Tafsir al-Riwai
Makala hii inazungumzia Tafsir al-Riwai. Ili kuona Faharast ya tafsiri za riwai, angalia makala ya Faharast Tafsir al-Riwai Shia.
Tafsir al-Riwai / maathur / naqli (Kiarabu: التفسير الروائي، أو التفسير بالمأثور أو التفسير النقلي) ni aina ya kufasiri Qur’ani kwa kutumia hadithi. Waislamu wa madhehebu ya Kishia wakiwa na lengo la kufasiri Qur’ani kwa kutumia hadithi wanatumia hadithi za Mtume (s.a.w.w) na Maimamu Maasumu (a.s), Wafasiri wa Qur’ani wa Kishia wanaamini kwamba, hadithi zinazonasibishwa (zinazoaminika kuwa zimepokewa) na Mtume (s.a.w.w) na Maimamu Maasumina (a.s) ni aina bora kabisa na za kutegemewa za tafsiri na kubainisha Qur’ani tukufu; pamoja na hayo, kuna hadithi bandia pia ambazo zimeripotiwa kuweko katika hadithi za kufasiri Qur’an.
Vitabu vya tafsiri kama Tafsir Ayyashi, Tafsir Qummi, Tafsir Nur al-Thaqalein na Tafsir al-Burhan ni mifano ya tafsiri za Qur’ani kwa mujibu wa hadithi za Waislamu wa madhehebu ya Shia, huku Tafsir Jami’ al-Bayan ikiwa ni mfano wa tafsiri ya Qur’ani kwa mujibu wa hadithi kwa Waislamu wa madhehebu ya Sunni. Muhammad Hadi Maarefat anaamini kuwa, athari muhimu kabisa ya tafsiri katika Ulimwengu wa Kiislamu awali iliundika kwa kutegemea hadithi za tafsiri.
Utambuzi wa maana
Tafsir al-Riwai, Tafsir al-Maathur au Tafsir Naqli [1] kwa mujibu wa mtazamo na rai ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ni aina ya tafsiri ya Qur’ani ambayo inategemea hadithi zilizopokewa na kunukuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) na Maimamu wa Shia. [2] Waislamu wa madhehebu ya Ahlu-Sunna wao wanatambua maneno ya masahaba na tabiina pia kwamba, ni msingi wa kutumia katika kufasiri Qur’ani kwa mujibu wa hadithi. [3]
Umuhimu na itibari ya hadithi za kufasiri Qur’ani
Wafasiri wa Qur’ani wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume (s.a.w.w) mbali na kuwa alikuwa na jukumu la kufikisha ujumbe wa Wahyi, alikuwa na wadhifa pia wa kubainisha na kufafanua maneno ya Mwenyezi Mungu. [4] Itikadi ya wafasiri hawa imetegemea Aya za 44 na 46 za Surat al-Nahl. Kwa msingi huo wafasiri wa Shia na Sunni wanaamini kwamba, maneno au hadithi za kufasiri Qur’ani zinazonasibishwa kwa Mtume (s.a.w.w) endapo itathibiti usahihi wake, ni moja ya aina bora kabisa na kutegemeka ya aina ya tafsiri. [6] Waislamu wa madhebu ya Shia wakitegemea Hadithi ya Thaqalaini (Hadithi ya Vizito Viwili) wanaamini kwamba, Maimamu wa Kishia nao pia ni katika vyanzo vya Tafsir al-Riwai. [7]
Licha ya umuhimu wa hadithi za tafsiri, lakini wafasiri wanaamini kuwa, kuna hadithi bandia pia baina ya hadithi tajwa ambazo zilipachikwa na kubandikwa kwa minajili ya kuinua daraja ya mmoja wa masahaba. [8] Kuwekwa hadithi bandia kuhusiana na sababu ya kushuka Aya ya 113 ya Surat al-Tawba yametambuliwa kuwa moja ya maeneo ambayo Tabari na Bukhari wameyatambua kuwa, wafasiri wa Ahlu-Sunna walipachika. [9] Kwa mujibu wa sababu iliyotajwa ya kushuka Aya ya 113 ni kuhusiana na Abu Talib baba yake Imamu Ali (a.s) ambayo ilishuka wakati wa kuaga kwake dunia na inabainisha kuwa kwake mshirikina mpaka mwishoni mwa umri wake (yaani hakuwa Mwislamu mpaka anaaga dunia). Katika hali ambayo Tabari na Bukhari wanaamini kwamba, Abu Talib aliaga dunia miaka mitatu kabla ya Hijira (kuhama Mtume kutoka Makka na kwenda Madina) na Aya hii ilishuka mwaka wa 9 Hijiria. [10] Hadithi kama hizi zinaaminiwa na wahakiki kwamba, aghalabu zilipachikwa na Mayahudi waliosilimu na zinatambuliwa kwa jina la Israiliyat. [11]
Mifano ya Tafsir val-Riwai
Muhammad Hadi Maarefat, mmoja wa wahakiki na wafasiri wa Qur’ani wa zama hizi anaamini kuwa, vitabu muhimu kabisa vya tafsiri ya Qur’ani vya waliotangulia viliandikwa kwa kuegemea hadithi za kifafanuzi na tafsiri na kutegemea maana za kifalsafa, kiteolojia na kifasihi za Qur’ani. Ni idadi ndogo tu inayoonekana ya tafsiri hizi za awali. [12] Vitabu muhimu vya Tafsir al-Riwai ni:
- Tafsir al-Ayyashi: Mwandishi Muhammad bin Mas’oud al-Ayyash, mmoja wa mafakihi wa Kishia katika karne ya 14 Hijiria, na Ustadh Muhammad bin Omar Kashi. [13] Ayyashi katika kitabu chake hadithi za kitafsiri alizonukuu kutoka kwa Maimamu wa Kishia amenukuu pia na sanadi na mapokezi yake. [14] Pamoja na hayo, ni sehemu ndogo tu ya Tafsiri ya Ayyash ambayo inapatikana. [15]
- Tafsir Qummi: Tafsiri hii inanasibishwa na Ali bin Ibrahim al-Qummi ambapo mwanafunzi wake yaani Abul-Fadhl al-Abbas bin Muhammad mmoja wa wajukuu wa Imamu Mussa al-Kadhim (a.s) ndiye aliyeiandika ambapo alistafidi na hadithi zilizonukuliwa na Ali bin Ibrahim na vilevile Tafsir Abi Jarud. [16] Kuhusiana na Abul-Fadhl al-Abbas bin Muhammad yaani mwandishi wa kitabu hiki, hakuna taarifa zaidi ya kuwa alikuwa Alawi (kutoka katika kizazi cha Imamu Ali) na ni katika wanafunzi wa Ali bin Ibrahim. [17] Tafsiri hii licha ya kuwa kiujumla imetambuliwa kuwa haina mushkili, lakini kuna hadihi zilizotumika ndani yake ambazo imeelezwa kuwa ni dhaifu. [18]
- Jami’u al-Bayan: Mwandishi Muhammad bin Jarir Tabari, mmoja wa wafasiri wa Qur’ani wa Kisunni. Tabari ametambuliwa kama baba wa elimu ya tafsiri kutokana na kitabu chake cha tafsiri kuwa kipana na jumuishi. [19] Hata hivyo ametuhumiwa kwamba, amenukuu hadithi dhaifu, bandia na kuamini wapokezi maj’hul (wasiofahamika). [20]
- Tafsir al-Burhan: Mwandishi Sayyid Hashim Bahrani (takribani 1050-1107 au 1109 Hijiria). Katika utanguzlizi wa kitabu chake hiki cha tafsiri, Bahrani anakitaja kitabu hiki kuwa kina mchango mkubwa kwa wasomaji katika kuwatambulisha na kuwafahamisha siri za elimu ya Qur’ani, masuala ya elimu ya kisheria, visa na habari za Manabii pamoja na fadhila za Ahlul-Bayt (a.s) kwani hadithi zake zimechukuliwa kutoka kwa Ahlul-Bayt (a.s) ambao Wahyi ilishuka katika nyumba yao. Alichukua hadithi za kitabu chake cha al-Burhan kutoka katika vitabu vyenye itibari na vya kuaminika ambavyo waandishi wake ni katika walimu wa kutegemeka na aghalabu alinakili hadithi kwa njia ya Maimamu na katika baadhi ya sehemu amenukuu hadithi za Ahlu-Sunna ambazo zinaafikiana na hadithi za Ahlul-Bayt (a.s) au ambazo zinabainisha fadhila za Ahlul-Bayt (a.s). Ibn Abbas pia (kutokana na kuwa alikuwa mwanafunzi wa Imamu Ali (a.s) amenukuu kiwango kidogo katika kufasiri Aya za Qur’ani. [21]