu vinavyojitokeza mbele yangu, kuwa ni nadama (toba) itakayonihakikishia upendo Wako, Ewe Mwenye kuwathamini wanaorejea Kwako.
Rejea
- ↑ Mamduhi Kermanshahi, Shuhud wa Shenakht, 1388, juz. 3, uk. 251.
- ↑ Mamduhi, Shuhud wa Shenakht, 1388, juz. 3, uk. 251-258. Sherh Ferezhaye Duaye Sio Hashtom Az Site Irfan.
- ↑ Mamduhi Kermanshahi, Shuhud wa Shenakht, 1388, juz. 3, uk. 249-258.
- ↑ Fahri, Sherh wa Tafsir Sahifa Sajjadih, 1388, juz. 3, uk. 119-126.
- ↑ Madani Shirazi, Riyadh al-Salikin, 1435 AH, juz. 5, uk. 273-298.
- ↑ Mughniyah, Fi Dhilal al-Sahifa, 1428 AH, uk. 445-448.
- ↑ Darabi, Riyadh al-Arifin, 1379 AH, uk. 475-478.
- ↑ Fadhlullah, Afaq al-Ruh, 1420 AH, juz. 2, uk. 253-272.
- ↑ Faydh Kashani, Ta'baqat al-Sahifa al-Sajjadiyyah, 1407 AH, uk. 74-75.
- ↑ Jazairi, Sharh al-Sahifa al-Sajjadiyyah, 1402 AH, uk. 193-194.
Vyanzo
- Ansarian, Hussein, Diyar Asheqan, Tafsir Jamii Sahifa Sajjadiyah, Tehran, Payam Azadi, 1374.
- Jazairi, Izu-Din, Sherh al-Sahifa al-Sajjadiyyah, Beirut, Dar al-Taaruf Lil-Matbuat, 1402 AH.
- Khalji, Muhammad Taqi, Asrar al-Khamushan, Qom, Parto Khorshid, 1383 S.
- Darabi, Muhammad bin Muhammad, Riyadh al-Arifin Fi Sherh Sahifa Sajjadiyah, Muhaqiq Hussein Dargahi, Tehran, Nashr Us-wah, 1379.
- Fadhlullah, Sayyid Muhammad Hussein, A'faq al-Ruh, Beirut, Dar al-Malik, 1420 AH.
- Fahri, Sayyid Ahmad, Sherh wa Tarjume Sahifa Sajjadiyeh, Tehran, Us-wah, 1388 S.
- Faidh Kashani, Muhammad bin Murtaza, Taaliqat Ala Sahifa Sajjadiyah, Tehran, Muasase al-Bahth wa al-Tahqiqat al-Thaqafiyah, 1407 AH.
- Mughniyeh, Muhammad Jawad, Fi Dhilal al-Sahifa al-Sajjadiyyah, Qom, Dar al-Kitab al-Islami, 1428 AH.
- Madani Shirazi, Sayyid Ali Khan, Riyadh al-Salikiin Fi Sherh Sahifa Sayyid al-Sajidin, Qom, Muasase al-Nashr al-Islami, 1435 AH.
- Mamduhi Kermanshahi, Hassan, Shuhud wa Shenakhte: Tarjume wa Sherh Sahifa al-Sajjadiyyah, Ba Muqadime Ayatullah Jawadi Amuli, Qom, Bostan Kitab, 1385 S.