Umaharimu wa kuchangia ziwa
- Makala hii inahusiana na wasifu kuhusu mafuhumu na maana ya kifikihi na hivyo haiwezi kuwa kigezo cha amali na matendo ya kidini. Kwa ajili ya amali za kidini, rejea katika vyanzo vingine.
- Makala hii inahusiana umaharimu wa kuchangia ziwa. Ili kufahamu kuhusiana na wa kuchangia ziwa (kunyonya) angalia makala za Maharimu na kunyonyesha.
Umaharimu kwa kunyonya au kuchangia ziwa moja (Kiarabu: التحريم بالرضاع) ni aina ya umaharimu unaopatikana kutokana na watu wawili au zaidi kuchangia ziwa (kunyonya ziwa moja) na kwa mujibu wa hilo, watu hawa haijuzu kwao kuoana. Aina hii ya umaharimu una masharti yake na miongoni mwayo ni: Mwanamke anayenyonyesha awe amepata ujauzito kwa njia ya halali, unyonyeshaji uwe ni wa mara kadhaa na baina ya mwanamke anayemnyonyesha mtoto huyu kusiweko na mwanamke mwingine anayemnyonyesha mtoto huyo au mtoto kupewa chakula kingine na umri wa anayenyonyeshwa uwe chini ya miaka miwili kwa mujibu wa kalenda ya Hijiria.
Watu ambao kutokana na kuchangia ziwa inakuwa haramu kwao kuoana wanatambulika kama maharimu wa kunyonya au kuchangia ziwa na kuna hukumu na sheria maalumu kuwahusu kama vile kuwa haramu kuoana. Katika umahramu wa kuchangia ziwa, kama aliyenyonyeshwa ni mtoto wa kiume basi anakuwa maharimu wa mama wa kumnyonyesha, (mwanamke ambaye amemnyonyesha), mama, bibi, dada, binti, mjukuu, shangazi na mama wadogo wa mama aliyemnyonyesha. Kama aliyenyonyeshwa ni binti, basi anakuwa maharimu wa baba wa kunyonya (mume wa mke aliyemnyonyesha) na vilevile baba, kaka, amu, mjomba, mtoto, na wajukuu wa baba huyo ambaye ni mume wa mama yake wa kunyonya. Kadhalika, kaka, mtoto, mjukuuu, baba, babu na mjomba wa mama aliyemnyonyesha wanakuwa maharimu wake.
Baadhi ya mafakihi wa Kisunni wanasema kuwa, kunyonya mwanaume mwenye umri mkubwa (aliyebaleghe) matiti ya mwanamke asiye maharimu wake ni miongoni mwa mambo ambayo yanapelekea kupatikana umaharimu. Akthari ya mafakihi wa Kisunni na mafakihi wote wa Kishia wamepinga hukumu hii na kukitaja kitendo hicho kuwa ni haramu.
Utambuzi wa Maana (Conceptology)
Umaharimu wa kuchangia ziwa ni aina ya udugu ambao unapatikana kutokana na kuchangia ziwa watu wawili au zaidi na kwa mujibu wa kitendo hicho, ni haramu kwa wahusika hao kuoana. [1] Maharimu wa kuchangia ziwa ni watu ambao wamekuwa ndugu kupita kuchangia ziwa na hivyo wanakuwa maharimu na kwa msingi huo kuna sheria maalumu ambazo zinawahusu kama vile kuwa haramu kuoana. [2] Katika maandiko ya fiq'hi mtoto ambaye amenyonya maziwa ya asiyekuwa mama yake katika mazingira maalumu anafahamika kwa jina la "Murtadhiu", mwanamke mwenye kunyonyesha "Mur'dhiah" na mwenye maziwa (mume ambaye alimpa ujauzito mwanamke anayenyonyesha) anaitwa "fahal" au "Swahib Laban". [3]
Istilahi hizi zinajadiliwa katika milango ya fiq'hi ya nikaha na mirathi. [4] Kwa mujibu wa kifungo cha 1046 cha katiba ya Iran na kwa kufuata fiq'h ya Shia Imamiyyah, ni marufuku kwa ndugu wa kuchangia ziwa kuoana. [5]
Masharti
Wanazuoni na mafakihi wa Kishia wakitegemea Aya za Qur'an na hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maasumina (a.s) wametaja masharti ambayo kupitia kwayo inatimia umahramu wa kuchangia ziwa.
- Mwanamke anayenyonyesha awe amepata ujauuzito kwa njia ya halali. [7]
- Mtoto anayenyonyeshwa anyonyeshwe kwa kiwango ambacho nyama itaota na mifupa yake itaimarika. [8]
- Anayenyonyeshwa kwa akali anyonye kwa mwanamke huyo anayemnyosha usiku na mchana, na katika kipindi hiki chakula cha mtoto huyu kiwe ni maziwa tu ya mwanamke huyo. [9] Kunywa maji kwa ajili ya kuondoa kiu, kula chakula au kunywa dawa kwa ajili ya tiba ambazo ananyweshwa mtoto, kama haya hayatakuwa yametoka katika hali ya kawaida na mazoea, hayatatia dosari hukumu hii. [10]
- Mafakihi kama Sheikh Mufid, [11] Salar Daylami, [12] Ibn Barraj, [13] Abu Salah Halabi, [14] na Allama Hilli [15] wamesema kuwa, idadi ya mtoto kunyonyeshwa inapaswa kuwa mara 10 huku mafakihi kama Sheikh Tusi, [16], Muhaqqiq Hilli, [17] na Shahid al-Awwal, [18] wao wametaja idadi hiyo kuwa ni mara 15.
- Muda na idadi ambayo mtoto ananyonyeshwa vinapaswa kuwa mtawalia na hilo liwe ni kwa mwanamke mmoja na baina ya kunyonyeshwa mtoto huyo asipewe chakula au kunyonya maziwa ya mwanamke mwngine. [19]
- Mtoto anapaswa kunyonya moja kwa moja maziwa kutoka katika matiti na sio kupitia njia nyingine. [20].
- Umri wa mtoto anayenyonya unapaswa kuwa chini ya miaka miwili kwa mujibu wa kalenda ya Hijria. [21] Kama sehemu fulani ya unyonyaji maziwa wa mtoto huo ni baada ya miaka miwili, umahramu hautatimia. ]22]
Imekuja katika tafsiri ya Nemooneh kwamba, falsafa ya umaharimu wa kuchangia ziwa ni mshabaha ambao wanao watoto wa kunyonya maziwa na watoto wa nasaba kutokana na kukua nyama na kuimarika mifupa kutokana na maziwa ya mnyonyeshaji na kila mmoja kati yao anahesabiwa kuwa ni sehemu ya mwili wake. (mwili wa mamma mnyonyeshaji) [23]
Maharimu wa Kunyonya
Mafakihi wakitegemea hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) inayosema "kila ambacho ni haramu kutokana na nasaba, basi ni haramu pia kutokana na kunyonya (kuchangia ziwa)", wanasema kuwa, wanawake wote ambao ni haramu kuoana nao kutokana na nasaba, ni haramu kuoana nao pia kutokana na sababu ya kuchangia ziwa. [25] Endapo umaharimu huo utathibiti kutokana na kuchangia ziiwa, watu wafuatao pia huwa maharimu baina yao:
- Kama aliyenyonyeshwa ni binti, basi anakuwa maharimu wa baba wa kunyonya (mume wa mke aliyemnyonyesha au baba wa kunyonya) na vilevile baba, kaka, amu, mjomba, mtoto, na wajukuu wa mume wa yule mwanamke. Na kadhalika baba, babu, kaka, mtoto, mjukuu, amu na mjomba wa mama aliyemnyonyesha wanakuwa maharimu wake. [26]
- Kama aliyenyonyeshwa ni mtoto wa kiume basi anakuwa maharimu wa mama wa kumnyonyesha, (mwanamke ambaye amemnyonyesha, mama wa kunyonya), na vilevile mama, bibi, dada, binti, mjukuu, shangazi na mama wadogo wa mama aliyemnyonyesha wanakuwa maharimu wake. [27] Watu waliotajwa wanakuwa maharimu wa mtoto aliyenyonyeshwa na hawawi maharimu wa ndugu wa mtoto huyo, hata baba na kaka zake (kaka na ndugu wa mtoto aliyenyonyeshwa) hawawi maharimu. [28]
Kumnyonyesha Mtu Mzima
Hii ni anuani ambayo inapatikana na kuzungumziwa katika maandiko ya hadithi na ya kifikihi ya Waislamu wa madhehebu ya Kisunni [29] na maana yake ni kumnyonyesha maziwa mtu mzima au aliyebaleghe kupitia matiti ya mwanamke ambaye si maharimu wake. [30] Baadhi ya mafakihi wa Kisunni wakitegemea hadithi kutoka kwa Bibi Aisha ambayo kwa mujibu wake, ili kupatikana umaharimu, Mtume (s.a.w.w) alimruhuusu mwanamke mmoja amnyonyeshe maziwa yake mwanaume mtu mzima aliyekuwa baleghe ili kwa njia hiyo awe maharimu wake, [31] wamelitambua suala la mwanaume aliyebaleghe kunyonya maziwa ya mwanamke anayenyonyesha kuwa ni miongoni mwa sababu za kupatikana umahramu na udugu. [32] Kwa mujibu wa nukuu ya Ibn Rushd katika kitabu cha Bidayat al-Mujtahid ni kwamba, kuna tofauti za kimitazamo kuhusiana na kupatikana umahramu kupitia kunyonya maziwa baada ya mtoto kufikisha umri wa miaka miwili. [33] Yeye anaamini kwamba, akthari ya mafakihi wa Ahlu-Sunna kama vile Malik, Abu Hanifa na Shafii hawajakubaliana na mtazamo wa kupatikana umaharimu kupitia kunyonya maziwa (mtu mzima) baada ya miaka miwili na wanasema kuwa, kitendo hicho ni haramu. [34]
Benki ya Maziwa
Benki ya maziwa ya mama ni kitendo kinachohusika na kukusanya maziwa, kuyahifadhi na kisha kuyagawa kwa watoto wagonjwa, wachanga na watoto waliozaliwa kabla ya wakati ambao wamekosa fura ya kunyonya maziwa ya mama. [36] Fikra ya kuasisi na kuanzisha benki ya maziwa ilipendekezwa mwaka 1909 na Shirika la Afya Duniani (WHO) na mwaka mmoja baadaye, kituo cha kwanza cha Benki ya maziwa ya mama kikaanzishwa nchini Marekani. Kituo cha kwanza cha Benki ya Maziwa nchini Iran kiliasisiwa mwaka 2016 katika mji wa Tabriz. [38]
Kwa mtazamo wa mafakihi wa Kishia ni kwamba, kutumia maziwa ya Benki ya Maziwa hakupelekei kupatikana umaharimu. [39] Kwani kwa mujibu wa mtazamo wao ni kwamba, umahramu unatimia tu kupitia kunyonya mtoto kupitia matiti. [40] Hata hivyo baadhi ya mafakihi wa Ahlu-Sunna wanasema kuwa, kutumia watoto wachanga maziwa ya Benki ya Maziwa kunapelekea kuvurugika na kuchanganyika vizazi na nasaba na kwamba, hicho ni kitendo kisicho cha Kiislamu. [41] Hii ni kutokana na kuwa, mafakihi kama Malik bin Anas anaamini kwamba, kunyonya maziwa mtoto kupitia matiti au kwa njia nyingine yoyote ile ambayo inaingiza maziwa katika koo lake ni mambo ambayo yanapelekea kupatikana umaharimu. [42]
Rejea
Vyanzo
- Ḥillī, Jaʿfar b. al-Ḥusayn al-. Sharāʾiʿ al-Islām fī masāʾil al-ḥalāl wa l-ḥarām. Edited by ʿAbd al-Ḥusayn Muḥammad ʿAlī Baqāl. Qom: Muʾassisa-yi Ismāʿīlīyān, 1408 AH.
- Ḥillī, Ḥasan b. Yūsuf al-. Tabṣirat al-mutaʿallimīn fī aḥkām al-dīn. Edited by Muḥammad Hādī Yūsifī Gharawī. Tehran: Wizārat-i Farhag wa Irshād-i Islāmī, 1411 AH.
- Ibn Māja, Muḥammad b. Yazīd. Sunan. Edited by Muḥammad Fuʾād ʿAbd al-Bāqī. Beirut: Dār al-Fikr, [n.d].
- Jazīrī, ʿAbd al-Raḥmān al- & et. al. Al-Fiqh ʿalā l-madhāib al-arbaʿa wa madhhab Ahl al-Bayt. Beirut: Dār al-Thaqalayn, 1419 AH.
- Kulaynī, Muḥammad b. Yaʿqūb al-. Al-Kāfī. Edited by ʿAlī Akbar Ghaffārī & Muḥammad Ākhūndī. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmīyya, 1407 AH.
- Mālik b. Anas. Al-Muwaṭṭaʾ. Edited by Muḥammad Fuʾād ʿAbd al-Bāqī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-ʿArabī. 1406 AH.
- Najafī, Muḥammad Ḥasan al-. Jawāhir al-kalām. Edited by ʿAbbās Qūchānī & ʿAlī Ākhūndī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, 1404 AH.
- Qurṭubī, Muḥammad b. Aḥmad al-. Tafsīr al-Qurṭubī. Edited by Aḥmad ʿAbd al-ʿAlīm Bardūnī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-ʿArabī, 1405 AH.
- Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Khilāf. Edited by Khurasānī. Qom: Daftar-i Intishārāt-i Islamī, 1407 AH.