Nenda kwa yaliyomo

Dua ya kumi na tisa ya Sahifa Sajjadiyya

Kutoka wikishia

Dua ya kumi na tisa ya Sahifa Sajjadiyya: ni maombi yanayosomwa kwa ajili ya kuomba mvua, baada ya kipindi kirefu cha ukame. Maombi ni miongoni mwa yalionukuliwa kutoka kwa Imamu Sajjad (Ali bin Al-hussein) (a.s). Muktadha hasa uliofafanuliwa na Imamu Zainu al-Abidin (Ali bin Al-hussein) (a.s) ndani ya dua hii, unahusiana na manufaa ya mvua kwa binadamu pamoja na sifa za mvua yenye faida. Imamu Sajjad (a.s) anautuja upepo na mvua kama ni ishara ya ufufuo wa viumbe Siku ya Hukumu. Aidha, anatoa shukrani kwa Mola wake kutokana na neema ya kushuka kwa mvua kama moja ya neema za Mwenye Ezi Mungu.

Dua hii ya kumi na tisa imefafanuliwa katika vitabu mbali mblai vilivyotoa tafsiri chambuzi za Sahifa Sajjadiya. Miongoni mwa vitabu vilivyochambua dua hii kwa lugha ya Kiajemi (Kifarsi au Kipashia) ni kama vile; Diyare Asheqan, kazi ya Hussein Ansarian pamoja na Shohud wa Shenakht, kazi ya Hassan Mamdouhi Kermanshahi. Pia kuna tafsiri nyingi zilizochambua dua hii kwa lugha mbali mbali ulimwenguni. Kwa upande wa lugha ya Kiarabu, tafsiri maarufu chambuzi kuhusiana na dua hii, inapatikana katika kitabu kiitwacho Riyadhu al-Salikin, kilichoandikwa na Sayyid Ali Khan Madani.


Mafunzo ya Dua ya Kumi na Tisa

Dua ya kumi na tisa ya Sahifa Sajjadiya ni miongoni mwa maombi yaliyokuwa yakiombwa na Imamu Sajjad (a.s) wakati wa ukame na kukosekana kwa mvua. Katika dua hii, Imamu huyu wa Nne anatuelezea sifa za mvua yenye manufaa, pamoja na kutufafanulia faida za mvua hiyo kwa binadamu. Mafundisho ya dua hii yameorodheshwa katika sehemu saba [1] kama ifuatavyo:

·       Dua Mahususi kwa ajili ya unyeshaji wa mvua yenye Wingi wa Tija

·       Vigezo bainifu vya mvua yenye manufaa kwa mazingira na jamii:

·       Mvua kama kichocheo cha uhuishaji wa ardhi kame (tasa)

·       Mvua kama mhimili wa ustawi na kiini cha kutokomeza baa la njaa

·       Mvua kama kigezo cha urahisishaji wa gharama za maisha mijini

·       Mvua kama chachu ya kuimarisha na kuongeza uwezo wa uzalishaji

·       Vipengele vya mvua yenye kuleta maafa:

·       Mvua ambayo kivuli cha mawingu yake huwa na joto, huku ubaridi wa mvua yake ikiwa ni shari.

·       Mvua ambayo mnyesho wake ni adhabu na maji yake yana kiwango cha juu cha chumvi (chachu).

·       Maombi ya riziki itokanayo na baraka za Mbinguni na Ardhini

·       Mvua kama kielelezo cha rehema za Mwenye Ezi Mungu

·       Upepo na mvua kama kielelezo cha ufufuo wa viumbe katika Siku ya Kiyama. [2]

Tafsiri Chambuzi za Dua ya Kumi na Tisa

Kuna tafsiri kadhaa chambuzi zilizofafanua Dua hii ya Kumi na Tisa ya Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa tafsiri hizo chambuzi zilizoandikwa kwa lugha ya Kiajemi ni pamoja na; Diyare Asheqan, [3] cha Hussein Ansarian, Shuhud wa Shenakht, cha Mohammad Hassan Mamdouhi Kermanshahi, [4] na Sharh wa Tarjomeh Sahifeh Sajjadiyeh, cha Sayyid Ahmad Fahri. [5]

Pia kuna tasfiri kadhaa za Dua hii zilizoandikwa kwa mbali mbali ikiwemo lugha ya Kiarabu. Miongoni tafsiri zinazopatikana kwa Kiarabu ni kama vile; Riyad al-Salikin, kitabu kilichoandikwa na Sayyid Ali Khan Madani, [6] Fi Dhilali al-Sahifati al-Sajjadiyya, cha Muhammad Jawad Mughniyya, [7] Riyadhu al-Arifina, cha Muhammad ibn Muhammad Darabi, [8] na Afaqi al-Ruh, cha Sayyid Mohammad Hussein Fadlallah. [9] Aidha, msamiati wa dua hii umeelezwa na kuchambuliwa kilugha ndani ya kitabu kiitwacho Taliqat Ala al-Sahifati al-Sajjadiyya, cha Faidhu Kashani [10] pamoja na Sharh al-Sahifati al-Sajjadiyya, cha Izzu al-Din Jaza'iri. [11]


Matini ya Dua na Tafsiri Yake

وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ، عَلَيْهِ السَّلَامُ عِنْدَ الاِسْتِسْقَاءِ بَعْدَ الْجَدْبِ

Na ifuatayo ni miongoni mwa dua tukufu za Imamu (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake), aliyokuwa akiitumia wakati wa kumnyenyekea Mola wake Mtukufu kwa ajili ya kuomba neema ya mvua:

اللَّهُمَّ اسْقِنَا الْغَيْثَ، وَ انْشُرْ عَلَيْنَا رَحْمَتَكَ بِغَيْثِكَ الْمُغْدِقِ مِنَ السَّحَابِ الْمُنْسَاقِ لِنَبَاتِ أَرْضِكَ الْمُونِقِ فِي جَمِيعِ الْافَاقِ.

Ewe Mwenyezi Mungu, tunyeshezee mvua, na utusambazie rehema Zako kupitia mvua zako nyingi zitokayo kwenye mawingu yaliyosukumwa, kwa ajili ya mimea ya ardhi yako katika pande zote duniani.

وَ امْنُنْ عَلَى عِبَادِكَ بِإِينَاعِ الَّثمَرَةِ، وَ أَحْيِ بِلَادَكَ بِبُلُوغِ الزَّهَرَةِ، وَ أَشْهِدْ مَلَائِكَتَكَ الْكِرَامَ السَّفَرَةَ بِسَقْيٍ مِنْكَ نَافِعٍ، دَائِمٍ غُزْرُهُ، وَاسِعٍ دِرَرُهُ، وَابِلٍ سَرِيعٍ عَاجِلٍ.

Na uwakirimu waja wako kwa kuyaivisha matunda ya mime hiyo, na uihuishe nchi yako kwa kuchanua kwa maua (yake). Na uwafanye Malaika wako watukufu, ambao ni waandishi (makarani wako), waishuhudie mvua hiyo yenye manufaa kutoka Kwako ambayo; endelevu katika unyeshaji wake, mpana mtiririko wake, kubwa ya haraka na isiyochelewa.


تُحْيِي بِهِ مَا قَدْ مَاتَ، وَ تَرُدُّ بِهِ مَا قَدْ فَاتَ وَ تُخْرِجُ بِهِ مَا هُوَ آتٍ، وَ تُوَسِّعُ بِهِ فِي الْأَقْوَاتِ، سَحَاباً مُتَرَاكِماً هَنِيئاً مَرِيئاً طَبَقاً مُجَلْجَلًا، غَيْرَ مُلِثٍّ وَدْقُهُ، وَ لَا خُلَّبٍ بَرْقُهُ.

Mvua ambayo kwayo utahuisha na kuhuisha kile kilichokufa, na kwayo utarejesha kile kilichopotea, na utaleta kile kilichonjiani kupitia mvua hiyo. Na kwayo utatua ustawi wa riziki (vyakula). (Tunakuomba utuletee) mawingu yaliyorundikana, yenye kufurahisha na yenye manufaa, yaliyoenea na yenye ngurumo, ambayo mvua yake si hafifu, wala umwesa wake (mwemweto wa radi zake) si danganyifu.

اللَّهُمَّ اسْقِنَا غَيْثاً مُغِيثاً مَرِيعاً مُمْرِعاً عَرِيضاً وَاسِعاً غَزِيراً، تَرُدُّ بِهِ النَّهِيضَ، وَ تَجْبُرُ بِهِ الْمَهِيضَ

Ee Mola wetu! Tunakuomba utunyeshezee mvua yenye ukombozi, na yenye kutokomeza baa la njaa. Mvua itakaotesha mimea na kustawisha nyanda na mbuga kwa kuzivika (tena) rangi ya kijani. Mvua enevu na yenye ujazo wa kutosha. Iwe ni mvua itakayorejesha ustawi wa kila mmea uliodumaa na kuufanya urejee tena kwenye mkondo wa ustawi. Na uijalie mvua hiyo iwe ni yenye ufufuo kwa ardhi kame (kavu) iliyopoteza mimea yake.

اللَّهُمَّ اسْقِنَا سَقْياً تُسِيلُ مِنْهُ الظِّرَابَ، وَ تَمْلَأُ مِنْهُ الْجِبَابَ، وَ تُفَجِّرُ بِهِ الْأَنْهَارَ، وَ تُنْبِتُ بِهِ الْأَشْجَارَ، وَ تُرْخِصُ بِهِ الْأَسْعَارَ فِي جَمِيعِ الْأَمْصَارِ، وَ تَنْعَشُ بِهِ الْبَهَائِمَ وَ الْخَلْقَ، وَ تُكْمِلُ لَنَا بِهِ طَيِّبَاتِ الرِّزْقِ، و تُنْبِتُ لَنَا بِهِ الزَّرْعَ وَ تُدِرُّ بِهِ الضَّرْعَ وَ تَزِيدُنَا بِهِ قُوَّةً إِلَي قُوَّتِنَا.

Ewe Mola wangu! Tuteremshie mvua ya rehema, ambayo kwayo utatutiririshia maji kutoka milimani, na kutajaza visima (vyetu). Kwayo uifanye mito ichirizike, na miti nayo iote, mvua ambayo itapelekea bei ziwe rahisi miji mwote. Na kupitia mvua hiyo uwaimarishe wanyama wenye miguu minne pamoja na viumbe wote. Na utupe ukamilifu wa riziki njema zilizo halali, utuoteshee mimea yetu, na uyajaze maziwa matiti ya wanyama, na utuzidishie nguvu juu ya nguvu tulizonszo.

اللَّهُمَّ لَا تَجْعَلْ ظِلَّهُ عَلَيْنَا سَمُوماً، وَ لَا تَجْعَلْ بَرْدَهُ عَلَيْنَا حُسُوماً، وَ لَا تَجْعَلْ صَوْبَهُ عَلَيْنَا رُجُوماً، وَ لَا تَجْعَلْ مَاءَهُ عَلَيْنَا أُجَاجاً.

Ewe Mola wetu! Usikifanye kivuli cha wingu lake kuwa ni lenye kuzalisha upepo wa joto dihi yetu na kutudhuru; na wala usiifanye baridi yake kuwa ni mkosi (hilaki). Usijaalie mnyesho wake kuwa ni chanzo cha maangamizi dhidi yetu, na wala maji yake yasiwe na uchungu wa kupindukia.

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِ مُحَمَّدٍ، وَ ارْزُقْنَا مِنْ بَرَكَاتِ السَّمَاوَاتِ وَ الْأَرْضِ، إِنَّكَ عَلَى كُلِّ شَيْ‌ءٍ قَدِيرٌ.

Ewe Mola wetu! Mbariki Muhammad na Aali zake. Na utukidhie mahitaji yetu kutoka katika hazina ya baraka za mbinguni na ardhini. Hakika, wewe ni Muweza wa kila jambo.