Dua ya kumi na nne ya Sahifa Sajjadiyya
Dua ya kumi na nne ya Sahifa Sajjadiyya: ni miongoni mwa dua zilizorithiriwa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s), ambayo ndani yake Imamu anatafuta nusura ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kupata ukombozi na ulinzi dhidi ya uonevu wa watawala dhalimu. Ndani ya dua hii, Imamu Sajjad (a.s) amegusia utambuzi wa Mwenye Ezi Mungu juu ya hatima za wahanga wa dhuluma za watawala madhalimu katika zama mbali mbali, na anamuomba Mungu mbele ya hadhara Yake, ili amwezeshe kuzishinda hisia za chuki na ghadhabu zinazoweza kumvaa dhidi ya mahasimu wake. Kadhalika, Imamu Sajjad (a.s) anaiomba kupata hadhi daraja ya ridhaa (umaridhawa) na kuwa na taslimu (kujisalimisha kikamilifu) mbele ya Mwenye Ezi Mungu.
Aidha, dua hii ya kumi na nne imechambuliwa na kufafanuliwa katika tafsiri mbali mbali zilizochambua maandiko ya Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa tafsiri zilizoandikwa kwa lugha ya Kiajemi ni pamoja na; Diyare Asheghan cha Hussein Ansarian na Shuhud wa Shenakht cha Hassan Mamduhi Kermanshahi. Pia kuna waandishi waliotoa uchambuzi na ufafanuzi wa dua hii kwa lugha ya Kiarabu, moja ya vikitabu mashuhuri katika uwanja huu, ni Riyadhu al-Salikina, kilichoandikwa na Sayyid Ali Khan Madani.
Mada ya Dua ya Kumi na Nne
Muhimili mkuu wa dua ya kumi na nne ya kitabu cha Sahifa Sajjadiyya umejikunjua katika kuwaombea himaya waliodhulumiwa, pamoja na kuomba nusura ya Mwenye Ezi Mungu dhidi ya watawala dhalimu. [1] Kwa mujibu wa maelezo ya Mohammad Jawad Haji Aliakbari, Mwenyekiti wa Baraza la Urasimishaji wa Sera za Maimamu wa Sala za Ijumaa nchini Iran, ni kwamba; Kiongozi wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, Ayatollah Khamenei, alitoa agizo rasmi la usomaji wa dua hii mahususi kwa ajili ya kuomba ushindi kwa wapiganaji wa Harakati za Ukinzani dhidi ya Israeli. Maagizo hayo yalijiri wakati wa uvamizi wa Israeli nchini Lebanoni mwaka 2024. [2] Kufuatia agizo hilo, imeripotiwa kuwa; dua hii ilianza kusomwa kijumuiya katika misikiti mbali mbali nchini Iran. [Uthibitisho wa rejea unatakikana]
Mafunzo Msingi Yaliomo Duani Humu
Dua hii inamwelekezea Mwenye Ezi Mungu ombi la kumpa hifadhi mdhulumiwa anayekabiliwa na matendo ya kidhalimu dhidi yake, na kumwezesha kuzidhibiti na kuzishinda hisia zake za kinyongo na ghadhabu zake. Kadhalika, inatilia mkazo umuhimu wa tohara ya nafsi (self-purification) dhidi ya kasoro za kiakhlaqi (kimaadili). [3] Mafundisho ya dua ya kumi na nne, yaliyonukuliwa katika vifungu 16 [4] kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s.), yameainishwa kama ifuatavyo:
- Upeo wa maarifa kamilifu ya Mungu; Ukwasi wa elimu ya Mungu juu ya hatima ya wahanga wa dhuluma
- Ushahidi wa Mungu ni kamilifu na usiopingika katika uwepo wote
- Mungu ni msaidizi wa wanyonge na hasimu wa madhalimu
- Uungaji mkono wa msimamo imara dhidi ya uonevu na ukosoaji wa wanyonge wa kukubali dhuluma
- Udhaifu na uduni wa wakandamizaji
- Kuwasilisha shtaka mbele ya Mungu dhidi ya dhuluma na mdhalimu
- Umuhimu wa kudumisha adabu za kiuja (ubudiyya) katika mazingira yote
- Ombi la kupatiwa hifadhi dhidi ya kutendea wengine dhuluma
- Dua kwa ajili ya kudhibiti hisia za kinyongo na ghadhabu dhidi ya hasimu fulani
- Kuomba rehema za Mwenye Ezi Mungu kama ni fidia ya kustahimili dhulma
- Mungu kama mtoa suluhu pekee dhidi ya changamoto za waja wake
- Ombi la kuwajibishwa kwa madhalimu na kumwombea uokozi muhanga wa dhuluma
· Ombi la kutaka kuepushwa na matamanio (mielekeo hasi ya nafs) na tabia mbaya, pamoja na tabia ya kuto tosheka (kutoridhika).
· Kuridhika na maamuzi ya Mungu kwa kuwa na kuhisi za moyoni juu ya malipo ya Mungu, pamoja na kuwa na taswira ya adhabu ya maadui na madhalimu.
· Kuomba malipo (ya amali) kutoka kwa Mwenye zi Mungu peke yake.
· Kuomba na kutaraji mwitikio wa Mungu juu ya dua tuziombazo
· Kutafuta hifadhi ya uimara wa itikadi (imani)
· Mdhulumiwa yupo katika mtihani wa kudhulumiwa na dhalimu yupo katika mtihani wa dhulma dhidi ya wengine
· Ombi la kutaka kuepushwa na kukata tamaa juu ya malipizo ya Mungu dhidi ya dhalimu
· Ombi la kuomba kufikia daraja la umaridhawa na kusalimu amri mbele ya matukio mbali mbali, yawe ya kheri au shari, na kukabidhi mambo yetu kwa Mungu, na kwamba kama kheri yetu ni kupata malipo ya Akhera badala ya yale ya kiduni, basi tumtake Allah atupe uwezo wa kuwa na Subira na uvumilivu hapa duniani. [5]
Matini ya Dua na Tafsiri Yake
وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ عَلَيْهِ السَّلَامُ إِذَا اعْْتُدِيَ عَلَيْهِ أَوْ رَأَي مِنَ الظَّالِمِينَ مَا لَا يُحِبُّ
Na ifuatayo ilikuwa ni miongoni mwa dua zake (a.s), pindi anapokabiliwa na ukandamiza Fulani au anaposhuhudia jambo lisilomridhisha kutoka kwa madhalimu Fulani:
يَا مَنْ لَا يَخْفَى عَلَيْهِ أَنْبَاءُ الْمُتَظَلِّمِينَ
Ewe usiyefichikiwa na malalamiko ya wanaodhulumiwa.
وَ يَا مَنْ لَا يَحْتَاجُ فِي قَصَصِهِمْ إِلَى شَهَادَاتِ الشَّاهِدِينَ .
Na Ewe usiyehitaji maelezo ya mashahidi katika kuelewa kwako matukio na visa vya ukandamizwaji wao.
وَ يَا مَنْ قَرُبَتْ نُصْرَتُهُ مِنَ الْمَظْلُومِينَ
Na Ewe Ambaye nusura yake iko karibu na wanaodhulumiwa.
وَ يَا مَنْ بَعُدَ عَوْنُهُ عَنِ الظَّالِمِينَ
Na Ewe Ambaye, msaada Wake uko mbali na madhalimu.
قَدْ عَلِمْتَ ، يَا إِلَهِي ، مَا نَالَنِي مِنْ فُلَانِ بْنِ فُلَانٍ مِمَّا حَظَرْتَ وَ انْتَهَكَهُ مِنِّي مِمَّا حَجَزْتَ عَلَيْهِ ، بَطَراً فِي نِعْمَتِكَ عِنْدَهُ ، وَ اغْتِرَاراً بِنَكِيرِكَ عَلَيْهِ .
Hakika Ee Mungu wangu! umeshayajua, yale yaliopata kutoka kwa fulani bin fulani, miongoni mwa yale uliyoyakataza; na jinsi alivyonivunjia heshima kwa kufanya yale uliyomzuia asiyafanye, amefanya hivyo kwa jeuri kutokana na yale uliomneemesha, na akijidanganya kuwa yuko salama, na yumbali na hasira Zako dhidi yake.
اللَّهُمَّ فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ خُذْ ظَالِمِي وَ عَدُوِّي عَنْ ظُلْمِي بِقُوَّتِكَ ، وَ افْلُلْ حَدَّهُ عَنِّي بِقُدْرَتِكَ ، وَ اجْعَلْ لَهُ شُغْلًا فِيما يَلِيهِ ، وَ عَجْزاً عَمَّا يُنَاوِيهِ
Ewe Mola wangu, mshushie rehma Zako Muhammad na Aali zake, na umdhibiti kwa nguvu Zako mkandamizaji wangu na hasimu wangu (huyu ili) asiweze kunidhulumu, na uyapunguze makali yake dhidi yangu kwa kudura Yako, na umshughulishe na yale yanayomwelekea (yanayomdhuru) yeye mwenyewe, na umtie ajizi ya kutoweza kufafikia yale anayonikusudia.
اللَّهُمَّ وَ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ لَا تُسَوِّغْ لَهُ ظُلْمِي ، وَ أَحْسِنْ عَلَيْهِ عَوْنِي ، وَ اعْصِمْنِي مِنْ مِثْلِ أَفْعَالِهِ ، وَ لَا تَجْعَلْنِي فِي مِثْلِ حَالِهِ
Ewe Mola wangu, na umshushie rehema na amani Muhammad na Aali zake. Na usimruhusu (dhalimu huyu) wala kumrahisishia udhalimu wake dhidi yangu, na unipe nusura kamili dhidi yake. Unihifadhi dhidi ya hisia za kuiga nyenendo zake, na usinijaalie kuwa na hali (au sifa) kama yake.
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ وَ أَعْدِنِي عَلَيْهِ عَدْوَى حَاضِرَةً ، تَكُونُ مِنْ غَيْظِي بِهِ شِفَاءً ، وَ مِنْ حَنَقِي عَلَيْهِ وَفَاءً .
Ewe Mungu, mpe mshushie rehema zako Muhammad na Aali zake, na unisaidie dhidi ya [adui] huyu kwa kumpatiliza mara moja; kitendo kitakachokuwa ni tiba kwa hasira yangu dhidi yake, na kitakachotosheleza (kukidhi kiwango cha) chuki yangu dhidi yake.
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ عَوِّضْنِي مِنْ ظُلْمِهِ لِي عَفْوَكَ ، وَ أَبْدِلْنِي بِسُوءِ صَنِيعِهِ بِي رَحْمَتَكَ ، فَكُلُّ مَكْرُوهٍ جَلَلٌ دُونَ سَخَطِكَ ، وَ كُلُّ مَرْزِئَةٍ سَوَاءٌ مَعَ مَوْجِدَتِكَ .
Ewe Mola, zishushie swala na salamu Muhammad na Aali zake, na unifidie kwa msamaha Wako dhidi ya uonevu wake kwangu, na ubadilishe ubaya wa kitendo chake dhidi yangu kwa huruma Yako. Hakika, kila tukio hasi ni duni mbele ya ghadhabu Yako, na kila janga ni hafifu mbele ya fadhila Yako.
اللَّهُمَّ فَكَمَا كَرَّهْتَ إِلَيَّ أَنْ أُظْلَمَ فَقِنِي مِنْ أَنْ أَظْلِمَ .
Ewe Mungu, kama vile ulivyonifanya nichukie kudhulumiwa, basi vilevile nilinde nisiwe ni mwenye kuwadhulum wengine.
اللَّهُمَّ لَا أَشْكُو إِلَى أَحَدٍ سِوَاكَ ، وَ لَا أَسْتَعِينُ بِحَاكِمٍ غَيْرِكَ ، حَاشَاكَ ، فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ صِلْ دُعَائِي بِالْإِجَابَةِ ، وَ اقْرِنْ شِكَايَتِي بِالتَّغْيِيرِ .
Ewe Mola wangu, mimi simlalamikii yeyote yule isipokuwa Wewe, wala sitafuti msaada wa mwamuzi (hakimu) yeyote yule ghairi Yako, Hasha wa Kalla (katu siwezi kuwa maamuzi kama hayo) ! Basi, mrehemu Muhammad na Aali zake, na uiunganishe dua yangu hii na kabuli (yako), na liweke shitaka langu hili sambamba na maboresho (mabadiliko).
اللَّهُمَّ لَا تَفْتِنِّي بِالْقُنُوطِ مِنْ إِنْصَافِكَ ، وَ لَا تَفْتِنْهُ بِالْأَمْنِ مِنْ إِنْكَارِكَ ، فَيُصِرَّ عَلَى ظُلْمِي ، وَ يُحَاضِرَنِي بِحَقِّي ، وَ عَرِّفْهُ عَمَّا قَلِيلٍ مَا أَوْعَدْتَ الظَّالِمِينَ ، وَ عَرِّفْنِي مَا وَعَدْتَ مِنْ إِجَابَةِ الْمُضْطَرِّينَ .
Ewe Mungu, usinitahini kwa mtihani wa kukata tamaa ya insafu Yako, na wala usimtahi yeye (adui yangu) kwa mtihani wa kujiona yuko salama na yumbali na adhabu yako. Kwani hilo litamfanya yeye aendelee kunidhulumu na kunizuilia haki zangu. Na umuonjeshe hivi karibuni kile ulichowaahidi madhalimu, na unionyeshe kile ulichowaahidi katika kuwajibu walio na dhiki.
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ وَفِّقْنِي لِقَبُولِ مَا قَضَيْتَ لِي وَ عَلَيَّ وَ رَضِّنِي بِمَا أَخَذْتَ لِي وَ مِنِّي ، وَ اهْدِنِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ ، وَ اسْتَعْمِلْنِي بِمَا هُوَ أَسْلَمُ
Ewe Mola wangu, mshushie swala na salamu Muhammad na Aali zake. Na unipe taufiki (uniwezeshe) ya kukubali yale uliyokadiria kwa ajili yangu na dhidi yangu, na nijaalie niwe na ridhaa (nitosheke) kwa yale uliyonitunukia na uliyonipokonya. Na nielekeze kwenye mwenendo ulio adilifu zaidi, na uniajiri (nitumikishe) kwenye shughuli zenye amani zaidi.
اللَّهُمَّ وَ إِنْ كَانَتِ الْخِيَرَةُ لِي عِنْدَكَ فِي تَأْخِيرِ الْأَخْذِ لِي وَ تَرْكِ الِانْتِقَامِ مِمَّنْ ظَلَمَنِي إِلَى يَوْمِ الْفَصْلِ وَ مَجْمَعِ الْخَصْمِ فَصَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ ، وَ أَيِّدْنِي مِنْكَ بِنِيَّةٍ صَادِقَةٍ وَ صَبْرٍ دَائِمٍ
Ewe Mola wangu, na iwapo kheri yangu mbele Yako ipo katika kuakhirisha kunichukulia haki yangu na kuacha kisasi kwa aliyenidhulumu hadi Siku ya Upambanuzi na makusanyiko ya mahasimu (Siku ya Kiama), basi mswalie Muhammad na Aali zake, na unithibitishe kwa kunipa nia safi na subira ya kudumu kutoka Kwako.
وَ أَعِذْنِي مِنْ سُوءِ الرَّغْبَةِ وَ هَلَعِ أَهْلِ الْحِرْصِ ، وَ صَوِّرْ فِي قَلْبِي مِثَالَ مَا ادَّخَرْتَ لِي مِنْ ثَوَابِكَ ، وَ أَعْدَدْتَ لِخَصْمِي مِنْ جَزَائِكَ وَ عِقَابِكَ ، وَ اجْعَلْ ذَلِكَ سَبَباً لِقَنَاعَتِي بِمَا قَضَيْتَ ، وَ ثِقَتِي بِمَا تَخَيَّرْتَ
Na unihifadhi dhidi ya shauku ovu na jazba ya watu wenye uchu wa kupidukia mipaka. Na unichoree moyoni mwangu taswira ya kile ulichonihifadhia katika thawabu Zako, na kile ulichomuandalia hasimu wangu katika jazaa na adhabu Yako. Na jaalia (taswira au mchoro huo) uwe ni chimbuko la qanaa yangu kwa yale uliyokadiria, na (uwe ni msingi wa) uthabiti wa imani juu ya yale uliyonichagulia.
آمِينَ رَبَّ الْعَالَمِينَ ، إِنَّكَ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ ، وَ أَنْتَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ
Amina (iwe hivyo), Ewe Mola wa walimwengu wote. Bila shaka Wewe ni mwenye wema wa kupindukia (adhimu), Nawe ni Mweza wa kila kitu.