Zahra (lakabu)
Zahra (Kiarabu: الزهراء) ni moja ya lakabu za Bibi Fatima Zahra (a.s)[1] ambayo ina maana ya weupe wenye mng’ao[2] kama lulu inayong’ara. [3] Allama Majlisi katika kufasiri hadithi kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) inayoeleza sababu ya Bibi Fatima (a.s) kupewa lakabu hii amesema: Kung’ara kwake huku kuna maana ya nuru ya kimaanawi.[4] Neno Zahra au Fatima Zahra ni miongoni mwa majina ambayo hadithi na maandiko ya Ziara yamemhutubu Bibi Fatma. Kadhalika Maimamu wa Kishia wameondokea kuwa mashuhuri kwa jina la watoto wa Fatma.[5]
Katika hadithi zilizopokewa na Waislamu wa madhehebu ya Shia, kumetajwa sababu mbalimbali za Bibi Fatima (a.s) kupewa lakabu ya Zahra; miongoni mwazo ni hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) ambapo imeelezwa kuwa, Fatima ameitwa kwa lakabu ya Zahra kwa sababu sura yake ina nuru mbele ya Imamu Ali (a.s).[6] Imekuja katika hadithi nyingine kwamba, wakati Fatima alipokuwa akisimama na kufanya ibada, nuru yake ilikuwa ikiwaangazia watu wa mbinguni kama nyota zilizoko angali zinavyowaangazia watu wa ardhini.[7] Kadhalika imeelezwa katika hadithi ya kwamba, Mwenyezi Mungu alimuumba Fatima kutokana na nuru ya adhama yake na wakati alipomuumba alizifanya mbingu na ardhi kung’ara kwa nuru yake na macho ya Malaika yakang’ara.[8] Bibi Aisha amenukuu hadithi kuhusiana na kuwa na nuru uso wa Fatima.[9]
Imekuja katika hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Swadiq (a.s) kuhusiana na majina ya Bibi Fatima (a.s) kwamba, yeye (Fatima) ana lakabu na majina tisa mbele ya Mwenyezi Mungu: Fatima, Siddiqah, Mubarakah, Tahirah, Zakiyyah, Radhia, Mardhia, Muhadathah na Zahra.[10] Kwa mujibu wa kile kinachopatikana katika hadithi inafahamika kwamba, uchaguzi na uteuzi wa majina ya Bibi Fatima (a.s) ulifanyika kwa mujibu wa fadhila zake.[11]
Katika vitabu vya hadithi vya Waislamu wa madhehebu ya Shia, kumetengwa milango maalumu ya kubainisha lakabu za Zahra; kiasi kwamba, Sheikh Swaduq ametenga faslu maalumu katika kitabu chake cha Ilal al-Shari’i[12] na Allama Majlisi ametenga sehemu katika juzuu ya 43 ya kitabu chake cha Bihar al-Anwar kwa ajili ya maudhui hii.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotangazwa kuhusiana na majina katika Idara ya Usajili wa Majina ya Watoto ya Iran, wanawake wengi nchini Iran wana jina la Zahra. Kwa mfano katika mwaka 1392 Hijria Shamsia jina la Zahra lilishika nafasi ya pili nchini Iran kwa idadi ya wanawake wanaoitwa kwa jina hilo.[13]