Shirikisho la Kimataifa la Shia Khoja Ithnaasharia
Shirikisho la Kimataifa la Shia Khoja Ithnaasharia (The World Federation of Khoja Shia Ithna-Asheri Muslim Communities) [1] ni kituo muhimu cha maamuzi cha Mashia Makhoja Ithnaashari ulimwenguni ambapo asasi zake zote zinafanya kazi chini ya usimamizi na uangalizi wa shirikisho hili. Shirikisho hili lina mchango na nafasi pia ya kuleta uratibu baina ya vikundi vya Kikhoja na makao yake makuu yanapatikana London, Uingereza.
Historia yake
Jiwe la msingi la Shirikisho la Kimataifa la Shia Khoja Ithnaasharia liliwekwa London katika muongo wa 1970 kufuatia kufukuzwa kwa jamii yenye asili ya Asia kutoka Uganda. Kabla ya Shirikisho la Afrika na Jumuiya ya Khoja Ithnaasharia kuanzishwa katika nchi mbalimbali ulimwenguni, viongozi wa baadhi ya jumuiya hiyo, walijadili suala la kuanzishwa kwa Shirikisho la Kimataifa. Iliamuliwa katika mkutano huo kwamba, kuundwe kamati ya kuandaa katiba ya shirikisho hilo. Katika mkutano uliofanyika mwaka wa 1980, makundi mbalimbali yaliidhinisha na kupasisha hilo na Shirikisho la Kimataifa likawa limeanza rasmi shughuli zake. Katika mwaka huo huo, shirikisho hilo lilisajiliwa kama shirika la kutoa misaada ya kidini nchini Uingereza. [3]
Jawad Naqvi, Mulla Asghar na baada yake Hasnain Walji na Hashem Jawad walishika wadhifa wa ukuu na kiongozi wa shirikisho hilo. [4]
Majukumu
- Kusimamia shirikisho la kieneo na Jumuiya za Khoja Ithnaasharia ulimwenguni. [5]
- Kuunganisha sera kuu kuhusiana na kumchagua Marjaa Taqlid, kutoa Khumsi, Zaka n.k. [6]
Kutangaza takwimu makini za Makhoja
Mashirikisho na Jumuiya za Makhoja, hutangaza kwa sekretarieti ya Shirikisho la Kimataifa la Shia Khoja Ithnaasharia idadi ya Makhoja miezi sita kabla ya kufanyika mkutano wa shirikisho hilo ambao hufanyika mara moja kila baada ya miaka mitatu. Takwimu hizo huwa msingi na kigezo cha idadi ya Mashia Khoja Ithnaasharia duniani. [7]
Muundo
Jumuiya hii ina wajumbe 135 ambao huchaguliwa miongoni mwa mashirikisho 40 na Jumuiya 26 za Makhoja Shia Ithnaasharia. [8] Makao yake makuu yanapatikana mjini London, Uingereza [9] na sekretarieti yake ipo katika Wilaya ya Stanmore katika mji huo. [10]
Kulingana na katiba, shirika hili ni taasisi huru ambayo mwenyekiti wake na wajumbe wa bodi huchaguliwa kushikilia wadhifa huo kwa muda wa miaka mitatu kupitia uchaguzi mkuu. Sera ya shirika hili huamuliwa wakati wa mkutano kila baada ya miaka mitatu. [11] Bodi ya Wakurugenzi wa jumuiya hii inaundwa na Rais, naibu, katibu mkuu na mweka hazina. [12]
Sera na mipango ya asasi hii huainishwa katika kongamano linalofanyika mara moja kila baada ya miaka mitatu. [13] Maamuzi yake ni ya lazima kutekelezwa na mashirikisho yote ya kikanda.[14]
Malengo
- Kumairisha madhehebu ya Shia Ithnaasharia.
- Kuinua kiwango cha kifedha kwa wanachama.
- Kuongeza kiwango cha ufahamu wa kielimu na kimadhehebu cha wanachama.
- Ustawi wa kijamii na kusaidia wasiojiweza. [15]
Huduma
Tangu kuanzishwa kwake, Shirikisho la Kimataifa la Shia Khoja Ithnaasharia limechukua hatua za kuboresha maisha ya jamii za Khoja ulimwenguni, haswa katika bara Hindi, nyingi ya shughuli hizi zilifanywa katika miaka ya 1980-1990, katika uwanja wa kutatua shida za kitamaduni, kijamii na kiuchumi ya Makhoja nchini India, hasa katika jimbo la Gujarat na Wilaya ya Kutch India na katika baadhi ya majimbo ya Pakistan. [16]
Mashirikisho ya kikanda
Shirika hili lina mashirikisho ya kikanda katika mabara ya Afrika, Amerika, Ulaya na Asia na katika baadhi ya makundi mengine. [17] Mashirikisho ya kikanda na vikundi vya wanachama wake, ambao wawakilishi wao ni wanachama wa shirika hili, wana jukumu muhimu katika maamuzi ya Shirikisho la Kimataifa [18]
Shirikisho la Shia Khoja Ithnaasharia Afrika
- Makala asili: Shirikisho la Shia Khoja Ithnaasharia Afrika
Shirikisho la Shia Khoja Ithnaasharia Afrika (The African Federation of Khoja Ithna-Asheris) linaundwa na Mashia wenye asili ya India (wahindi) walioko katika eneo la Afrika Mashariki ambapo makao yake makuu ni Dar es Salaam. [19]
Kujikimu kigharama
Sehemu kubwa ya mapato ya mashirika ya Khoja Ithnaasharia, yakiwemo mashirikisho ya kimataifa na kikanda na taasisi zao zenye mafungamano, hutolewa kwa usaidizi wa Mashia Khoja Ithnaasharia wanaoishi katika nchi za Afrika Mashariki na Amerika ya Kaskazini. Wengi wa watu hawa ni wafanyabiashara wakubwa na kila mwaka hutoa sehemu ya faida ya biashara zao kwa maafisa wa mashirikisho ya ulimwengu au ya kikanda. [20] Zaidi ya hayo, maofisa wa mashirikisho, kwa idhini ya Marjaa wao, Ayatullah Sistani, wanatumia sehemu ya hisa ya Imam (fungu) na Masayyid inayotolewa kwa ajili ya kutekeleza shughuli kitablighi na kiujenzi. [21]