Nenda kwa yaliyomo

Vita vya Qarqarat al-Kudr

Kutoka wikishia

Vita vya Qarqarat al-Kudr ni moja ya vita alivyopigana Bwana Mtume (saww) katika mwaka wa tatu Hijria. Kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, vita hivyo vilitokea mwaka wa pili Hijria katika eneo lililojulikana kwa jina la Qarqarat al-Kudr. Katika vita hivyo idadi kadhaa ya watu wa makabila mawili ya Bani Salim na Ghatafan walikusanyika katika eneo la Kudr ili waushambulie mji wa Madina. Hata hivyo baada ya jeshi la Waislamu kuwasili hapo, waliondoka katika eneo hilo. Katika vita hivyo, bendera ya jeshi la Waislamu ilikuwa imebebwa na Imam Ali (as) na Waislamu walifanikiwa kuchukua ghanima.

Sababu ya Kuitwa Jina Hilo

Eneo la Kudr lipo umbali wa takribani kilomita 170 kutoka Madina. Baadhi wanaliita eneo hilo kwa jina la Qarqarat al-Kudr. Na baadhi yao wanalitambua kama Qararat al-Kudr. Katika eneo kulikuwa na kisima cha maji ambacho kilikuwa ni cha kabila la Bani Salim. Kwa kuzingatia kuwa, eneo hilo likuwa ni mahali pa kukusanyika makabila mawili ya Bani Salim na Ghatafan, kwa ajili ya kupigana vita na Waislamu, jina la vita hivyo vikaondokewa kuwa mashuhuri kwa jina la Qarqarat al-Kudr. Aidha tukio hilo linajulikana pia kwa jina la vita vya Qarqarat al-Kudr na Ghatafan.

Tukio

Mwaka wa 3 Hijria, idadi kadhaa ya watu wa makabila mawili ya Bani Salim na Ghatafan walikusanyika katika eneo la Kudr ili waushambulie mji wa Madina. Habari ya hiyo ikamfikia Bwana Mtume (saww). Mtume (saww) akamteua Ibn Abi Maktum , au kwa riwaya nyingine akamteua Muhammad bin Maslamah al-Ansari au Siba’ bin Urfuta al-Ghifari kuwa mrithi na kiongozi wa Madina wakati yeye hayupo, kisha akaondoka na kuwafuata watu wale. Bendera ya jeshi la Waislamu ilikuwa imebebwa na Imam Ali (as). Wanajeshi wa Bani Salim na Ghatafan waliondoka katika eneo hilo, kabla hata ya kuwasili jeshi la Waislamu. Mtume (saww) akawatuma baadhi ya askari wake katika maeneo ya miinuko ili wakafanye uchunguzi kuhusiana na hali ya adui. Walipofika huko walikutana na idadi kadhaa ya wachunga kondoo na ngamia ambapo miongoni mwao alikuwemo kijana aliyejulikana kwa jina la Yasar. Wakawachukua pamoja na ngamia zao na kuwakabidhi kwa Bwana Mtume (saww). Kisha Waislamu wakarejea Madina na kisha wakagawana ghanima katika nyumba ya Sarar. Yasar kwa kuwa alikuwa akiswali wakamuweka katika hisa ya Bwana Mtume. Mtume naye kwa upande wake akamuachilia huru.

Zama za Kutokea Kwake

Vitabu vya historia vinaeleza kuwa, vita vya Qarqarat al-Kudr vilitokea baada ya vita vya Sawiq. Baadhi ya waandishi wa historia wanasema kuwa, vita hivi vilitokea Mfunguo Mosi Shawwal mwaka wa Pili Hijria , huku baadhi wakiamini kwamba, vilitokea Mfunguo Nne Muharram mwaka wa tatu Hijria. Kuanzia siku Mtume alipoondoka Madina hadi kurejea kwake katika mji huo, ilimchukua siku 15.

Vyanzo

  • Ibn Abdul-Bar, Yusuf bin Abdallah, al-Isti’ab Fi Ma’arifat al-Sahabah, Mhakiki: Ali Muhammad Bijawi, Beirut, Daru;-Jil, 1412 Hijria/1992 Miladia.
  • Ibn Sa’ad, Muhammad bin Sa’ad, al-Tabaqat al-Kubra, mhakiki: Muhammad Abdul-Qadir Ataa, Beirut, Darul-Kutub al-llmiyah, 1410 Hijria/1990 Miladia.
  • Ibn Hisham, al-Sirat al-Nabawiyah, mhariri: Mustafa Saqa, Ibrahim Abiyari na Abdul-Hifdh Shibli, Beirut, Darul-Ma’arifah, Bita.
  • Baladhuri, Ahmad bin Yahya, Insan al-Ashraf, jz.1, mhakiki: Muhammad Hamidullah, Misri, Darul-Ma’arif, 1959 Miladia.
  • Hamawi, Yaaqut bin Abdallah, Mu’jam al-Buldan, Beirut, Dar Sadir, 1995 Miladia.
  • Maqrizi,Ahmad bin Ali, Imtina al-Asmaa, Mhakiki: Muhammad Abdul-Hamid Numeisi, Beirut, Darul-Kutub al-Ilmiyah, 1420 Hijria/1999 Miladia.
  • Waqidi, Muhammad bin Omar, al-Maghazi, mhakiki: Marsden Jones, al-Maghazi, Beirut, Taasisi ya al-A’lami, 1409 Hijiria/1989 Miladia.