Bal’am bin Ba’ura
Bal’am bin Ba’ura (Kiarabu: بلعام بن باعوراء) alikuwa mmoja wa wasomi na wanazuoni katika zama za Nabii Mussa (a.s) na Mustajab al-Da’wah (mtu ambaye dua yake inakubaliwa). Lakini shetani alimrubuni na akampoteza. Bal’am bin Baura ametajwa katika hadithi za Kiislamu na katika torati. Kadhalika baadhi ya wafasiri wa Qur’an Tukufu wanaitambua Aya ya 175 katika Surat al-A’raf ambayo inazungumzia mtu aliyepotea ambaye alipewa ishara za Mwenyezi Mungu (kwa maana ya ufahamu na welewa wa jina la Mwenyezi Mungu au mjuzi wa kitabu cha Mwenyezi Mungu) kwamba, inamzungumzia Bal’am bin Ba’ura. Kumenukuliwa na kutolewa simulizi tofauti kuhusiana na visa vya Bal’am bin Ba’ura ambapo baadhi ya wafasiri wameviweka visa hivyo katika israiliyat (simulizi zilizokuwako katika zama za kale katika torati na vyanzo vingine na ambazo hazipo katika Qur’ani wala hadithi).
Sifa maalumu; kuwa na ujuzi wa kitabu cha Mwenyezi Mungu
Bal’am [1] au Bal’aam [2] alikuwa mtu anayetokana na Bani Israili [3] ambaye alikuwa akiishi katika ardhi ya Sham. [4] Nabii Mussa (a.s) alikuwa akimtumia Bal’am bin Ba’ura kama mubalighi (mhubiri). [5] Baba yake ametajwa kwa majina kama Ba’ura [6], Baur [7] na Awr [8] na mkewe alitambulika kwa jina la Bisus. [9]
Baadhi ya wafasiri wa Qur’an wanasema kuwa: Aya ya: ((وَ اتْلُ عَلَیهِمْ نَبَأَ الَّذِی ءَاتَینَاهُ ءَایاتِنَا فَانسَلَخَ مِنْهَا فَأَتْبَعَهُ الشَّیطَانُ فَکاَنَ مِنَ الْغَاوِین ; Na wasomee khabari za yule ambaye tulimpa Ishara zetu, naye akajivua nazo. Na Shetani akamuandama, akawa miongoni waliopotea)), [10] inaashiria mkasa na tukio la Bal’am bin Ba’ura. [11]. Hata hivyo wafasiri wana mitazamo tofauti kuhusiana na neno ishara zetu (آیاتنا) lililokuja katika Aya hii. Kundi miongoni mwao linaamini kwamba, lina maana ya Bal’am bin Ba’ura kufahamu jina tukufu la Mwenyezi Mungu (jina kubwa zaidi la Allah ambapo hakuna jina miongoni mwa majina ya Allah lenye adhama na utukufu kama hilo), [12] na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana dua zake zilikuwa zikikubaliwa. [13] Kundi jingine linaamini kwamba, neno آیاتنا (ishara zetu) katika Aya hii lina maana ya kuwa na ujuzi kuhusu kitabu cha Mwenyezi Mungu na sio kufahamu Ismul A’dham (jina kubwa zaidi la Mwenyezi Mungu). [14]
Kuporomoka kutoka katika daraja za juu
Kwa mujibu wa Aya ya 175 ya Surat al-A’raf, licha ya Bal’am bin Ba’ura kuwa na jina kubwa zaidi la Mwenyezi Mungu, lakini shetani alimrubuni na kumhadaa na hivyo akampoteza. [15] Kuhusiana na sababu ya kupotea kwake kuna mitazamo tofauti ambapo miongoni mwayo ni:
- Bal’am alisimama dhidi ya Nabii Mussa (a.s) na akamsaidi Firauni. [16]
- Kwa mujibu wa Mas’udy mwanahistoria wa Kiislamu katika kitabu chake cha Ithbat al-Wasiyyah ni kuwa, Bal’am alimsaidia mfalme wa nchi yake katika vita vyake na Nabii Joshua bin Nun (a.s) na Bani Israil. [17]
- Allama Muhammad Hussein Tabatabai anasema kuwa, muelekeo wa Bal’am wa kupenda ladha za dunia na kushikamana navyo ni mambo yaliyoandaa uwanja na mazingira ya yeye kupotea na kunyimwa hidaya na uongofu. [18]
Visa tofauti
Kumenukuliwa visa mbalimbali kuhusiana na Bal’am bin Ba’ura. Baadhi ya wafasiri wameviweka visa hivyo katika israiliyat (simulizi zilizokuwako katika zama za kale katika torati na vyanzo vingine na ambazo hazipo katika Qur’ani wala hadithi) na hivyo haviwezi kuaminiwa. [19] Baadhi yavyo ni:
- Bal’am alikuwa akitaka kuangamiza jeshi la Nabii Mussa (a.s). Kwa msingi huo akamtaka mtawala awatume wanawake kwa ajili ya kwenda kuwapokea Bani Israil huenda wakatumbukia katika zinaa na Mwenyezi Mungu akawaangamiza. [20]
- Bal’am alipewa ahadi ya kujibiwa dua tatu. Mkewe aliomba amuombee dua maalumu. Bal’am akakubali. Mkewe alimuomba aombe dua ili awe mwanamke mzuri na mrembo zaidi miongoni mwa wanawake wa Bani Israil. Bal’am aliomba dua na mkewe akawa kama alivyotaka. Baada ya mkewe kuona kwamba, hakuna mtu mrembo zaidi yake baina ya Bani Israil, aliamua kumuacha Bal’am. Bal’am akaomba dua na mkewe huyo akabidilika na kuwa mbwa. Watoto wa Bal’am walimuomba na kumtafadhalisha baba yao na kumtaka aombe dua na kumuondoa mama yao katika hali hiyo. Naye alifanya hivyo na mkewe akarejea kama alivyokuwa mwanzo. [21]
- Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo, Bal’am alichukua uamuzi wa kwenda kumlaani Nabii Mussa (a.s) na kaumu yake. Alipanda katika punda wake, hata hivyo punda aligoma kutembea. Bal’am alimchapa punda lakini wapi, punda hakuwa tayari kutembea na kuanza safari. Kitendo hicho kikajiriri mara tatu na kwa amri ya Mwenyezi Mungu punda yule akazungumza na kumwambia Bal’am kwamba: Anawaona Malaika wapo mbele yake ambao wanamzuia. [22] Kisa hiki kimenukuliwa pia katika kitabu cha Torati. [23]
Rejea
Vyanzo
- Ālūsī, Maḥmūd b. ʿAbd Allāh al-. Rūḥ al-maʿānī fī tafsīr al-Qurʾān al-ʿaẓīm. Edited by ʿAlī ʿAbd al-Bārī al-ʿAṭīyya, Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1415 AH.
- ʿAyyāshī, Muḥammad b. Masʿūd al-. Tafsīr al-ʿAyyāshī. Edited by Rasūlī Maḥallātī. Tehran: al-Maṭbaʿa al-ʿIlmīyya, 1380 AH.
- Baḥrānī, Sayyid Hāshim. Al-Burhān fī tafsīr al-Qurʾān. Tehran: Bunyād-i Biʿthat, 1416 AH.
- Fayḍ al-Kāshānī, Muḥsin. Tafsīr al-Ṣāfī. Edited by Ḥusayn Aʿlamī. Second edition. Tehran: Intishārāt-i Ṣadrā, 1415 AH.
- Ibn ʿAsākir, ʿAlī b. al-Ḥasan. Tārīkh madīnat Damascus. Beirut: Dār al-Fikr, 1415 AH.
- Ibn Kathīr, Ismāʿīl b. ʿUmar. Tafsīr al-Qurʾān. Edited by Muḥammad Ḥusayn Shams al-Dīn. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1419 AH.
- Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī & Muḥammad Ākhūndī. Fourth edition. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
- Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1374 Sh.
- Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Ithbāt al-waṣīyya. Third edition. Qom: Intishārāt-i Anṣārīyān. 1384 Sh.
- Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Edited by Mūsawī Jazāʾirī. Third edition. Qom: Dār al-Kitāb, 1404 AH.
- Rashīd Riḍā. Al-Manār. Cairo: al-Hayʾa al-Miṣrīyya al-ʿĀmma li-l-Kitāb, 1990.
- Rāwandī, Quṭb al-Dīn Saʿīd b. Hibat Allāh. Qiṣaṣ al-anbīyāʾ. Edited by Ghulāmriḍā ʿIrfānīyān Yazdī. Mashhad: Markaz-i Pazhūhishhā-yi Islāmī, 1409 AH.
- Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Jāmiʿ al-bayān fī tafsīr al-Qurʾān. Beirut: Dār al-Maʿrifa, 1412 AH.
- Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad Abū l-Faḍl Ibrāhīm. Beirut: Dār al-Turāth, 1387 AH