Al-Hadi al-Abbasi

Kutoka wikishia

Mussa bin Mahdi bin Mansour (Kiarabu: موسى بن المهدي بن المنصور) (145-175 AH) mashuhuri kwa lakabu ya al-Hadi al-Abbasi, ni khalifa wa nne kutoka katika ukoo wa Bani Abbas. Hadi Abbas alishika hatamu za uongozi kwa takribani miezi 14. Katika zama za utawala wake, watu wa ukoo wa Alawi walikuwa chini ya uangalizi na posho na marupurupu yao yalikatwa. Katika zama za utawala wake kulitokea harakati na mapinduzi ya Sahib Fakhkh katika mji wa Madina ambayo yalikandamizwa na kusambaratishwa na khalifa. Hadi Abbasi alikuwa akiamini kwamba, Imamu Kadhim (a.s) ndiye aliyewachochea maalawi katika mapinduzi ya Fakhkh na kwa msingi huo kama vilivyosema baadhi ya vyanzo alikuwa akitaka kumuua Imamu Kadhim (a.s). Lakini akaaga dunia kabla ya kufanya alilolikusudia. Al-Hadi al-Abbasi alikuwa akifuata mkondo wa siasa za baba yake Mahdi al-Abbasi katika kuamiliana na wazandiki na aliwaangamiza wengi miongoni mwao.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, Hadi Abbasi alitaka kumfanya Jafar, mwanawe mdogo, kuwa mrithi wa kiti cha ufalme badala ya Harun, lakini hakufanikiwa, baada yake Harun ambaye ni kaka yake akawa khalifa.

Historia ya Maisha yake

Mussa bin Mahdi bin Mansour, aliyepewa lakabu ya al- Hadi, alikuwa khalifa wa nne wa Bani Abbas baada ya Safah, Mansour Dawaniqi na Mahdi Abbasi. [1] Lakabu yake ilikuwa Abu Jaafar [2] au Abu Muhammad. [3] Baba yake ni Mahdi Abbasi, na mama yake alikuwa kijakazi aliyeitwa Khayzaran [4] Alishika hatamu za Ukhalifa mwezi Muharram 169 Hijiria akiwa na umri wa miaka 25. [5] Mwanzoni mwa ukhalifa, alikuwa na umri mdogo zaidi ikilinganishwa na Makhalifa wa kabla yake. [6]

Mahdi Abbasi, yaani baba yake alikuwa akimjali sana Hadi, [7] kiasi kwamba, alipokuwa na umri wa miaka 16 alimfanya kuwa mrithi wa kwanza wa kiti cha uongozi na akawa kamanda wa jeshi. [8] Mwishoni mwa maisha yake, Mahdi alikuwa akifikiria kumfanya mwanawe mwingine yaani Harun kuchukua mahali pa Hadi (mrithi wa kiti cha ufalme), lakini alikufa kabla ya kufanikiwa kutekeleza hilo. [9]

Wakati baba yake anafariki dunia, Mahdi Abbasi alikuwa Jurjan [10] na alikuwa katika vita na watu wa Tabaristan [11] na kaka yake Harun akala kiapo cha utii kwake siku hiyo hiyo [12] na akachukua pia baia (kwa ajili ya kaka yake) kutoka kwa shakhsia wakubwa wa familia ya Abbasi na makamanda wa jeshi. [13]

Khalifa wa nne wa Bani Abbas, yaani al-Hadi al-Abbasi, alitaka kuhamisha cheo cha urithi wa kiti cha utawala kutoka kwa kaka yake Harun hadi kwa mtoto wake wa miaka 7, [14] aliyekuwa akiitwa Jafar. [15] Alifanya juhudi nyingi katika njia hii. [16] Alijitahidi sana kumkinaisha Harun ili yeye mwenyewe aachie ngazi ya cheo hicho, lakini Harun alikimbia ili asikabidhi cheo cha urithi wa kiti cha utawala na hakurejea katika mji mkuu hadi kaka yake alipofariki dunia. [17]

Al-Hadi alikuwa na nguvu kimwili. [18] Ingawa anasifika kwa ushujaa na ustadi wake katika mambo ya serikali na vilevile kusamehe, wakati huo huo, amechukuliwa kuwa mtu katili, shujaa, shupavu na mwenye taasubi. [19] Al-Hadi al-Abbasi kutokana na kasoro aliyokuwa nayo katika midomo yake alijulikana kama "Musa Atbaq". [20] Alipendezwa na fasihi ya Kiarabu na historia na alipenda sana kuimba. [21]

Kifo

Alitawala kwa takriban miezi 14 na alifariki mwaka 170 Hijria huko Baghdad [22] akiwa na umri wa miaka 25 [23] au 26. [24] Sababu ya kifo chake, kulingana na wengine, ilikuwa ugonjwa, na kwa mujibu wa baadhi ya wengine aliuawa usingizini kwa amri ya mama yake. [25] Kaka yake Harun alimswalia na akazikwa katika eneo la Isabad huko Baghdad [26].

Muamala wake kwa Familia ya Alawi

Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria, Hadi Abbasi alikuwa mkali kwa Maalawi na akawatendea ukatili na aliwakatia ruzuku na posho zote ambazo zilianishwa kwa ajili yao katika zama za utawala wa Mahdi al-Abbasi. [27] Abul Faraj Esfahani alisema vitendo hivyo vilitokana na khofu ya Alawi kufanya mapinduzi. [28] Hadi Abbasi pia aliwaamuru maajenti wna makachero wake kufuatilia nyendo zote za Alawi na wawe wakienda kila usiku katika makao makuu ya utawala kwa ajili ya kusajili uwepo wao. [30]

Kukandamizwa Harakati ya Fakhkh

Makala Asili: Mapinduzi ya Shahid Fakh

Ukali na mbinyo wa Hadi Abbasi kwa kizazi cha Alawi katika Hijaz uliwaweka katika hali ya mbinyo; ili kuondokana na hali yao ya mtafaruku, walimgeukia mmoja wa wazee na shakhsia wakubwa wa Kialawi aliyeitwa Hussein bin Ali bin Hassan aliyejulikana kwa jina la Sahib Fakhkh, ambaye anatokana na wajukuu wa Imamu Hassan (a.s) na wakamhimiza na kumshajiisha aanzishe mapinduzi. [31]. Pamoja na hayo baadhi wanaamini kuwa, Hussein bin Ali kwa muda mrefu nyuma alikuwa akitaka kuchukua serikali na alikuwa akaiona kuwa utawala huo ni haki ya Maalawi, na ukandamizaji wa Hadi Abbasi ulitoa fursa ya harakati na mapinduzi yake. [32]

Hussein bin Ali bin Hassan, baada ya kutayarishwa uwanja wa harakati hiyo, alianza harakati zake mwaka 169 Hijiria. [33] Kwanza aliiteka na kuikomboa Madina na kuwaachia huru wafungwa [34] na kuwafunga viongozi wa serikali ya Abbas [35] na akaufanya Msikiti wa Mtume kuwa makao makuu ya uongozi. Kisha akaelekea Makka na akapiga kambi katika bonde liitwalo Fakhkh, maili sita kutoka Makka. [36]

Katika hali hiyo, jeshi la serikali ya Abbas, chini ya uongozi wa Issa bin Mussa, lilifika eneo la Fakhkh [37] na baada ya mapigano, Hussein na masahaba wake walishindwa na kuuawa. [38] Tukio hili lilijulikana katika historia kama tukio la Fakhkh, na Hussein bin Ali baada ya hapo, alitambulika kama Shahidi Fakhkh au Sahib Fakhkh. [39] Kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Jawadi (a.s) ni kwamba, baada ya tukio la Karbala, harakati ya Fakhkh lilikuwa tukio gumu zaidi la majaribu ya Ahlul-Bayt (a.s). [40] Na kuna mambo mengi yaliyoandikwa kuhusiana na maombolezo ya tukio hili. [41]

Kuamiliana kwake na Imamu Kadhim (a.s)

Hadi Abbasi alikuwa akimtuhumu Imamu Musa Kadhim (a.s) ndiye aliyewachochea Alawiyyun katika mapinduzi ya Fakhkh na kwa msingi huo kama walivyosema baadhi ya watafiti ni kuwa alikuwa akitaka kumuua Imamu Kadhim (a.s). Lakini akaaga dunia kaba ya kufanya alilolikusudia. (42]

Kuendelea Sera za Kukabiliana na Wazandiki

Hadi Abbasi, kama alivyokuwa baba yake Mahdi, aliwachukia wazandiki na alikuwa akiwasaka na kuwaadhibu. [43] Aliangamiza kundi miongoni mwa wazandiki; [44] akiwemo Yazdan bin Badhan [45] na pia aliua kundi miongoni mwao ambao walikuwa wameanzisha harakati katika eneo la Jazira. [46]

Vyanzo

  • Abū l-Faraj al-Iṣfahānī, ʿAlī b. al-Ḥusayn. al-Aghānī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1994.
  • Abū l-Faraj al-Iṣfahānī, ʿAlī b. al-Ḥusayn. Maqātil al-ṭālibīyyīn. Edited by Sayyid Aḥmad Ṣaqar. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
  • Bilādhurī, Aḥmad b. Yaḥyā al-. Ansāb al-ashrāf. Edited by Suhayl Zakār & Riyāḍ al-Ziriklī. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
  • Ibn al-Jawzī, ʿAbd al-Raḥman b. ʿAlī. Al-Muntaẓam fī tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad ʿAbd al-Qādir ʿAṭāʾ & Muṣṭafā ʿAbd al-Qādir ʿAṭāʾ. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1412 AH.
  • Ibn al-Ṭaqṭqaī, Muḥammad b. ʿAlī. Al-Fakhrī. Edited by ʿAbd al-Qādir Muḥammad Māyū. Beirut: Dār al-Qalam al-ʿArabī, 1418 AH.
  • Ibn Aʿtham al-Kūfī, Aḥmad. Al-Futūḥ. Edited by ʿAlī Shīrī. Beirut: Dār al-Aḍwāʾ, 1411 AH.
  • Ibn Athīr, ʿAlī b. Muḥammad. Al-Kāmil fī l-tārīkh. Beirut: Dār al-Ṣādir, 1965.
  • Ibn Ḥazm. Jumhurat ansāb al-ʿarab. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1403 AH.
  • Ibn Kathīr, Ismāʿīl b. ʿUmar. Al-Bidāya wa l-nihāya. Beirut: Dār al-Fikr, [n.d].
  • Ibn Miskawayh, Abū ʿAlī. Tajārub al-umam. Edited by Abū l-Qāsim Imāmī. Tehran: Surūsh, 1379 Sh.
  • Ibn Qutayba, ʿAbd Allah b. Muslim. Al-Maʿārif. Edited by Tharwat ʿAkāsha. Second edition. Cairo: al-Hiyʾa al-Miṣrīyya al-ʿĀmma li-l-Kitāb, 1992.
  • Jāsim Ḥusayn. Tārīkh-i sīyāsī-yi ghaybat-i Imām dawāzdahum. Edited by Muḥammad Taqī Āyatollāhī. Tehran: Amīr Kabīr, 1376 Sh.
  • Khiḍrī, Sayyid Aḥmad Riḍā. Tārīkh-i khalāfat-i ʿabbāsīyān. Terhan: Samt, 1383 Sh.
  • Maqdisī, Muṭahhar b. Ṭāhir al-. Al-Bidaʾ wa l-tārīkh. Beirut: Maktabat al-Thiqāfa al-Dīnīyya, [n.d].
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Al-Tanbīh wa l-Ishrāf. Edited by ʿAbd Allāh Ismāʿīl al-Ṣāwī. Cairo: Dār al-Ṣāwī, [n.d].
  • Masʿūdī, ʿAlī b. al-Ḥusayn al-. Murūj al-dhahab. Edited by Asʿad Dāghir. Qom: Dār al-Hijra, 1409 AH.
  • Ṭabarī, Muḥammad b. Jarīr al-. Tārīkh al-umam wa l-mulūk. Edited by Muḥammad Abū l-Faḍl Ibrāhīm. Beirut: Dār al-Turāth, 1387 AH.
  • Ṭaqūsh, Suhayl. Dawlat-i ʿabbāsīyān. Translated to Farsi by Ḥujjat Allāh Jūdakī. Qom: Pazhūhishkada-yi Ḥawza wa Dānishgāh, 1380 Sh.
  • Yaʿqūbī, Aḥmad b. Abī Yaʿqūb al-. Tārīkh al-Yaʿqūbī. Beirut: Dār al-Ṣādir, [n.d].