Dua ya arubaini na tatu ya Sahifa Sajjadiyya
Dua ya arubaini na tatu ya Sahifa Sajjadiyya: ni mojawapo ya dua zilizonukuliwa kutoka kwa Imamu Sajjad (a.s). Imam alikuwa na desturi ya kuisoma dua hii pindi tu anapouona mwezi mwandamo. Katika matini ya dua hii, Imamu Sajjad (a.s.) akizungumzia mfumo wa mzunguko wa mwezi, anasimamisha hoja isemayo kwamba; uumbaji wa mwezi na mfumo wa mzunguko wake, ni kielelezo dhahiri kinachoashiria mipango madhubuti na hekima takatifu za Mwenyue Ezi Mungu. Aidha, ameonekana kulitumia tukio la kuandama kwa mwezi na kuonekana na kuchomoza kwa mwezi mpya, kama ni nyenzo ya kuomba toba kutoka kwa Mwenye Ezi Mungu, pamoja na kumsihi Mola wake ampe siha na afya njema, na amkinge dhidi ya shari na madhara mbali mbali. Dua hii ya Arubaini na Tatu, imefafanuliwa na kushereheshwa katika vitabu mbalimbali vya ufafanuzi wa Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa vitabu hivyo vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiajemi (Kifarsi), kwa ajili ya kutoa tafsiri chambuzi pamoja kusherehesha dua zilizozomo katika kitabu cha Sahifa Sajjadiyya ni pamoja na; 'Diare Asheqan', kilichoandikwa na bwana Hussein Ansarian, pamoja na kitabu kiitwacho 'Shuhud wa Shenakht', cha Hassan Mamduhi Kermanshahi. Vilevile, kwa upande wa lugha ya Kiarabu, dua hii sambamba na dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya, zimefafanuliwa kupitia kazi mbali mbali zilizofanywa na wanazuoni waliotumia wakati wao muhimu kwa ajili ya huduma hii muhimu. Miongoni mwa vitabu vilivofanya kazi hiyo muhimu ni pamoja na; 'Riadhu as-Salikin', kilichoandikwa na Sayyid Ali Khan Madani, pamoja na 'Al-Hadiqa al-Hilaliyya' kilichotungwa na Sheikh Baha'i. Mafundisho Yaliyomo Ndani ya Dua ya Arubaini na Tatu Dua ya Arubaini na Tatu ni miongoni mwa dua za kitabu cha Sahifa Sajjadiya. Imamu Sajjad (a.s.) alikuwa na desturi ya kuisoma dua hii kila alipouona mwezi mwandamo (mwezi mpya). Kwa mujibu wa maezezo ya mwanazuoni Mohammad Hussein Fadhlullah katika kitabu chake 'Aafaq al-Ruh,' ni kwamba; kuutafakari mfumo mzima wa maumbile, humpelekea mwanadamu kugundua siri asili za tabia nchi (maumbile), pamoja na kutambua nafasi yake halisi ndani ya ulimwengu huu. [1] Vilevile, bwna Mamduhi Kermanshahi, ambaye pia ni mmoja wa wafasiri wa kitabu cha Sahisa Sajjadiyya, anasema kwama; Imamu Sajjad (a.s) alitumia kila fursa, ikiwemo kuuona mwezi, kama njia na nyenzo ya kumomba Mola wake, pamoja na kujikurubisha kwa Mwenye Ezi Mungu. Hii ni kutokana na umuhimu wa kupata ukuruba na Mungu, hivyo basi ni muhimu kutumia kila fursa bila ya kupoteza wakati, ili kulifikia lengo hilo muhimu. [2] Mafundisho yaliyomo ndani ya dua ya arubaini na tatu yemekuja katika vipengele vifuatavyo: • Mwezi unaelezewa kama ni kiumbe dhaifu cha Mwenye Ezi Mungu kinachofuata amri na kuzunguka angani chini ya mpango Wake. • Kuonekana kwa mwezi mpya ni ishara ya mamlaka na uwezo wa Mwenye Ezi Mungu. • Maajabu ya mipango ya Mwenye Ezi Mungu yanaonekana katika uumbaji Wake mwezi na jinsi unavyotembea mwezi kupitia mfumo wake maridadi. • Mwenye Ezi Mungu pekee, ndiye anayesimamia na kuendesha ulimwengu mzima. • Uwepo wa mwezi ni uthibitisho wa nguvu za Mwenye Ezi Mungu. • Dua ya kumuomba Mwenye Ezi Mungu auletee mwezi mpya wenye baraka. • Mafunzo ya kuomba dua ili mwezi mpya huo uwe ni wenye matukio mazuri na ulinzi dhidi ya mabaya. • Ni ombi la kuomba dua ya kumtaka Mwenye Ezi Mungu akufanye uwe ni mtu mwenye mwenye furaha na ridhaa nyingi zaidi miongoni mwa waja wake wanaochomozewa na mwezi huo mpya. • Ombi la kupata wepesi wa kutubu kutokana na dhambi zetu. • Umuhimu wa kushukuru neema za Mwenye Ezi Mungu kila uingiapo mwezi mpya. • Ombi la kuomba majaliwa ya afya njema na kuepushwa na hasara pamoja na uovu. • Ombi la kupata neema kamili za Mwenye Ezi Mungu kwa njia ya kumtii Yeye kikamilifu. • Ombi la kujaliwa usalama na afya njema. [3]
Kuna watafiti na wanazuoni wengi wa lugha mbali mbali ulimwenguni, waliifasiri Dua ya Arubaini na Tatu, sambamba na dua nyengine zilizoko ndani ya kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa wanazuoni walioifanya kazi hiyo kwa lugha ya Kifarsi ni pamoja na; Hussein Ansarian, aliyanya kazi hiyo kupitia kitabu chake kiitwacho Diare Asheqan, [4] bwana Mohammad Hassan Mamduhi Kermanshahi, katika kitabu chake kiitwacho Shuhud wa Shenakht, [5] na Sayyid Ahmad Fahri, aliyestawisha kazi hii muhimu kwenye kitabu chake kiitwacho Sharh wa Tarjomeh Sahifeh Sajjadiyyeh. [6] Aidha, kuna wanazuoni kadhaa walioifasiri dua hii kwa lugha ya Kiarabu, sambamba na dua nyengine za Sahifa Sajjadiyya katika kazi zao mbalimbali. Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na; Riadhu al-Salikin (cha Sayyid Ali Khan Madani), [7] Fi Dhilali al-Sahifat al-Sajjadiyya (cha Mohammad Jawad Mughniyah), [8] Riadhu al-Arifina (cha Mohammad bin Mohammad Darabi), [9] pamoja na Afaqi al-Ruh (cha Sayyid Mohammad Hussein Fadhlullah). [10] Zaidi ya hayo, pia kuna wanazuoni maalumu waliokaa kitako kwa ajili ya kuchambua kilugha maneno na msamiati uliyotumika katika dua hii, sambamba na dua nyengine zilizomo ndani ya kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa kazi hizo za kilugha, ni pamoja na; Ta'liqat 'ala al-Sahifat al-Sajjadiyya (cha Faidhu Kashani), [11] na Sharhu al-Sahifat al-Sajjadiyya (cha Izzu al-Din al-Jaza'iri). [12]
Miongoni mwa wafasiri wazuri walioifasiri na kuichambua Dua ya 43 kwa Kiarabu, ni Sheikh Baha'I, kazi ambayo inapatikana katika kitabu chake kiitwacho Al-Hadiqah Al-Hilaliyyah. Katika kitabu chake hicho, Sheikh Baha'i anaanza kwa kujadili maana halisi ya neno 'hilal' yaani mwezi mwandamo (wa siku ya kwanza kabisa ya kuandama mwezi), pamoja na suala la kukubaliwa kwa dua wakati wa kuonekana kwa mwezi. Baada ya hapo, anafafanua maudhui ya dua hiyo kwa ufafanuzi maridadi kabisa. Uchunguzi wa mambo ya nyota (astronomia) ulio katika kitabu hichi, pia umeonekana umetumiwa na wafafanuzi wengine waliofasiri na kuchambua dua za kitabu cha Sahifa Sajjadiyya. Miongoni mwa wachambuzi waliotumia nadharia zilielezwa na Sheikh Baha’I, ni bwana Sayyid Ali Khan katika kazi yake iitwayo Riyad al-Salikin. Kitabu hichi kimekusanya maudhui za fani mbaIi mbali ndani yake, ikiwemo fani ya; fasihi, kiroho (kiirfani/kisufi) pamoja nafiqhi. Aiha mwandishi wa kitabu hichi amenukuu Hadithi kadhaa na kuziorodhesha kitabuni make humo. Baadae kitabu cha Al-Hadiqa Al-Hilaliyyah, kilikuja kuhaririwa na bwana Sayyid Ali Musawi Khorasani. [13]
Matini ya Kiarabu ya Dua ya Arubaini na Tatu Pamoja na Maelezo Yake kwa Kiswahili
وَ كَانَ مِنْ دُعَائِهِ عَلَيْهِ السَّلَامُ إِذَا نَظَرَ إِلَى الْهِلَالِ Na (ifuatayo ilikuwa ni) miongoni mwa dua zake (rehema na amani ziwe juu yake), aliyokuwa akiisoma pale anapouangalia mwezi mchanga. أَيُّهَا الْخَلْقُ الْمُطِيعُ، الدَّائِبُ السَّرِيعُ، الْمُتَرَدِّدُ فِي مَنَازِلِ التَّقْدِيرِ، الْمُتَصَرِّفُ فِي فَلَكِ التَّدْبِيرِ.
Ewe kiumbe mtiifu, mwenye mwendo wa kudumu na wa kasi, wewe unayepita katika vituo vya mipango ya (uendeshaji wa) Mwenye Ezi Mungu, na mtawala tendaji katika mzingo (uzingo) wa utawala maalumu.
آمَنْتُ بِمَنْ نَوَّرَ بِكَ الظُّلَمَ، وَ أَوْضَحَ بِكَ الْبُهَمَ، وَ جَعَلَكَ آيَةً مِنْ آيَاتِ مُلْكِهِ، وَ عَلَامَةً مِنْ عَلَامَاتِ سُلْطَانِهِ، وَ امْتَهَنَكَ بِالزِّيَادَةِ وَ النُّقْصَانِ، وَ الطُّلُوعِ وَ الْأُفُولِ، وَ الْإِنَارَةِ وَ الْكُسُوفِ، فِي كُلِّ ذَلِكَ أَنْتَ لَهُ مُطِيعٌ، وَ إِلَى إِرَادَتِهِ سَرِيعٌ
Nimemwamini Yule aliyeliangaza giza (la usiku) kupitia mwanga wako (aliyekutumia wewe kama ni tochi ya kuondolea giza), na akaweka wazi yaliyo magumu (kuonekana) kupitia mwanga wako, na akakufanya wewe kuwa ni ishara miongoni mwa ishara za ufalme Wake, na alama miongoni mwa alama za mamlaka Yake. Akakupa mtihani wa kuongezeka na kupungua, kuchomoza na kuzama, na kung'aa na kupatwa. Nawe ukawa ni mtiifu kwake juu yote hayo aliyokukpangia, na ukawa ni mharakiaji wa kuharakia kutekeleza matakwa Yake.
سُبْحَانَهُ مَا أَعْجَبَ مَا دَبَّرَ فِي أَمْرِكَ! وَ أَلْطَفَ مَا صَنَعَ فِي شَأْنِكَ! جَعَلَكَ مِفْتَاحَ شَهْرٍ حَادِثٍ لِأَمْرٍ حَادِثٍ
Ametakasika Mwenye Ezi Mungu! Ni wa kustaajabisha mno mpango (na mkakati) alioutekeleza kwa ajili ya jukumu lako! Na ni wa usahihi wa hali ya juu mno aliyoutumia katika utendaji wake kuhusiana nawe (kuhusiana na suala lako)! Amekufanya wewe kuwa ufunguo wa mwezi mpya kwa ajili ya tukio jipya. فَأَسْأَلُ اللَّهَ رَبِّي وَ رَبَّكَ، وَ خَالِقِي وَ خَالِقَكَ، وَ مُقَدِّرِي وَ مُقَدِّرَكَ، وَ مُصَوِّرِي وَ مُصَوِّرَكَ: أَنْ يُصَلِّيَ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ أَنْ يَجْعَلَكَ هِلَالَ بَرَكَةٍ لَا تَمْحَقُهَا الْأَيَّامُ، وَ طَهَارَةٍ لَا تُدَنِّسُهَا الْآثَامُ
Basi, ninamuomba Mwenye Ezi Mungu—ambaye ni Mola wangu Mlezi na Mola wako Mlezi, Muumba wangu na Muumba wako, aliyenikadiria mambo yangu na aliyekukadiria wewe mambo yako, na aliyenifumia umbile la muonekano wangu, na aliyekufumia wewe umbile la muonekano wako—Amrehemu Mtume Muhammad (s.a.w.w) pamoja na Aali zake, na (ninamuomba) akufanye wewe (ewe mwezi) kuwa ni mwezi wa mwandamo wenye baraka zisizofutwa kwa mapito ya masiku (zisizochakazwa na mpito wa masiku), na (akufanye) uwe ni (chanzo cha) usafi usiochafuliwa na (uchafu wa) madhambi. هِلَالَ أَمْنٍ مِنَ الْآفَاتِ، وَ سَلَامَةٍ مِنَ السَّيِّئَاتِ، هِلَالَ سَعْدٍ لَا نَحْسَ فِيهِ، وَ يُمْنٍ لَا نَكَدَ مَعَهُ، وَ يُسْرٍ لَا يُمَازِجُهُ عُسْرٌ، وَ خَيْرٍ لَا يَشُوبُهُ شَرٌّ، هِلَالَ أَمْنٍ وَ إِيمَانٍ وَ نِعْمَةٍ وَ إِحْسَانٍ وَ سَلَامَةٍ وَ إِسْلَامٍ.
(Akufanye) uwe ni mwezi mchanga wa amani dhidi ya maafa, na usalama wa kusalimika na matendo maovu. (Akufanye) uwe ni mwezi wa bahati njema isiyo na nuhusi, na baraka isiyo na dhiki, na wepesi usiochanganyika na ugumu, na kheri isiyo na chembe za shari. Uwe ni mwezi wa amani na (wa kujenga) imani, na (ni mwezi wa) neema na (kujenga) wema, na ni mwezi wenye usalama na (wa kujenga) Uislamu.
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ، وَ اجْعَلْنَا مِنْ أَرْضَى مَنْ طَلَعَ عَلَيْهِ، وَ أَزْكَى مَنْ نَظَرَ إِلَيْهِ، وَ أَسْعَدَ مَنْ تَعَبَّدَ لَكَ فِيهِ، وَ وَفِّقْنَا فِيهِ لِلتَّوْبَةِ، وَ اعْصِمْنَا فِيهِ مِنَ الْحَوْبَةِ، وَ احْفَظْنَا فِيهِ مِنْ مُبَاشَرَةِ مَعْصِيَتِكَ
Ewe Mwenye Ezi Mungu, mrehemu Muhammad na Aali zake. Na utujaalie tuwe ni miongoni mwa walioridhiwa zaidi kuliko wengi wote waliochomozewa na mwezi huu, na (utujaalie tuwe ni) watakatifu zaidi kuliko wote walioiutazama (mwezi huu), na ni wenye furaha na heri nyingi zaidi kuliko wengine wote waliokuabudu katika siku hii. Na (tunakuomba) utupe taufiki (mafanikio) ya kutubia ndani yake (ndani ya masiku ya mwezi huu), na utukinge na uchafu wa dhambi ndani ya msiku yake, na utuhifadhi na kuingia ndani ya maasi yako. وَ أَوْزِعْنَا فِيهِ شُكْرَ نِعْمَتِكَ، وَ أَلْبِسْنَا فِيهِ جُنَنَ الْعَافِيَةِ، وَ أَتْمِمْ عَلَيْنَا بِاسْتِكْمَالِ طَاعَتِكَ فِيهِ الْمِنَّةَ، إِنَّكَ الْمَنَّانُ الْحَمِيدُ، وَ صَلَّى اللَّهُ عَلَى مُحَمَّدٍ وَ آلِهِ الطَّيِّبِينَ الطَّاهِرِينَ. Na (tunakuomba) utuwezeshe (utupe taufiki ya) kushukuru neema zako, ndani ya masiku ya mwezi huu, na utukinge kwa ulinzi wa afya njema [na utuvishe ngao za afya njema]. Na (twakuomba), uikamilisha neema Yako juu yetu kwa kutuwezesha kutimiza kikamilifu wajibu wetu katika utiifu Kwako. Kwa hakika, Wewe ndiye Mneemeshaji Mkuu, Mstahiki wa Sifa njema (Mhimidiwa). Na (tunamuomba) Mwenye Ezi Mungu amemshushia baraka zake Muhammad na Aali zake walio wema na watoharifu.